Tafuta

Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu, ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo. Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu, ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo.  (Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Nne Mwaka A: Heri za Mlimani Katiba ya Maisha ya Kiroho Kwa Wakristo

Kiini cha ujumbe wa masomo ya dominika hii ya 4 ya Mwaka A wa Kanisa, umejikita katika Heri nane alizozitoa Yesu mlimani kuwa mwongozo wa kuupata ufalme wa Mungu. Heri hizi ni kama katiba ya maisha ya kikristo ambayo tukiishi vizuri tutastahilishwa kuingia katika ufalme wa Mungu. Huu ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa waja wake yazingatiwe!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Liturujia ya Neno la Mungu, dominika ya 4 ya Mwaka A wa Kanisa, kipindi cha kawaida. Injili ya Dominika ya 3 Mwaka A ilionesha jinsi Yesu alivyoanza utume wake wa hadharani, akitangaza kukaribia kwa Ufalme wa Mungu na madai yake – kufanya toba. Yesu alianza kuhubiri Habari Njema Galilaya, kwa watu ambao walionekana wasio na maana kwa kuwa hawakuijua sheria ya Musa. Lakini ndio walitubu na kusamehewa dhambi zao, wakapewa maisha mapya ya kiroho, wakajazwa mioyo yao kwa amani, furaha na uhuru wa kweli. Kiini cha ujumbe wa masomo ya dominika hii ya 4 ya Mwaka A wa Kanisa, umejikita katika Heri nane alizozitoa Yesu mlimani kuwa mwongozo wa kuupata ufalme wa Mungu. Heri hizi ni kama katiba ya maisha ya kikristo ambayo tukiishi vizuri tutastahilishwa kuingia katika ufalme wa Mungu. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Nabii Sefania (Sef. 2: 3, 3: 12-13). Itakumbukwa kuwa katika Biblia, Kitabu cha Sefania ni kitabu cha 9 kati ya vitabu vinavyojulikana kama “Manabíi wadogo.” Sefania aliishi muda mfupi kabla ya kuharibiwa kwa Hekalu la Yerusalemi. Yeye alihubiri Yerusalemu miaka michache kabla ya Nabii Mkuu Yeremia. Aliishi wakati wa machafuko ya kidini, Kijamii na kisiasa Yerusalemu.

Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu
Heri za Mlimani ni muhtasari wa mafundisho makuu ya Kristo Yesu

Watu walikuwa wanaabudu sanamu. Tabaka la viongozi hawakuwa na maisha maadilifu. Hata viongozi wa dini hawakuwa na adabu katika maadhimisho ya ibada kwa Mungu. Katika maneno yanayotangulia somo hili, Nabii Sefania anatabiri kwamba siku ya hukumu na adhabu i karibu watenda maovu (1:8-12). Sehemu tunayoisoma dominika ya 4 mwaka A inawaasa wanaomcha Bwana waendelee kumtafuta wasije nao wakakengeuka na kuadhibiwa. Na kwa maskini na walioonewa wasikate tamaa bali wlitumainie jina la Bwana. Hii ilikuwa ni sala ya Mzaburi kama tunavyoimba katika wimbo wa mwanzo tukisema; “Ee Bwana Mungu wetu, utuokoe, utukusanye kwa kututoa katika mataifa, tulishukuru jina lako takatifu, tuzifanyie shangwe sifa zako (Zab. 106:47). Kumbe Nabii Sefania alikuwa ni sauti ya wanyonge na maskini walioonekana kama wamelaaniwa na Mungu kwa dhambi zao. Itakumbukwa kuwa katika Agano la Kale, utajiri, Afya, mafanikio na usitawi ilichukuliwa kuwa ni dalili na ashirio la baraka za Mungu kwa watu wamchao. Manabii walipoanza kuhubiri: polepole watu walianza kuelewa kuwa kile walichofikiri ni Baraka na upendeleo wa Mungu kwa watu wake inawezekana ndivyo-sivyo.

Heri za Mlimani ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo
Heri za Mlimani ni dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo

Pengine Utajiri huo unatokana na rushwa, wizi, udanganyifu, unyonyaji wa maskini, dhuluma na udanganyifu au ufisadi. Nyakati zetu mtazamo huu haujatuacha salama ndiyo maana tunashuhudia na kuona watu wakifurika kusikiliza wahubiri wanatangaza Injili ya usitawi na mafanikio kinyume na Injili ya Msalaba, kuwa ukiwa na Imani tajiri, afya na usitawi vitakufuata na matatizo ni sababu ya uasi kwa Mungu! Lakini uhalisia ni kuwa maskini ni maskini si kwa sababu ya balaa au laana bali dhuluma ya watu wengine dhidi yao. Tunashuhudia wenye mamlaka na nguvu wanavyotumia hali yao kujitukuza na kujilimbikizia utajiri kwa jasho la maskini. Wapo wanaotumia nguvu za giza wakiwatoa watu wengine kafara ilimradi tuu wapate utajiri. Wengine wanaingia mkataba na shetani kutumia Jina la Yesu ili kuwavuta watu wafike kwenye majumba yao wanakomwabudu shetani chini ya kivuli cha Yesu. Makanisa yanazidi kuibuka kila kukicha yakitangaza injili ya mafanikio. Bahati mbaya au nzuri mali ya namna hii hairithiwi. Inateketea na walio nayo.

Heri Maskini wa Roho Maana Ufalme wa Mbinguni ni wao
Heri Maskini wa Roho Maana Ufalme wa Mbinguni ni wao

Somo la pili ni la Waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Wakorintho (1kor 1:26-31). Katika somo hili Mtume Paulo anatueleza kuwa Mungu amewachagua maskini, wanyonge na waliodharauliwa ili awaibishe matajiri na wenye hekima ya mwili, wenye nguvu na vyeo vya kidunia pasipo Mungu. Maskini wanainuliwa kwani wana Hekima, Haki, Utakatifu, na Ukombozi wa Kimungu. Mateso wanayopata sasa si kitu yakilinganishwa na utukufu na fahari itokanayo na Mungu. Matajiri na wenye mamlaka wanapata hukumu ya Mungu kutokana na ufidhulu wao. Wao wanategemea mali, vyeo na matumbo yao, ndio miungu yao mzaburi anasema binadamu hatadumu katika fahari yake, atakufa tuu kama mnyama na mali na vyote alivyojikusanyia vitakuwa vya nani? (Zab 49). Sisi katika ukristo wetu hatuna lo lote la kujivunia kama stahili tulilolipata kwa nguvu zetu bali kufanywa kwetu wakristo ni neema pekee ya Mungu. Paulo anasema; “Angalieni mwito wenu, ya kwamba si wengi wenye hekima ya mwilini, si wengi wenye nguvu, si wengi wenye cheo walioitwa; bali Mungu aliyachagua mambo mapumbavu ya dunia awaaibishe wenye hekima; tena Mungu alivichagua vitu dhaifu vya dunia ili aviaibishe vyenye nguvu; tena Mungu alivichagua vitu vinyonge vya dunia na vilivyodharauliwa, il mwenye mwili awaye yote asije akajisifu mbele za Mungu”. Basi tusiogope na kukata tamaa bali tuendelee kuweka tumaini letu kwa Mungu hakimu mwenye haki.

Heri Maskini wa Roho Maana Ufalme wa Mbinguni ni wao
Heri Maskini wa Roho Maana Ufalme wa Mbinguni ni wao

Injili ni kama ilivyoandikwa na Mathayo (Mt 5:1-12). Katika sehemu hii ya Injili, Yesu anatoa sifa za wale watakaoingia katika ufalme wa Mungu. Ni wale wamtegemeao Mungu katika yote na wanaotia jitihada yao yote katika kuleta haki na amani hapa duniani. Nao ni maskini wa roho, wenye huzuni, wenye upole, wenye njaa na kiu ya haki, wenye rehema, wenye moyo safi, wapatanishi, wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki, wanaoshutumiwa na kuudhiwa na kunenewa kila neno baya kwa uongo, kwa ajili ya Kristo. Hawa wote Kristo anawaambia wafurahi kwa kuwa thawabu yao ni kubwa mbinguni. Ni ujumbe ulio wazi ambao kila mmoja wetu anapaswa kujiuliza kama yupo kati ya hawa wateule wa Mungu. Hizi heri nane alizozitoa Yesu mlimani ni mhutasari wa katiba ya maisha ya kikristo. Umaskini hata wakati wa Yesu ulionekana kama laana, balaa na ashirio la Dhambi. Yeyote asiyekuwa tajiri alinyooshewa kidole kuwa ni mdhambi. Viongozi wa Wayahudi waliwadharau sana maskini. Walifundisha kwamba umaskini wao ni matunda ya uzembe wa kutokuishika sheria ya Musa, na kwa sababu hiyo hakuna uwezekano wa wao kuokolewa. Haya ni maneno ya moja ya viongozi wa Wayahudi: “Lakini makutano hawa wasioifahamu Torati wamelaaniwa” (Yn 7:49). Kumbe tukumbuke kuwa, umaskini wa roho anaosema Kristo si kutokuwa na mali au vitu bali ni kuweka maisha yetu yote mikononi mwa Mungu. Kila tulicho nacho ni mali ya Mungu na tuvitumie atakavyo yeye. Katika raha na taabu, tuseme, “tumaini letu ni kwa Bwana”. Tukifanya hivyo, tutapata tuzo mbinguni kwa kuzingatia mafundisho ya Yesu kwa maneno na matendo.

Heri wapatanishi maana hao watairithi nchi
Heri wapatanishi maana hao watairithi nchi

Ili tuweze kuwa na umaskini wa roho lazima tuwe na upole na unyenyekevu. Kristo ndiye kielelezo chetu; “jifunzeni kwangu kwa maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo (Mt. 11:29). Upole na unyenyekevu ni matunda ya Roho Mtakatifu tunavyojaliwa na Mungu vitusaidie kuishi vyema na wengine. Tukikosa upole na unyenyekevu, tutaingia katika kilema cha majivuno yatakayotusabashia kutomjali Mungu na hivyo kukosa furaha na amani. Ufalme wa Mungu unatudai tuwe na moyo safi, maana yake ni kuwa na msimamo safi na sahihi kwa maneno na matendo. Heri hii ndiyo inayozivuta na kuzipa maana heri zingine. Mwenye moyo safi si mtu asiyejihusisha na mambo ya uasherati au ngono kwa ujumla wake tu bali ni kuwa na msimamo safi na sahihi kwa maneno na matendo kulingana na mapenzi ya Mungu. Ni usafi na unyoofu wa akili na utashi wa mtu machoni pa Mungu. Tunautaja moyo kama kielelezo kwa kuwa ndio kiini cha utu wa mtu (Mith 4:23) na humo ndimo hutoka mawazo mabaya (Mk 7:20 – 23). Kuingia katika ufalme wa Mungu kunatudai kuwa na kiu ya kutenda mapenzi ya Mungu. Tunaalikwa na Kristo mwenyewe kuzipa kipaumbele shughuli ya ufalme wa Mungu; na hayo mengine yote tutapewa kwa ziada.  Tahadhari hapa ni kuwa Yesu halaumu shughuli zetu za kupata mahitaji ya mwili, bali anatukumbusha pia tushughulikie kuupata uzima wa milele kwani huu uzima wa kimwili una mwisho lakini uzima wa kiroho hudumu milele. Tukishughulikia haki za Mungu, yeye atatushibisha kiroho na kimwili.

Heri wenye njaa na kiu ya haki
Heri wenye njaa na kiu ya haki

Kumbe, tukizishika hizi heri kiaminifu, tutapata furaha ya kweli na tutakuwa mwanga wa ulimwengu hivyo kuuonesha ulimwengu kuwa sisi ni taswira ya Yesu Kristo mwenyewe. Kwa kufanya hivyo, ufalme wa Mungu utaonekana wazi katika maisha yetu ya kila siku, ufalme uliojaa furaha na amani. Basi tumwombe Mungu atujalie moyo wa unyenyekevu wa kutamani na kutafuta kutimiza mapenzi yake. Mafundisho ya Yesu mlimani yawe dira katika maisha yetu ya kikristo; tuweze kupata furaha ya kweli katika ufalme wa mbinguni. Hvyo sala ya koleta anayosali Padre kwa niaba ya waamini akisema; “Ee Bwana Mungu wetu, utujalie kukuheshimu kwa moyo wetu, na kuwapenda watu wote kwa mapendo ya kweli”, na ile ya kuombea dhabihu akisema; “Ee Bwana, tunaleta dhabihu za ibada yetu kwenye madhabahu yako; uwe radhi kuzipokea na kuzifanya ziwe sakramenti ya ukombozi wetu zitakuwa na dhamani katika maisha ya sasa na hivyo kutustahilisha kuingia katika maisha yajayo huko mbinguni kama sala baada ya Komunyo inavyohitimisha ikisema; “Ee Bwana, sisi tuliokula sadaka ya ukombozi wetu, tunakuomba utuzidishie daima imani ya kweli kwa chakula hicho kiletacho uzima wa milele”. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika ya IV Mwaka A
27 January 2023, 17:02