Tafuta

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 26 ya Mwaka C wa Kanisa: Sikilizeni na kujibu kwa vitendo kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 26 ya Mwaka C wa Kanisa: Sikilizeni na kujibu kwa vitendo kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. 

Tafakari Dominika 26 ya Mwaka C wa Kanisa: Onjeni na Kujibu Kilio cha Maskini Kwa Vitendo

Mtakatifu Yohane paulo II anasema, “Upendo kwa wengine, na kwanza upendo kwa maskini, ambao Kanisa linamwona Kristo mwenyewe, unafanywa kuwa thabiti katika kukuza haki. Haki haitapatikana kamwe isipokuwa watu wamuone maskini, ambaye anaomba msaada ili kuishi, si kero au mzigo, lakini fursa ya kuonesha wema na nafasi ya utajiri zaidi." Upendo katika matendo!

Na Padre Kelvin Onesmo Mkama, Pozzuoli, Napoli, Italia.

Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa Kitume “Centesimus Annus” yaani “Maadhimisho ya mwaka wa 100 tangu kutolewa Waraka wa Kitume wa Rerum Novarum anasema, “Upendo kwa wengine, na kwanza upendo kwa maskini, ambao Kanisa linamwona Kristo mwenyewe, unafanywa kuwa thabiti katika kukuza haki. Haki haitapatikana kamwe isipokuwa watu wamuone maskini, ambaye anaomba msaada ili kuishi, si kero au mzigo, lakini fursa ya kuonesha wema na nafasi ya utajiri zaidi” (Centesimus Annus, namba 58). Anachosisitiza Mtakatifu Yohane Paulo II ndiyo kinachofundishwa leo katika masomo yetu. SOMO LA KWANZA: Amosi 6:1, 4-7. Nabii Amosi anatambulikana kama “Nabii ambaye ni mtetezi wa haki za wanyonge.” Ujumbe wake wa leo ni huu; “Ole wao wanaoishi maisha ya starehe ilihali hawaguswi na mateso ya watu wanyonge.” Amosi alihubiri kipindi ambacho taifa la Israeli lilikuwa limestawi kiuchumi na watu walikuwa na maisha mazuri. Hata hivyo uchumi unapostawi kunajitokeza makundi mawili: kundi linalonufaika (matajiri, wafanyabiashara na viongozi) na kundi linaloathirika (maskini na wanyonge). Kwa kuwa uchumi wa himaya ya kaskazini (Northern kingdom) ya Israeli ulikuwa mzuri, watu wengi (hasa matajiri na wenye madaraka) waliridhika na maisha ya malimwengu: hawakuwaza tena mambo ya dini wala kushika agano lao na Mungu, waliishi maisha ya anasa (walijenga majumba ya kifahari, walikula na kunywa vyakula na vinywaji vya gharama kubwa sana, walijipamba kwa marashi ya gharama na kukesha kwenye burudani za muziki kila uchao); waliwanyanyasa na kuwaibia watu maskini na hawakujihusisha kutatua mahangaiko/maumivu/mateso ya watu wanyonge/maskini. Watu wengi wenye uwezo walijitazama na kujifurahisha wenyewe ilihali wenzao wengi wanaishi maisha magumu yenye mahangaiko na mateso.  Hivyo, nabii Amosi anawaonya watu wa namna hii kuacha mwenendo wao mbaya vinginevyo Mungu ataleta taifa la kigeni liwatawale kama adhabu ya maovu yao.

Chakula ni kati ya mahitaji msingi ya binadamu, lakini kuna watu wanakufa kwa njaa
Chakula ni kati ya mahitaji msingi ya binadamu, lakini kuna watu wanakufa kwa njaa

Hawa matajiri na wenye uwezo wanaoonywa na Nabii Amosi si wengine bali ni mimi na wewe kwani tunaishi maisha mazuri ilihali wenzetu wanaishi maisha ya mateso/mahangaiko. Tena jambo baya zaidi tunatumia mali/karama/uwezo wetu kuwanyanyasa wanyonge na tena wakati mwingine utajiri wetu tumeupata kutokana na kuwaibia, kuwagandamiza na kuwanyonya watu maskini. Ni mara ngapi tumejipatia maisha mazuri kwa kutumia fedha za miradi iliyopaswa kuwasaidia watu maskini? Ni mara ngapi tumetumia uwezo/mali/karama zetu kuwanyanyasa wanyonge kwa kuwatumikisha kazi nzito kwa ujira mdogo au kwa kununua haki zao katika mifumo ya utoaji haki? Ni mara ngapi tunatumia kiasi kikubwa cha pesa kununua mavazi, vinywaji na vyakula vya gharama kubwa ilihali kuna yatima wanakosa pesa ya karo au wajane wanakosa mahitaji yao ya msingi? Ni mara ngapi tunalala kwenye nyumba za kifahari ilihali kuna ndugu zetu na hata wazazi wetu wa kutuzaa hawana makazi bora? Mafundisho makubwa kutoka somo letu la kwanza ni haya: (i) tunapobarikiwa kuwa na hali nzuri ya maisha ni vizuri kukumbuka kuwasaidia wengine ambao ni wanyonge, wahitaji na wasiojiweza. Tunapaswa kuonja na kushiriki mateso yao. (ii) tunapaswa kuwa na kiasi na nidhamu katika matumizi ya mali tulizopewa na Mungu. Tusitumie mali na utajiri kwa starehe, kwa kufanya kufuru, kwa majigambo, kwa anasa au uonevu dhidi ya wanyonge. Mafundisho haya tunayapata pia katika somo letu la Injili ya leo.

SOMO LA PILI: 1 Tim. 6:11-16. Nyaraka mbili za Mtume Paulo kwa Timotheo na nyaraka yake moja kwa Tito kwa pamoja huitwa “barua/nyaraka za kichungaji.” Hii ni kwa sababu Timotheo na Tito walikuwa ni wachungaji waliosimamia makanisa mahalia ya Efeso na Krete. Hivyo Paulo anawaandikia Timotheo na Tito kuwapa maelekezo ya namna ya kuongoza makanisa wanayoyasimamia na kutoa mfano bora kwa wale wanaowaongoza. Mtume Paulo, katika somo letu la pili, anamwandikia Timotheo kumwelekeza namna ya kutoa mfano bora wa maisha kama kiongozi wa kanisa. Paulo anamtaka Timotheo awe mtu wa haki, mchaji, mwenye kuishi imani na mapendo, mwenye saburi na upole. Ikiwa Timotheo ataishi fadhila hizi ataweza kutoa mfano bora kwa Kanisa analolisimamia (waamini anaowaongoza). Paulo anamtaka Timotheo awe shuhuda mwaminifu wa imani kama Kristo alivyokuwa shuhuda mwaminifu wa imani mbele ya Pilato. Maelekezo na mausia anayoyatoa Paulo kwa Timotheo yanatuhusu sisi sote kwani kila mmoja wetu analo kundi analoliongoza (Ofisi, familia, jamii, serikali, taasisi, chama, n.k) na hivyo anapaswa kuonesha mfano mzuri wa maisha ya fadhila kwa wale anaowaongoza. Tunapaswa kutoa mfano mzuri wa fadhila maana Kristo tunayemfuasa alitoa mfano mzuri wa imani thabiti, haki, mapendo, saburi na upole. Kwa bahati mbaya wengi wetu maisha yetu hayatoi mfano bora kwa wengine: hatutendi haki maana tunaminya haki za wengine (tunadhulumu mali za yatima na wajane, tunauza ardhi za wanyonge kwa matajiri, n.k); wengi wetu tumejaa chuki na fitina sehemu zetu za kazi badala ya kuonesha upendo na kuishi kidugu; wengi wetu hatuna imani thabiti kwani tumekuwa tukipeperushwa kiimani huku na kule kama makapi (mara kwa waganga, mara kutafuta miujiza na maombezi kwa wahubiri feki, n.k); tumekosa saburi (uvumilivu) tukutanapo na misukosuko ya maisha ya familia, misukosuko sehemu za kazi na changamoto za ndoa; wengi tumetawaliwa na hasira. Tuombe neema ya Mungu itusaidie kutubu na kumwongokea Mungu.

Kutokana na vita na majanga asilia, kuna watoto wanakufa kwa njaa.
Kutokana na vita na majanga asilia, kuna watoto wanakufa kwa njaa.

SOMO LA INJILI: Lk. 16:19-31 Yesu, katika Injili ya Dominika ya 26 ya Mwaka C wa Kanisa, anatufunulia ujumbe mzito kuwa “ili kuwa Wakristo wa kweli inatupasa kutambua, kuonja na kushiriki kujibu mahitaji ya wenzetu hasa wanyonge na wahitaji.” Katika kuelezea ukweli huu Yesu anatoa mfano wa tajiri na maskini aitwaye Lazaro. Huu ndio mfano pekee katika mifano ya Yesu ambapo mmojawapo wa wahusika anatajwa kwa jina, yaani Lazaro. Kwenye mfano huu kuna wahusika wawili: tajiri mmoja (ambaye hatajwi kwa jina) na maskini mmoja (ambaye anatajwa kwa jina la Lazaro). Hebu tuangalie wasifu/tabia ya kila mhusika ili tupate ujumbe uliokusudiwa kwa undani zaidi. Kwa upande mmoja kuna tajiri: tajiri alikuwa akivaa vazi la rangi ya zambarau na kitani safi. Mavazi haya yalikuwa mavazi yaliyovaliwa hasa na wafalme na makuhani wakuu, hivyo yalikuwa mavazi ambayo matajiri wachache tu wangeweza kuyanunua na kuyavaa. Hivyo mavazi haya yanaonesha kuwa huyu jamaa alikuwa tajiri kupita kiasi. Kadhalika tunaambiwa kuwa alikuwa akila sikuzote kwa anasa. Injili haisemi alikuwa anakula mara moja moja kwa anasa bali “sikuzote”. Labda tuone kwanza maana ya anasa: “anasa ni raha na starehe tele; anasa ni kitu kisichokuwa na umuhimu katika maisha ya mwanadamu.” Hivyo tajiri alikuwa akila sikuzote kwa anasa: aliishi maisha ya raha na starehe tele, alitumia pesa zake kwa mambo yasiyokuwa na umuhimu: vyakula na vinywaji vya gharama kubwa, mavazi ya bei mbaya. Kwa kifupi, kila siku kwake ilikuwa ni sherehe/sikukuu.

Kwa upande mwingine kuna maskini aitwaye Lazaro: hajiwezi kabisa (na ndiyo maana huwekwa na watu mlangoni pa nyumba ya tajiri), hana makazi (ndiyo maana hukaa/hulala mlangoni pa tajiri), ana vidonda vingi (hapati huduma ya matibabu), hutamani kula makombo yanayoanguka katika meza ya Tajiri (hapati huduma ya chakula bora), na mbwa (ambaye kwa Wayahudi ni mnyama najisi) huramba vidonda vyake. Haya ndiyo yalikuwa maisha ya Lazaro. Pamoja na kufahamu hali hii ya Lazaro, tajiri huingia na kutoka nyumbani kwake kila siku bila kuguswa na mateso/maumivu ya Lazaro licha ya kwamba alikuwa na uwezo na nafasi ya kumsaidia. Dhambi kubwa ya tajiri huyu ni kutotambua mahitaji, mahangaiko na maumivu ya mtu mwingine: hakutambua kuwa Lazaro anahitaji makazi mazuri, hakutambua kuwa Lazaro anahitaji chakula, hakutambua kuwa Lazaro anahitaji huduma ya matibabu ya vidonda vyake, hakutambua kuwa Lazaro anahitaji walau hata nguo ya kawaida itakayofunika vidonda vyake ili visirambwe na mbwa. Tajiri huyu alitenda pia “dhambi ya kutotenda kile alichopaswa kutenda” (he committed the sin of omission): alipaswa kuonesha upendo lakini hakuonesha; alipaswa kuwa mkarimu lakini hakuwa mkarimu; alipaswa kumhurumia Lazaro anayeteseka kwa njaa na magonjwa lakini hakuwa na huruma; alipaswa kutambua utu wa Lazaro lakini alimwona Lazaro kama mnyama tu. Haya aliyoshindwa kutenda ndiyo yanayomfikisha mahali pa mateso.

Majanga asilia ni chanzo cha umaskini, njaa na maradhi
Majanga asilia ni chanzo cha umaskini, njaa na maradhi

Injili inatukumbusha mambo makubwa mawili: (1) Tunapaswa kuguswa na kutatua mahitaji ya watu wengine. Ndugu zangu, huenda tukashawishika kumcheka na kumdharau tajiri huyu kwa alichotenda. Hata hivyo tukumbuke kuwa maisha, hulka na mwenendo wa tajiri huyo vinatuwakilisha mimi na wewe. Tajiri anayezungumziwa kwenye Injili yetu ni mimi na wewe: mara nyingi tunaishi maisha ya anasa, yaani tunatumia pesa kupita kiasi kwenye starehe (kukesha kwenye matamasha ya muziki, kukesha baa, kuvaa mavazi ya gharama kubwa, kujinafasi ndani ya magari ya kifahari, kuishi kwenye nyumba za kifahari, kufanya safari za nje ya nchi kwa lengo la “kula bata”, kuifurahisha miili yetu kwa pombe za bei mbaya, kutumia pesa nyingi kustarehe na wanawake, n.k) ilihali tunawapita maskini na wanyonge tulionao kana kwamba hatuwaoni. Ni wangapi wanakufa kwa kushindwa kulipia huduma za matibabu ilihali tuna uwezo wa kuwasaidia? Ni wangapi wanakufa kwa njaa ilihali sisi tunachezea vyakula na kuponda maisha na makahaba? Sisi nasi tunatenda dhambi ya kutojali mahitaji ya watu wengine, hasa maskini, wasiojiweza na wanyonge- tunatenda dhambi ya kutoguswa na mahangaiko/maumivu/mateso ya wenzetu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu kama tulivyo sisi. Mara nyingi tukiona wenzetu wanahangaika tunasema, “maisha yake hayanihusu mimi.” Dhambi hii ndiyo anayoikemea Nabii Amosi kwenye somo letu la kwanza kwani watu wa zama zake walifanya starehe, waliishi kwenye majumba ya kifahari, walilala kwenye vitanda vilivyopambwa kwa pembe za ndovu, walikesha kwenye burudani za nyimbo, walikula na kunywa vinywaji vya gharama kubwa ilihali hawaguswi/hawahuzunishwi kabisa na “mateso ya Yusufu” (neno “Yusufu” linawakilisha watu wa taifa la Israeli wa himaya ya kaskazini “Northern kingdom” maana chimbuko lao ni makabila mawili ya Efraimu na Manasse ambao ni watoto wa Yusufu.

Papa Francisko: Vipaumbele: Maskini, Mazingira na amani
Papa Francisko: Vipaumbele: Maskini, Mazingira na amani

Kwa hiyo neno “mateso ya Yusufu” linamaanisha watu wote wa Israeli ambao wanateseka kwa sababu mbalimbali). Kila mmoja anayo nafasi ya kushiriki maumivu/mateso ya wengine. Mtakatifu Mama Theresa wa Calcutta anasema, “Ikiwa huwezi kulisha watu mia, basi lisha walau mtu mmoja.” Kila mmoja wetu achague “mtu mmoja wa kulisha”. Kila mmoja wetu akitimiza jambo hili tutajikuta tunasaidia watu wengi kwa wakati mmoja. Tukumbuke kuwa kuna maisha baada ya kifo ambayo yanategemea namna tulivyohusiana na wenzetu hasa wahitaji. (2) Tunapaswa kuishi kile ambacho Neno la Mungu linatuasa na kutubidiisha. Tajiri anapomsihi Ibrahimu amtume Lazaro aende nyumbani kwa baba yake awaonye ndugu zake ili wasije nao wakapelekwa mahali pa mateso watakapokufa, Ibrahamu anamjibu akisema, “Wanao Musa na Manabii; na wawasilikize wao” na tena “Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishika hata mtu akifufuka katika wafu.” Maneno haya ya Ibrahimu yana maana kubwa sana. Kwa Wayahudi Musa anawakilisha sehemu ya kwanza ya Biblia yao ijulikanayo kama Torati au Sheria (vitabu vitano vya mwanzo katika Biblia ambavyo waliamini vimeandikwa na Musa) na sehemu ya pili ya Biblia ni vitabu vya Manabii na sehemu ya tatu, ambayo haijatajwa iliitwa Maandiko. Hivyo Ibrahimu ananuia kusema kuwa wasihangaike kusubiri mtu atoke katika wafu kuwakumbusha wajibu wao bali waiishi kile ambacho wameagizwa kwenye Neno la Mungu ili kuepuka kufika mahali pa mateso. Hata sisi tunakumbushwa kuwa ikiwa tutaishi kwa uaminifu Neno la Mungu tutaepuka kwenda mahali pa mateso baada ya kufa maana Neno la Mungu linahimiza kuwajali wengine na hasa maskini, wanyonge na waliotengwa na jamii, Neno la Mungu linakataza maisha ya starehe na anasa. Kwa ufupi Neno la Mungu linasisitiza upendo kwa Mungu na upendo kwa jirani. Kumbe hatuna sababu ya kusubiri watakatifu washuke toka mbinguni kutuhimiza mambo ya kufanya ilihali tunalo Neno la Mungu (Biblia) ambalo limeweka wazi yote tunayopaswa kufanya na tusiyopaswa kufanya ili kufikia uzima wa milele. Dominika njema

22 September 2022, 14:51