Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema: Siku ya 62 ya Kuombea Miito Mitakatifu
Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.
Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Jumapili ya 4 ya Pasaka mwaka C wa Kanisa. Ni Dominika ya, “KRISTO MCHUNGAJI MWEMA” Dominika ya kusali na kuombea miito ulimwenguni. Kila mwaka katika Dominika hii ya nne ya Pasaka tunapata nafasi ya kumtafakari Kristo Mchungaji wetu mwema. Kristo Mchungaji wetu Mwema alijitoa uhai wake kwa ya kondoo wake, anawajua kondoo wake, anawalinda, anawatafuta, anawaongoza kwenye malisho na anawajali wote. Huu ni wajibu si wa watu waliojitoa kwa maisha ya wakfu tu bali ni wito wetu sote, kwanza kabisa kama wabatizwa, lakini pia kwa njia ya miito mbalimbali katika Kanisa, kwa Ndoa Takatifu, kwa wito wa Utawa na Daraja Takatifu, sisi sote tunapewa wajibu huu wa kuwa wachungaji. Tunashirikishwa ofisi tatu za Kristo Yesu yaani: Unabii, Ukuhani na Ufalme. Tuombe neema ya kupokea wito wa Mungu na kuutekeleza kwa uaminifu kwa Mfano wa Kristo Mchungaji wetu Mwema. Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji mwema sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 62 ya Kuombea Miito Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu: Mahujaji wa matumaini: Zawadi ya maisha kwa ukarimu. Hayati Papa Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 62 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa kwa mwaka 2025 anasema, wito ni zawadi ya thamani ambayo Mungu hupanda mioyoni, wito wa kutoka ndani ya nafsi yako ili kuanza safari ya upendo na huduma. Tunasali kuombea miito mitakatifu katika Kanisa.
Tumwombee Baba Mtakatifu wetu Leo wa XIV, Maaskofu, mapadre, watawa, wanandoa na viongozi wote wa dini na serikali, ili waweze kutimiza kwa uaminifu wajibu wao wa kuwa watumishi, kwa kuhudumia kwa upendo, haki, unyenyekevu, sadaka, usawa, kudumisha umoja na amani kati ya kondoo ambao Mungu amewakabidhi kuwachunga kwa niaba yake. Tuombee familia zote ziwe na umoja, amani, imani, matumaini, upendo na mshikamano ili humo ichipuke miito mitakatifu, tukifahamu kuwa wito wa Ndoa Takatifu ndicho kitalu cha kustawisha miito mingine yote.Leo tarehe 11/05 ni siku ya akina Mama ulimwenguni. Tunamshukuru Mungu kwa zawadi ya akina Mama wote kwa kuitika wito wa Mungu wa kuwa Mama. Kwa maombezi ya Mama yetu Bikira Maria, ambaye alikubali wito wa kuwa Mama wa Mungu na kuutimiza kwa uaminifu mkubwa, tunawaombea akina Mama wote, ili waendelee kujitoa kwa mapendo, huruma na sadaka kwa ajili ya familia zetu, kwa ajili ya kanisa, na kwa ajili ya taifa lote la Mungu. Tunafahamu mchango mkubwa wa akina Mama katika jamii na katika kanisa. Tuwaombee waendelee kuwa vyombo vya amani na upendo katika kuunganisha familia zetu. Tuwaombee pia akina mama wanaopitia katika changamoto mbalimbali na wale waliotutangulia mbele za haki Mwenyezi Mungu awape pumziko la milele mbinguni.
Somo la Injili: Ni Injili ya Yohane 10:27-30. Katika somo la Injili Takatifu Dominika iliyopita, kutoka Injili ya Yohane 21:1-19, Kristo Yesu mfufuka alipojidhihirisha kwa wanafunzi wake saba katika Bahari ya Tiberia, anamkabidhi Mtume Petro wajibu wa kuwa Mchungaji na kiongozi wa Kanisa la Kristo. Msingi wa wajibu huu mkubwa ambao Petro na Mitume walipewa kuuendeleza mara baada ya Pentekoste, ni katika somo la Injili hii tuliyoisikia ambapo Kristo, katika sura hii ya kumi ya Injili ya Yohane (10:1-30) anajitambulisha kama Mchungaji mwema. Yesu anawajibu Mafarisayo ambao mara kwa mara walikua wakipinga mafundisho na kazi zake, hasa baada ya kumponya kipofu katika sura ya 9. Mafarisayo hawa walikuwa ni viongozi lakini walikua vipofu kwa kuwa hawakutambua na kuzikubali kazi za Mungu ndani ya Kristo. Ndipo Yesu anatoa mafundisho marefu kuhusu Mchungaji Mwema leo ikiwa ni mwishoni mwishoni mwa sura hii ya kumi. Kumbe dhana ya Yesu Mchungaji Mwema yatupa picha juu ya uwepo wa wachungaji wasio wema, wachungaji wasio na upendo, wachungaji vipofu wasioona wala kuguswa na shida na mahangaiko ya kondoo wao, wachungaji wa faida, wachungaji wa mshaharaa ambao kondoo si mali yao. Yesu sasa anatoa vigezo, mfano na sifa za mchungaji mwema kwa maisha na utume wake mwenyewe.
Somo la 1: Ni kitabu cha Matendo ya Mitume 13:14, 43-52. Kitabu cha Matendo ya Mitume chatueleza mwendelezo wa kazi ya utume wa Kristo Mchungaji Mwema iliyofanywa na Mitume baada ya Pentekoste. Somo hili kutoka sura hii ya kumi na tatu latueleza utume wa mitume Paulo na Barnaba huko Antiokia. Wanaingia katika Sinagogi na humo wanahubiri na kuwatia watu wa mataifa moyo wadumu katika neema ya Mungu. Kwa njia ya Kristo, utume wa Mitume hawa uliopokelewa kwa furaha na watu wa mataifa. Watu waliguswa na mafundisho na pamoja na mtindo wa maisha wa Mitume hawa wa Yesu ambao walikua tayari kuyatoa maisha yao kwa ajili ya Injili na kwa ajili ya Kristo. Kanisa likaendelea kukua na kustawi na kuenea kwa nguvu. Katika Dominika hii ya Kristo Mchungaji Mwema tuna mafundisho yafuatayo ya kujifunza. Kwanza: Maana ya Mchungaji katika Agano la Kale na Agano jipya. Katika mazingira, tamaduni na Historia ya Taifa la Israeli katika Agano la Kale, dhana hii ya Mchungaji haikua jambo jipya. Tutazame dhana hii ya Mchungaji katika Agano la Kale, kisha katika Agano jipya. Kwanza, jamii ya Wayahudi ilikua ni jamii ya wachungaji, na hivyo walifahamu vyema Mchungaji ni nani na kazi ile ilikua ni ya namna gani. Yesu anatumia picha ya Mtu atendaye kazi ambayo waliifahamu vyema. Walifahamu Mchungaji alipaswa kuwa na sifa zipi, walifahamu tabia za kondoo, walifahamu maadui dhidi ya kondoo, walifahamu uwezekano mkubwa wa kupotea kwa kondoo nk. Yesu anajengea fundisho lake katika uelewa huu, maana ya kawaida kabisa ya Mchungaji. Pili, mahusiano ya taifa la Israeli na Mwenyezi Mungu yalijengeka katika misingi ya kichungaji, Mwenyezi Mungu akijitambulisha na kujidhihirisha katika Agano la Kale katika kama Mchungaji wa Kundi lake yaani Nyumba ya Israeli (Eze 34:15). Mfalme Daudi katika zaburi ya 23 anamtambua Mungu kama mchungaji, ambaye kwake hatapungukiwa na kitu anaposema, “Bwana ndiye Mchungaji wangu, sitapungukiwa na kitu.”Tatu, Kazi ya kulichunga kundi lake, Mwenyezi Mungu aliwapatia, aliwakabidhi pia viongozi mbalimbali kwa niaba yake tangu katika Agano la Kale, kuanzia Musa, Manabii, makuhani na Wafalme na aliwataka kuifanya vyema na kwa uaminifu. Waliposhindwa kuifanya kazi hiyo Mwenyezi Mungu aliwakataa na kuahidi kuwa yeye mwenyewe atalichunga kundi lake (Eze 34:15).
Katika Agano Jipya, Bwana wetu Yesu Kristo anajitambulisha kwetu kama Mchungaji Mwema, anayeutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo zake, anayewajua kondoo wake nao wamjua, anayewatafuta na kuwaleta katika kundi moja kondoo wote hata wale ambao si wa zizi lake, anayewapa uzima wa milele kondoo wake, asiyekubali kamwe kumpoteza hata kondoo mmojawapo na anayewalinda kondoo wake dhidi ya maadui. Ni utimilifu wa ile ahadi ya Mungu kwamba, “Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo wangu” katika kitabu cha Nabii Ezekiel 34:15 inatimia kwa ujio wa Kristo. Kristo akiwa ameungana na Baba, anaunganika vilevile na kondoo wake. Ni kwa njia ya sadaka ya Kristo katika Fumbo la Pasaka, Mwenyezi Mungu ametukusaya tena pamoja watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa, tuliokuwa mbali naye kwa sababu ya dhambi na ametupatia zawadi ya ukombozi na uzima wa milele, ametufanya kuwa kundi moja chini yake yeye Mchungaji wetu Mwema. Kila mbatizwa hivyo anashirikishwa kwa nafasi ya kwanza kazi hii ya Kristo lakini kwa namna ya pekee kila mmoja kwa nafasi yake katika miito mitakatifu.
Pili: Sifa za Kristo Mchungaji Mwema tofauti na wachungaji wasio wema. Bwana wetu Yesu Kristo anatufundisha kuwa yeye ni Mchungaji Mwema na anatupatia sifa za mchungaji mwema. Twaweza pia kuona katika sifa hizi za mchungaji mwema namna tunaweza pia kuwa na wachungaji wasio wema. Sisi sote tunajifunza kutoka kwa Kristo Bwana na Mwalimu wetu. Kwanza: Kristo Yesu Mchungaji Mwema anawajua Kondoo wake nao waisikia sauti yake. Katika Injili hii ya Yohane Kristo anatupa sifa ya Mchungaji mwema, kwamba ni yule anayewajua kondoo wake, na kondoo hali kadhalika kwa kuwa ni mali yake basi waisikia sauti yake. Mchungaji asiye mwema hali kadhalika hawezi kuwajua wala kuwajali kondoo wake nao kondoo hali kadhalika hawawezi kumtambua wala kumsikia na kumfuata. Ndugu wapendwa, sisi tunamtambua Kristo kama Mchungaji wetu kwa kuwa alijitoa sadaka kwa ajili yetu, yeye alitupenda sisi kwanza. Kristo anatufahamu sisi kondoo wake kwa kuwa alitwaa hali ya kibinadamu, akawa sawa na sisi katika kila jambo isipokuwa dhambi. Anafahamu mahangaiko yetu, changamoto zetu, anafahamu vita vikali kati yetu sisi na mwovu shetani na anatuombeakwa Mungu. Anatualika kila siku katika Neno lake tumsikilize sauti yake. Anakuja kwetu kila siku katika Sakramenti zake akiendelea kutuita kwake kwa upole. Sisi tunatafakari pia wajibu wetu wa kumsikiliza Kristo na kumfuata. Katika kumfuata tunakumbushwa pia kwamba sisi sote tu wachungaji. Je tunawajua kondoo wetu? Je, tupo katibu kiasi gani na kondoo wetu? Uchungaji wetu kwa kundi ambalo Mungu ametukabidhi unaakisi uchungaji wa Kristo? Je, maisha yetu na huduma zetu kwa taifa la Mungu vinawasaidia wale tunaowachunga, iwe katika familia, iwe katika kanisa, katika jumuiya zetu au katika jamii kuisikia sauti ya Mungu na kumtuata katika utakatifu na haki? Kila mmoja afanye tathmini leo ya uchungaji wake. Na pale ambapo tumeshindwa tumwombe Kristo atusaidie kila mara kukumbuka kuwa tunapaswa kumwiga Kristo katika kuwatumikia wengine. Tunaalikwa kuwa karibu na wale tunaowahudumia, tufahamu furaha yao, tufahamu huzuni zao, tufahamu uwezo na udhaifu wao na kuwapokea wote, kuwasaidia kwa upendo ili waweze kupiga hatu moja mbele zaidi. Je ninawapokea wote katika mazuri na madhaifu yao? Ninawahudumia wote pasi na ubaguzi na pendeleo? Je, nina sauti juu ya kondoo wangu? Katika malezi ya watoto wangu, nina sauti ya kuonya, kuelekeza, kukemea na kufundisha? Tunaposhindwa katika wajibu huu tunapoteza sifa ya kuwa wachungaji wema, tunakuwa kama wachungaji wa mshahara ambao kondoo si mali yao.
Pili: Kristo Mchungaji Mwema anawatafuta na kuwaleta pamoja Kondoo wake. Kristo anawatafuta na kuwakusanya kondoo wote hata wale ambao si wa zizi lake na anawaleta pamoja katika kundi moja. Mchungaji mwema yupo tayari kuwaacha kondoo tisini na tisa na kwenda kumtafuta kondoo mmoja aliyepotea. Mchungaji Mwema hayupo tayari kumpoteza hata mmoja wa Kondoo wake. Sisi sote kwa njia ya Fumbo Pasaka Kristo ametuleta karibu, ametuunganisha tena sisi na Mungu, sisi ambao hapo mwanzo tulikua mbali kwa sababu ya dhambi. Ndugu wapendwa, Kristo Mchungaji wetu Mwema anatutafuta. Kristo anatuunganisha sote tunakua na umoja kama alivyosali na kuomba katika sala yake ya kikuhani, kwamba, ili wawe na umoja. Tunakua na umoja kati yetu sisi naye, kati yetu sisi na Mungu na kati yetu sisi kwa sisi. Kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio anatuleta tena karibu naye tunapokua mbali kwa sababu ya dhmabi kwa kuwa hafurahii kifo na kupotea kwetu. Sisi sote tunakabidhiwa wajibu huu wa kuwaleta wengine kwa Kristo. Mitume waYesu mara baada ya Pentekoste walitumwa kwenda kutangaza Injili, kwenda kuwa wavuvi wa watu, kwenda kuwatafuta na kuwaleta kwa Kristo kondoo waliopotea kwa njia ya kuhubiri Neno la Mungu, kufundisha na kubatiza. Kristo Yesu ametukabidhi sisi sote kwa njia ya ubatizo wetu na kwa njia ya miito mingine mbalimbali katika kanisa wajibu wa kuwakusanya na kuwaleta wengine kwa Kristo. Kila mbatizwa ni mmisionari wa habari Njema ya Kristo Yesu Mfufuka kwa watu wote. Anatupa wajibu wa kuwatafuta na kuwakusanya pamoja katika umoja na mapendo wale wote ambao Kristo ametukabidhi kuwatunza. Katika familia zetu tuwe tayari kutafutana na kurudishana kundini. Mmoja wetu anaporudi nyuma na kukata tamaa kiimani tunapaswa kumtatuta na kumleta tena katika jumuiya, katika familia, katika kanisa. Tusiseme kama Kain kwamba, “Mimi sio mlinzi wa ndugu yangu” Familia nyingi zimevunjika kwa sababu ya kutotimiza vyema wajibu wa kuwa wachungaji wema, hakuna amani, hakuna upendo, hakuna msamaha, hakuna upatanisho. Watoto wanakosa malezi mazuri kwa sababu ya migogoro ya kifamilia. Katika jamii yetu, katika jumuiya zetu, changamoto za wenzetu tunaziona na kuguswa nazo? Kila mmoja amwombe Kristo leo ili atupe moyo na nguvu ya kurudi sisi kwa Kristo tunapokwenda mbali naye, na pia kuwaleta pamoja kondoo tuliokabidhiwa na Mungu.
Tatu: Kristo Mchungaji Mwema anawapa Kondoo wake uhai na uzima wa milele. Kristo aliutoa uhai wake kwa ajili yetu sisi sote kwa njia ya mateso kifo na ufufuko wake. Kwa njia ya sadaka ya Kristo sisi sote tumepewa uhai na uzima. Bado anaendelea kutupa uhai kwa njia ya Neno lake na Sakaramenti mbalimbali katika kanisa. Sisi nasi tunapomtafakari Kristo Mchungaji wetu mwema, tunapata nafasi ya kujihoji ni kwa jinsi gani tunatoa uhai wetu kwa kukubali kuyabeba kwa uaminifu na sadaka majukumu tuliyokabidhiwa na Mungu kwa niaba yake. Katika utumishi wangu, ninajitoa kuwa sehemu ya furaha kwa wale ninaowatumikia? Maisha yangu yamekua sehemu ya kuinuka kwa wengine kwa njia ya kushirikisha kwa upendo vipaji na karama ambazo Mungu amenijali bure kabisa kwa njia ya Roho Mtakatifu? Je, nimekuwa chanzo cha upendo na faraja katika familia yangu, kwa mwenzangu wa ndoa, kwa wanajumuiya wenzangu, kwa watawa wenzangu? Maisha na utume wangu vina faida gani kwa wale wanaonizunguka? Wanahisi uwepo wa Mungu chanzo cha uhai na uzima aishiye ndani yangu katika huduma yangu na mahusiano yangu ya kila siku kwa wengine? Mara kadhaa tunashindwa kutimiza wajibu huu wa kutoa uhai wetu kwanza kabisa tunapokwepa mateso na misalaba yetu. Tunaposhindwa kutoka katika eneo letu la raha na faraja yaani comfort zone na kuingia katika kuhalisia wa maisha ya wengine wanaoteseka. Mara kwa mara tunajijali sisi, tunajali maslahi yetu sisi, tunatafuta furaha na amani yetu sisi, wala kondoo si mali yetu. Kama viongozi wa watu, tunapaswa kutimiza wajibu kweli wa kuleta maendeleo ya kimwili na kiroho kwa kondoo tunaowahudumia.
Nne: Kristo Mchungaji Mwema anawalinda kondoo wake dhidi ya maadui. Kristo Mchungaji Mwema anawalinda daima Kondoo wake dhidi ya maadui. Adui mkubwa hapa ni yule mwovu shetani. Kristo Yesu anatuweka daima na salama mikononi mwa Mungu, akitukinga na vita na hila za mwovu shetani. Ndugu wapendwa, Kristo kuhani wetu mkuu anatuweka salama dhidi ya hila na mitego ya mwovu shetani. Kristo anatuombea daima kwa Mungu kwa kuwa anafahamu mahangaiko yetu, anajua mapambano yetu dhidi ya dhambi, kwa kuwa yeye alikuwa sawa na sisi katika kila jambo isipokuwa dhambi. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, tunapokea nguvu ya kutambua na kukwepa hila na mitego ya mwovu shetani. Kwa njia ya malaika walinzi wetu, Kristo anatukinga dhidi ya hatari zote za mwili na za roho. Kwa njia ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu anatupa nguvu ya kuwa imara katika imani, na tunapata uzima rohoni. Sisi pia kwa namna ya pekee tunao wajibu wa kuwa walinzi wa kondoo wetu. Tunapaswa kuzilindia familia zetu, kulinda miito yetu, kuwalinda watoto wetu dhidi ya mmomonyoko wa maadili na utandawazi, kuilinda jamii yetu dhidi ya mila na desturi ambazo si zetu, dhidi ya vitendo viovu vya unyanyasaji na uvunjifu wa haki, umoja na amani na upendo. Sisi tu walinzi wa kila mmoja wetu kila mmoja kadiri ya nafasi yake na wito ambao Kristo ametutupatia. Tulinde imani yetu dhidi ya hila na mitego ya wachungaji wa uwongo, dhidi ya matamanio na maelekeo ya kiulimwengu. Tumtazame Kristo Mchungaji wetu, tumfuate ili tuupate uzima wa milele.
Tano: Kristo Mchungaji mwema ameungana daima na Mungu Baba yake. Kristo ni Mungu, nafsi ya pili ya utatu Mtakatifu, aliyetwaa mwili na kukaa kati yetu. Ameungana daima na Mungu Baba yake na daima alitafuta kuyafanya mapenzi ya Baba. Ndugu wapendwa, sisi pia tunaalikwa kuungana daima na Kristo ili tupate nguvu ya kutimiza daima mapenzi ya Mungu. Kazi ya kuwa wachungaji wa kondoo wa Kristo, yaani kutimiza yale majukumu yote yatupasayo katika miito yetu kwa uaminifu si kazi rahisi. Yahitaji daima kupata maongozi ya Kristo, kukaa daima miguuni pake ili atufundishe yale yote tupaswayo kuwaza na kutenda kwa ajili ya ustawi wa kiroho na kimwili wa kondoo wa Mungu. Hatuweza kuongoza familia bila maongozi ya Mungu, hatuwezi kuongoza wakristo wetu bila kuungana na Mungu, hatuwezi kuongoza serikali bila maongozi ya Mungu, hatuwezi kufanya kazi vizuri bila nguvu ya Mungu. Tunaalikwa leo kuunganisha maisha yetu na Mungu, unganisha msalaba wako na msalaba wa Kristo, mateso yako ma mateso ya Kristo, kuanguka kwako na kuinuka kama vile Kristo alivyoanguka na kuinuka na msalaba wake na kusonga mbele. Tukiwa na Mungu tunayaweza mambo yote kwa kuwa anatutia nguvu.
Somo la Pili: Ni kitabu cha Ufunuo wa Yohane 7:9, 14-17. Mwandishi wa Kitabu hiki, Mtume Yohane, aliwaandikia Wakristo waliokuwa wakiteseka katika kisiwa cha Patmos katika Asia ndogo, ili kuwapa moyo na kuwaimarisha Imani yao katika nyakati ngumu utumwa na mateso kutoka kwa watawala wa Kirumi. Anatueleza kuwa, ni Kristo aliyemwamuru kuandika kitabu hiki, ili kuwahakikishia wakristo hawa waliokuwa katika mateso uwepo wa Kristo Mfufuka kati yao hata katika nyakati ngumu waliozokuwa wanapitia. Mtume Yohane anaona katika maono watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa wamesimama mbele ya Mwanakondoo aliyechinjwa, Kristo aliyeshinda Mauti, Mchungaji wetu mwema katika kiti cha enzi cha Mungu. Ni Kristo ambaye kwa Fumbo la Pasaka ameleta ukombozi wa milele kwa watu wa mataifa yote, ishara ya kanisa linalowajumuisha watu wote kwa njia Kristo. Watu hawa walivumilia katika mateso, walipita katika ile dhiki kuu, wamefua mavazi yao katika damu ya Mwana kondoo. Waliteswa na kufa kwa ajili ya kumshuhudia Kristo, kwa ajili ya Injili. Nguvu ya kufa kifo dini waliipata kutoka kwa Kristo mwenyewe. Nasi sote tunaposherehekea siku hii ya miito duniani, tumwombe Kristo atupe nguvu na ujasiri wa kutimiza kikamilifu wito ambao kila mmoja wetu ameitiwa. Hakuna wito rahisi, hakuna njia rahisi. Lazma tukubali kubeba msalaba na kuvumilia katika mateso. Baada ya dhiki na mateso haya, Kristo mwenyewe atatupa tuzo ya uzima wa milele. Yesu atatuongoza kwenye chemchemi ya maji yenye uhai mbinguni, na atafuta machozi yote katika macho yetu. Hitimisho: Tunasali kuombea miito mitakatifu katika kanisa. Kwanza kabisa wito wa Ndoa Takatifu ambao ndio msingi na kiini cha miito mingine yote katika Kanisa. Tuombee familia zote ziwe na umoja, amani, imani, matumaini, upendo na mshikamano ili humo ichipuke miito mitakatifu. Tuwaombee pia wote walio katika maisha ya wakfu ili wawe kielelezo cha huduma ya upendo na sadaka kwa mfano wa Kristo Yesu Mchungaji wetu mwema.