Afrika/Nigeria:Wasichana kadhaa wa shule watekwa nyara shuleni
Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.
Baada ya kumuua Naibu Mkuu wa Shule hiyo, Malam Hassan Yakubu Makuku, ambaye alikuwa amejaribu kuwalinda wanafunzi, na kumjeruhi mlinzi, washambuliaji waliwateka nyara wasichana wengi wasiojulikana. Kulingana na Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari (Fides), imebainisha kuwa “Shambulio hilo lilitokea yapata saa kumi asubuhi, muda mfupi kabla ya sala ya asubuhi. Watekaji nyara walikimbia na wasichana hao hadi Serikali ya Zamfara iliyo karibu.
Eneo ambalo utekaji nyara huo ulifanyika ni la Waislamu wengi. Eneo la Serikali ya Mitaa ya Danko/Wasagu (LGA) ni sehemu ya Zuru (ambayo inajumuisha Fakai, Sakaba, na Zuru). Katika wilaya ya Kebbi, kumekuwa na historia ya utekaji nyara wa wanafunzi na magenge yanayovamia taasisi za elimu. Mnamo tarehe 7 Juni 2021, wanaume wenye silaha waliwateka takriban watu 80, wakiwemo wafanyakazi na wanafunzi wa Chuo cha Serikali huko Yauri.
Baadhi ya mateka waliachiliwa huru na jeshi la Nigeria siku chache baada ya kutekwa nyara kwao, huku wengine wengi wakiripotiwa kuachiliwa huru baada ya fidia kulipwa. Majambazi hao kisha wakaachilia mateka 57 baada ya miezi saba. Wa mwisho waliachiliwa kati ya Aprili na Mei 2023, baada ya kukaa zaidi ya siku 707 kifungoni.