Kuendelea kujinga na Ebola huko DRC Kuendelea kujinga na Ebola huko DRC  (ANSA)

UN:Juhudi za kuleta utangamano wa kitaifa kwenye maeneo yenye hali tete ya amani

Wanawake takriban 60 kutoka maeneo ya Beni,Butembo,na Lubero yaliyoko jimboni Kivu Kaskazini nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, waliahidi kukuza amani,ushirikiano wa kijamii,na kupambana na uenezwaji wa habari potofu.Makubaliano hayo yamefanyika kufuatia warsha maalumu iliyofanyika tarehe 21 na 22 Mei 2026 mjini Beni.

Umoja wa Mataifa

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa kwenye wavuti wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kulinda Amani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, MONUSCO, ilifanyika warsha ya wanawake takriban 60 iliyoandaliwa na Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kitengo cha Masuala ya Kiraia, kwa ushirikiano na BEARIC na pamoja  mamlaka ya mkoa wa Kivu Kaskazini ili kukuza amani, mshikamano wa kijamii, na mapambano dhidi ya habari potofu tarehe 21 na 22 Mei 2026.

Washiriki wa fursa hiyo ni wanawake kutoka mashirika ya kijamii, asasi za kiraia, wanawake waliokimbia vita, walemavu, wajumbe wa vyama vya siasa, taasisi za kidini, na makundi ya vijana ambao kwa pamoja wamefundishwa kuhusu michakato ya amani inayoendelea nchini DRC, hasa ile inayofanyika maeneo mbalimbali duniani ikiwemo katika miji ya Washington(Marekani), Doha (Qatar), Luanda (Angola), na Nairobi (Kenya), huku wakihimizwa kufuata maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa namba 1325 na 2773 yanayohusu ushiriki wa wanawake kwenye amani na ulinzi wa raia.

Wito kwa wanawake kuchukua hatua madhubuti

Kutokana na hali ya usalama kuendelea kuwa tete mashariki mwa DRC, Afisa programu wa BEARIC na mwezeshaji wa warsha hiyo, Jean-Paul Lusenge, amefafanua lengo kuu akionesha umuhimu wa wanawake kutumia mbinu za utatuzi wa migogoro ili kuzuia vijana kujiunga na makundi ya waasi. "Tulitaka kuinua ari ya wanawake kuhusu changamoto zilizopo hivi sasa, hasa makubaliano ya Washington na Doha, na tusiwafanye kuwa watazamaji tu bali washiriki hai, kwa sababu nafasi yao ipo kwenye meza ya maamuzi” Amesema Lusenge

Ameeleza pia yale waliyotekeleza mpaka sasa “ Tumefanya kazi kwenye uongozi, utatuzi wa migogoro, na mbinu za utetezi, kwani nchi yetu inakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji majibu ya namna mbalimbali, ikiwa ni pamoja na utetezi na utatuzi wa migogoro kwa njia ya amani. Ilikuwa muhimu kushirikisha maudhui ya makubaliano yanayoendelea sasa hivi ili kuzuia upotoshaji wa habari na ushawishi mbaya unaoweza kuwasukuma baadhi ya vijana kujiunga na makundi ya waasi”.

Wanawake waahidi kuchukua hatua katika ngazi ya jamii

Kwa upande wake, mshiriki Julienne Masika amesisitiza wanawake wamepewa nguvu ya kisheria kushiriki kwenye mazungumzo ya amani kuanzia ngazi ya kijiji hadi kikanda. "Wanawake lazima washiriki katika kuzuia migogoro, hasa kuhusu ukatili unaotokana na migogoro hiyo. Sio tu ukatili wa kijinsia, kwa sababu kuna namna nyingi za ukatili. Kwa hiyo, wanawake lazima washirikishwe; lazima waweze kushawishi na kubadili maamuzi, kwa kuzingatia kwamba Azimio namba 1325 linatupa nguvu ya kushiriki katika mazungumzo ya amani katika ngazi zote ndani ya mfumo wa kuzuia, iwe ni katika ngazi ya ndani hapa Beni au katika ngazi ya kikanda," amebainisha Julienne.

Makamu wa Rais wa Asasi ya Kiraia ya Kyambogho katika eneo la Lubero, Guilaine Kavira Mwangaza, ameeleza utayari wao wa kwenda kufanya kazi mashinani, "Tumejitolea kuelimisha na kuhamasisha wanawake wote ili kuchangia katika ushirikiano wa kijamii na kupambana na upotoshaji wa habari. Mafunzo haya yametuwezesha kuelewa vizuri masuala kadhaa na kurekebisha mitazamo fulani potofu. Kuhusu Azimio namba 1325, tutawahimiza wanawake kujisogeza mbele zaidi katika utekelezaji wake madhubuti. Na kuhusu mbinu za utetezi, sasa hivi tumewezeshwa vizuri zaidi kujua nini cha kuandika na kwa nani tunapaswa kuelekeza changamoto zetu.

Imesasishwa tarehe 28 Mei 2026 saa 2.40 na Angella Rwezaula - Vatican.

Asante kwa kusoma makala yetu. Unaweza kuendelea kupata habari mpya kwa kujisajili kwa jarida letu la kila siku: Just click here.

28 Mei 2026, 08:33