Kutoka kambi ya wakimbizi hadi Mashindano Makuu ya Taekwondo Duniani
Vatican News
Kuanzia tarehe 4 Juni hadi 7, Roma itakuwa mwenyeji wa Mashindano Makuu ya Taekwondo Duniani ya 2026. Miongoni mwa watakaohudhuria watakuwa wanariadha 8 watoto wenye umri wa miaka 10 hivi kutoka Kambi ya Wakimbizi ya Azraq huko Jordan, ambayo kwa sasa inahifadhi watu wapatao 60,000. Kwa mara ya kwanza maishani mwao, watoto hawa watapata fursa ya kuondoka katika kambi ya wakimbizi, kutokana na mpango wa Mfuko wa Kibinadamu wa Taekwondo, kwa usaidizi wa Shirikisho la Taekwondo la Italia.
Mashindano ya“Kim na Liù”
Kundi hilo litashiriki katika mashindano ya “Kim na Liù,” yatakayoandaliwa kama sehemu ya Mashindano Makuu ya Dunia ya Taekwondo ya 2026, ambayo yatawaruhusu watoto kushindana katika ukumbi na nafasi sawa na mabingwa wa dunia wanaopambania taji la ‘Grand Prix’ na kufuzu kwa Olimpiki ya Majiara ya kiangazi ya Los Angeles ya 2028. Kama sehemu ya kukaa kwao Roma, kundi la wanariadha watoto pia litaweza kukutana na Papa Leo XIV na kutembelea jiji kuu na maeneo yake ya kiutamaduni na kihistoria. Mfuko wa Kibinadamu wa Taekwondo unafanya kazi na Shirikisho la Kimataifa la Taekwondo (ambalo Athletica Vaticana, shirika rasmi la michezo na chama cha Vatican —ni sehemu yake), kuwasaidia wakimbizi na watu waliohamishwa duniani kote kupitia Taekwondo na zana zingine za kielimu. Kupitia mipango yao wanakuza uwezeshaji, amani, uendelevu na maadili ya Olimpiki.
Usemi halisi wa maadili ya Olimpiki
"Tangazo la ushiriki wa watoto lilizua hisia za haraka na za kina: kutoamini, shauku, na matarajio yanayoongezeka yanayoambatana kila siku kuelekea kuondoka kwao," Angelo Cito, Rais wa Shirikisho la Taekwondo la Italia, aliandika katika toleo la Kiitaliano la Osservatore Romano kuwa, "Mipango hii inawakilisha usemi halisi wa maadili ya Olimpiki, ambayo hayawezi kubaki yamesemwa tu lakini lazima yatekelezwe kwa vitendo halisi kupitia vitendo vinavyoonekana," alisema. "Inamaanisha kufanya kazi kwa umakini, kuingilia kati moja kwa moja katika mazingira dhaifu zaidi, na kuchangia katika kuboresha hali ya maishahasa kwa watoto, ambao mara nyingi huathiriwa zaidi na vita na ubaguzi." Bwana Cito alielezea kwamba mradi wa Mfuko wa Kibinadamu wa Taekwondo, ambao utaadhimisha miaka 10 mwaka huu, tayari umetoa matarajio mapya kwa maelfu ya vijana na familia zao.
Mbali na Jordan, Mfuko huo pia una mipango kama hiyo nchini Rwanda na Uturuki. "Uzoefu wa uwanjani, kama ule wa Jordan, unashuhudia azimio la ajabu la wavulana na wasichana ambao wanajua changamoto wanazokabiliana nazo lakini pia wamejitolea kusoma na kufanya mazoezi ya michezo ili kujenga mustakabali bora," Bwana Cito alisisitiza. "Katika enzi iliyojaa ukosefu wa usawa unaoongezeka na migogoro inayoendelea, michezo bado inaweza kutumika kama nafasi ya muunganisho na uwezeshaji," Bw. Cito alihitimisha. "Taekwondo, pamoja na nidhamu na maadili yake, inatoa somo wazi leo: mafanikio ya kweli si tu kuhusu kusimama kwenye jukwaa, bali kuhusu kumpatia mtu, popote duniani, nafasi ya hatimaye kufanya hivyo."
Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.