Tafuta

Dominika VI ya Kipindi cha Pasaka: Umoja na mshikamano ni matunda na kazi ya Roho Mtakatifu mhimili mkuu katika mchakato wa Uinjilishaji unaofumbatwa kwenye ushuhuda. Dominika VI ya Kipindi cha Pasaka: Umoja na mshikamano ni matunda na kazi ya Roho Mtakatifu mhimili mkuu katika mchakato wa Uinjilishaji unaofumbatwa kwenye ushuhuda.  (Vatican Media)

Dominika VI ya Kipindi Cha Pasaka: Mtaguso Wa Kwanza Wa Yerusalemu: Roho Mtakatifu

Kanisa Katoliki ni moja na Muasisi wake ndiye Yesu Kristo, Nafsi ya pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kiongozi wake mkuu ni Baba Mtakatifu khalifa wa Mtume Petro ambaye Kristo alilijenga Kanisa juu yake na mafundisho yake ya kiimani, kimaadili, kiliturujia yote ni mamoja. Alama hii ya umoja wa Kanisa inajidhihirisha wazi tangu nyakati za Mitume kwa maongozi ya Roho Mtakatifu.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 6 ya Pasaka. Masomo ya Dominika ya VI yanasisitiza juu ya fundisho la kuwa; Kanisa Katoliki ni moja maana yake Mwanzilishi ni mmoja ndiye Yesu Kristo Nafsi ya pili katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Kiongozi wake mkuu duniani ni mmoja ndiye Baba Mtakatifu khalifa wa Mtume Petro ambaye Kristo alilijenga Kanisa juu yake na wala milango ya kuzimu haitalishinda, mafundisho yake ya kiimani, kimaadili, kiliturujia yote ni mamoja. Alama hii ya umoja wa Kanisa inajidhihirisha wazi tangu nyakati za Mitume kwa maongozi ya Roho Mtakatifu, atokaye kwa Baba na Mwana anayeabudiwa na kutukuzwa na Baba na Mwana milele yote. Somo la kwanza la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 15:1-2, 22-29); ni maamuzi na mafundisho yaliyotolewa na Mitume na wazee wa Kanisa katika mkutano wa Yerusalemu wakiongozwa na Roho Mtakatifu kuhusu masharti ya kuwapokea wapagani katika Kanisa kwamba; wapagani wenye nia thabiti ya kuwa wakristo hawalazimishwi kutahiriwa na kushika Torati yote ya Wayahudi. Wokovu wao hutegemea imani yao katika Kristo na sio katika Torati kama walivyodai Wayahudi na kuwafundisha wapagani ya kwamba, “Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka”.

Katika jamii nyingi Jando kwa watoto wa kiume lilifanyika mara umri wa kubalehe ulipofika. Jando lilikuwa ni moja ya madhehebu ya kumwingiza mtoto wa kiume katika rika la vijana – mtu mzima mwenye wajibu na haki katika ukoo. Katika madhehebu yaliyoambatana na tukio hili kulikwa na mafundisho ya maisha ya ndoa kumuandaa kijana kwa maisha ya ndoa na familia. Kwa wayahudi, jando lilikuwa tendo takatifu, la kidini, ishara ya Agano la Mungu na taifa teule la Israeli. Madhehebu ya tendo hili yalifanyika siku ya 8 baada ya mtoto kuzaliwa ambapo mtoto alipewa jina kama ilivyokuwa kwa Mtoto Yesu (Lk 2:21) licha ya kuwa Ibrahamu baba wa imani alitahiriwa katika uzee wake yeye na watu wa nyumba yake (Mwa 17:9-14, 23-27). Kutokutahiriwa kwa wayahudi ilikuwa ni sawa na kutokushirikishwa katika Agano kati ya Mungu na Israeli, na kutokushirikishwa katika Ahadi za Mungu kwa Abrahamu na uzao wake wote. Walioongokea dini ya Kiyahudi ili washiriki katika ibada, mikutano, milo hususani wakati wa Pasaka walipaswa kutahiriwa (Kut 12:48). Walipotwaliwa na mataifa ya kigeni, na kukatazwa kuyaishi mapokeo yao ya kidini, Wayahudi wacha Mungu walikuwa tayari kufa kuliko kuyavunja na kuyapuuza mapokeo yao (1Mak 1:51, 60, 63; 6:10).

Wayahudi waliheshimu sana Agano kati yao na Mwenyezi Mungu
Wayahudi waliheshimu sana Agano kati yao na Mwenyezi Mungu

Katika hali hii, Wayunani (Wayahudi walioongokea Ukristo) walioona taabu sana kuwapokea Wapagani/watu wa matifa walioongokea Ukristo pasipo kushika mapokeo na sheria ya Musa hasa kutahiriwa wakisema hakuna sheria yoyote ya Musa itakayopunguzwa wala kuachwa, na kwamba ikiwa wapagani wanaongokea Ukristo, sharti waishike Sheria ya Musa na Sheria ya Kristo katika Ukamilifu wake. Hivyo waliwaambia wapagani; “Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka.” Nao wapagani/watu wa mataifa nao waliona shida kuacha tamaduni za ona kuyafuata mapokeo ya sheria za Musa ili kuongokea ukristo. Hivyo kukatokea malumbano na mtafaruku kwa Kanisa la Antiokia, hata likisukumwa na Roho Mtakatifu, lilituma wajumbe Yerusalemu ili walifikishe jambo hili kwa Mitume na wazee wa Kanisa. Wakiongozwa na Roho Mtakatifu Mitume na wazee walilipokea, wakaitisha mkutano wakajadili wakatoa suluhisho kuwa; Mbele za Mungu watu wote wanaokolewa kwa njia ya ubatizo, haijalishi ni Myahudi au Mpagani, mwanaume au mwanamke, wote wanakuwa familia moja ya Mungu ndani ya Kristo, tena wanapokea maisha mapya ndani ya Roho Mtakatifu, wote wakifanywa kuwa Wana wa Mungu na Ndugu (kaka na dada) wa Kristo, bila kuwa na tofauti au matabaka. Hivyo wapagani hawalazimiki kuzishika Sheria za Musa bali wajiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, wajiepushe na damu au nyama zilizosongolewa, wajiepushe na Uasherati.

Petro aling’amua fundisho hili alipoamriwa katika maono ale vyakula vivyokatazwa na Sheria ya Musa akiambiwaa; “Vilivyotakaswa na Mungu usiviite wewe najisi (Mdo 10:15), na aliposhuhudia jinsi Roho Mtakatifu alivyomshukia Kornelio na familia yake yote hata akasema: “Ni nani awezaye kukataza maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu kama sisi? (Mdo 10:47).  Naye Paulo katika safari zake za kimisionari baada ya kushuhudia Roho Mtakatifu akiwashukia watu Wayahudi na Wapagani alisema; “Hakika Mungu hana upendeleo, wote wanakubalika kwake.” Hivyo naye akafundisha kuwa sheria ya Musa ilikuwa muhimu kabla ya ujio wa Kristo. Kwa sasa tunaokolewa siyo kwa kuishika sheria ya Musa, bali kwa kuwa na imani kwa Yesu Kristo kwa kuiishi Amri ya mapendo. Yakobo, ndugu wa Yesu, mtu mcha Mungu na mshika Sheria ya Musa, akiongozwa na Roho wa Mungu, alisisitiza kwa; Wapagani walioongokea Ukristo hawalazimiki kuishika Sheria ya Musa, na Wayahudi waliomwamini Kristo wakipenda kuishika sheria ya Musa hakuna shida ili mradi sheria hiyo isiwe kikwazo cha mshikamano ndani ya jumuiya ya kikristo. Nao wapagani walioongokea Ukristo walipaswa kuachana na mambo yaliyokinyume na Imani ya Kikristo hasa kujiepusha na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, kujiepusha na damu au nyama zilizosongolewa, kujiepusha na Uasherati. Mitume waliandika barua kwa kila Jumuiya iliyoathiriwa na mvurugano ule, wakitaarifiwa juu ya maamuzi hayo wakisema; “Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo ya lazima” (Mdo 15:28). Maamuzi haya yalileta maridhiano, furaha, amani na utulivu kwa jumuiya zote.

Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa uinjilishaji mpya.
Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu wa uinjilishaji mpya.

Somo la pili la Kitabu cha Ufunuo (Ufu. 21:10-14, 22-23); ni ufunuo wa hatua za Fumbo la ukombozi jinsi Mungu alivyoliteua taifa la Israeli katika makabila yake kumi na mawili, jinsi alivyojidhihirisha kwao kwa njia ya hekalu na baadae kwa njia ya Mitume kumi na wawili aliowachagua Yesu ambao kwa njia yao Imani ya kikristo ikajengwa juu ya msingi yao. Katika maisha ya hapa duniani sisi wakristo tunahitaji bado hekalu, Kanisa - Mwili wa Kristo kama ishara ya uwepo wa Mungu; lakini mwishoni mwa nyakati wale watakaofika maisha ya utakatifu hawatahitaji tena hekalu sababu watamwona Mungu uso kwa uso katika utukufu wake. Injili ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 14:23-29); ni wosia wa Yesu akisistiza juu ya Amri ya Mapendo na ahadi ya Roho Mtakatifu kama msadidizi wetu katika kuiishi vyema Amri ya Mapendo ili Yesu mwenyewe, Mungu Baba na Roho Mtakatifu waweze kuwa nasi daima katika maisha yetu. Yeyote anayempenda Yesu kwa moyo wote ataweza kushika amri yake kuu ya mapendo. Moyo wa mtu huyo utajazwa na furaha kwani amani itokayo kwa Mungu Baba, Mungu Mwana na Mungu Roho Mtakatifu itakuwa naye daima. Katika somo hili Yesu anakamilisha ufunuo wa Utatu Mtakatifu kwamba katika Mungu mmoja kuna nafsi tatu; Mungu Baba nafsi ya kwanza ndiye muumbaji, Mungu mwana nafsi ya pili, ndiye Mkombozi na Mungu Roho Mtakatifu Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu ndiye anayeliongoza, kulisimamia, kuliimarisha na kulitakatifuza Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume.

Katika somo hili, Yesu anawahakikishia mitume uwepo wake kati yao, na mwanga wa kumtambua yeye katika: Kuishika na kuiishi Amri kuu ya Mapendo. Kwa kuishika Amri ya Mapendo, Yesu mwenyewe, Mungu Baba na Roho Mtakatifu watafanya maskani mioyoni mwao, na Kristo atakuwa mgeni wa kudumu maishani mwao. “Mtu akinipenda atalishika neno langu, na Baba yangu atampenda, nasi tutakuja kwake na kufanya maskani kwake.” Roho Mtakatifu, atawatunza na kuwa mwalimu na kiongozi wao. Atawafundisha na kuwakumbusha yote aliyofundisha Kristo, na kuwaongoza kufanya wanayopaswa kuyatenda. Baba, Mwana na Roho Mtakatifu wataijaza mioyo yao amani pekee ya Mungu - “Amani nawaachieni...niwapayo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo.” Atawajaza furaha ya kina ambayo haiwezi kuondolewa na huzuni au mateso ya aina yoyote hapa duniani. Nasi tumruhusu Roho Mtakatifu atuangaze na kutuongoza katika maisha yetu ili tuweze kutambua mambo tunayopaswa kufanya katika kuishuhudia imani yetu na yale ambayo tunapaswa kuyaepuka ili tuweze kuwa kweli wafuasi wa Yesu na mwisho tukaurithi uzima wa milele mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 6 Pasaka Q
10 May 2022, 15:27