Tanzania,Zanzibar Cup:Mchezo wa kuunganisha watu na tamaduni kwa kujenga urafiki
Na Angella Rwezaula - Vatican.
Karibu ndugu msikilizaji wa Vatican News, katika kipindi cha Michezo, na hasa leo hii ninakuletea mahojiano na Dk. Stefano, Conte, Daktari wa jumla na Daktari wa upasuaji wa moyo wa watoto kutoka Roma, Mhusika mkuu wa maandalizi ya Toleo la IV la “Zanzibar Cup,”wa Kite Surf, shindano la kimataifa lililofanyika tarehe 31 Agosti 2025. Shindano hilo lilifuatiwa na matoleo mengine matatu ambayo yameleta pamoja ushiriki kutoka pande za dunia huko Pwani ya Kiwengwa, Zanzibar kama urafiki na udugu na amani na mshikamano kupitia mchezo. Dk. Conte anatupatia mrejesho.
Dk. Stefano hatimaye Toleo la nne la ZANZIBAR CUP limeweza kufanyika tarehe 31 Agosti. Unaweza kusimulia ilivyokuwa tukio hilo la shidano?
Mbio zilikwenda vizuri sana. Jumamosi ya tarehe thelatini Agosti ilitubidi kughairi programu kwa sababu ya ukosefu wa upepo, lakini Jumapili upepo ulirudi na tukaweza kufanya nusu fainali mbili za regatta, fainali na shindano la (freestyle) yaani mtindo huru, lakini zote kwa siku moja.
Je washiriki wa shindano hilo walikuwa wangapi na walitoka nchi gani?
Tulikuwa na washiriki thelathini na watatu waliojiandikisha kwa mbio hizo mbili kutoka nchi nne (Tanzania, Poland, Jamhuri ya Czech na Ubelgiji). Kwa Zanzibar Cup ijayo tunatarajia kuwakaribisha washiriki zaidi wa kimataifa ikiwa tutakuwa na bajeti kubwa na tiketi za ndege kuwapa mabingwa wa dunia wa mchezo wetu.
Kuhusiana na hilo mbona Afrika Mashariki kuna Tanzania tu, unafikiri ni kwa nini wengine wa kutoka Bara la Afrika hawajafika?....
Asante kwa swali. Ningependa sana kuwakaribisha wanariadha kutoka nchi nyingine za Afrika, lakini katika bara hili, tofauti na Ulaya, Amerika au Asia, tiketi za ndege ndani ya bara hili zinagharimu sawa na safari za mabara. Sera ya bei iliyopitishwa na mashirika ya ndege barani Afrika, ambayo ni bara maskini zaidi, haiwezi kuhalalishwa. Tiketi kutoka Roma kwenda Paris, kutoka Toronto hadi New York, au kutoka Kuala Lumpur hadi Bangkok inagharimu karibu dola mia moja au mia mbili, wakati tiketi ya kutoka Lagos kwenda Zanzibar inagharimu sawa na ile ya kutoka Roma kwenda Zanzibar. Nimesikitishwa sana na hili.
Toleo hili lilikuwa na tofauti gani kati ya matoleo mengine yaliyotangulia kwa sababu sasa limeanza kuingia uhai wake kujulikana kupitia vyombo mbali mbali vya matangazo?
Tofauti kuu iliyoashiria toleo hili la Zanzibar Cup ilikuwa mashindano ya freestyle yaani mtindo huru. Kwa hivyo tuliweza kufurahia tamasha la miruko mingi ya sarakasi na walio bora zaidi katika utaalamu huu. Shindano hilo lilitolewa lilisimamiwa na Riccardo Nobile, Jaji wa kimataifa ambaye tayari yuko kwenye mashindano ya Ulimwengu ya freestyle yaliyopita.
Washindi walitoka sehemu gani?
Washindi wa mashindano hayo mawili wote wanatoka Zanzibar - Tanzania, na wamezindua changamoto kwa mabingwa mbalimbali wa kimataifa kwa toleo lijalo la Zanzibar Cup. Majina yao ni Omar Abdalla kwa Regatta, na Seif Seif kwa Freestyle.
Dk. Stefano hii inaendelea kukuaminisha kwamba kukutana kunaweza kweli kuwa njia ya kuleta amani kati ya watu?
Ndiyo, ninazidi kusadikishwa kwamba mashindano yetu ya kimataifa ya michezo barani Afrika yanaweza kuchangia kuleta amani na udugu kati ya watu. Ujumbe wangu uko wazi: kuonyesha kwamba unaweza kuishi kwa furaha kati ya ndugu na kidogo bila hitaji la vifaa vyote vilivyowekwa na jamii ya watumiaji wa kibepari. Na kisha ni muhimu kutenga haraka iwezekanavyo Mataifa yote ambayo yanakandamiza wanyonge na Mataifa yote ambao ni washirika wao hata kama hii mara nyingi inamaanisha kupoteza pesa na biashara. Ni kwa njia hiyo tu watu wa kike na kiume watapata heshima inayofaa kwao wenyewe. Pia ninaamini kuwa wimbo wetu wa “Zanzibar Cup Song,” unaweza kusaidia sana katika kuhamasisha na kupeleka ujumbe wetu duniani. Lakini bado ninatafuta kundi maarufu la muziki wa Tanzania litakalo rekodi wimbo mzima na kuusambaza duniani kote. Wito wangu ni kwamba iwapo mwanamuziki yeyote maarufu wa Tanzania anatusikiliza, bado tafadhali awasiliana nasi mapema iwezekanavyo kupitia barua pepe kwa: stefconte@yahoo.it
Toleo jingine litakalofuata ni lini?
Nina furaha kuwatangazia wasikilizaji wote wanaozungumza Kiswahili wa Radio Vatican kwamba Zanzibar Cup ijayo (regatta na freestyle) itafanyika katika maji ya Kiwengwa siku ya Jumamosi tarehe saba Februari elfu mbili ishirini na sita (7 Februari 2026). Tayari ninafanya kazi ya kuandaa mbio muhimu zaidi kuliko zilizotangulia. Natumaini kwamba wasikilizaji wengi wanaweza kuja kutazama mbio hizo na hata wengine kushiriki.
Hatimaye Dk. Stefano kuna jambo ambalo bado unataka kumfahamisha msikilizaji wa Radio Vatican kuhusiana na tukio hilo ?
Kwa furaha kubwa, asante. Awali ya yote napenda kuwashukuru viongozi wa Tanzania na Zanzibar, yaani marais Hassani na Mwinyi na mawaziri Kombo na Soraga, waliotusaidia sana. Kisha niwashukuru wanachama wote wanaoendelea kuiamini ndoto yetu na kujiunga na Kombe la Zanzibar. Hatimaye, tunawashukuru wale wote waliotusaidia katika kutekeleza shughuli zetu, ikiwa ni pamoja na msaada wa Radio Vatican. Ikiwa mtu yeyote anasikiliza na anataka kuuliza habari, kutoa ushauri au kujiunga na kikundi chetu cha wafadhili, anaweza kuniandikia kupitia barua pepe kwa: stefconte@yahoo.it au kupitia Instagram kwa: Stef_kitesurf.events.
Kadhalika Wadhamini wetu ambao tunawashukuru sana ni: makampuni ya Asas na Vigor, na hoteli za Melia, Mapenzi, Baobab, Neptune, Dongwe, Kendwa Rocks, Serena na Marumaru. Kwa siku za usoni, kadiri wafadhili wetu wanavyotupatia uungwaji mkono, ndivyo idadi ya mabingwa wa kimataifa tutakavyoweza kuwaalika na hivyo kuifanya Zanzibar Cup kuwa maarufu duniani kote. Asante kwa kila mmoja na ninawakaribisha tena tuonane mwezi Februari tarehe saba, elfu mbili ishirini na sita(2026).
Asante sana Dk. Stefano kwa ushuhuda huo na juhudi hizo za kutaka kuleta pamoja watu wa mataifa ili kuwakutanisha kupitia njia za mchezo ambazo hakuna kitu cha msingi zaidi ya "kuishi udugu, mshikamano amani na mapendo kati ya Ndugu!"
Ndugu msikilizaji na Msomaji wa Vatican News, hayo yalikuwa ni mahojiano kati ya Vyombo vya Radio Vatican na Dk. Stefano, Conte, Daktari wa jumla na Daktari wa upasuaji wa moyo wa watoto kutoka Roma, Mhusika mkuu wa maandalizi ya Toleo la IV la “Zanzibar Cup,”shindano la kimataifa lililofanyika tarehe 31 Agosti 2025 na ambaye ametupatia mrejesho. Hadi wakati mwingine.