Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu: Miaka 60 ya Maisha na Utume Tanzania
Na Padre Chesco Peter Msaga, C.PP.S. - Roma
Baba Mtakatifu Leo XIV tarehe 18 Septemba 2025 alikutana na kuzungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 22 wa Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, C.PP.S., ulionogeshwa na kauli mbiu: “Damu ya Kristo, Tumaini la Ulimwengu” na kuwapongeza waasisi wa Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, waliokuwa wazi kwa utendaji wa Roho Mtakatifu, wakaweza kusoma na kufasiri alama za nyakati na hatimaye, kujibu kwa njia yenye mwanga angavu kwa mahitaji ambayo yalijitokeza hatua kwa hatua. Baba Mtakatifu Leo XIV pamoja na mambo mengine alikazia kuhusu wito wa maisha ya kitawa yanayosimikwa katika ujenzi wa jumuiya, kama mahali patakatifu na chemchemi ya maongozi; ushuhuda na nguvu katika utume; ili katika ushirika, wema uweze kuongezeka na kukua. Pili ni Utii kama kielelezo cha upendo, ili hatimaye, kutafuta na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha na utume wao. Baba Mtakatifu Leo XIV anasema, Utii, katika maana yake ya ndani kabisa unakita mizizi yake katika dhana ya kuwasikiliza wengine kwa bidii na ukarimu; Utii ni tendo kuu la upendo linalosimikwa katika imani, sadaka na ujenzi wa mahusiano ya kudumu; maisha ya pamoja na hivyo kuimarishwa katika uaminifu. Utii ni shule ya uhuru katika upendo. Mtakatifu Gaspari alisoma alama za nyakati. Alikuwa na uwezo wa: kutazama, kutathmini, kupenda na kisha kuyamwilisha yote haya katika matendo, tayari kuwahudumia watu katika mahitaji yao msingi, huku wakiitambua sauti ya Mungu katika umaskini wa jirani zao. Hii ni changamoto kwa wanashirika katika ulimwengu mamboleo kujikita katika maadili, ili kusonga mbele! Tasaufi ya Damu Azizi ya Yesu ni msaada kwa kila Mkristo kwa kuwa Damu ya Kristo ni msingi wa ukombozi wa mwanadamu na ni kielelezo cha juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa watu wote. Tasaufi hii ina msingi wake katika Neno la Mungu na katika Fumbo la Ekaristi Takatifu ambalo ndilo chanzo na kilele cha maisha ya kila siku ya Kanisa na maisha ya Mkristo kwa jumla. Tena Ekaristi Takatifu ni ujumuisho mzima wa imani ya Kikristo na ni msingi wa mitazamo sahihi ya Kikristo. Rej KKK 1324 na 1327.
Maisha ya Wamisionari wa Damu Azizi nchini Tanzania ni simulizi ya ukuaji mkubwa na wa kina, kutoka kuwa misheni ndogo ya wageni hadi kuwa Kanda yenye kujitegemea na yenye nguvu, ambayo mwaka huu 2026 inaadhimisha miaka 60 tangu kuanzishwa kwake. Safari yao imeambatana na hatua mbalimbali muhimu zinazoonesha dhana za uongofu, mabadiliko na upyaisho. Kupitia misingi hii, wamisionari wanajitahidi kukuza uaminifu wa kina zaidi kwa wito wao, unaojengwa juu ya mabadiliko endelevu na utayari wa kujibu mahitaji ya wale ambao mara nyingi husahaulika katika jamii. Kiini cha utume huu ni maisha ya sala na daima kupitia Neno la Mungu. Kupitia ushirika na watu wa Mungu pamoja na malezi endelevu katika karama yao ya kitawa, wamisionari wanajitahidi kuwa mawakala wa kweli wa mabadiliko ya kijamii na kiroho. Dhamira yao imejikita katika mambo ya kiroho na kwa vitendo kwa wakati mmoja, wanapoifanya Injili kuwa hai kwa matendo yanayogusa maisha ya maskini, walio dhaifu zaidi na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Chagizo kutoka katika Maandiko Matakatifu: Andiko moja linalofupisha vyema Ari ya kimisionari ni Luka 4:18: "Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta niwahubirie maskini Habari Njema; amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru wanaoonewa." Hamasa hii ya kibiblia inaimarisha mwito wa kimisionari wa uongofu na huduma, ikiwakumbusha nguvu ya imani inayobadilisha maisha inapodhihirishwa katika ulimwengu wa kila siku. Maisha na Utume wa C.PP.S. nchini Tanzania: Mabadiliko ya misheni ya Tanzania yanaonekana wazi zaidi kupitia hatua mbalimbali za maendeleo yake na uongozi wake.
Misheni ilianzishwa tarehe 19 Mei 1966 huko Manyoni, Mkoa wa Singida, na wamisionari watatu waanzilishi kutoka Italia: Don Giuseppe Montenegro, C.PP.S., Don Dino Gioia, C.PP.S., na Bruda Franco Pallumbo, C.PP.S. Baadaye wamisionari kutoka Kanada na Marekani walijiunga nao. Eneo hilo lilikuwa kubwa sana na lilikuwa na upungufu mkubwa wa miundombinu, huku umaskini na hali ya kutengwa vikileta changamoto kubwa kwa wale waliokuja kuhudumu. Badala ya kuanza mara moja kujenga majengo makubwa, wamisionari walifanya uamuzi wa kipekee wa kuishi pamoja na wananchi wa eneo husika. Walijifunza lugha ya Kiswahili ili kujenga mawasiliano ya kweli na wakajibu mahitaji yaliyokuwa ya lazima zaidi. Katika mazingira hayo, utume wao ulitoka katika mahubiri ya maneno pekee na kuelekezwa katika matendo halisi kama vile kuchimba visima vya maji, kujenga shule na zahanati. Hivyo, Karama ya Damu ya Kristo iligeuka kuwa ishara hai ya ukombozi kutoka katika kiu, magonjwa na ujinga. Kama Bwana asemavyo: “Nalikuja ili wawe na uzima, kisha wawe nao tele” (Yn 10:10.) Upyaisho Kupitia Jubilei na Hija: Maadhimisho ya miaka 60 ya uwepo wa Wamisionari wa Damu Azizi nchini Tanzania, yanayoadhimishwa mwaka 2026, yanaashiria kuanza kwa Jubilei ya Almasi; kipindi maalumu cha upyaisho wa kijumuiya na wa kila mmoja binafsi. Kuwashwa kwa Mshumaa wa Jubilei mwezi Februari 2026 ni ishara ya kuwaletea watu mwanga na “kuhuisha moto” wa utume kwa kuwasha upya ari ya huduma. Kwa miaka yote, upyaisho wa kiroho umekuwa sehemu muhimu ya kazi yao. Hija ya masalia matakatifu, hasa yale ya Mwenyeheri Giovanni Merlini, ni ushuhuda wa hamu yao ya kuimarisha imani katika jumuiya za waamini. Kwa kusafiri na masalia hayo katika majimbo mbalimbali nchini Tanzania, wamisionari huwasaidia waamini kujifunza maisha ya Mwenyeheri Merlini, kupata hamasa kutokana na fadhila zake na kuimarisha mizizi ya kiroho ya utume wao.
Wongofu Kupitia Athari za Kijamii: Katika mapokeo ya C.PP.S., “uongofu” unaeleweka kama kuelekea kwa walioko pembezoni mwa jamii na kushiriki katika “ukombozi wa binadamu” kupitia matendo halisi ya huduma. Maana hii ya uongofu inazidi mabadiliko ya kiroho pekee; inajumuisha pia dhamira ya vitendo ya kuboresha maisha ya watu wasiojiweza. Miradi ya Kijamii na Kiuchumi: Wamisionari wamekuwa na mchango mkubwa katika kubadilisha maeneo yenye ukame kupitia miradi inayolenga kuboresha kilimo, huduma za afya na upatikanaji wa maji safi. Katika maeneo kama Dodoma na Singida, wanafanya kazi kwa ushirikiano na jamii za wenyeji ili kukabiliana na changamoto za usalama wa chakula na umaskini. Miradi hii haionekani tu kama juhudi za kibinadamu, bali pia kama udhihirisho muhimu wa Karama ya Damu Azizi, ambapo imani huoneshwa kwa matendo na huduma za kijamii huwa ishara ya tunu za Kiinjili. Kupitia ushirikiano huu, wamisionari wanakuza maendeleo endelevu yanayowezesha jamii kuvunja mzunguko wa uhaba na umasikini. Kwa kuchimba visima vya maji, kutoa huduma za afya na kusaidia shughuli za kilimo, wameweka msingi wa jamii zenye afya bora na uwezo mkubwa wa kustahimili changamoto. Kazi yao inaakisi mwito wa uongofu: kuwaelekea walioko pembezoni mwa jamii na kuwasaidia kujikomboa kutoka katika vifungo vya umaskini na kunyimwa fursa.
Elimu Kama Chombo cha Uwezeshaji: Kwa kutambua kwamba mabadiliko ya kweli yanahitaji zaidi ya msaada wa muda mfupi, wamisionari wameanzisha shule na vituo vya mafunzo ya ufundi katika maeneo kama Manyoni, Dodoma na Dar es Salaam. Mipango hii ya kielimu imelenga “kubadilisha hali halisi ya maisha” ya vijana, kuwasaidia kutoka katika utegemezi na kuwa washiriki hai katika maendeleo ya jamii. “Kuwasaidia Watu Kujisaidia Wenyewe” imekuwa kaulimbiu ya miradi ya C.PP.S. nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka hamsini ya utendaji wake. Shule na vituo hivi vya mafunzo vinawapatia vijana nyenzo wanazohitaji ili kufanikiwa maishani. Kwa kuwapa fursa ya elimu na stadi za vitendo, wamisionari wanawezesha kizazi kijacho kuwa mawakala wa mabadiliko katika jamii zao wenyewe kwani kupitia Elimu inaonekana kuwa ni njia ya ukombozi inayowawezesha vijana kujenga maisha yenye maana na kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla. Kupitia juhudi hizi, wamisionari wanaonesha kwamba uongofu, mabadiliko na upyaisho si dhana za kinadharia tu, bali yenye misingi inayotekelezwa kila siku katika maisha. Dhamira yao ya huduma na uwezeshaji imejengwa juu ya Karama ya Damu Azizi, inayounganisha urithi wa imani na hali halisi ya maisha ya Watanzania.
Wamisionari wa Damu Azizi wanapoendelea na safari yao ya utume, wanabaki imara katika kujitoa kwao kwa wale walioko pembezoni mwa jamii, wakidhihirisha mtazamo unaojikita katika Injili unaolenga kukomboa, kubadilisha na kuhuisha maisha ya watu na jumuiya. Kazi yao ni ushuhuda wa nguvu ya imani inayotafsiriwa katika matendo; ambapo uongofu unaonekana katika kuwaelekea wanaoonewa, mabadiliko yanaonekana katika kujenga fursa mpya, na upyaisho unaonekana katika dhamira endelevu ya haki, amani na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Leo hii, Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu linatekeleza dhamana na utume wake katika majimbo yafuatayo nchini Tanzania: Jimbo kuu la Dar es Salaam, Jimbo la Bagamoyo, Jimbo la Morogoro, Jimbo kuu la Dodoma, Jimbo la Singida, Jimbo la Ifakara, Jimbo la Bariadi, Jimbo la Mpanda, Jimbo la Mbulu, Jimbo la Rulenge-Ngara pamoja na Jimbo la Musoma. Wamisionari kutoka Tanzania wanafanya utume wao pia nchini Italia, Marekani na Vatican.