Shemasi Theogenes Petro Madushi, kutoka Jimbo Kuu la Mwanza, Tanzania. Alipewa Daraja ya Ushemasi tarehe 3 Mei 2025 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Shemasi Theogenes Petro Madushi, kutoka Jimbo Kuu la Mwanza, Tanzania. Alipewa Daraja ya Ushemasi tarehe 3 Mei 2025 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. 

Shemasi Theogenes Petro Madushi Jimbo kuu la Mwanza: Historia ya Wito Wake!

Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, Jumamosi tarehe 4 Julai 2026 anatarajiwa kuwaweka wakfu Shemasi Michael Eligi Kimario SMA kutoka Parokia ya Magu, Shemasi Francis Makungu Iggosha kutoka Parokia ya Ihimbili pamoja na Shemasi Theogenes Petro Madushi kutoka Parokia ya Kahangara Jimbo kuu la Mwanza kuwa Mapadre, yaani wahudumu wa Neno la Mungu, waadhimishaji wa Sakramenti za Kanisa zinazomwilishwa katika matendo.

Na Theogenes Petro Madushi, Chuo Kikuu cha Urbaniana Roma, - Roma.

Mama Kanisa anasemaa, katika mchakato wa uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ikumbukwe kwamba hii ni dhamana shirikishi na nyeti katika azma ya utekelezaji shughuli za kitume. Kristo Yesu mwenyewe aliwatuma Mitume wake kwenda ulimwenguni kote kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa kila kiumbe na kwamba, kila atakayeamini na kubatizwa, huyo atapata uzima wa milele. Mapadre wanakumbushwa kwamba, dhamana na wito waliopewa na Mama Kanisa wakati wa kupokea daraja takatifu ya Upadre, ni kutekeleza utume wa kutangaza Habari Njema ya Wokovu kwani Mapadre ni wahudumu makini wa Neno la Mungu kati ya watu wao na kwamba wanapaswa kuendelea kutangaza Fumbo la Pasaka, yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo bila kuchoka wala kukata tamaa. Huu ni wito wao ambao wanapaswa kuutekeleza kwa ari na moyo mkuu, kwani wamempokea Roho Mtakatifu anayewapatia nguvu ya kufundisha kwa Mamlaka ya Kanisa, Kuongoza na Kuwatakatifuza watu wa Mungu. Utume huu, utekelezwe kadiri ya taratibu na kanuni za Mama Kanisa, kwa hekima na busara ya hali ya juu. Mapadre hawatumwi kamwe na Mama Kanisa kujitangaza wenyewe, wala kutangaza mawazo yao, au kutoa tafsiri ya Neno la Mungu kwa malengo binafsi, bali wanapaswa kutambua ukuu wa Yesu Kristo mkombozi wa dunia, anayewashirikisha katika azma ya utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu. Hii ni changamoto kwa Mapadre kusoma, kutafakari na kujinoa mara kwa mara katika ujuzi na man'gamuzi ya Neno la Mungu, na katika nyanja mbalimbali za maisha na utume wa Kanisa.

Papa Leo XIV akitoa Sakramenti ya Daraja Takatifu
Papa Leo XIV akitoa Sakramenti ya Daraja Takatifu   (@Vatican Media)

Lengo la Injili ni kuwasaidia watu wa Mungu katika ujumla wao kutolea ushuhuda wa maisha yao ya kiinjili kwa kuendelea kuwa ni Injili hai. Kristo ndiye kiini na Habari Njema yenyewe. Anaendelea kuwaalika mapadre kufanana naye katika maisha na matendo yao, wakijitahidi daima kuwa ni wakamilifu na watakatifu. Neno la Mungu na Maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa ni nyenzo zinazokwenda sanjari katika maisha na utume wa kipadre. Liturujia inahitaji hekima ya hali ya juu, kwa kutoa kipaumbele kwa Mungu katika matendo ya kiliturujia. Lengo ni kuwawezesha waamini kukutana na Mungu wao, katika adhimisho la Sadaka takatifu ya Altare. Hekima inamwezesha Padre kusoma alama za nyakati na kutenda mintarafu moyo na maagizo ya Mama Kanisa anayeendelea kuhifadhi amana na utajiri wa Injili, kwa takribani miaka elfu mbili na ishirini na sita. Wahudumu wa Neno wanapaswa daima kukumbuka kwamba, Mwenyezi Mungu anaendelea kutenda ndani mwao, anaandaa mioyo ya watu kupokea mbegu ya Neno la Mungu, ili iweze kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha; tunu zinazosimikwa katika matendo ya huruma. Mapadre wanakumbushwa kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda na kuwajali zaidi wale wote wanaojitoa kwa moyo na furaha kubwa bila ya kujibakiza, kwani wanaweza kupata ujasiri hata wa kuweza kukumbatia Fumbo la Msalaba linapopiga hodi katika maisha yao ya huduma kwa Mungu na jirani. Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza, Jumamosi tarehe 4 Julai 2026 anatarajiwa kuwaweka wakfu Shemasi Michael Eligi Kimario SMA kutoka Parokia ya Magu, Shemasi Francis Makungu Iggosha kutoka Parokia ya Ihimbili pamoja na Shemasi Theogenes Petro Madushi kutoka Parokia ya Kahangara Jimbo kuu la Mwanza kuwa Mapadre.

Mapadre wanawekwa wakfu ili kuongoza, kutakatifuza na kufundisha
Mapadre wanawekwa wakfu ili kuongoza, kutakatifuza na kufundisha   (@Vatican Media)

Jina langu ni Theogenes Petro Madushi, kutoka Jimbo Kuu la Mwanza, Tanzania. Nilizaliwa tarehe 26 Februari 1995 katika kijiji na Kata ya Mwamanga, Wilaya ya Magu, Mkoa wa Mwanza ndani ya Parokia ya Mtakatifu Bernadeta – Kahangara. Mimi ni mtoto wa kwanza katika familia ya watoto wawili. Baba yangu anaitwa Emanuel Sama na Mama yangu anaitwa Angela Migozi, maarufu kwa jina la “Edda Ndindagi.” Ndugu yangu wa pili anaitwa Jovini Sama. Kwa sasa tunaishi katika kijiji na Kigango cha Ilungu ndani ya wilaya ya Magu, katika Parokia ya Mtakatifu Bernadeta Kahangara. SAFARI YA ELIMU: Nilianza elimu ya msingi mwaka 2003 katika Shule ya Msingi Mwamanga, na nikahitimu mwaka 2009. Baadaye, niliendelea na elimu ya sekondari ya O-level katika shule sekondari Mwamanga inayopatikana katika kijiji cha Kisesa “B” kuanzia mwaka 2010 hadi 2013. Mwaka 2014 hadi 2016, nilisoma A-level katika Shule ya Sekondari ya wavulana Kahororo, iliyopo katika Manispaa ya Bukoba mjini, Mkoa wa Kagera. Nikichukua masomo ya Fizikia, Kemia na Biolojia PCB. MAISHA YA KIROHO: Nilipokea Sakramenti ya Ubatizo na Komunyo Takatifu tarehe 25 Juni 2006 katika Kigango cha Yichobela, Parokia ya Kahangara, nikiwa na umri wa miaka 11, na nilibatizwa na Padre Moses Mapela. Namba yangu ya ubatizo ni B000363. Mwaka huo huo 2006 tarehe 28 Oktoba, katika Kanisa la Parokia yaani Kahangara, nilipokea Sakramenti ya Kipaimara kutoka kwa Padre Nicholaus Segeja, aliyekuwa Paroko wa Parokia ya Kahangara na Makamu Askofu Jimbo wa kipindi hicho. Na namba yangu ya Kipaimara ni A000366.

Askofu Mkuu Renatus Leonard Nkwande Jimbo kuu la Mwanza
Askofu Mkuu Renatus Leonard Nkwande Jimbo kuu la Mwanza   (©TANZANIA EPISCOPAL CONFERENCE)

MWANZO WA WITO: Hamu ya kuwa Padre ilianza nilipokuwa bado mdogo, hasa kila tulipokuwa tukishiriki Ibada ya Misa Takatifu katika Kigango cha Mwamanga. Kwa kuwa tulikuwa hatupati Misa mara kwa mara, kutokana na uhaba wa Mapadre, hivyo ujio wa Padre ulikuwa sherehe kubwa. Nilivutiwa sana na namna walivyohubiri, kuimba, na kuongoza Misa – hasa Padre alipoimba sala na Prefacio Hapo ndipo moyo wangu ulianza kutamani, nami siku moja nifanye kama wao. Mbali na hilo, malezi ya nyumbani pia yalichangia kwa kiasi kikubwa kuimarisha hamu yangu ya kumtumikia Mungu kama Padre kwa sababu tulikuwa na utaratibu wa kusali kila siku sala za jioni na Rosari Takatifu tukiungana na familia rafiki ya Mwl. Dafroza Thomas ambapo watoto tulipewa nafasi ya kuongoza sala, kitendo hiki kilinijenga kiimani. Hivyo wakati mwingine nikiwa nyumbani, nilikuwa nikiigiza jinsi Padre anavyo adhimisha Ibada ya Misa. Ni mambo ya kawaida sana na pengine ya kushangaza lakini ni kupitia mambo madogo madogo Mungu hujidhihirisha na kutupa ujumbe wake au wito wake pasipo sisi kujua, na hivyo tunahitaji watu kama Eli wanaotusaidia kutafsiri ujumbe huo wa Mungu kama tunavyosoma katika Kitabu cha Kwanza cha Samueli, 1Sam 3:9. Wazazi na watu wa karibu ndio akina Eli katika familia na jamii zetu.

Shemasi Theogenes Petro Madushi, Jimbo kuu la Mwanza
Shemasi Theogenes Petro Madushi, Jimbo kuu la Mwanza

UKUAJI WA WITO: Tofauti na kipindi nilipokuwa mtoto mdogo, baada ya kuanza mafundisho ya Ubatizo, ndipo nilihisi kuimarika na kukua kwa wito na hii ilitokana na kukutana na watu mbalimbali kutoka sehemu tofauti. Mafundisho ya Makatekista wa kigangoni Mwamanga na Yichobela pia yalichochea zaidi hamu yangu ya kumtumikia Mungu. Nilianza kuelewa maana ya kuitwa kuwa Padre. Wakati wa masomo yangu hasa ya sekondari, niliendelea kuwa na shauku ya kuwa Padre. Ingawa kwa wakati fulani nilitamani pia kuwa Daktari, lakini shauku ya kuwa Padre ilikuwa kubwa zaidi kwani kwa wakati huo sikujua kama mtu anawaeza kuwa Padre na Daktari kwa wakati mmoja. Nikiwa shule ya sekondari Mwamanga, nilihudumu kama Mwenyekiti wa TYCS na pia kama Katekista – si kwa wanafunzi tu bali hata katika kigango cha Kisesa B, hasa Katekista alipokuwa hayupo. Nawashukuru sana Makatekista Dioniz Kakwene na Polycarpo Maige walionifundisha na kunielekeza namna ya kuongoza Ibada ya bila Padre na hivyo wakawa wananipa nafasi ya kuongoza ibada vigangoni Kisesa “B” na Mwamanga. Huduma hii ya Ukatekista niliendelea nayo hata nilipokuwa Kahororo Sekondari, nilihudumu kama Katekista kati ya wanafunzi wenzangu. Huduma hizi zilinilea kiroho na kunifanya niwe na moyo wa utumishi.

Malezi ya Kipadre na hatimaye kushamiri wito wa Kipadre
Malezi ya Kipadre na hatimaye kushamiri wito wa Kipadre

MALEZI YA KIPADRE: Baada ya kumaliza A-level mwaka 2016, nilijiunga rasmi na nyumba ya malezi Parokia ya Kirumba, na baadaye Nyumba ya Askofu Mkuu Kawekamo, nikipokelewa na Mkurugenzi wa Miito, Padre Frances Mtema. Mwaka huo huo, mwezi Oktoba, nilianza masomo ya Falsafa katika Seminari Kuu ya Mtakatifu Agustino – Peramiho, Jimbo Kuu la Songea. Nilihitimu Falsafa mwaka 2019, na nikaendelea na masomo ya Taalimungu katika Seminari hiyo hiyo hadi Februari mwaka 2021. Kisha, Baba Askofu alinituma Roma kuendelea na malezi na masomo, mpaka mwaka Juni 2024 nilipohitimu masomo ya Taalimungu na kuanzia Oktoba 2024 niliendelea na masomo ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana, nikisomea Mafundisho Tanzu ya Kanisa, “Dogmatic theology” na kuhitimu tarehe 26 Juni 2026. Kwa neema ya Mungu, nilipokea Daraja Takatifu ya Ushemasi tarehe 3 Mei 2025, katika Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kwa kuwekewa mikono na sala ya kuwekwa Wakfu na Mwadhama Kardinali Luis Antonio Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu.

Jumuiya ya Wanafunzi Wakatoliki wanaosoma Italia.
Jumuiya ya Wanafunzi Wakatoliki wanaosoma Italia.

Padre kama kuhani si kwa ajili ya kuadhimisha na kutoa Sadaka bali anaalikwa yeye pia kuwa sadaka yaani kuwa Ekaristi, kwani Maisha ya Padre yanapaswa kumegwa kwa ajili ya wengine, kama Kristo alivyojitoa. Ninapojiandaa kwa daraja ya Upadre, moyo wangu umejaa unyenyekevu na furaha nikimwomba Mungu ili kile alichokianzisha ndani mwangu yeye mwenyewe akitimize. Pamoja na Mwinjili Moyo wangu pia unaimba kiitikizano cha maneno ya Kristo ukisema: “Maana Mwana wa Mtu hakuja kutumikiwa, bali kutumika na kutoa nafsi yake iwe fidia kwa wengi.” Marko 10:45, Mungu aniongoze kuishi dira hii katika utumishi wangu. Katika roho hiyohiyo na kwa Maombezi ya Mtakatifu Agustino anikumbushe daima kuwa: “Yesu alichukua hali ya mtumwa ili kutufanya sisi kuwa huru; alihudumu ili tujifunze kutumikiana; alijinyenyekeza ili kutuinua.” Naomba Mungu anifundishe moyo wa utumishi, kwa sababu yeye ndiye kielelezo halisi cha huduma ya kweli.

Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Italia
Jumuiya ya Watanzania wanaoishi Italia

PAROKIA ZA MAZOEZI YA UTUME

Katika kipindi chote cha malezi nimefanya Utume katika Parokia zifuatazo:

2017- Parokia ya Mtakatifu Peter Clavery, Nyambiti

2018-Parokia ya Mtakatifu Yohane Mwinjili, Usagara

2019- Parokia ya Mtakatifu Yohane Mwinjili, Usagara

2020-Nyumba ya Askofu Mkuu, Kawekamo

2021-Nyumba ya Askofu Mkuu, Kawekamo

2022- 2023-Kituo cha watu wenye uhitaji maalum, (walemavu), Piazza della Trinità dei Pellegrini Roma.

2023-2024-Madhabahu ya Huruma ya Mungu, (Santo Spirito in Sassia), Roma

2024-2025-Parokia ya Mtakatifu Lucia, Roma

2025-2026- Parokia ya Mtakatifu Yosefu Cottolengo, Roma.

Majandokasisi Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, Roma
Majandokasisi Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbaniana, Roma

SHUKRANI NA HITIMISHO: Ninawashukuru Wazazi wangu kwa kukubaki kunitoa kuwa Mtumishi katika Kanisa la Mungu, walimu wangu wote katika shule na seminari zote nilizopitia, familia yangu, ndugu na marafiki wote mlionilea na kuniongoza katika safari hii ya neema. Bado naomba msaada wa sala zenu ili nisimame imara katika wito huu wa kipadre, nikiwa mfano mwema na hai wa Kristo Mchungaji mwema. Ninawakaribisha wote tarehe 4 Julai 2026, katika Misa Takatifu itakayoadhimishwa na Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo kuu la Mwanza katika Parokia ya Mtakatifu Bernadeta Kahangara, Jimbo kuu la Mwanza ambapo kwa neema na huruma ya Mungu mimi pamoja na wenzangu wawili tutawekwa wakfu kuwa Mapadre katika katika Kanisa la Mungu. Bikira Maria Mama wa Msaada wa daima... Utuombee. Ni Shemasi Theogenes Petro Madushi, Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania.

Shemasi Madushi
02 Julai 2026, 15:36