Dominika ya Nne ya Pasaka: Siku ya 62 ya Kuombea Miito Ndani ya Kanisa 2025
Na Padre Paschal Ighondo – Vatican
Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 4 ya Pasaka. Dominika imepewa jina la “Dominika ya Mchungaji Mwema” na Yesu Kristo ndiye mchungaji wetu mwema. Ni siku ya 62 ya kuombea Miito mitakatifu katika Kanisa tukifuata agizo la Yesu alilosema; “Mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika shamba lake” (Mt 9:37, Lk 10: 2). Mwaka huu tuko siku ya 62 ya kuombea miito mitakatifu katika Kanisa. Ujumbe wa siku hii uliotolewa na Hayati Baba Mtakatifu Francisko tarehe, 19 Machi 2025, katika Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria, unaongozwa na kauli mbiu ya Jubilei 2025, nao unasema hivi; “Mahujaji wa matumaini: zawadi ya maisha”. Ujumbe huu ni wosia wa Hayati Baba Mtakatifu Francis kwa vijana akiwatia moyo wasikate tamaa katika mahangaiko ya kimaisha, bali wajivike moyo wa ujasiri, waitikie sauti ya Mungu na kuupokea wito anaowaita kumtumikia iwe katika maisha ya Upadre, Utawa, Ndoa, au wito wa kazi za kawaida. Ili wafanikiwe, wanapaswa wakubali kuelekezwa na kuongozwa na viongozi wa Kanisa wanaomwakilisha Kristo Mchungaji mwema. Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuelekeze kwenye furaha za mbinguni, kusudi sisi kondoo wako wanyonge tufike huko alikotoka mchungaji wetu shujaa.” Nao wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya siku hii unasema hivi; “Nchi imejaa fadhili za Bwana. Kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, aleluya” (Zab. 33:5-6).
Somo la kwanza ni la Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 13:14, 43-52). Somo hili linasimulia safari ya kwanza ya kimisionari ya Mtume Paulo akiwa na Barnaba (13:1-14:28), jinsi walivyoihubiri Injili. Kwanza walianza kwa Wayahudi nao walikataa kuipokea, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana. Ndipo Paulo na Barnaba walipowageukia wapagani, nao wakalipokea Neno la Mungu kwa furaha. Mtume Paulo anashuhudia hili akisema; “Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza. Lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana; Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia”. Simulizi linasema kuwa Wayahudi waliwafitinisha wanawake wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao. Nao wakawakung’utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio wakiongozwa na Roho Mtakatifu. Nasi kama Mtume Paulo na Barnaba kwa ubatizo na kipaimara tumeitwa kumshuhudia Kristo Mfufuka kwa maneno na matendo yetu kama mzaburi katika wimbo wa katikati anavyotuelekeza akisema; “Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote; mtumikieni Bwana kwa furaha; Njoni mbele zake kwa kuimba. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu; Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake; Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. Kwa kuwa Bwana ni mwema; Rehema zake ni za milele na uaminifu wake ni wa vizazi na vizazi” (Zab. 100 : 11-3, 5).
Somo la pili ni la Kitabu cha Ufunuo (Uf. 7:9,14b-17). Somo hili linatupa picha ya hali yetu itakavyokuwa huko mbinguni, tutakapokuwa chini ya ulinzi na uangalizi wa mchungaji Mwema, Yesu Kristo. Huko tutakuwa na furaha na amani daima. Hali hii Yohane aliifunuliwa ili kuishuhudia kwa kuoneshwa watu wa kila taifa, kabila, jamaa, na lugha, waliosimama mbele ya kiti cha enzi, na mbele za Mwana-kondoo, wakiwa wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao, wametoka katika dhiki kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwan-kondoo. Watu walio katika hali hii hawaoni njaa tena, wala kiu, wala jua haliwapigi, wala hari yoyote ile. Kwa maana Mwana-kondoo, ndiye Yesu Kristo Mchunguja Mwema, aliye katikati ya kiti cha enzi, anawachunga, na kuwaongoza kwenye chemichemi za maji yenye uhai, na Mungu anayafuta machozi yao yote. Hawa ndio walioisikia sauti ya Mchungaji mwema, wakamfuata, na zawadi yao kuu ni uzima wa milele.
Injili ni kama ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 10 : 27-30). Katika sehemu hii ya Injili Kristo Yesu anajidhihirisha kuwa Yeye ni Mwana wa Mungu na mchungaji mwema naye anawalinda kondoo wake kwa kuutoa uhai wake. Kondoo wake wanamjua, wanamwamini na kumfuata naye anawapa uzima wa milele. Wezi na wanyang’anyi hawawezi kamwe kuwapokonya kutoka katika mikono yake. Hili ndilo tumaini ambalo Hayati Baba Mtakatifu Francisko alilisisitiza katika ujumbe wake wa siku ya 62 ya kuombea miito 2025, akiwaasa vijana na watu wote, kuwa wasiogope, dhiki, mahangaiko na masumbuko ya dunia hii, bali waisikilize sauti ya Kristo kwa ujasiri, waitikie wito anaowaitia katika maisha yao kama walivyofanya watakatifu vijana kama vile Rosa wa Lima, Dominiko Savio, Teresa wa Mtoto Yesu, na hata Mweyeheri Carlo Acutis ambaye yuko katika hatua ya kutangazwa mtakatifu. Nasi tukiisikiliza sauti ya Mungu inayotuita, tukamjua, tukampenda, na kumtumikia, hakika tutafika kwake mbinguni. Hivyo kila mmoja anapaswa kufungua moyo wake amruhusu Roho Mtakatifu amuangaze aweze kutambua na kung’amua aina ya wito ambao Mungu anamuita kuuishi. Maana Mungu ndiye anayeita na kuchagua na hakuna awezaye kujitwalia zawadi hii mwenyewe. Hivyo kila mmoja ana wajibu na jukumu la kuisikiliza sauti yake na kufanya mang’amuzi sahihi kwa njia ya sala na kufuata maongozi ya viongozi wa Kanisa.
Mwaliko ni huu, tusichoke kusali na kumwomba Mungu Roho Mtakatifu awaangaze na kuwasaidia vijana waweze kutambua na kung’amua mpango wa Mungu kwao, awape na kuwajalia ujasiri wa kufuata na kutembea katika njia ya wito anaowaitia. Lakini zaidi tutie mkazo malezi ya awali katika familia kuhusu miito, tukiongozwa na Neno la Mungu, kwani waswahili wanasema; Mtoto umleavyo ndivyo akuavyo. Ndiyo maana Hayati Baba mtakatifu Francis alisisitiza kuwa tuwasaidie vijana waweze kuisikia na kuitambua sauti ya Mungu ili wawe na uwezo wa kuchagua kwa uhuru wito anaowaita na waufuate bila kusita, kwa kuyatoa maisha yao bila kujibakiza katika kumtumikia Mungu katikati ya watu wake bila ubaguzi. Haya Baba Mtakatifu anasisitiza juu ya hali hii kwa sababu katika ulimwengu wa utandawazi kuna sauti nyingi zinazowafanya vijana washindwe kuitambua sauti ya Mungu na hivyo wanakuwa hatarini kuchagua kwa makosa miito wasiyoitiwa. Mama Kanisa akilitambua hili katika sala baada ya komunio anapohitimisha maadhimisho ya siku hii anasali hivi; “Ee Mchungaji mwema, ututazame kwa mapendo sisi kundi lako. Upende kutuweka katika malisho ya milele sisi kondoo wako uliotukomboa kwa damu takatifu ya Mwanao.” Basi nasi tuhitimishe tafakari hii kwa kusali sala ya kuombea miito mitakatifu.
Tuombe: Ee Baba, uamshe ndani ya waamini wako, Miito mitakatifu ya Upadre na Utawa, ili kuimarisha Imani na kulinda uzuri wa kumbukumbu ya mwanao Yesu Kristo, kwa njia ya kueneza neno lake, na kutoa sakramenti ambazo hufanya upya Waamini wako. Utupe watumishi watakatifu kujongea altare yako, ambao ni waangalifu, na wenye kuheshimu Ekaristi Takatifu, kama zawadi kubwa ya Yesu kukomboa ulimwengu. Kwa huruma yako uite watumishi, ambao kwa njia ya sakramenti ya kitubio, wataeneza furaha yako ya msamaha kwa watu. Ee Baba ulijalie Kanisa lako lipokee kwa furaha Roho ya Mwanao, na kuwa waaminifu kwa mafundisho yake. Kanisa lako litunze miito ya wale walioitwa kwa maisha ya wakfu ya Upadre na Utawa. Uwaimarishe Maaskofu, Mapadre, Mashemasi na Watawa wote wa kike na wa kiume, waliojitoa kwa maisha ya wakfu. Pia uwaimarishe wote waliobatizwa kwa Jina la Kristo, ili wawe waaminifu katika Utume kwa huduma ya kutangaza Enjili. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana Wetu. Amina. Maria Malkia wa Mitume, Utuombee.