Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi ateuliwa na Chama cha Mapinduzi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi ateuliwa na Chama cha Mapinduzi kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania 

Uteuzi: Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi: Makamu wa Rais Tanzania

Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi, aliyekuwa Waziri wa Nishati ndiye Mwanachama wa CCM anayependekezwa kwa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuziba nafasi ya Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi aliyejiuzulu masuala ya kisiasa na utumishi wa umma na hatimaye, kufukuzwa uwanachama wa Chama cha Mapinduzi, tarehe 26 Agosti 2026 kadiri ya taarifa iliyotangazwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Asha-Rose Migiro,

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chama cha Mapinduzi kimemteua Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi, 43, aliyekuwa Waziri wa Nishati kuwa Mwanachama wa CCM anayependekezwa kwa nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili kuziba nafasi ya Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi aliyejiuzulu masuala ya kisiasa na utumishi wa umma na hatimaye, kufukuzwa uwanachama wa Chama cha Mapinduzi, tarehe 26 Agosti 2026 kadiri ya taarifa iliyotangazwa na Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Asha-Rose Migiro, aliyesema kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM iliyokutana chini ya Uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan imempendekeza Ndejembi kuwa Makamu mpya wa Rais wa Tanzania. Itakumbukwa kwamba, Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi alizaliwa tarehe 12 Julai 1983. Ni Mtoto “mjukuu” wa Mwanasiasa mkongwe mkoani Dodoma Marehemu Mzee Pancras Mtemi Ndejembi ambaye kwa muda mrefu yaani kuanzia mwaka 1982 hadi Mwaka 2007 alikuwa ni kiongozi wa Chama cha Mapinduzi mkoani Dodoma na hivyo kuwa ni sehemu muhimu sana wa historia za siasa za mkoa wa Dodoma.

Dkt Emmanuel Nchimbi ametangaza kujiuzulu wadhifa wake 4 Septemba 2026
Dkt Emmanuel Nchimbi ametangaza kujiuzulu wadhifa wake 4 Septemba 2026

Kwa mujibu wa taarifa za Bunge, mwaka 2012 alikuwa Meneja wa A1 Outdoor, kabla ya kuwa Mkuu wa Mauzo wa “Smile Communication” kati ya 2012–2014. Mwaka 2014 alihamia kwenye Kampuni ya Tigo kama Meneja wa Kanda, nafasi aliyoshikilia hadi mwaka 2015. Mwaka 2016 akateuliwa kuwa Mkuu wa Masoko wa GSM Group. Baada ya uzoefu huo, safari yake ya utumishi wa umma ilianza kupanda kwa kasi. Mwaka 2016 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya, kabla ya kuendelea na majukumu mbalimbali ndani ya serikali. Na kunako Mwaka 2020 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Chamwino kupitia CCM, kisha mwaka 2021 akaingia serikalini kama Naibu Waziri, akihudumu katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Deogratius John Ndejembi amependekezwa kuwa Makamu wa Rais Tanzania
Deogratius John Ndejembi amependekezwa kuwa Makamu wa Rais Tanzania

Baadaye akashika nafasi ya Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, TAMISEMI, kabla ya kupanda zaidi na kuwa Waziri katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu. Kunako Mwaka 2024 aliteuliwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, na mwaka 2025 akahamishiwa kuwa Waziri wa Nishati, nafasi ambayo hadi kuteuliwa kwake kuwania nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kulingana na taratibu za Katiba ya Tanzania, jina la Ndejembi limepelekwa Bungeni Jijini Dodoma kwa ajili ya kupigiwa kura ya ithibati na wabunge katika kikao kinachotarajiwa kuanza tarehe 31 Agosti 2026 kabla ya kuapishwa rasmi na kuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa kumi na tatu! Mheshimiwa Deogratius John Ndejembi ana shahada ya Uhusiano wa Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Lincoln kati ya mwaka 2006 hadi mwaka 2009 alisoma pia Stashahada ya juu kutoka katika Taasisi ya Uongozi kati ya mwaka 2009 hadi mwaka 2012; ana elimu ya uzamili aliyoipata kutoka Chuo Kikuu cha Cumbria. Hii inaonesha kwamba, ni kiongozi ambaye amepikwa kutoka katika sekta binafsi, masuala ya kisiasa, utawala, ubunge na kama waziri. Kupendekezwa kwake na Chama cha Mapinduzi, CCM kuwa ni Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kunafungua ukurasa mwingine wa maisha yake, akiweka rekodi ya kuwa ni Makamu wa Rais kijana zaidi kuwahi kuteuliwa.

Makamu wa Rais
27 Agosti 2026, 15:54