Dunia inawaka moto kwa ukosefu wa amani na kuwa na matatizo ya njaa
Habari za Ulimwengu
Kuanzia Kusini, Kaskazini, Magharibi na Mashariki ya Dunia, sauti zinazosikika ni za wasiwasi mkubwa kutokana na migogoro ya kivita, janga la njaa na majanga ya asili na mengine mengi. Kwa mtazamo huo ulimwengu kiukweli umekatishwa na kuenea vita vilivyogawanyika vipande vipande, hasa kukabiliwa na migogoro mingi ya kisilaha na mivutano inayoendelea na ya kisiasa. Ukweli huu hutoa hisia kali ya kusikitisha kwa kutokuwa na nguvu na utafutaji wa nafasi za mazungumzo ya kweli na maelewano na kuwafanya wengi kujihoji juu ya asili ya mwanadamu. Tutazame baadhi ya kile kinachoendelea katika baadhi ya nchi duniani kuhusiana na hayo niliyotangulia kusema.
Urusi/Ukraine
Wizara ya Ulinzi ya Urusi iliripoti kwamba mifumo ya ulinzi wa anga ya Urusi ilizuia na kuharibu ndege zisizo na rubani 138 za Ukraine usiku kucha katika eneo la Urusi. Moscow na Kyiv Mei 14, walitangaza hata hivyo kukamilika kwa ubadilishanaji wa wafungwa 410 wa vita: wanajeshi 205 wa Urusi na 205 wa Ukraine walirudishwa katika nchi zao. Mkataba huo, uliotangazwa katika siku za hivi karibuni na Rais wa Marekani Donald Trump, unawakilisha mojawapo ya ishara chache halisi za mazungumzo kati ya pande hizo katika juma za hivi karibuni.
Marekani/China/Taiwan
Serikali ya Taiwan ilijibu kauli za Trump mwishoni mwa safari yake nchini China. Rais wa Marekani alionya dhidi ya tangazo lolote la uhuru ambalo linaweza kusababisha vita na Beijing. Baada ya Trump, Putin anatarajiwa Beijing Mei 19. Utulivu wa kimkakati wenye kujenga: huu ndio ufafanuzi uliojitokeza jana baada ya mkutano mjini Beijing kati ya Rais wa China Xi Jinping na mwenzake wa Marekani Donald Trump, ili "kutoa mwongozo wa kimkakati kwa miaka mitatu ijayo kuhusu uhusiano wa pande mbili kati ya China na Marekani." Hii iliripotiwa na shirika la habari la serikali ya China Xinhua, na ni neno linalopendekeza jinsi ya kuelewa uhusiano kati ya mataifa hayo mawili yenye nguvu.
Nigeria
Kiongozi wa ISIS aliuawa katika operesheni ya pamoja kati ya jeshi la Nigeria na wanajeshi wa Marekani. Abu Bilal al-Minuki alikuwa mtu namba mbili katika kile kinachoitwa ‘Islamic State.’
Israeli/Libanon
Usitishaji mapigano umeongezwa kwa siku 45 wakati wa mazungumzo zaidi kati ya nchi ya Israeli na Lebanoni huko Washington, licha ya mashambulizi mapya ya Israeli kusini mwa Lebanon siku ya Ijumaa tarehe 15 Mei 2026. Usitishaji mapigano kati ya Israeli na Lebanon ulitakiwa kuisha Dominika Mei 17 lakini baada ya siku mbili za mazungumzo nchini Marekani, umeongezwa kwa siku nyingine 45, hadi duru inayofuata ya mazungumzo iliyopangwa kufanyika Juni 2 na 3. "Mpango wa usalama" utatekelezwa na Pentagon kuanzia Mei 29. Hata hivyo, kiukweli, makubaliano haya ya kusitisha mapigano hayajawahi kuheshimiwa: mashambulizi ya jeshi la Israeli yanaendelea ardhini, kama vile kisasi cha Hezbollah.
Hali mbaya Lebanon
Tangu kuanza kutumika kwa makubaliano ya kusitisha mapigano, watoto 23 wamefariki na 93 wamejeruhiwa. Takriban watoto 770,000 nchini Lebanon wanaaminika kuishi katika hali ya udhaifu mkubwa wa kisaikolojia.
Iran
Mjini Tehran, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema "amepokea ujumbe" kutoka Washington unaounga mkono kuanza tena kwa mazungumzo ili kukomesha mzozo katika Mashariki ya Kati, akiongeza kuwa yuko tayari kwa msaada wa Beijing.
Brazil
Podikasti ya kuelewa changamoto za nchi hiyo ya Amerika Kusini, kati ya cracolandias na Amazonia "Off the Radar" inachunguza biashara ya dawa za kulevya nchini Brazil, mtumiaji wa pili kwa ukubwa wa kokeini duniani. Mauzo ya nje kwenda Afrika na Ulaya, jukumu la jiografia, na juhudi za wamisionari kubadili mwelekeo huo. Kipindi cha podikasti cha Off the Radar "In the Brazilian Cracolandias"(La puntata del podcast Off the Radar “Nelle cracolandias brasilane”) kinasimulia hali ilivyo kwa ushuhuda wa Padre Renato Chiera, mwanzilishi wa Casa do Menor, chama kilichoanzishwa mwaka 1986 ambacho leo hii kina zaidi ya makazi 7,500 na wakujitolea 5,000 nchini kote, na Padre Wellington Abreu, mmisionari wa Kisalesian na Padre wa Parokia ya Mtakatifu Malaika Mkuu Mikaeli huko Iauareté, katika Jimbo la Mtakatifu Gabarieli WA Cachoeira, katika Amazonia ya Brazil.
Italia
Kuanzia Aprili 29 hadi Mei 2, 2026, Mkutano wa Kitaifa wa Mapadre wa Gerezani na Wafanyakazi wa Uchungaji ulifanyika huko Assisi kwa mada: "...ili aweze kuilima na kuitunza" (Mwa 2:15) - Kazi, ukarimu na huduma.
Azerbaijan
Kongamano la Umoja wa Mtaifa la XIII la Miji Duniani linafunguliwa Dominika tarehe 17 Mei 2026 mjini Baku, Azerbaijan, ambapo washiriki wanatarajiwa kujadili namna ya kukabiliana na mgogoro unaozidi kuongezeka wa makazi duniani. Mkutano huo, ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Makazi, UN-HABITAT kwa ushirikiano na serikali ya Azerbaijan, utawakutanisha viongozi wa dunia, mameya, wataalamu wa mipango miji pamoja na wawakilishi wa serikali, sekta binafsi, mashirika ya kiraia na taasisi za kimataifa.
Siria
Naibu Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Siria Claudio Cordone akizungumza Mei 15, 2026 kwenye kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kinachomulika hali ya kisiasa na kibinadamu nchini humo alisema “Nchini Siria, “tumeshuhudia maendeleo kuelekea uwajibikaji na ushirikiano endelevu wa kimataifa na kikanda.” Katika masuala ya usalama, Bwana Cordone alieleza wasiwasi mkubwa kuhusu uwepo unaoendelea na shughuli za kijeshi za Vikosi vya Ulinzi vya Israel mashariki mwa mstari wa kusitisha mapigano, jambo ambalo amesema linakiuka Mkataba wa Kutenganisha Vikosi wa mwaka 1974. Cordone alisema, “Hatua hizi zinakiuka mamlaka na ukamilifu wa ardhi ya Syria, zinatishia uthabiti wa Syria na kuwaathiri raia.”
Congo DR
Mapigano yanayoendelea na wimbi kubwa la wakimbizi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DR yamewaacha watu milioni 26.5 wakikabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula na kuhitaji msaada wa kibinadamu kwa haraka limesema shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO.
Somalia
Mashirika manne ya Umoja wa Mataifa, yametoa onyo kali kuhusu hali ya ukosefu wa chakula inayoongezeka kwa kasi nchini Somalia ambayo tayari imewasukuma watu milioni 6, sawa na asilimia 31 ya idadi ya watu wote nchini humo, katika viwango hatari vya ukosefu wa uhakika wa chakula kati ya mwezi Aprili na Juni mwaka huu.
Imesasishwa tarehe 16 Mei 2026 saa 4.09 asubuhi na Angella Rwezaula.
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.