Türk,OHCHR:Mauaji na ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa uchaguzi Tanzania lazima vichunguzwe
Habari za Umoja wa Mataifa (UN)
Katika taarifa yake iliyotolewa mjini Geneva Uswiss , tarehe 11 Novemba 2025 na kufafanuliwa na msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu za Umoja wa Mataifa( OHCHR) Seif Magango Bwana Volker Türk, alitoa wito wa kufanyika uchunguzi wa mauaji na ukiukaji mwingine wa haki za binadamu uliotekelezwa katika muktadha wa uchaguzi Mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025 nchini Tanzania kufuatia na ripoti kwamba miili ya watu huenda imepelekwa na vyombo vya usalama katika maeneo yasiyojulikana.
Mkuu huyo wa Umoja wa mataifa alisema “taarifa zilizokusanywa na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kutoka vyanzo mbalimbali nchini Tanzania zinaonesha kuwa mamia ya waandamanaji na watu wengine wameuawa, huku idadi isiyojulikana ya watu wakijeruhiwa au kukamatwa.” “Ofisi hiyo imeshindwa kuthibitisha kwa uhuru idadi kamili ya vifo kutokana na hali tete ya usalama na kuzimwa kwa mtandao kulikofuata baada ya uchaguzi.”
Ombi la Tanzania ikabidhi miili ya waliouawa kwa ndugu zao
Türk alisema “Ripoti za familia zinazotapatapa kutafuta wapendwa wao kila mahali, wakitembelea kituo kimoja cha Polisi baada ya kingine na Hospitali moja baada ya nyingine, ni za kusikitisha sana. ”Aliongeza kuwa “Natoa wito kwa mamlaka za Tanzania kutoa taarifa kuhusu hatima na mahali walipo wote waliopotea, na kukabidhi miili ya waliouawa kwa familia zao ili wapate mazishi yenye heshima.”
Aliendelea kusema kwamba “Pia kuna ripoti za kutia wasiwasi kwamba vikosi vya usalama vimeonekana vikiondoa miili mitaani na hospitalini na kuichukua katika maeneo yasiyojulikana, katika kile kinachoonekana kuwa ni jaribio la kuficha ushahidi”. Kamishna Mkuu huyo wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa (OHCR) alizitaka mamlaka za Tanzania kufanya uchunguzi wa kina, huru na wa wazi kuhusu madai haya mazito ya ukiukaji wa haki za binadamu, na kuwawajibisha wote waliohusika. Aidha, alirejea wito wake wa “kuachiliwa bila masharti kwa viongozi wote wa upinzani waliokamatwa kabla ya uchaguzi mkuu, wakiwemo kiongozi wa chama cha Chadema, Tundu Lissu, na watu wengine wote waliokamatwa kiholela tangu siku ya uchaguzi.”
Kuhusu idadi ya watu waliokamatwa
Inaripotiwa kuwa zaidi ya watu 150 walikamatwa tangu kura kupigwa, bila msingi wa kisheria ulio wazi huku baadhi yao, wakiwemo watoto, wameripotiwa kufunguliwa mashitaka ya uhaini.” Kwa njia hiyo, Türk alisisitiza “Ni muhimu kwamba wote waliokamatwa au kuwekwa kizuizini kwa mashitaka ya jinai wafikishwe haraka mbele ya hakimu, na wapewe fursa ya kupinga uhalali wa kizuizi chao. Wote walioko kizuizini lazima wapatiwe haki kamili za kisheria zinazolindwa chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu.”