Jubilei ya Miaka 50 ya Utawa; Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi OFM Cap., wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania. Jubilei ya Miaka 50 ya Utawa; Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi OFM Cap., wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania. 

Askofu Mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi, Jubilei ya Miaka 50 Ya Utawa

Askofu mkuu Ruwa'ichi alisema kuwa safari ya nusu karne ya maisha ya kitawa ni ushuhuda wa uaminifu wa Mungu kuliko nguvu za mwanadamu. Alisisitiza kuwa historia ya wito wa Nabii Samweli inaonesha wazi kwamba kila mwito unahitaji walezi, walimu na watu wenye busara na hekima wanaomsaidia mwamini kutambua sauti ya Mungu. Wito wa kitawa haujengwi juu ya uwezo au mastahili ya mwanadamu; wito huu ni zawadi ya upendo na huruma ya Mungu.

Na Fredy William - Dar es Salaam

Hayati Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, mintarafu Maandiko Matakatifu, Jubilei ni muda muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia huruma na kuambata msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake. Ni kipindi cha kushukuru na kuomba tena neema na baraka za kuweza kujizatiti zaidi katika maisha na wito, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani, kama mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Ni wakati murua sana wa mapumziko; muda wa kujichotea nguvu na neema pamoja na kufurahia matunda ya kazi ya uumbaji. Ni wakati wa kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi OFM Cap., wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania amesema kuwa wito wa kitawa haujengwi juu ya uwezo au ustahili wa mwanadamu bali ni zawadi ya upendo na huruma ya Mungu anayemwita mtu ili amtumikie, atangaze na kushuhudia Injili. Akihubiri katika Misa Takatifu ya Shukrani ya Miaka 50 ya Maisha ya Kitawa iliyoadhimishwa katika Parokia ya Mtakatifu Martha, Mikocheni, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Askofu mkuu Ruwa'ichi alisema kuwa safari ya nusu karne ya maisha ya kitawa ni ushuhuda wa uaminifu wa Mungu kuliko nguvu za mwanadamu. Alisisitiza kuwa historia ya wito wa Nabii Samweli inaonesha wazi kwamba kila mwito unahitaji walezi, walimu na watu wenye busara na hekima wanaomsaidia mwamini kutambua sauti ya Mungu.

Mapadre waliohudhuria Ibada ya Misa Takatifu Mikocheni
Mapadre waliohudhuria Ibada ya Misa Takatifu Mikocheni

"Kila wito halali unatoka kwa Mungu. Mungu hamwiti mtu kwa sababu ya mastahili yake; anamwita kwa sababu anampenda na anamuhurumia," alisema Askofu mkuu Ruwa'ichi. Akisimulia historia yake, Askofu mkuu Ruwa'ichi alisema kuwa mwanzoni hakuwa sehemu ya Shirika la Ndugu Wadogo Wafrancisko Wakapuchini (OFM Cap.)  bali alikuwa mpostulanti wa Shirika la Roho Mtakatifu (Holy Ghost Fathers and Brothers) lililoasisiwa na Kijana Claude Poullart Des Places akiwa na umri wa miaka 24, kule Rennes, Ufaransa, mnamo tarehe 27 Mei 1703, Sherehe ya Pentekoste; kabla ya kufanya uamuzi wa kuhamia katika Shirika la Wakapuchini baada ya kushauriana na walezi na kutafakari kwa kina. Alieleza kuwa kati ya watawa wanane waliokuwa pamoja katika nyakati zile, ni wawili pekee waliobaki hadi leo. Kwa mujibu wa Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi OFM Cap., anasema kufikisha miaka 50 ya utawa si matokeo ya akili, uwezo au ustahimilivu wa kibinadamu bali ni ushuhuda wa neema ya Mungu iliyowaongoza katika kila hatua ya maisha yao. "Kufika miaka 50 ya Utawa si kwa ujanja wetu wala kwa nguvu zetu, bali kwa msaada wa Mwenyezi Mungu. Hata kama nisingekuwa Askofu, mwaka huu ningekuwa bado nasherehekea miaka 50 ya Utawa," alisema. Utawa ni kuitwa kuwa chumvi na nuru ya ulimwengu. Akirejea Injili ya Mtakatifu Mathayo, Askofu mkuu Ruwa'ichi alisema kuwa maisha ya kitawa yanapaswa kuwa ushuhuda unaobadilisha jamii kwa kuwa watawa wameitwa kuwa chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu.

Watawa wamewakilisha barabara
Watawa wamewakilisha barabara

Chumvi ni kielelezo cha utukufu, utakatifu, huruma na upendo wa Mungu unaoganga na kuponya udhaifu na mapungufu ya binadamu. Kumbe, watawa wanaitwa na kutumwa kuwa ni chumvi na nuru ya ulimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto, kielelezo makini cha imani tendaji. Wanaalikwa kuwa ni chumvi ya ulimwengu kwa kutambua kwamba kwa kuzaliwa katika Maji na Roho Mtakatifu, Wabatizwa wote wamewekwa wakfu kuwa ni Makuhani, Manabii na Wafalme ili kumtolea Mwenyezi Mungu dhabihu ya sifa na shukrani; kutangaza fadhila za Mungu, ili kuwaita watu watoke gizani na kuingia katika nuru yake ya ajabu, kwa kujitoa wenyewe ili waweze kuwa ni sadaka safi na yenye kumpendeza Mwenyezi na kumshuhudia Kristo Yesu popote pale walipo kama majibu ya habari za tumaini na uzima wa milele lililoko ndani mwao. Rej. Lumen gentium 9-11. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi OFM Cap., amefafanua kuwa kama ilivyo chumvi inayokoleza chakula, kuponya majeraha, kuhifadhi chakula na kuunganisha watu kupitia "agano la chumvi" linalotajwa katika Maandiko Matakatifu, ndivyo maisha ya kitawa yanavyopaswa kuleta ladha ya Injili, uponyaji, matumaini na umoja katika jamii. Aliwaalika waamini kumwomba Mungu ili Kanisa na jamii viendelee kuwa ni "chumvi ya utakatifu," ambayo hujenga maisha yenye imani, matumaini, mapendo na mshikamano wa udugu wa kibinadamu. Katika tafakari yake, Askofu mkuu Ruwa'ichi alitumia simulizi la utotoni mwake kueleza umuhimu wa Kristo Yesu kuwa nuru ya maisha.

Waamini walei waliohudhuria Jubilei ya Miaka 50 ya Utawa.
Waamini walei waliohudhuria Jubilei ya Miaka 50 ya Utawa.

Alikumbuka kuwa siku moja akiwa mdogo alidhani ameona chui akiwa njiani kuelekea Kanisani alfajiri, lakini alipokaribia aligundua kuwa kilichomuogopesha kilikuwa ni gogo. Kutokana na uzoefu huo alisema kuwa giza hubadilisha namna tunavyoona vitu, lakini mwanga huonesha ukweli ulivyo. Aliwataka waamini waendelee kumwomba Mwenyezi Mungu awafanye kuwa wafuasi waaminifu na wenye kudumu katika miito yao. Akihitimisha mahubiri yake Askofu mkuu Ruwa'ichi aliwashukuru waamini, watawa, mapadri na wageni wote walioshiriki katika Ibada ya Misa hiyo ya Jubilei, huku akiwaomba waendelee kuwaombea ili waendelee kuzeeka katika utakatifu na uaminifu kwa Kristo Yesu. "Mzidi kutuombea tuzidi kuzeeka vizuri na kuzeeka kitakatifu," alisema. Maadhimisho hayo ya Miaka 50 ya Utawa yalifanyika katika Parokia ya Mtakatifu Martha Mikocheni, yakikusanya waamini, viongozi wa Kanisa, watawa na mapadri walioungana kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha ya kitawa yaliyodumu kwa nusu karne katika huduma ya Kanisa.

Jubilei Miaka 50 ya Utawa
15 Julai 2026, 15:09