Tafuta

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Tamko la Mwanza 2021 ni kuhusu mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Tamko la Mwanza 2021 ni kuhusu mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. 

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Tamko la Mwanza 2021

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mkutano wake wa Mwanza limezindua maandalizi ya Mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA utakaofikia kilele chake mwezi Julai 2022. Limezindua maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu katika ngazi ya Kijimbo kwa Jimbo; Jubilei ya Miaka 50 ya Hospitali ya Rufaa Kanda ya Bugando na Uchaguzi wa viongozi wa TEC: Tamko la Mwanza!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC., katika mkutano wake uliofanyika Jimbo kuu la Mwanza limezindua Maandalizi ya Maadhimisho ya Mkutano Mkuu wa 20 wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Tanzania ndiye mwenyeji wa Mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA utakaofikia kilele chake mwezi Julai 2022. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, katika maadhimisho haya, aliwashukuru viongozi wa AMECEA kwa kuichagua Tanzania kuwa ni mwenyeji wa mkutano mkuu wa 20 wa AMECEA, ambao kwa sasa watanzania wanausubiri kwa hamu kubwa. Dhamira kuu ya mkutano huu ni jukumu la kutunza mazingira kwani athari zake ni kubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Maandalizi ya mkutano huu ni jukumu la watu wa Mungu nchini Tanzania, ili wageni watakapofika na hatimaye kurejea nchini mwao waweze kukiri kwamba, kwa hakika wameonja wema na ukarimu wa watu wa Mungu nchini Tanzania; wameshuhudia imani hai; umoja na mshikamano wa watu wa Mungu.

Askofu mkuu Nyaisonga anasema, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote ni mchakato unaowadai waamini kuinjilika ili waweze kuinjilisha kwa kuwa na mtazamo na mwelekeo mpya kuhusu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Maandalizi haya yanakwenda sanjari na sala maalum ya AMECEA, ili mkutano huu uweze kupata kibali cha baraka na amani inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Mishumaa ya AMECEA iwe ni mwanga mpya katika maisha na utume wa waamin. Maadhimisho haya yalifanyika kwenye Kituo cha Hija cha Bikira Maria wa Kawekamo Jimbo Kuu Katoliki la Mwanza. Ndiyo maana maamuzi yaliyofanyika huko kwa mwaka 2021 yanaitwa Tamko la Mwanza! Tukio hili limenogeshwa pia na uzinduzi wa Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu katika ngazi ya Jimbo kuu la Mwanza pamoja na kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Kanisa kuu la Jimbo kuu la Mwanza ulioanzishwa na Hayati Askofu mkuu Anthony Petro Mayala. Ukaendelezwa na Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi na sasa ni zamu ya Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wa matashi mema kwenda kwa Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, aliwapongeza watu wa Mungu nchini Tanzania kwa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando, BMC.

Baba Mtakatifu aliungana na watanzania wote kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa matunda maridhawa yanayotokana na huduma mbalimbali za afya na elimu na kwa namna ya pekee katika miezi ya hivi karibuni katika mapambano dhidi ya janga la Ugonjwa wa Virusi vya Korona, UVIKO-19 ambalo kwa sasa ni janga la afya duniani na watu wameathirika kwa viwango tofauti. Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania lilitumia fursa hii kufanya mabadiliko makubwa katika safu ya viongozi kwa kuwachagua wenyeviti wa Kamati, wenyeviti wa Idara, Wenyeviti wa Tume pamoja na Maaskofu wawakilishi kwenye Taasisi za: AMECEA, CUEA, Programu za CSSC, Maaskofu pia wamewateuwa Wakurugenzi pamoja na wakuu wa Idara. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga ndiye Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita ndiye Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, TEC. Wengine ni kama ifuatavyo:

Askofu mkuu Isaac Amani Massawe, Jimbo Kuu la Arusha, Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Kichungaji na Katibu wake ni Padre Florence Rutaihwa. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam: Mwenyekiti Kamati ya Huduma za Kijamii na Katibu wake ni Padre Paul Steve Chobbo. Askofu Anthony Lagwen, Jimbo Katoliki la Mbulu, Mwenyekiti Kamati ya Fedha na Rasilimali Watu na Katibu wake ni Bwana Erick Mwelula. Askofu Augustine Ndeliakyama Shao, Jimbo Katoliki la Zanzibar Mwenyekiti Kamati ya Ukaguzi na Maadili na Katibu wake ni Padre Daniel Dulle. Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa wa Jimbo Katoliki Mpanda, Mwenyekiti Idara ya Mawasiliano na Katibu wake ni Padre Chesco Peter Msaga, C.PP.S.

WAKUU WA IDARA: Askofu Simon Chibuga Masondole wa Jimbo la Bunda, Mwenyekiti Idara ya Liturujia. Askofu Edward Mapunda Jimbo Katoliki la Singida, Idara ya Utume wa Walei na Katibu wake ni Padre Florence Rutaihwa. Askofu Msaidizi Stephano Lameck Musomba, Idara ya Katekesi na Katibu wake ni Padre Liston Lukoo. Askofu mkuu Isaac Amani Massawe, Jimbo Kuu la Arusha, Mwenyekiti Idara ya Kichungaji na Katibu wake ni Padre Florence Rutaihwa. Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande, Jimbo kuu la Mwanza, Idara ya Afya na Katibu wake ni Padre Paul Chobbo. Askofu Flavian Matindi Kassala wa Jimbo Katoliki la Geita, Idara ya Elimu. Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwa’ichi wa Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Tume ya Uadilifu wa Uumbaji, Haki na Amani na Katibu wake ni Dr. Cammilus Kassala. Caritas Tanzania: Ms Masho Mpokoma.

Askofu Eusebius Alfred Nzigilwa wa Jimbo Katoliki Mpanda, Idara ya Mawasiliano ya Ndani na Katibu wake ni Padre Chesco Peter Msaga, C.PP.S. Askofu Bernardin Mfumbusa, Jimbo Katoliki la Kondoa, Idara ya Mawasiliano ya Nje na Katibu wake Padre Chesco Peter Msaga. Idara ya Mawasiliano ambayo ina umuhimu wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa bado inaendelea kusukwa ili iweze kuhudumiwa na Maaskofu watatu: Mawasiliano ya Mitandao, Mawasiliano Analogia na Mawasiliano ya Televisheni: Askofu Titus Joseph Mdoe, Jimbo Katoliki la Mtwara. Padre Adalbert Donge, Idara ya Ushuru na Usafirishaji. Askofu Anthony Lagwen, Jimbo Katoliki la Mbulu, Idara ya Fedha na Katibu wake ni Bwana Erick Mwelula. Askofu Msaidizi Methodius Kilaini, Rasilimali watu. Askofu Beatus Urassa ALCP/OSS- Jimbo Katoliki Sumbawanga, Usimamizi wa Mali na Manunuzi na Katibu wake ni Alfred Kwene. Askofu Lazarus Vitalis Msimbe, S.D.S., Uwekezaji. Askofu Josefu Roman Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma, Maadili. Askofu Titus Joseph Mdoe, Jimbo Katoliki la Mtwara: Utambulisho wa Kikatoliki na Dhamira Katika Taasisi za Kitaifa, TEC.

Maaskofu waliochaguliwa katika Tume Mbalimbali ni pamoja na: Askofu  Msaidizi Henry Mchamungu, Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tume ya Sheria za Kanisa na katibu wake ni Padre Daniel Dulle. Askofu Rogath Kimaryo, Tume ya Masuala ya Kisheria, Katibu wake ni Padre Daniel Dulle. Askofu Josefu Roman Mlola wa Jimbo Katoliki Kigoma, Tume ya Mapadre na Waseminari wakuu na Katibu wake ni Padre Jovitus Mwijage. Askofu John Chrisostom Ndimbo Jimbo Katoliki la Mbinga, Tume ya Majadiliano ya Kidini na Katibu wake ni Padre Christian Likoko. Askofu Prosper Lyimo, Tume ya Majadiliano ya Kiekumene na Katibu wake ni Padre Sigfrid Rusymbia. Askofu Filbert Felician Mhasi Jimbo Katoliki la Tunduru-Masasi, Mwenyekiti Tume ya Utamaduni.

Askofu Michael George Mabuga Msonganzila wa Jimbo Katoliki la Musoma, Utume wa Familia na Katibu wake ni Padre Novatus Mbaula. Askofu mkuu Damian Denis Dallu wa jimbo kuu la Songea Tume ya Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, PMS., Katibu wake ni Padre Jovitus Mwijage na Padre Alfred Kwene. Askofu mkuu Beatus Kinyaiya, Jimbo kuu la Dodoma, Tume ya Watawa na Maisha ya Wakfu. Askofu Ludovick Joseph Minde, ALCP/OSS wa Jimbo Katoliki Moshi, Tume ya Taalimungu na Katibu wake ni Victor Tumaini. Askofu Liberatus Sangu, Jimbo Katoliki la Shinyanga, Tume ya Wahamiaji na Wahamaji. Askofu Almachius Rweyongeza Mwenyekiti wa Tume ya Magereza na Vikosi vya Ulinzi na Usalama.

Maaskofu Wawakilishi: Askofu Rogath Kimaryo, C.S.S.P, atawawakilisha Maaskofu Katoliki Tanzania kwenye Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na Kati, AMECEA. Askofu Bernardin Mfumbusa, CUEA. Askofu mkuu Gervas John Mwasikwabhila Nyaisonga, mwakilishi CSSC-Fedha; Askofu mkuu Renatus Leonard Nkwande, CSSC-Programu. Itakumbukwa kwamba, Padre Charles Kitima na Padre Chesco Peter Msaga, C.PP.S., ndio walioteuliwa kuwa Katibu mkuu na Msaidizi wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.

Tamko la Mwanza
30 November 2021, 15:59