Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 26 ya Mwaka B wa Kanisa. Wivu usiokuwa na mashiko ni mzizi wa dhambi Tafakari ya Neno la Mungu Jumapili 26 ya Mwaka B wa Kanisa. Wivu usiokuwa na mashiko ni mzizi wa dhambi 

Tafakari Jumapili 26 ya Mwaka B wa Kanisa: Wivu Ni Mzizi wa Dhambi

Wivu ni mzizi wa dhambi ni hali ya kutokuwa tayari kufurahia mafanikio au mazuri ya wengine. Ni kuumia na kufa ndani kwa kuwa mwingine amefanikiwa. Wivu ni ugonjwa mbaya wa kiroho kwani unatupelekea kukosa mapendo ya kweli kwa Mungu na kwa wengine. Ni kilema ambacho hatuna budi kuwa sana macho nacho, tuking’oe na kukitoa ndani mwetu ili kufurahia mafanikio!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Mwinjili Marko bado anatuonesha Yesu akiwa njiani kuelekea Yerusalemu, kwenda kwenye utume ule mkuu ya mateso, kifo na ufufuko wake, ndio safari ya kuelekea wokovu wetu sisi wanadamu. Yesu akiwa njiani pamoja na wanafunzi wake wa karibu, yaani, Mitume anatumia nafasi hiyo kuwafundisha mada kadha wa kadha, mada ambazo bado zinaonekana kuwa ngumu kwao kumwelewa aliye Bwana na Mwalimu wetu. Mwinjili Marko katika sura hii ya tisa anatuonesha matukio mawili yanayotutafakarisha. Tukio la kwanza ni yule mtu aliyemleta kwa mitume mtoto wake mvulana, aliyekuwa amepagawa na mapepo; “Mwalimu, nimemleta mwanangu kwako, ana pepo bubu. Kila mara anapompagaa anamwangusha chini, hata akatokwa na povu kinywani, akasaga meno na kuwa baridi. Niliwaambia wafuasi wako wampunge pepo, lakini walishindwa.” (Marko 9:16-18). Na tukio la pili ndio lile tunalolisikia katika sehemu ya Injili ya Dominika ya Ishirini na Sita ya Mwaka B wa Kanisa, simulizi la mtu mmoja asiyetajwa kwa majina anayepunga mapepo kwa kutumia jina la Yesu.

“Yohane akamwambia, Mwalimu, tulimwona mtu akipunga pepo kwa jina lako, nasi tukamkataza kwa kuwa yeye si mmoja wetu.” Ndio maneno ya Mtume Yohane yanayokuwa ni utangulizi wa somo la Injili yetu ya leo. Ni maneno ya mmoja anayesumbuka na kuhangaika kwa kuona ameingiliwa katika utume na kazi yake. Ni hapa tunaweza kujiuliza, Je, pale mwingine anapofanya kile ninachofanya mimi, ninapaswa kujawa na wivu au kufurahi? Labda hata yafaa tukajiuliza leo, Je, ni sisi tu ndio wenye mamlaka ya kutumia jina la Yesu? Maneno ya Mtume Yohane juu ya mtu yule; “si mmoja wetu”, ni maneno yenye kuonesha mipaka anayoiweka, mipaka ya kuwaweka wengine pembeni, wengine hawapaswi kutumia jina la Yesu, wengine hawapaswi si kutumia jina hilo bali hata kujihusisha na Yesu. Ni sawa na kujimilikisha Yesu, ni mali yao, ni wao tu ndio wenye haki na uhalali wa kutumia jina hilo. Yeyote mwingine asiye mmoja wao ni mpinzani wao, ni hatari na hata tungeweza kusema ni sawa na adui kwao, na ndio maana anajaribu kumwambia Mwalimu wao na wetu walipomwona mtu yule walimkataza asitumie jina lile la Yesu.

Je, kuna mmoja wetu atakayejisikia vibaya na kukasirika kuona mmoja tusiyemfahamu anakuja na kutusaidia kazi shambani ya kupanda au kupalilia au kuvuna? Na tena ikiwa mtu yule anafanyakazi kwa bidii kubwa na weledi hata ikiwa anafanya kutuzidi sisi wenye shamba lile? Somo la Injili ya leo pamoja na lile la kwanza tuonaona kilema na mzizi mkubwa wa dhambi unaojitokeza, yaani, wivu. Kama Yohane mtume anavyojaribu kumwambia Mwalimu na Bwana wetu juu ya kumkataza mtu yule, vile vile na Yoshua anajaribu kumwambia Musa kuwakataza kufanya kazi ya unabii Eldadi na Medadi. “Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini. Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze.” Na tunaona jibu la Musa linakuwa sawa na lile la Yesu tunalolisikia katika somo la Injili ya leo. “Je, umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii, na kama Bwana angewatia roho yake.”

Mtakatifu Tomaso wa Akwino anatusaidia kutupa maana ya wivu akisema; “Envy/jelousy is the irrational anger at the success of others”, wivu ni hasira isiyo na mashiko juu ya mafanikio ya wengine, kwa tafsiri yangu isiyo rasmi. Ni kutokuwa tayari kufurahia mafanikio au hata mazuri iwe ni karama au vipaji vya wengine, ni kuumia na kufa ndani kwa kuwa mwingine amefanikiwa au amekuwa na kitu cha kutuzidi. Wivu ni ugonjwa mbaya wa kiroho kwani unatupelekea kukosa mapendo ya kweli kwa Mungu na kwa wengine. Ni kilema ambacho hatuna budi kuwa sana macho nacho, tuking’oe na kukitoa ndani mwetu. Jibu la Yesu katika somo la Injili ya leo; “Msimkataze, kwa kuwa hakuna mtu atakayefanya mwujiza kwa jina langu akaweza mara kuninenea mabaya; kwa sababu asiye kinyume chetu, yu upande wetu.” Ndilo jibu linalotuonesha na kuwaalika si tu mitume bali hata nasi leo kutambua kuwa Yesu Kristo sio mali yangu au ya kikundi fulani tu bali ni kwa ajili yetu sisi sote, bila ubaguzi wa aina yeyote ile. Na ndio tunaona mtaguso wa pili wa Vatikano unakazia Kanisa kama jumuiya shirikishi, kumuoni ya wabatizwa na kamwe sio mali ya makuhani au ya watu fulani tu.

Nafasi mbalimbali ni nafasi za utumishi tu na kamwe asiwepo hata mmoja wetu wa kujimilikisha na kuona wengine wanabaki kando kama watazamaji tu. Hiki kinaweza kuwa kishawishi kikubwa iwe katika jumuiya zetu, vigango, parokia na hata majimbo yetu, kishawishi cha kuibuka watu au kikundi fulani cha kujimilikisha, sisi sote kama wabatizwa kila mmoja wetu ni wa muhimu katika kulijenga Kanisa la Kristo, kila mmoja ni jiwe hai katika kulijenga Kanisa. “Upepo huvuma upendako, na sauti yake waisikia, lakini hujui unakotoka wala unakoenda; ndivyo ilivyo kwa wote waliozaliwa katika Roho.” (Yohane 3:8) Roho wa Mungu anafanyakazi si tu ndani na pamoja na Kanisa bali hata nje ya Kanisa. Hivyo kamwe tusijimilikishe au kujidanganya kuwa Roho wa Mungu anafanyakazi au na baadhi ya watu tu au kikundi fulani na si kwa wengine, kwani anavuma anakotaka.

Sehemu ya pili ya Injili ya leo tunakutana na misemo kadhaa ya Yesu. “Kwa kuwa ye yote atakayewanywesha ninyi kikombe cha maji, kwa kuwa ninyi ni watu wa Kristo, amini, nawaambia, hatakosa thawabu yake.” Na agizo hili tunaliona pia hata kutoka kitabu cha Mithali; “Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula, akiwa na kiu, mpe cha kunywa.” (Mithali 25:21). Tunaweza kuona ni kitendo kidogo tu cha kumpa maji, lakini ndio kusema Yesu anatualika sisi sote kuwa wakarimu kwa wahitaji, kwa wenye shida na dhiki mbali mbali tunaokutana nao. Ni mwaliko wa kuwa wakarimu daima kwa wengine. Mara baada ya msemo na mwaliko huo wa Yesu, tunaona pia anatupa angalisho la ukali dhidi ya makwazo, na hasa kuwakwaza walio wadogo, sio wadogo kwa umri bali wadogo katika imani. Kikwazo ni kile kinachotupelekea kujikwaa, ni jiwe linalotupelekea kuanguka, kushindwa kusonga mbele katika safari yetu ya imani. Kikwazo kwa lugha ya Kigiriki ni “skandalon”, likiwa na maana ya jiwe la kujikwaa tunapokuwa njiani au safarini, hivyo ni kipingamizi au kizuizi katika kusonga mbele.

Na tunaweza kuona mara moja kikwazo kikubwa katika maisha yetu ya ufuasi ndio kile ambacho Yesu ametukumbusha katika Dominika iliyopita, ya kutaka kuwa nafasi ya kwanza, ya kutaka kutumikiwa na sio kutumikia wengine. Ndio makwazo ya majivuno na kujikweza katika maisha yetu, kishawishi cha kutaka kuwatawa wengine, cha kuwatumia na kuwatumikisha wengine badala ya kuwa wadogo na watumishi. Sehemu ya mwisho ya Injili ya leo, inatuonesha pia upande mwingine wa makwazo ni ile inayotoka ndani mwetu, ndani ya kila mmoja wetu. Ndio makwazo yatokanayo na mikono, miguu na macho yetu. Ndio mwaliko wa kukata yale yote yanayotukwaza au yanayotupelekea kushindwa kuishi kweli za Injili. Na ndio tunaona Yesu anatumia lugha ya picha yenye kutisha, sio ili tutishike na kuogopa kwani Neno na Ujumbe wake daima ni Habari njema ya wokovu wetu, lakini anatumia lugha ile kutuonesha umuhumi wa kuwa macho dhidi ya vilema na yale yote yanayotupelekea kuharibu maisha yetu, mahusiano yetu na Mungu na jirani.

Ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kuingia ndani mwake na kujitafiti na kuona ni wapi anapaswa kufanyia kazi zaidi, ni wapi anapaswa kukata na kutupa, ndio kutokujishikamanisha na kila aina ya kilema au jiwe linalotupelekea kujikwaa na kushindwa kusonga mbele katika safari yetu ya utakatifu. Kama ni mguu, mkono au jicho basi hatuna budi kuling’oa na kulikata, ndio mwaliko wa kuwa macho kwa maisha yetu ya kiimani. Daima hatuna budi kutambua hatuwezi kutenda kadiri ya Injili kwa akili na uwezo wetu peke yetu bali daima kwa msaada wa neema zake Mwenyezi Mungu, hivyo hatuna budi kumuomba atujalie neema zake ili zitusaidie katika safari yetu.Nawatakia Dominika na tafakari njema.

22 September 2021, 08:08