Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio: Tema kuuu ni toba na wongofu wa ndani. Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya Pili ya Kipindi cha Majilio: Tema kuuu ni toba na wongofu wa ndani. 

Dominika ya Pili Kipindi cha Majilio: Toba Na Wongofu wa Ndani

Safari yetu ya majuma manne ya Kipindi cha Majilio inaingia katika juma la pili. Liturujia ya dominika hii ya pili inamweka mbele yetu Yohane Mbatizaji na mwaliko wake wa toba wa wongofu wa ndani. Yohane anafanya hivyo kwa kuhubiri ubatizo wa toba na kutoa mwaliko wa kuitengeneza njia ya Bwana na kuyanyoosha mapito yake. Ubatizo ni mlango wa imani na Sakramenti za Kanisa.

Na Padre William Bahitwa, - Vatican.

UTANGULIZI: Dominika ya pili ya Majilio. Safari yetu ya majuma manne ya Kipindi cha Majilio inaingia katika juma la pili. Liturujia ya dominika hii ya pili inamweka mbele yetu Yohane Mbatizaji na mwaliko wake wa toba wa wongofu wa ndani. Yohane anafanya hivyo kwa kuhubiri ubatizo wa toba na kutoa mwaliko wa kuitengeneza njia ya Bwana na kuyanyoosha mapito yake. Tuyaangalie kwanza kwa kifupi masomo yote matatu ya Misa ya dominika hii kabla ya kuuangia kwa undani mwaliko wa Yohane Mbatizaji kuhusu toba na wongofu wa ndani. MASOMO KWA UFUPI: Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha nabii Baruku (Bar. 5, 1-9). Kwa kifupi kabisa, somo hili linatangaza kuwa “baada ya dhiki, faraja”. Dhiki inayozungumzwa ni ile ya utumwa walioyokuwa nayo Waisraeli zamani zile za Babeli. Faraja inayoahidiwa ni wokovu wa Mungu. Wokovu unaojionesha kwa kuwatoa utumwani na kuwarudisha nyumbani. Ujumbe huo huo unatangazwa kwetu leo, kwamba Mungu hajaacha kuwapa faraja wote wale walio katika dhiki lakini hawachoki kumtumainia.

Somo la pili ni kutoka Waraka wa Mtume Paulo kwa Wafilipi (Fil. 1:4-6, 8-11). Katika somo hili tunayasikia maneno haya ya Paulo kwa Wafilipi; “niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeianzisha kazi njema mioyoni mwenu, ataikamilisha hata siku yake Yesu Kristo”. Kazi njema anayozungumzia Paulo ni imani, ambayo wafilipi waliipokea kwa ubatizo. Imani sio fadhila ya kuipokea halafu basi inaishia hapo, hapana. Ni fadhila ambayo inahitaji kukua siku hadi siku hadi ifikie ukamilifu wake ambao ni kumuwezesha muumini kuufikia uzima wa milele. Hii ndiyo kazi njema ambayo sisi sote waamini tunahitaji kuifikisha katika ukamilifu wake kwa msaada wa Mungu. Somo la Injili, kutoka mwinjili Luka (Lk. 3:1-6) ndilo linalotupatia mwaliko wa Yohana Mbatizaji. Ni kama linatuambia kuwa ili kujiandaa vema kumpokea Kristo ni lazima turudi nyuma tukauanze upya ubatizo wetu. Maana ni kwa njia ya ubatizo tuliianza safari yetu ya wongofu, sasa inabidi turudi kuianza tena upya safari hiyo ili tuwe tayari daima kwa ujio wa pili wa Bwana wetu Yesu Kristo.

TAFAKARI YA JUMAPILI: Injili inamtambulisha Yohane Mbatizaji kwanza kabisa kwa kueleza aliishi kipindi gani katika historia. Inataja kuwa ni mwaka wa 15 wa utawala wa Kaisari Tiberio na inataja pia viongozi waandamizi waliokuwapo, viongozi waliotawala maeneo mbalimbali ya uyahudi. Sasa wakati watawala hao wakitajwa pamoja na ukuu wao wote pamoja na majumba yao ya kifahari ya kifalme, Yohane yeye anatajwa kuwa alikuwa jangwani. Na Neno la Mungu linapokuja, haliendi mahala pengine popote isipokuwa jangwani aliko Yohane Mbatizaji. Hapa kuna ujumbe mzito tunaopewa sisi ambao mara nyingi tunatafuta kuisikia sauti ya Mungu katika nyakati mbalimbali za maisha lakini hatuisikii. Kinachozungumwa hapa sio nyumba kama nyumba au mahala tunapoishi. Kinachozungumwa ni kile kinachousonga moyo na kuzuia kusikia sauti ya Mungu. Jangwa linawakilisha mahala pa utupu, na hivi kutukumbusha kuwa hata sisi kama tunahitaji kulisikia Neno la Mungu katika mioyo yetu ni lazima tuipeleke mioyo yetu jangwani, yaani tuiweke huru dhidi ya vurugu za kila siku za maisha na tuiondolee mambo yanayouchanganya na kuukosesha utulivu.

Yohane Mbatizaji anahubiri ubatizo wa toba. Ubatizo ndio mlango wa kuipokea imani na ndio mwanzo wa safari ya wongofu. Ni kwa njia ya ubatizo mtu anasema “naam” kwa mwaliko wa Mungu. Sasa kama alivyotufundisha mtume Paulo katika somo la pili, huu ubatizo hatuupokei tu halafu inaishia hapo. Ni mwitikio endelevu unaohitaji kufanywa upya tena na tena katika maisha yetu. Ni hivyo hivyo hata kwa anayepokea sakramenti ya Daraja, anayefunga nadhiri za kitawa na anayefunga ndoa Takatifu. Vyote hivyo vinaalika mwitikio unaohitaji daima kufaywa upya. Kinyume chake ni kukaribisha kuchoka katika safari ya imani, kupoteza ladha ya kusonga mbele na wakati mwingine kupoteza kabisa mwelekeo na kubaki kuwa “mkristo jina”. Huu ndio ujumbe anaotupatia Yohane Mbatizaji akisema “itengenezeni njia ya Bwana, yanyoosheni mapito yake.” Kipindi hiki cha Majilio ni kipindi mahsusi cha kurudi nyuma, kujitazama, kujikosoa na kujipa nguvu ili kuuendea kwa matumaini wokovu wa Mungu tulioahidiwa. Nawatakia kipindi chema cha Majilio.

Liturujia J2 Majilio

 

03 December 2021, 17:11