Askofu Jean Miguina, OFM Cap., Jimbo Katoliki La Sarh, Chad
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Leo XIV ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Askofu Miguel Angel Sebastián Martínez, wa Shirika la Wamisionari wa Moyo Mtakatifu wa Yesu (Comboni Missionaries of the Heart of Jesus, vifupi: M.C.C.J.) Jimbo Katoliki la Sarh, nchini Chad na kumteuwa Mheshimiwa sana Padre Jean Miguina wa Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini (OFM Cap.) kuwa Askofu mpya wa Jimbo Katoliki la Sarh nchini Chad, kabla ya uteuzi wake, alikuwa ni Mlezi wa Watakaji na Mkuu wa Shirika Chad na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati. Itakumbukwa kwamba, Askofu mteule Jean Miguina OFM Cap., alizaliwa tarehe 12 Septemba 1978, huko Lai, Jimbo Katoliki la Sarh nchini Chad. Baada ya malezi na majiundo yake ya Kitawa na Kipadre, tarehe 21 Novemba 2009 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre huko Moundou.
Baada ya masomo yake kama Padre, amebahatika kuwa Mkuu Msaidizi wa Utume wa Vijana wa Kifranciskani Jimboni Bangui kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2012. Baadaye akatumwa na Shirika kwenda mjini Roma, kuendelea na masomo ya juu kwenye Chuo Kikuu cha Kipapa cha “Santa Croce” kilichoko mjini Roma na kujipatia Shahadaya Uzamili kwenye Sheria za Kanisa kunako mwaka 2025. Na kati ya Mwaka 2016 hadi mwaka 2019 aliteuliwa kuwa Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya “Saint Laurent” huko Bouar, Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Katibu mkuu wa Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini, Afrika ya Kati na Mashariki. Kati ya Mwaka 2019 hadi mwaka 2022 alichaguliwa kuwa Mkuu wa Shirika la Wakapuchini Afrika ya Kati na Magharibi. Na kunako mwaka 2020 alitumwa kwenda nchini Cameroon kujiendeleza kwa masomo ya juu na hatimaye kujipatia Shahada ya Uzamivu katika Haki Msingi za Binadamu kutoka “l’Université Catholique d’Afrique Centrale di Yaoundé” nchini Cameroon mwaka 2024. Tangu mwaka 2024 aliteuliwa kuwa ni kati ya Washauri wa Jimbo Katoliki la Moundou, Padre wa maisha ya kiroho wa Masista Wafranciskani, huko Donia, Mwalimu wa Lugha ya Kilatini Seminari kuu ya “Saint Mbaga Tuzinde Jimboni Sarh, Mlezi wa Watakaji wa Shirika la Wakapuchin nchini Chad na Mshauri wa Shirika nchini Chad na Jamhuri ya Afrika ya Kati na Mjumbe wa Tume ya Sheria.