RD Congo,Kujenga Ulimwengu wa haki ili kuponya majeraha!
Na Jean Paul Kamba – Vatican.
Kama mahujaji wa matumaini, sote tunaalikwa kufanya kazi kwa ajili ya ujio wa haki. Huu ni wito wa dharura, hasa kwa sisi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako vita na migogoro, ambayo sasa ni ya mzunguko, inaendelea kusumbua jamii na kusambaratisha familia, na kusababisha mgogoro wa kibinadamu katika eneo hili la Afrika." Haya ni kwa mujibu wa Tony Tshibanda Tondoyi, wakili wa Congo kutoka Lubumbashi, mji ulioko kusini mashariki mwa nchi hiyo ya Afrika, katika mahojiano na vyombo vya habari vya Vatican , wakati Jubilei ya kwanza ya Wafanyakazi wa Haki ikiadhimishwa, tarehe 20 Septemba 2025.
Kupindua mfumo uliovunjika
"Sote tumeitwa kujenga ulimwengu wa haki," Tshibanda Tondoyi alisisitiza, akibainisha kuwa "haki si kamilifu karibu kila mahali duniani, lakini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kuna sababu ya kuhoji iwapo haki bado ipo." Hivi karibuni, Rais wa Congo Félix Tshisekedi pia alielezea mfumo wa mahakama wa nchi hiyo kama "mgonjwa." Ni mfumo wa mahakama, kulingana na wakili huyo, "unaosumbuliwa na rushwa, hongo, ushawishi wa biashara, uzembe na kunyimwa haki".
Mpango wa Kanisa Katoliki
Ili kuishi imani yao kwa uhalisi, katika muktadha ulio na maafikiano mengi, wanasheria wa Kikristo na mahakimu wameungana pamoja katika chombo kiitwacho Muungano wa Mahakimu na Wanasheria Wakatoliki ulipewa jina kwa (CMABAC). Mpango huu ulizinduliwa hivi karibuni na Askofu Mkuu wa Lubumbashi, Fulgence Muteba Mugalu, rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Congo (CENCO). Lengo ni kukuza maadili ya Kikristo ndani ya mfumo wa mahakama wa Congo kupitia programu za mafunzo, mafungo, na kubadilishana uzoefu. CABAC pia husaidia maskini ambao hawawezi kumudu ada za kisheria na kuingilia kati katika baadhi ya kesi, kama vile unyakuzi wa ardhi.
Bila haki, vurugu, na kutokujali
"Pia inahusu haki ya kijamii, upatikanaji sawa wa haki na ulinzi wa kijamii, haki ya mgawanyo, na haki ya malipo," mwanasheria huyo anatoa maoni, akisisitiza haja ya "kukumbatia" kati ya haki na matumaini ya kupindua "mfumo wa mahakama ambao unawakutanisha wenye nguvu dhidi ya wanyonge, matajiri dhidi ya maskini." Na ukosefu wa haki huzaa chuki, ambayo baadaye husababisha vurugu na kutokujali. "Kinachotokea mashariki mwa nchi," anahitimisha, "ni matokeo ya kutokujali na kwa hivyo ukosefu wa haki." Lakini kwa kujitolea kwa kila mtu, "haki siku moja itastawi tena."