Dominika ya Nne ya Pasaka: Kristo Mchungaji Mwema: Siku ya 62 ya Kuombea Miito Duniani
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya Neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo Dominika ya Nne ya Pasaka hujulikana kama Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 62 ya Kuombea Miito Duniani inayonogeshwa na kauli mbiu: Mahujaji wa matumaini: Zawadi ya maisha kwa ukarimu. Hayati Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Dominika ya Kristo Yesu Mchungaji Mwema, Siku ya 62 ya Kuombea Miito Mitakatifu ndani ya Kanisa kwa mwaka 2025 anasema, wito ni zawadi ya thamani ambayo Mungu hupanda mioyoni, wito wa kutoka ndani ya nafsi yako ili kuanza safari ya upendo na huduma. Na kila wito katika Kanisa uwe wa waamini walei au wa huduma ya maisha ya wakfu ni ishara ya tumaini ambalo Mungu analo kwa ulimwengu na kwa kila mmoja wa watoto wake. Katika Ulimwengu mamboleo, vijana wengi wanahisi kupotea, hawana uhakika na fursa za ajira; wanakosa utambulisho na mwelekeo wa kimaadili; kuna udhalimu mkubwa kwa wanyonge na maskini, vita, vurugu na kinzani mbalimbali, lakini Kristo Yesu anapenda kuwahamasisha waja wake kutambua kwamba, anapendwa, anaitwa na kutumwa kama msafiri wa matumaini. Viongozi wa Kanisa wanahimizwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwakaribisha, kutambua na kuwasindikiza vijana wa kizazi kipya kwa ufundi na ustadi mkuu. Vijana ni wahusika wakuu, kwa kushirikiana na Roho Mtakatifu ambaye huamsha ndani yao hamu ya kufanya maisha yao kuwa ni zawadi ya upendo.
Katika mwaka wa Jubilei ya Matumaini (2025), tafakari hii inakuwa ya kipekee zaidi, kwani tunatambua kwamba matumaini yetu hayajengwi juu ya mazingira bali juu ya uaminifu wa Yesu anayetuongoza kwa upendo. Kwa namna ya pekee, tunamkumbuka hayati Baba Mtakatifu Francisko ambaye maisha yake na mafundisho yake yalikuwa taswira hai ya Kristo Mchungaji Mwema: aliyeliongoza Kanisa kwa huruma, aliyejali waliopuuzwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, na aliyewachochea waamini kuwa mashuhuda wa matumaini katika dunia iliyojaa changamoto. ‘Hivi ni kwa nini tunafananishwa na Kondoo?’ muulizaji alikuwa amedhamiria hasa kutokana na muonekano wa sura yake, ‘Mafundisho ya Kanisa yangetufananisha na Simba, Chui au Dubu mweusi hata imani yetu isingechezewa’… oooh, ikabidi tuketi kabisa tujadili ipasavyo… Kuwa kondoo wa Kristo sio unyonge, sio ujinga, sio ukichaa bali ni baraka, ni neema… Mwanakondoo ni mnyama mpole na msikivu, hana shida na yeyote, mnyama wa sadaka tangu kale, Mwanakondoo wa Mungu aondoaye dhambi za ulimwengu, kwa damu yake tunaoshwa uovu wetu na mavazi yetu kuwa meupe kwa utakaso kamili (somo II-Ufu 7:9,14b-17)… pamoja na kuwa mpole, wafugaji waliokwisha kupigwa vichwa na kondoo machungani wanajua huwa inakuwaje hivi kuwa mwanakondoo katika zizi la Kristo sio unyonge, ni wito wa maisha. Kristo ndiye Mchungaji wetu Mkuu na Mzuri kuliko Yakobo, Musa na Daudi katika ubora wao… mabegani mwake tunasafiri, kifuani pake tunastarehe, mikononi mwake tunajipatia usalama, nyuma yake tunamfuata akituongoza polepole kwenye malisho mema na pumziko zuri… tuwapo popote hatuogopi mabaya, hata uvuli mchungu wa mauti, gongo lake na fimbo yake vyatufariji (Zab 23:4).Yesu anasema: “Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao hunifuata.” Huu ni msingi wa uhusiano wa karibu kati ya Kristo na waamini. Katika dunia ya leo iliyojaa kelele za hofu, tamaa, na giza la kutojali, tunahitaji kujifunza tena kusikia sauti ya Kristo – sauti ya upole, matumaini na mwongozo wa kweli. Hayati Papa Fransisko alisisitiza mara kwa mara juu ya “kusikiliza sauti ya Roho” na kuwa Kanisa linalosikiliza na kusindikiza. Alihimiza viongozi wa Kanisa wasiwe “wakuu wa ofisi,” bali wachungaji wanaonuka harufu ya kondoo – walioko karibu na watu. Katika Jubilei hii, tunaalikwa tujiulize: Je, tunaisikia sauti ya Mchungaji Mwema? Je, tunakuwa sauti ya matumaini kwa wengine hasa wanyonge na waliodhaifu?
UFAFANUZI: Hayati Papa Francisko alikuwa mdomo wa matumaini haya aliposisitiza Kanisa kutoka nje, kuwafikia waliotengwa, waliovunjika moyo, na wale wasiojihisi kuwa na nafasi. Alisema, “Upendeleo wa Mungu uko kwa walio maskini, waliovunjika, waliopotea.” Huo ndio moyo wa mchungaji mwema. Wito ‘original’ ni mmoja tu, na huo ni kwa ajili ya wote, wito wa kuwa WATAKATIFU kama Yeye aliyewaita alivyo mtakatifu (1Pet1:15-16) … Hata hivyo bila bahati hatujaitika vema katika hili, tumetenda dhambi na kupungukiwa utukufu wa Mungu (Rumi 3:23)… tumekuwa wanakondoo jeuri, tazama, Mchungaji mwema ametutoa zizini na kutupeleka malishoni, tumekula tumekunywa na kupumzika Yeye akitulinda na kutukusanya, halafu kakondoo kamoja kakorofi hakoo msituni kwenye miamba, Mchungaji huyu hakasiriki, hajihurumii, hajali njaa yake wala uchovu alionao, ananyanyuka na kuanza kuzunguka porini na baada ya mahangaiko mengi na hatari nyingi za wanyama wakali, ajali au maharamia anakakuta kamejibanza kwenye jiwe, kumbuka kameshiba hapo, ila sasa kanatetemeka baridi na hofu imekajaa, hakajui hata kalipo, hakajui kanataka nini, kanaangalia tu… Yeye anakapigapiga shingoni kwa upole na kukaweka mikononi mwake au begani pake na kukarudisha kundini… Katika maono ya Yohane, tunaona umati mkubwa ulioshinda dhiki kuu – wamefanywa safi kwa damu ya Mwanakondoo. Huu ni ujumbe wa tumaini kwa waamini wote: kwamba mateso hayana mwisho wa giza, bali mwisho wa utukufu na faraja. Papa Francisko alizungumza mara nyingi kuhusu "ushindi wa huruma" na kwamba hata katika mateso, Mungu yuko karibu nasi. Alitoa mfano kwa kwenda maeneo ya vita, wakimbizi, na maskini – akisisitiza kwamba matumaini yanazaliwa pale ambapo upendo unageuka kuwa tendo.
Ndugu unayesikiliza na kusoma ujumbe huu, jitahidi kuwa mwanakondoo mwema, acha kumsumbua Mchungaji wetu kwa dhambi, ukaidi, kiburi, ukandamizaji wa haki na ukorofi wa aina yoyote, anakupenda usimlipe huzuni… Hii ni Pasaka, siku aliyoifanya Bwana, tuishangilie na kuifurahia, amefufuka katika utukufu, tuache kumsulibisha tena na tena kwa kushindwa kutulia. Wito wa kuwa watakatifu unawezeshwa na mitindo ya maisha kadiri ya neema ya Mungu kwa kila mmoja wetu… Kwa wito wa Sakramenti ya Ndoa taswira ya Kristo na Mama Kanisa inajidhihirisha, kwa utakatifu wa maisha yao wanandoa wanakuwa sababu ya uhai mpya na chimbuko la miito mingine, kwa malezi yao familia ya mwanadamu inajipatia watu wema wenye imani, maadili na hofu ya Mungu, hawa wanalifaa Kanisa na kuitegemeza jamii… Yesu anasema: “Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao hunifuata.” Huu ni msingi wa uhusiano wa karibu kati ya Kristo na waamini. Katika dunia ya leo iliyojaa kelele za hofu, tamaa, na giza la kutojali, tunahitaji kujifunza tena kusikia sauti ya Kristo – sauti ya upole, matumaini na mwongozo wa kweli. Hayati Papa Francisko alisisitiza mara kwa mara juu ya “kusikiliza sauti ya Roho” na kuwa Kanisa linalosikiliza na kusindikiza. Alihimiza viongozi wa Kanisa wasiwe “wakuu wa ofisi,” bali wachungaji wanaonuka harufu ya kondoo – walioko karibu na watu.
Katika Jubilei hii, tunaalikwa tujiulize: Je, tunaisikia sauti ya Mchungaji Mwema? Je, tunakuwa sauti ya matumaini kwa wengine? Kama jamii inakosa watu wema na viongozi wacha Mungu, kwa mfano wananchi wakivuta pumzi ya moto kutokana na gharama za maisha halafu wenye dhamana wakafanya siasa tu kwa majibu mepesi, huenda changamoto ni malezi… tuombe leo neema ya Mungu ili wito wa Ndoa ustawi, wachumba wa muda mrefu wazindukane na kutamani sakramenti na sio sherehe, wenye ndoa wadumu katika amani na uelewano kwa upendo kamili, watunze uaminifu, kutoka kwao sote tumuone Kristo katika utukufu wake wa kipasaka. Tutaweza kuiishi wito wa kuwa watakatifu kwa njia ya Daraja tak na maisha ya wakfu… mapadre na watawa waishi kiaminifu wakiwa mfano mwema kwa wote, wasali na kudumisha maadili mema, washirikiane na wanakanisa wote kwa upendo, wasome alama za nyakati na kuipeleka Injili ya Kristo kadiri ya mazingira ya sasa ya zama hizi za kidigitali bila kuathiri asili ya tunu hii njema ya imani katoliki… walee miito michanga kusudi shamba la mizababu la Bwana lisitindikiwe watenda kazi… Mama Bikira Maria Malkia wa Mitume, utuombee amina. Tumeamua kumfuasa Kristo Mchungaji wetu mwema, basi tusikie anayotufundisha na kutuagiza, tujifunze kuiga tabia zake na kutenda kama Yeye… somo I (Mdo 13:14, 43-52) lasema ‘nimekuweka uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu hata miisho ya dunia’, kila mmoja awe nuru ya jirani yake ili kujaa furaha katika Roho Mt… Mwamini mpendwa, ona kwamba katika hali hiyo uliyomo, mbele ya hilo linalokukabili, zuri/baya, angekuwa Kristo angeamua na kutenda kama unavyotenda wewe muda huu, hapo ulipo… amina! Katika Jubilei ya Matumaini, hebu tumfuate Kristo Mchungaji Mwema, tukiwa mashahidi wa tumaini, kama alivyokuwa mtumishi wake mwaminifu, “Yesu ni Mchungaji wetu. Kamwe hatuachi peke yetu. Na sisi tunaitwa kuwa sauti, mikono na moyo wa Yesu kwa wale wanaohitaji zaidi.”