Kardinali Michael Czerny awataka Vijana wa Kanisa Katoliki wametakiwa kutambua kuwa wao ni mbegu ya matumaini kwa Kanisa na jamii. Kardinali Michael Czerny awataka Vijana wa Kanisa Katoliki wametakiwa kutambua kuwa wao ni mbegu ya matumaini kwa Kanisa na jamii. 

Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA: Ibada ya Misa ya Ufunguzi

Vijana wametakiwa kutambua kuwa wao ni mbegu ya matumaini kwa Kanisa na jamii, kwa kujenga madaraja ya upendo, haki, amani na umoja badala ya kuta za mgawanyiko, huku wakiongozwa na Roho Mtakatifu katika kutangaza na kushuhudia Injili. Wito huo umetolewa na Kardinali Michael Czerny wakati akihubiri katika Ibada hiyo ya Misa Takatifu kama sehemu ya ufunguzi wa Mkutano mkuu wa 21 wa AMECEA , kama safari ya Kisinodi ya AMECEA pamoja na vijana.

Na Fredy William – Nairobi, Kenya

Vijana wa Kanisa Katoliki wametakiwa kutambua kuwa wao ni mbegu ya matumaini kwa Kanisa na jamii, kwa kujenga madaraja ya upendo, haki na umoja badala ya kuta za mgawanyiko, huku wakiongozwa na Roho Mtakatifu katika kutangaza na kushuhudia Injili. Wito huo umetolewa na Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu, Dominika tarehe 19 Julai 2026. Akihubiri katika Ibada hiyo ya Misa Takatifu kama sehemu ya ufunguzi wa Ibada hiyo ya Misa takatifu iliyowakutanisha Maaskofu, mapadri, watawa, waamini walei na wajumbe wa vijana kutoka nchi mbalimbali za AMECEA. Kaulimbiu inayonogesha Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, “Association of Member Episcopal Conferences in Eastern Africa” AMECEA kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 26 Julai 2026, kwa kuwashirikisha zaidi ya Maaskofu 140 kutoka katika Majimbo 128 ni: “Safari ya Sinodi ya AMECEA pamoja na Vijana: Kujenga Madaraja ya Ushirika, Matumaini, Haki na Utawala Bora.” Mkutano huu unafanyikia kwenye Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Afrika Mashariki, CUEA, Jijini Nairobi, nchini Kenya.

Wajumbe wa Vijana Kutoka katika Nchi za AMECEA
Wajumbe wa Vijana Kutoka katika Nchi za AMECEA

Kardinali Czerny amesema Ufalme wa Mungu tayari uko katikati ya watu wake, lakini unahitaji kila Mkristo kushiriki kikamilifu katika kuujenga kupitia maisha ya kila siku. Akifafanua kuwa Ufalme wa Mungu unafanana na mbegu ya haradali, ambayo huanza ikiwa ndogo lakini hukua na kuwa mti mkubwa. Hivyo, hata matendo madogo ya uaminifu, upendo na huduma yana uwezo wa kuleta mabadiliko makubwa katika Kanisa na jamii katika ujumla wake. Akirejea katika unabii wa Nabii Isaya unaosema, "Tazama, nafanya jambo jipya," Kardinali Czerny amewahimiza waamini kutokata tamaa kutokana na changamoto za ulimwengu, bali kutambua njia mpya ambazo Mwenyezi Mungu anaendelea kuzifungua kwa watu wake. Kwa namna ya pekee aliwaelekeza vijana kutambua nafasi yao katika maisha na utume wa Kanisa, akisema hawapaswi kukubali kukata tamaa wala kuruhusu mazingira mabaya kuwanyima matumaini, bali wawe ni vyombo na wajenzi wa madaraja ya maridhiano, mshikamano na matumaini kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Maandamano ya Maaskofu wa AMECEA kuelekea kwenye Ibada ya Misa
Maandamano ya Maaskofu wa AMECEA kuelekea kwenye Ibada ya Misa

"Vijana ni mbegu inayokua. Msiwe watu wa kubomoa madaraja ya umoja, bali yajengeni kwa msingi wa upendo, haki na imani ya Kikristo," alisisitiza. Akifafanua mfano wa ngano na magugu, Kardinali Czerny amesema Mungu hufanya kazi kwa subira na hekima. Alisema mwenye shamba hakuruhusu magugu kung'olewa mara moja ili yasije yakaharibu pia ngano, jambo linalofundisha waamini kuwa uvumilivu ni sehemu muhimu ya ukuaji wa Ufalme wa Mungu."Dunia hukombolewa kwa subira ya Mungu, lakini mara nyingi huharibiwa na papara ya mwanadamu," alisema, huku akiwataka waamini kumwiga Mwenyezi Mungu anayehukumu kwa haki, huruma na uvumilivu. Aidha, aliwahimiza Wakristo kutoridhika na kukemea maovu pekee, bali wawe chachu ya mabadiliko mema ndani ya jamii kwa kuongozwa na nguvu za Roho Mtakatifu, wakisoma Maandiko Matakatifu, kwa kujikita katika maisha ya sala, ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa sanjari na kusoma alama za nyakati.

Maandamano ya Utoto Mtakatifu
Maandamano ya Utoto Mtakatifu

Katika Misa hiyo, Mwenyekiti wa shughuli za liturujia aliwakaribisha kwa upendo wajumbe wote, huku akieleza upendo wa Maaskofu wa AMECEA kwa vijana. Pia aliwashukuru vijana kwa kushiriki Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi pamoja na Maaskofu na kusisitiza umuhimu wa kukua katika upendo, haki, amani na imani inayojengwa juu ya maadili ya Kikristo na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Ishara ya Kanisa linalowajumuisha wote ilidhihirishwa wakati Somo la kwanza liliposomwa na kijana mwenye ulemavu wa macho, jambo lililoonesha kuwa kila mwamini ana nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Wajumbe wa waamini walei kutoka nchi za AMECEA
Wajumbe wa waamini walei kutoka nchi za AMECEA

Hitimisho Kwa ujumla: Mahubiri ya Kardinali Czerny yameweka msingi wa safari ya Mkutano Mkuu wa 21 wa AMECEA kwa kuwakumbusha waamini, na hasa vijana, kuwa Mungu anaendelea kufanya mambo mapya kupitia watu wake. Wakiwa na subira, imani na uongozi wa Roho Mtakatifu, wanaalikwa kuwa chachu ya mabadiliko, wajenzi wa umoja na mashuhuda wa Injili katika Afrika ya Mashariki na duniani. Sifa na utukufu apewe Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, kwani ni katika mukadha huu, AMECEA inaadhimisha kumbukizi ya Miaka 65 ya umoja, ushirika na mshikamano wa shughuli za kichungaji na huduma kwa watu wa Mungu. Huu ni umoja ulioanzishwa kunako mwaka 1961 na unasimikwa na kufumbatwa katika tofauti mbalimbali kutoka katika nchi tisa wanachama ambazo ni: Tanzania, ikiwa na Majimbo 34, Kenya Majimbo 27; Uganda Majimbo 19, Ethiopia Majimbo 13, Zambia Majimbo 12; Malawi Majimbo 8; Sudan ya Kusini Majimbo 7, Sudan Kongwe Majimbo 9 na Eritrea Majimbo 8. Itakumbukwa kwamba, Djibout na Somalia zimealikwa kushiriki kama nchi watazamaji.

AMECEA MIsa ya Ufunguzi
20 Julai 2026, 08:15