Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Uinjilishaji Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo kuu la Dodoma, 1973-2026 Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Uinjilishaji Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo kuu la Dodoma, 1973-2026 

Jubilei ya Miaka 50 ya Uinjilishaji Parokia ya Kiwanja Cha Ndege, Jimbo la Dodoma

Katika kilele cha Jubilei ya Miaka 50 ya Uinjilishaji Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo kuu la Dodoma vijana 155 wameimarishwa kwa Kipaimara. Waamini 21 wamefunga Ndoa Takatifu na kwa njia ya Agano la Ndoa ambalo, kwa njia yake, mwanaume na mwanamke huunda kati yao jumuiya kwa maisha yote, kwa tabia yake ya asili liko kwa ajili ya manufaa yao na kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Agano hili, limeinua na Kristo Bwana kwa hadhi ya Sakramenti. Uinjilishaji!

Na Ndahani Lugunya, -Dodoma, Tanzania.

Parokia inapaswa kuwa ni Jumuiya ya waamini inayoinjilisha na kuinjilishwa. Hii ni Jumuiya inayotangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji! Parokia ni mahali muafaka pa waamini kujisikia kupenda na kupendwa; mahali pa kukutana, ili hatimaye, kuweza kuutafakari Uso wa huruma ya Mungu katika kina na mapana yake. Ni mahali muafaka pa kusimama kidete, kulinda, kutetea na kutunza mazingira bora nyumba ya wote. Parokia ni mahali pa kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa na kurithisha imani, ili kuziwezesha familia kutekeleza dhamana na wajibu wake barabara yaani wa kuwa ni: Kanisa dogo la nyumbani, mahali ambapo watoto kwa njia ya: Sala, Sakramenti za Kanisa, Tafakari ya Neno la Mungu na Matendo ya huruma, wanapewa malezi na makuzi yatakayowawezesha watoto hawa kuwa kweli ni mashuhuda wa maisha ambayo yamepigwa chapa ya fadhila za Kimungu yaani: Imani, Matumaini na Upendo. Parokia ni mahali ambapo wanafamilia wanapaswa kujisikia kuwa wako salama salimini. Kuna haja ya Parokia kuendelea kushirikiana na kushikamana, ili kujenga Jumuiya kubwa zaidi ya watu wanaoinjilisha na kuinjilishwa. Katika mchakato huu, Paroko anapaswa kuwa ni mfano bora wa kuigwa na watu wa Mungu katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha na utume wake. Watu wote wa Mungu wanaitwa, wanatumwa na wanahamasishwa kushiriki katika safari hii ya imani, chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani, unaofumbatwa katika ari na mwamko mpya wa ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari. Ni katika muktadha huu, Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska, Kiwanja cha Ndege Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Dominika tarehe 5 Julai 2026 imeadhimisha kilele cha Jubilei ya miaka 50 ya Uinjilishaji kwa kunogeshwa na kaulimbiu “Jubilei miaka 50 Kiwanja cha Ndege, tunaendelea kukaza mwendo katika Kristo.”

Baadhi ya Maparoko walio wahi kufanya utume wao K/Ndege
Baadhi ya Maparoko walio wahi kufanya utume wao K/Ndege

Ibada hii ya Misa Takatifu imeadhimishwa na Askofu mkuu Beatus Michael Kinyaiya OFM Cap., wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma. Katika kilele hiki vijana 155 wameimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara inayoufanya muungano wa Wabatizwa na Kanisa kuwa mkamilifu zaidi kwa kutajirishwa kwa nguvu ya pekee ya Roho Mtakatifu, ili hatimaye, kuineza na kuitetea imani kwa maneno na matendo, kama mashuhuda wa kweli wa Kristo Yesu. Wanandoa 21 wamefunga Ndoa Takatifu na kwa njia ya Agano la Ndoa ambalo, kwa njia yake, mwanaume na mwanamke huunda kati yao jumuiya kwa maisha yote, kwa tabia yake ya asili liko kwa ajili ya manufaa yao na kwa ajili ya kuzaa na kulea watoto. Agano hili, kati ya wabatizwa, limeinuliwa na Kristo Bwana kwa hadhi ya Sakramenti. Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, mintarafu Maandiko Matakatifu, Jubilei ni muda muafaka wa kufanya toba na wongofu wa ndani, tayari kukimbilia huruma na kuambata msamaha unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya waja wake. Ni kipindi cha kushukuru na kuomba tena neema na baraka za kuweza kujizatiti zaidi katika maisha na wito, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani, kama mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu. Ni wakati murua sana wa mapumziko; muda wa kujichotea nguvu pamoja na kufurahia matunda ya kazi ya uumbaji. Ni wakati wa kuyatafakari yaliyopita kwa moyo wa shukrani, kuyaishi ya sasa kwa moyo wa hamasa na kuyakumbatia ya mbeleni kwa moyo wa matumaini. Katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Uinjilishaji Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Jimbo kuu la Dodoma, kuna waamini ambao wamemwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 25, 30, 35, 40, 45 na 50 ya Ndoa Takatifu.

Jubilei ya Miaka 50 ya Uinjilishaji Parokia ya K/Ndege, Dodoma
Jubilei ya Miaka 50 ya Uinjilishaji Parokia ya K/Ndege, Dodoma   (@TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

 Askofu mkuu Kinyaiya amesema, maendeleo makubwa ya kiroho na kimwili yaliyopatikana Parokiani hapa ni nguvu na kazi ya Roho Mtakatifu aliyewahuisha: Mapadre, Watawa, Makatekista na Wakristo wa nwanzo wa Parokia hii. Amemshukuru kwanza mwamini aliyetoa eneo la Kanisa hili, Wayesuit waliokubali kupokea dhamana ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu Parokia ya Kiwanja cha Ndege. Hapa imemwagika damu na jasho ili kupatengeneza na kuonekana jinsi palipo kwa sasa. Amewashukuru Mapadre wote waliohudumia Parokia hii tangu kuanzishwa kwake na kwamba, katika Kipindi cha Miaka 50 ya uinjilishaji wa kina, Sakramenti mbalimbali zimetolewa na Mama Kanisa. Hii ilikuwa ni Parokia kubwa Jimbo Katoliki la Dodoma, na waamini walipata huduma muhimu kwa njia ya Makatekista. Makatekista ni watu ambao kwa miaka mingi wamejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kufundisha Katekesi, ili kuwasaidia waamini kukutana na Kristo Yesu katika: Neno, Sakramenti na Huduma mbalimbali zinazotolewa na Mama Kanisa kwa watu wa Mungu kama kielelezo makini cha imani tendaji. Huduma ya Katekista ndani ya Kanisa inapaswa kupewa mwelekeo wa Kijumuiya, kwa kujali na kuthamini karama na tunu mbalimbali ambazo Roho Mtakatifu amewakirimia watu wa Mungu kwa ajili ya mchakato wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kumbe, Kipindi cha Miaka 50 ya Parokia ya Kiwanja cha Ndege imekuwa ni fursa ya kujenga na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari, kwa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu!

Vijana 155 wameimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara
Vijana 155 wameimarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara

Parokia ya Kiwanja cha Ndege ni chimbuko la Parokia nyingi, Jimbo Katoliki la Dodoma, kazi kubwa iliyofanywa na Makatekista pamoja na viongozi mbalimbali wa Halmashauri ya Walei. Waamini waliobariki ndoa zao katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 ya Uinjilishaji Parokia ya Kiwanja cha Ndege wawe ni chachu na hamasa kwa waamini wengine ambao bado wako kwenye “Uchumba sugu” kujitahidi kurekebisha hali zao, waamke na kupyaisha maisha yao, tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Wawe ni hamasa kwa waamini waliolegea, waliovunjika na kupondeka moyo, ili kila mmoja, ifikapo tarehe 31 Desemba 2026 aweze kumpelekea Askofu mkuu Kinyaiya, mtu mmoja ambaye alikuwa ni mlegevu wa imani; mtu ambaye mahudhurio ya Jumuiya Ndogondogo za Kikristo anaona kana kwamba, ni “Kituo cha Polisi” na wale ambao kwa miaka mingi wamesahau mahali ulipo Mlango wa Kanisa. Akisoma Historia ya Parokia hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Walei Parokia ya Kiwanja cha Ndege Mama Frola Masami amesema kwamba Parokia hiyo ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska Kiwanja cha Ndege ilianza mwaka 1973 mpaka 1975 ambapo wakati huo waamini waliokuwa wanaishi eneo hilo walikuwa wakisali chini ya mti na shule ya msingi Kiwanja cha Ndege na wengine wakienda kusali Jimboni. Baada ya kuonekana uhitaji kutokana na ongezeko la waamini mjini Dodoma mwaka 1973 baada ya Dodoma kuwa Makao makuu ya nchi waamini waliongezeka katika eneo la Mlimwa C, Mlimwa D, Oystabey, Mailimbili na Chamwino watu wakaendelea kuongezeka. Amesema wakati huo wakristo wakatoliki walioishi maeneo hayo walienda kusali Jimboni na wengine wakikusanyika kusali kwenye madarasa ya Kiwanja cha Ndege na baadhi ya waamini waliokuepo wakati huo ni Mzee Timoth Mashimbe, Mzee Kapama, Katekista Aidan, Mzee Kiteterike na wengine.

Tunaendelea Kukaza Mwendo katika Kristo Yesu
Tunaendelea Kukaza Mwendo katika Kristo Yesu

Hayati Askofu Mathias Josefu Isuja, “Mnyakaya na Babu” wa Jimbo Kuu la Dodoma kwa wakati huo wa mwaka 1975 alitoa mwaliko kwa Mapadri wa Shirika la Yesu na kuwaomba waje Jimboni Dodoma kukidhi mahitaji ya kichungaji na kitume, ambapo mwaliko huo ulitolewa kufuatia ongezeko la watu katika maeneo ya mjini na hivyo kuibua changamoto ya uhitaji wa huduma za kichungaji kwani Jimbo halikuwa limejiandaa vema wakati huo kwa ongezeko la haraka la waamini. Parokia ya Kiwanja cha Ndege, Kanisa la kwanza lilianza kujengwa mwaka 1976 na mwaka huo huo 1976 ikaanzishwa na kuzinduliwa rasmi Parokia na wakati huo Paroko wa kwanza alikuwa ni Padri Ekta Almeida akisaidiwa na Padri Fransis Rodrigaz. Baada ya Idadi ya waamini kuongezeka na kusababisha Kanisa lilikuepo kuwa dogo, Kanisa hili la sasa lilijengwa kwa ushirikiano wa waamini na mfadhili wa shirika la masista wa Mt. Peter Claver ambao ni watawa waishio Roma waliojitolea kufadhili ujenzi wa Kanisa hadi lilipokamilika mwezi Aprili 1984. Amesema baada ya kukamilizka na kuzinduliwa kwa Kanisa, Parokia ilipendekezwa na kukubaliwa iitwe Parokia ya Mwenyeheri Maria Theresa Ledochowska ambaye ni mwanzilishi wa Shirika la masista wa Peter Claver waliosaidia ujenzi wa Kanisa.

Baadhi ya Mapadre waliohudhuria katika Kilele cha Jubilei
Baadhi ya Mapadre waliohudhuria katika Kilele cha Jubilei

Kwa kipindi chote cha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Parokia hiyo, Parokia mbalimbali zimezaliwa kutoka Kiwanja cha Ndege, ambapo mpaka mwaka 2002 Parokia ilikuwa na Vigango 9 ambavyo ni Mpamaa, Chilonwa, Nzuguni Sokoine, Nzuguni Maweni, Ihumwa, Kizota, Makole, Nkuhungu na Miyuji. Mwaka 2002 Kigango cha Makole kikawa cha kwanza kupewa hadhi ya Parokia na kuviweka Vigango vya Nzuguni na Ihumwa chini yake ambapo Vigango hivyo kwa sasa ni Parokia na hao ni wajukuu zetu. Aidha mwaka 2005 Kigango cha Nkuhungu kikawa Parokia iliyochukua Kigango cha Kizota kuwa chini yake na Kizota nayo kwa sasa ni Parokia na ni Makao makuu ya Dekania ya Mt. Paulo wa Msalaba, mwaka 2006 Kigango cha Miyuji Mbwanga kilikuwa Parokia ikaitwa Parokia ya Mtakatifu Yohane Bosco na Kigango cha Mpamaa kikawa chini ya Parokia ya Miyuji Mbwanga. Mwaka 2019 Kigango cha Mtakatifu Inyasi wa Loyola, Miyuji Kusini nacho kikawa Parokia na hivyo kilele cha Jubilei ya miaka 50 ya Parokia, wanajiandaa kuanzisha Kigango kingine katika eneo la Mnadani. Jubilei hiyo ya miaka 50 ya Uinjilishaji katika kipindi cha mwaka mzima imenogeshwa na kaulimbiu “Jubilei miaka 50 Kiwanja cha Ndege, tunaendelea kukaza mwendo katika Kristu” ambapo kaulimbiu hii iliibuliwa baada ya sala na tafakari ya wapi walipotoka, walipo na wanakotamani kuwepo.”

Jubilei k/Ndege Dodoma

 

14 Julai 2026, 15:08