Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio: Andaeni Njia ya Bwana! Tafakari ya Neno la Mungu Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio: Andaeni Njia ya Bwana! 

Dominika ya Pili Kipindi Cha Majilio: Tayarisheni Njia ya Bwana

Ni jangwani ndipo waliweza kujiunda kama Taifa na huko kupata majifunzo na kubaki na yale ya msingi tu. Na pia kuishi kwa ushirika na udugu wa kibinadamu na hivyo kuweza kushirikishana yale waliyokuwa nayo kwa upendo na udugu. Ni wakati wa jangwani haswa walijifunza moja kubwa na muhimu ni katika kujikabidhi mikononi mwa Mungu pekee. Ni kipindi cha matumaini!

Na Padre Gaston George Mkude, - Roma.

Amani na Salama! Mwinjili Luka 3:1-6 katika utangulizi wa sehemu ya Injili ya leo, anaanza kwa kutupatia matukio ya kihistoria. Ni kwa njia hii inatupa urahisi kuweza kujua ni lini kwa hakika Yesu Kristo alianza utume wake hadharani katika nchi ile takatifu. Ni kwa njia hiyo ya kutaja matukio ya kihistoria tunajua kuwa anachoeleza Mwinjili Luka sio hadithi za kusadikika, au masimulizi ya ngano, bali ni matukio halisi, tunayoweza kuyapata hata katika historia ya Taifa lile la Israeli wakiwa chini ya utawala wa Kirumi. Hivyo uwepo wa Yesu Kristo ulimwenguni ni ukweli wa kihistoria usiokuwa na mashaka yeyote. Ni Mungu wa milele anayeingia katika historia ya mwanadamu. Zaidi ya kutuambia ni kipindi gani katika historia, pia Mwinjili Luka anatutajia hata na majina ya watawala mbalimbali wa nyakati zile iwe wa utawala wa Kirumi waliokuwa wapagani, na pia uongozi wa kidini kwa kuwataja makuhani wakuu wa wakati ule kama Ana na Kaifa.  Na ndio tunakutana na majina ya watu saba katika utangulizi wa sehemu ya Injili ya Dominika ya leo.

Namba saba katika Biblia ni ishara ya ukamilifu, ni namba kamili, ni kusema ni historia kamilifu ya mwanadamu, yenye uwakilishi kamilifu iwe ya watu wasiokuwa na dini au wapagani pamoja na ile ya Wayahudi ambao tayari walikuwa na dini na imani kwa Mungu mmoja. Ni kuonesha pia mwanzo mpya wa historia kwa ujio wake Masiha ambao hautabagua tena watu bali ni kwa ajili ya wanadamu wote. Ni mwanzo mpya katika historia ya mwanadamu. Ni mwanzo mkamilifu unaobeba watu wote. Ni Mungu anayeingia katika historia ya mwanadamu kwa njia ya Umwilisho wake Mwanae wa pekee, Bwana wetu Yesu Kristo. Wokovu ni kwa ajili ya Ulimwengu mzima bila kujali tofauti zetu mbali mbali. Ni baada ya utangulizi wake wenye taarifa za kihistoria ndipo Mwinjili Luka anamleta kwetu muhusika huyu Yohane Mbatizaji. Anatumia mtindo ule wa Agano la Kale; “Neno la Bwana likamjia…” ni aina ya maneno ya uandishi inayotambulisha daima manabii. Ni maneno yanayoakisi kuwa ujumbe wa Nabii ni wa Mungu mwenyewe, na kamwe si maneno yake. Nabii ni kinywa na msemaji wa Mungu kwa watu wake, ni mjumbe wa Habari Njema itokayo kwa Mungu mwenyewe.

Yote yanaanzia jangwani, sehemu ya upweke na hasa iliyokuwa na maana kubwa kwa watu wa Taifa lile la Israeli. Ni jangwani ndipo waliweza kujiunda kama Taifa na huko kupata majifunzo mengi.  Ni jangwani waliweza kujifunza kubaki na yale ya msingi tu. Kwani haikuwa rahisi kubeba kila kitu na kuepuka uzito usiokuwa wa lazima, hivyo kila mmoja alibaki na vitu vya msingi tu.  Na pia kuishi kwa ushirika na undugu na hivyo kuweza kushirikishana yale waliyokuwa nayo kwa upendo na undugu. Ni wakati wa jangwani haswa walijifunza moja kubwa na muhimu ni katika kujikabidhi mikononi mwa Mungu pekee.  Ni kipindi cha kumtumainia Mungu pekee. Hata katika nyakati za Yesu, bado baadhi ya Wanawaisraeli waliotaka kuiishi tena safari ile ya babu zao walijitenga na kwenda kuishi jangwani kama afanyavyo Yohane Mbatizaji. Ni kujitenga na maisha yale yasiozingatia machache ya msingi, kwa kujikita na kujishikamanisha na mambo mengi ya ulimwengu huu. 

Ni kwa kuishi jangwani waliachana na maisha ya uovu, uonevu na ya kukosa haki na kila aina ya ubaya. Ni kwa kuishi jangwani waliweza pia kuishi kile walichopitia babu zao, safari ile ambapo Mungu alijifunua kwao na kuweka nao agano la kuwa daima Mungu wao. Hivyo kurudi jangwani ni kutaka kuishi kiaminifu Agano lile na Mungu. Kipindi cha Majilio, ni mwaliko kwetu pia kwenda jangwani, kujaribu kujitenga na malimwengu, kubaki na yale machache yanayokuwa ya msingi na ya ulazima na umuhimu katika maisha yetu. Ni kutoka katika malimwengu ili tuweze kupata nafasi ya kubaki na Mungu, ya kumsikiliza na hata ya kumweleza hali zetu na mapambano yetu ya ndani kabisa. Majilio ni kipindi cha kurejea na kutaka kuyaishi tena kiaminifu maagano yetu tuliyoyaweka siku ile ya Ubatizo wetu. Na ndio baadhi ya wataalamu wa Maandiko wanaonesha kuwa yawezekana kabisa Yohane Mbatizaji alikuwa jangwani na Wamonaki wa Qumran. Ilikuwa ni jumuiya hasa ya wanaume wa Kiyahudi walioishi jangwani, ili nao waweze kuishi historia ya mababu zao waliokuwa jangwani kwa miaka ile 40 kabla ya kuingia nchi Takatifu, ni maisha ya matayarisho ya kuingia nchi Takatifu, ni wakati wa kukua kiimani na kujiachanisha na mambo yote yanayokuwa kinyume na mapenzi ya Mungu.

Ni kutokana na aina hii ya maisha hata baadhi ya mababa wa Wamonaki katika Ukristo waliiga na kuanzisha maisha ya jumuiya za Kitawa au ya Wamonaki katika Kanisa. Labda moja linalotushangaza pia tunaposoma Maandiko Matakatifu tunaona baba yake Yohane Mbatizaji, mzee Zakaria alikuwa ni kuhani aliyehudumu hekaluni: Na hivyo kushawishika kuwa na mwanawe pia angekuwa kuhani na kubaki hekaluni kumtumikia Mungu. Ila kinyume chake yupo jangwani akihubiri Ubatizo wa toba. Yohane Mbatizaji anajitofautisha sio tu na huduma ya baba yake bali hata na jamii nzima na hivyo kutaka kuleta mwanzo mpya unaoakisi Uwepo wa Mungu na hivyo kwenda na kuishi jangwani. Kwa kweli na ndio mwaliko kwetu leo pamoja na kuwa tunaishi ulimwenguni ila hatuna budi kuishi maisha ya jangwani. Ulimwengu unaokuwa na mengi maovu kinyume na mapenzi yake Mwenyezi Mungu, sisi tunaalikwa kwenda jangwani, kwa maana kuishi kadiri ya mapenzi ya Mungu. Kuishi kwa kushika Neno la Mungu na kukubali kuongozwa nalo. Kuishi kinyume na mantiki ya ulimwengu huu. Jangwani ni mahali ambapo tunakuwa na hakika ya kubaki kwa nafasi ya kwanza na Mungu mwenyewe, ni mahali ambapo tunaweza kujiachanisha na mengi yasiyokuwa ya msingi na maana katika maisha ya ufuasi.

Yohane Mbatizaji anafanya utume wake katika eneo la Mto Yordani, eneo la mpakani kati ya Nchi ile ya ahadi na mataifa ya kipagani. Bado ni mwaliko kama vile ili kuingia nchi ya ahadi, Wanawaisraeli walipaswa kuvuka kupitia mto Yordani na hivyo kwa njia ya Ubatizo wa toba wanaalikwa kuanza maisha mapya, kuacha maisha ya kale, maisha ya uovu na kuanza maisha kwa kumfuata huyu Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu. Ni mwaliko wa kubadili kichwa, kwa Kigiriki ni lile neno μετανοια (metanoia – likimaanisha hasa kubadili namna za kufikiri, kubadili kichwa na kuvaa kichwa kipya kwa maana namna zetu za maisha hazina budi kuwa na mwelekeo mpya). Wakati Nabii Baruki anatuonesha kuwa wokovu unatoka kwa Mungu, ni kwa njia ya neema na upendo wake. Nabii Isaya kama anavyonukuliwa na Mwinjili Luka anatuonesha wajibu wetu pia kama wanadamu. Na ndio kunyoosha njia na mapito ya Bwana na kufukia mabonde. Ni lugha ya picha inayotumiwa pia na Nabii Isaya aliyekuwa anawaalika Wanaisraeli, walikuwa wanahimizwa kurudi katika nchi yao ya ahadi baada ya kuchukuliwa mateka ya Babeli. Ni mwaliko wa faraja na matumaini kama ijulikanavyo sehemu ya pili ya kitabu cha Nabii Isaya, ni kitabu cha faraja kwani sasa wanaalikwa kurudi katika nchi yao takatifu na kuwa huru tena kiimani na hata kisiasa.

Milima na vilima ndio kiburi chetu, ukorofi wetu na hata kujikweza kwetu na kutaka kuwatawala wengine. (Rejea Isaya 2:11-17) Namna hizi za maisha ni kinyume na ufalme wa Mungu. Mabonde ya kufukiwa ndio unyonyaji wa kiuchumi unaotawala ulimwengu wetu ambao nabii anatualika kuachana nao kwa kujaza mabonde hayo na kuwa watenda haki na wenye kuguswa na shida za wengine. Na njia zilizopinda ndio maisha yetu yasiyoakisi Injili, Habari Njema ya Wokovu wetu, hivyo tunaalikwa kunyoosha njia zetu kwa maana ya maisha yetu. (Rejea Ezekieli 18:23) Metanoia anayoihubiri Yohane Mbatizaji ni mabadiliko ya dhati ya ndani kwa kila mmoja wetu katika kipindi hiki cha majilio wakati tunajiandaa kumpokea Mtoto Yesu anayetaka kuzaliwa katika maisha na nafsi ya kila mmoja wetu. Ni kwa kuwa na kichwa kipya, kwa maana ya kubadili namna zetu za kufikiri na kuenenda katika ulimwengu huu, kukubali kwenda jangwani ili kuachana na yale yote yasiyofaa katika ulimwengu huu. Ni kujitenga na namna za kiulimwengu kwa kuwa na maisha yanayoakisi kuwa kweli sisi tu Wabatizwa, ni wana wa Mungu, tuliofanyika upya kwa kushiriki fumbo la Bwana wetu Yesu Kristo, yaani mateso, kifo na ufufuko wake. Tumekufa pamoja naye kwa kuifia dhambi na kufufuka pamoja naye kwa kuwa na maisha mapya kwa kushiriki utakatifu wake.

Katika Biblia yetu tunasoma kila mtu atauona wokovu wa Mungu katika aya ile ya 6. Ila Biblia ya Kigiriki inatumia neno kila nyama, Nyama katika muktadha wa Biblia sio tu kutaka kuonesha sehemu ya mwili wa mwanadamu bali kuonesha mwanadamu mzima na madhaifu na mapungufu yake, ni sawa na kusema mwanadamu dhaifu, anayeweza kuugua na hata kufanya makosa na madhambi: Ila sasa Mungu mwenyewe anatoa ahadi kuwa pamoja na uduni na udhaifu wa mwanadamu bado atauona Utukufu wa wokovu wake. Ni ahadi ya Mungu kwa kila mwanadamu. Ni ujumbe wa faraja na matumaini kwa kila mmoja wetu. Mwinjili Luka kama tusomavyo ni Injili inayoakisi WEMA NA HURUMA YA MUNGU, na ndio maana tangu mwanzoni anakazia juu ya wema na huruma ya Mungu. Unabii wa Mzee Simeoni pia (rejea Luka 2:30-32) kuwa macho yake yameuona wokovu wake ulioandaliwa kwa ajili ya watu wote. Ni unabii unaoakisi wema na huruma ya Mungu sio tu kwa taifa moja la Israeli bali kwa watu wote ulimwenguni. Na kwa kweli Injili ya Luka tunaona ni Injili jumuishi, kuwa Wokovu wa Mungu ni kwa ajili ya watu wote bila ubaguzi wa aina yeyote.

Ni mwaliko kwetu sote kuushiriki kwa kuamua kubadili vichwa na namna zetu za maisha. Majilio ni kipindi cha kusubiri ujio wake Bwana na Mkombozi wetu aliyekuja kwetu kihistoria miaka elfu mbili iliyopita, anayebisha hodi kila siku kutaka kuingia katika maisha ya kila mmoja wetu na pia atakayekuja tena siku ile ya kuhukumu wazima na wafu. Majilio ni kipindi cha kukesha, ni kipindi cha matayarisho lakini zaidi sana kinachotualika kuwa tayari daima kwa kuishi maisha ya urafiki na Mungu na jirani, ndio maisha ya neema na utakatifu. Nawatakia Dominika na tafakari njema na maandalizi mema ya kuisherehekea Noeli, yaan Fumbo lile la Kihistoria la Umwilisho wake Bwana wetu Yesu Kristo.

30 November 2021, 15:32