Umoja wa Mataifa unaadhimisha miaka 80 ya kuzaliwa:hebu tushikamane na tukidhi ahadi yetu ya kipekee ya UNwetu!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika fursa ya siku ya Umoja wa Mataifa ya kutimiza miaka 80 tangu kuanzishwa kwake tarehe 24 Oktoba 1945, mara tu baada ya vita vikuu vya II vya Ulimwengu, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Bwana António Guterres, alituma ujumbe wake kwa njia ya Video huko jijini New York Marekani, katika Makao Makuu ya Umoja akisema kwamba “wakati wa kuundwa shirika hilo watu wote walizingatiwa na wote kupewa majukumu: “Sisi watu wa Umoja wa Mataifa... Haya si maneno tu ya utangulizi wa Chata ya Umoja wa Mataifa ni maneno yanayotuainisha sisi ni akina nani.”
Umoja wa Mataifa i zaidi ya Taasisi
Kiongozi huyo alisisitiza kuwa “Umoja wa Mataifa ni zaidi ya taasisi. Ni ahadi inayoishi ikivuka mipaka, ikiunganisha mabara, ikihamasisha vizazi. Kwa miaka themanini, tumefanya kazi kujenga amani, kukabili umaskini na njaa, kuhamaisha haki za binadamu, na kujenga dunia iliyo endelevu zaidi kwa pamoja.” Akiakisi siku zijazo, Bwana Gutterres alisema: “tunavyoangalia mbele, tunakabiliwa na changamoto kubwa: mizozo inayoongezeka, hali ya tabianchi, teknolojia za hali ya juu, na tishio la muundo wa taasisi yetu.
Bwana Gutterres alisema "Huu si wakati wa uoga au kurudi nyuma. Sasa, kuliko wakati wowote ule, dunia lazima ijizatiti kutatua matatizo ambayo si taifa moja linaweza kutatua peke yake. Alihitimisha ujumbe wake kwa kutaka “ushirikiano zaidi duniani huku watu wote wakitambua Umoja wa Mataifa ni wao. Katika siku hii ya Umoja wa Mataifa, hebu tushikamane na tukidhi ahadi yetu ya kipekee ya Umoja wenu wa Mataifa. Hebu tuoneshe dunia kile kinachowezekana pindi sisi watu tunapoamua kuchukua hatua kwa pamoja”.
Mkataba wa UN
Mkataba wa Umoja wa Mataifa ni muhimu kwa kudumisha amani na usalama wa kimataifa, maendeleo ya uhusiano wa kirafiki kati ya mataifa, na kukuza ushirikiano wa kimataifa. Umoja huu una umuhimu muhimu wa kiishara na kisheria, hasa kwa nchi zilizo ndogo, ambazo zinaona katika Mkataba huo kama chanzo cha utulivu na usalama dhidi ya utawala wa wenye nguvu zaidi. Zaidi ya hayo, Mkataba huo umechukua jukumu la msingi katika kuondoa ukoloni na katika kuhakikisha haki na utu wa binadamu.
Mkataba huo ulitiwa saini huko Mtakatifu Francisco mnamo tarehe 26 Juni 1945, na nchi 50 kati ya 51 wanachama (Poland, ambayo haikuwepo kwenye mkutano huo, ilisainiwa mnamo Oktoba 1945) mwishoni mwa Mkutano wa Umoja wa Mataifa kuhusu Umoja huo wa Kimataifa. Na kwa njia hiyo ulianza kutumika mnamo tarehe 24 Oktoba1945, baada ya kuidhinishwa na wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama (China, Ufaransa, Umoja wa Kisovieti, Uingereza, na Marekani) na na nchi nyingi zilizotia saini.
Vatican na Palestina zina wawakilishi wa Kudumu katika Umoja wa Mataifa
Kwa sasa, kuna nchi wanachama 193 wa Umoja wa Mataifa. Mataifa mengine mawili, Kiti Kitakatifu au Vatican na Palestina, yana hadhi ya Wawakilishi wa Kudumu. Nchi hizi 193 ni wanashama wa Shirika hilo na zimepiga kura kukubali Mkataba wa Umoja wa Mataifa, zikikubali majukumu yanayoambatana nao.Wawakilishi wa Kudumu kama Vatican na Palestina hushiriki katika shughuli za Umoja wa Mataifa lakini hazina haki ya kupiga kura katika Umoja huo.