Tafuta

Ni dominika ya Neno la Mungu kama ilivyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Aperuit illis” ya 30 Septemba 2019 Ni dominika ya Neno la Mungu kama ilivyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Aperuit illis” ya 30 Septemba 2019  

Dominika ya Neno la Mungu: Ushuhuda: Mema, Hukumu na Haki

Dominika ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2023 inanogeshwa na kauli mbiu “hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo.” 1Yn 1:3. Juma la kuombea Umoja wa Wakristo linaongozwa na kauli mbiu “Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki” Isa 1:17.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 3 ya mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Ni dominika ya Neno la Mungu kama ilivyotangazwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Aperuit illis” ya 30 Septemba 2019 katika maadhimisho ya kumbukumbu ya miaka 1600 ya kifo cha Mtakatifu Hieronimo Jalimu la Maandiko Matakatifu. Baba Mtakatifu anatualika kulisoma, kulitafakari, kuliishi na kulifanya neno la Mungu taa ya maisha yetu. Dominika ya Neno la Mungu kwa Mwaka 2023 inanogeshwa na kauli mbiu “hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo.” 1Yn 1:3. Dominika hii inaadhimishwa wakati wa Juma la kuombea Umoja wa Wakristo na maadhimisho haya kwa mwaka 2023 yanaongozwa na kauli mbiu “Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki” Isa 1:17. Masomo ya dominika hii yanatualika kuepukana nafasi za dhambi na kujiweka chini ya utawala wa upendo wa Mungu. Maisha na maelekeo yetu yalenge kuingia katika ufalme wa Mungu. Ni utawala wa mwanga ambapo Mungu anakuwa yote katika yote. Somo la kwanza latoka katika kitabu cha Nabii Isaya (Isa 9:1-4). Nabii Isaya anawapa matumaini wana wa Israeli walipokuwa katika vita na ghasia vilisababisha wao kuona giza nene katika nchi yao na kufikiri kwamba Mungu amewasahau na kuwaacha.

Kristo Yesu ndiye Nuru ya Mataifa
Kristo Yesu ndiye Nuru ya Mataifa

Itakumbukwa kuwa baada ya wana wa Israeli kufika Palestina, Nchi ya Ahadi, Yoshua, Kiongozi aliyemrithi Musa, aliigawa ardhi ile kwa makabila 12. Makabila mawili ya Zabuloni na Naftali walichukua mkoa wa Galilaya upande wa Kaskazini. Kila mara eneo hili lilivamiwa na Waashuru (Waassyria), hasa maeneo ya Kaskazini (Mikoa ya Zabuloni na Naftali) na kuharibu kila uzuri wa vitu waliokuwa navyo katika miji yao na kuwachukua watu wake mateka na kuwafanya watumwa wao. Hivyo watu waliona kutoka Galilaya kuna giza nene lililofunika nchi yote ya Kaskazini na hatua kwa hatua lilikuwa likisambaa katika nchi yote ya Palestina – nchi ya ahadi. Roho wa Mungu, alimuongoza Nabii Isaya aone kutoka mbali Nuru inayoanza kuangaza Nchi ya Ahadi, na furaha ya pekee ikiijaza mioyo ya watu. Isaya analinganisha furaha hiyo na furaha ya watu wanaoenda shambani kuchukua mavuno yao, au furaha ya watu wanaogawanya nyara baada ya kuwashinda maadui wao. Ushindi huu unafananishwa na ushindi wa Gideoni dhidi ya Wamidiani akiwa na jeshi dogo tu la askari 300 (Waamuzi 7:16-25). Utakuwa ni ushindi wa mwisho, kwa kuwa silaha zote za maadui zitakuwa zimeharibiwa kabisa na Mateka wote wataachiliwa huru.

Lakini itakumbukwa kuwa ushindi huu mkubwa, furaha hii kuu, Nuru hii kuu inayowafikia watu wa Galilaya, aliyotabiri Isaya, haikutimia wakati wake. Kinyume chake, maadui wa Waisraeli waliendelea kuvamia na kuitawala nchi ile, mkoa mmoja baada ya mwingine, na hatimaye Yerusalemu ilibomolewa na kuachwa magofu. Giza nene kweli liliifunika nchi yote. Nuru inayong’aa iliyotangazwa na Isaya ilitokea na kusambaa katika Mkoa wa Galilaya, na kuijaza mioyo ya watu furaha kwa kuzaliwa kwa Yesu Kristo, Emanueli Mungu pamoja nasi. Kama ilivyokuwa kwa wana wa Israeli ndivyo inavyokuwa hata kwetu. Shida na mahangaiko katika maisha; umaskini, magonjwa, njaa, chuki na vita, yote haya yanaweza kutukatisha tamaa na kuona kama vile tuko kwenye giza nene na kuona shaka juu ya uwepo wa Mungu. Hali hii inatokea pale tunatenda dhambi na kujitenga na Mungu. Lakini Mungu daima yuko nasi hasa pale tunapoingia kwenye shida kubwa. Sisi tunapaswa kuwa na matumaini na kujikabidhi kwake na kutokuwa na hofu kwa kuwa yeye daima yuko upande wa wanaomtumainia.

Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki
Jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki

Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1Kor 1: 10-13, 17). Ni maonyo na mashauri ya mtume Paulo kwa Wakorinto waliokuwa wametengana sababu ya imani yao kwa Kristo. Kulitokea mgawanyiko na kukawa na makundi yakifuata viongozi wao wapo waliojiita “watu wa Paulo, wengine wa Apollo, wengine wa Kefa na wengine wa Kristo”. Kila kundi likiwa na msimamo na itikadi zake. Kundi la Kefa/Petro lilishikilia mapokeo ya Kiyahudi na sheria za Musa, kundi la Paulo likiona sio lazima kuzishika sheria hizo, imani itokanayo na neema ya Kristo  inatosha kwa wokovu na kundi la Apollo likiifanya dini kuwa kifalsafa zaidi. Wasifu wa Apollo ni ule tunaoupata katika kitabu cha Matendo ya Mitume: “Basi Myahudi mmoja, jina lake Apollo, mzaliwa wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso, naye alikuwa hodari katika Maandiko” (Mndo 18:24). Na kundi la waliojiita wakristo wao walio kwamba kule kuwa wa Paulo, au wa Apollo, au wa Kefa, haidhuru cha maana ni kumfuata Kristo.

Makundi haya yalisababisha giza nene la ubaguzi na utengano katika jumuia ya Korinto. Mtume Paulo anawakumbusha kuwa kwa wakristo mambo haya ni ya aibu hayapaswi kuwepo. Nasi tunapaswa kujua kuwa Imani kwa Kristo ni moja. Kristo aliyekufa kwa ajili yetu msalabani ni mmoja na hajagawanyika na hawezi kugawanyika. Hatupaswi kubaguana. Sisi sote ni watu wa Mungu mmoja. Sote ni watoto wa baba mmoja wa mbiguni. Chuki ni mwiko. Hatupaswi kuchukiana wala kubaguana. Tusijigawe kadiri ya kipato, elimu, au kushikamana na Padri au Askofu fulani. Tukumbuke kuwa ubaguzi ni moja ya matendo ya giza, mengine yakiwa ni wivu, rushwa, ufisadi, uwongo, na kadhalika. Kwa kufanya matendo haya Mungu hayumo ndani mwetu. Tukumbuke daima kuwa sote tuna Imani moja na ubatizo mmoja. Kiini cha imani yetu ni Msalaba wake Kristo, na kiini cha dini yetu ni Kristo peke yake. Tusiwe na fitina kwa ajili ya imani au kwa kuwafuata wahubiri kwani hakuna mhubiri ambaye alisulibiwa kwa ajili yetu na hatukubatizwa kwa jina la mhubiri yeyote bali tumekombolewa kwa msalaba wa Kristo na tumebatizwa kwa jina la Kristo.

Kristo Yesu ni nuru ya Mataifa
Kristo Yesu ni nuru ya Mataifa

Injili tunayosoma katika kipindi cha kawaida cha mwaka A wa kilitrujia ni ya Matayo ambayo inamwonyesha Yesu kuwa ni utimilifu wa utabiri wote wa Agano la Kale. Katika dominika ya 3 tunasoma (Mt. 4:12-23) ambayo inasimulia jinsi Yesu alivyoanza rasmi kazi ya kutangaza habari njema ya Ufalme wa Mungu kwa watu na kuwaita mitume wake wa mwanzo – Simoni Petro, Andrea, Yakobo na Yohane wana wa Zebedayo – wote wavuvi wa samaki ili wawe wavuvi wa watu. Yesu anaanza utume wake baada ya kusikia kuwa Yohane Mbatizaji amefungwa gerezani. Ujumbe wa Kristo uko wazi; “Tubuni kwa maana ufalme wa mbinguni umekaribia”. Kuhubiri kwake kunaanzia katika mkoa wa Galilaya, Kapernaumu, mji ulioko pwani, mipakani mwa Zabuloni na Naftali ili kutimiliza utabiri wa nabii Isaya ya kwamba nchi ya Zabuloni na Neftali zitaona mwanga mkuu (Isa 9:12).

Kihistoria Zabuloni na Neftali ni makabila mawili ya waisraeli yaliyoishi katika eneo la mji wa Kapernaumu kandokando ya ziwa la Galilaya. Wakati wa Yesu mkoa wa Galilaya ulikaliwa wa watu mchanganyiko, wayahudi pamoja na watu wa mataifa mengine. Sababu ya mchanganyiko huu kwanza ni utumwa ambapo wayahudi walitolewa na kuwekwa watu wa mataifa mengine. Pili ni ukoloni wa kirumi ambapo askari wengi waliishi huko, mfano wa jemadari aliyemuomba Yesu amponye mtumishi wake. Tatu Kapernaumu ulikuwa ni mji uliochangamka sana kibiashara na kuwa na wasomi wengi hata upinzani mkubwa ulitoka huko na ndio waliokuwa wanapanga mapinduzi na hivi athari za kutoka nje zilipenya katika maisha ya wayahudi katika mji wa Galilaya hata ukadharauliwa na Mafarisayo na waandishi. Ndiyo maana Nikodemo mmoja wao alipojaribu kumtetea Yesu walimwambia; “Je, Wewe nawe umetoka Galilaya? Tafuta ukaone ya kuwa kutoka Galilaya hakutokei Nabii?” (Yn. 7, 52).

Dominika ya Neno la Mungu
Dominika ya Neno la Mungu

Katika hali hii watu wake walikaa katika giza. Maisha yao yaligubikwa na starehe na anasa. Kulikuwa na giza nene la dhambi. Hapakuwa na haki, matajiri waliwanyonya maskini na kuwatumikisha. Watu walikuwa kama vipofu maana hawakuona kukosekana kwa haki kuwa ni jambo baya. Dhambi ilitawala. Ndiyo maana Yesu anaanza kuhubiri na kukazia alichohubiri Yohane Mbatizaji mkoani Yudea akisema; “Tubuni; kwa maana ufalme wa Mungu umekaribia”. Kumbe toba yahitajika katika kuingia katika ufalme wa Mungu. Basi tujitahidi kufanya toba na kupokea sakramenti ya kitubio kila mara ili tuendelee kuujenga ufalme wa Mungu katika maisha yetu ya kila siku. Tujijengee utamaduni wa haki, usawa, ukarimu, upole, unyenyekevu na uadilifu katika kila fani ya maisha yetu ili mwisho wa maisha ya hapa duniani tupate kustahilishwa kuingia katika maisha ya uzima wa milele mbinguni. 

Dominika ya Neno 2023
19 January 2023, 14:11