Tanzania,TEC:Matamko ya mshikamano wa haki kwa Padre Kitima
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika taarifa kwa Umma lenye kichwa: "Kuvamiwa na kuumizwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu( TEC), Padre Charles Kitima iliyotiwa saini na Askofu Eusebius Nzigilwa, Makamu Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, ya Mei Mosi 2025, inabainisha kuwa: “Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limesikitishwa sana na linalaani tukio baya la uovu la kuvamiwa na kujeruhiwa kwa Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Tanzania, Padre Charles Kitima, lililotokea tarehe 30 Aprili 2025, majira ya saa 4 usiku katika makazi na Makao Makuu ya Baraza la Maaskofu- Kurasini–Dar Es Salaam. Padre Kitima alipata majeraha makubwa na amelazwa katika hospitali ya Aga Khan, jijini Dar Es Salaam. Tunawashukuru wote waliomsandikiza na kumfikisha Padre Kitima hospitalini mapena na kwa madaktari na wauguzi wanaoumhudumia mpaka sasa.
Wito wetu kwa vyombo vinavyohusika
Tunatoa wito kwa Jeshi la Polisi na vyombo vingine vya Usalama kuchukua hatua za haraka za kuwabaini na kuwakamata wale wote waliohusika katika kupanga na kutekeleza uhalifu huu wa kinyama na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria. Aidha, uchunguzi wa tukio hili ufanyike kwa haraka na taarifa zitolewa kwa uwazi na bila upotoshwaji wowote ili kurudisha imani na matumaini kwa watu wetu. Tunashukuru mpaka sasa kwa ushirikiano mzuri tunaoupata kutoka Serikalini na kwa vyombo vyetu vya usalama. Pia tunawashukuru watu binafsi, taasisi za ndani na za kimataifa zinazoendelea kulaani na kutupa pole kwa tukio hili baya na la aibu kwa Taifa letu. Tunaomba Waamini na watu wenye mapenzi mema muendelee kumuombea neema ya uponyaji Padre Kitima, na pia kuliombea Taifa letu amani na umoja. Aidha tunawaomba muwe na subira na uvumilivu wakati tukisubiri matokeo ya uchunguzi wa vyombo vinavyohusika.” Ujumbe wa TEC unahitimishwa.
Matashi mbalimbali ya kulaani kitendo cha kikatili
Pole nyingi na matashi mema ya kupona haraka kwa Padre Kitima yamefika katika Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, (TEC) kama vile Askofu Dk. Benson Bagonza (PhD), Mkuu wa Kanisa Kiinjili la Kiluteri Tanzania(KKKT) Dayosisi ya Karagwe Mei Mosi 2025 alitoa salamu za pole kufuatia shambulio la Katibu Mkuu wa Baraza hili Padre Charles Kitima (PhD). Katika salamu zake aliandika: “Kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Dayosisi ninayoingoza kwa neema, pokea salamu za pole kama Baraza, Kanisa na binafsi, kwa Padre Charles Kitima kwa tukio ovu lililofanyika na kumdhuru mtumishi wa Bwana. Shambulio hilo si kwa Padre Kitima, si la TEC, wala la Imani ya Kikristo tu. Ni shambulio kwa wapenda haki na amani wote. Zaidi ni shambulio kwa Mama Tanzania, kilichokuwa kitovu cha amani yetu. Tunasimama nanyi kumuombea apone. Tunasimama nanyi kuwaombea waliomjeruhi wabadilishwe bila kutaka, kuwa watu wema. Tunaiombea Serikali yetu isitishwe na ubaya bali iseme haitatokea tena," anahitimisha Askofu Bagonza
Sala za kupona haraka kutoka Jumuiya ya Mtakatifu Egidio
Kufuatia na tukio hilo baya sana, kiongozi wa Kanda ya Tanzania ya Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, Bwana Francesco de Palma amesikitishwa na tendo hilo la kushmbuliwa akimbombea uponyaji wa haraka, Padre Charles Kitima na kwamba Kanisa liendeleea kuonesha kwa mara nyingine tena safina ya amani, haki na kupinga ubaya.”
Chama cha Chadema
Katika uongozi wa kisiasa, wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) pia “kililaani kwa nguvu zote shambulio la kinyama dhidi ya Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki (TEC) Padre Charles Kitima lililotokea usiku wa tarehe 30 Aprili 2025 katika makazi yake kurasini - Dar Es Salaam. “Shambulio hili ni ishara ya njama za kusimamisha sauti za hoja na kueneza hofu kwa walioko mstari wa mbele kudai haki, uhuru na mageuzi ya kweli. Ni jambo lisilokubalika katika taifa linalozingatia misingi ya haki, amani na demokrasia.” Kwa hiyo: “Chadema inatoa pole kwa Padre Kitima, Familia yake na Baraza la Maaskofu kwa mshituko na madhila yaliyotokea. Tunaungana nao katika kusisitiza haja ya kulinda misingi ya utu, usalama na uhuru wa kujieleza.”
Ufuatiliaji wa Jeshi la Polisi Tanzania
Jeshi la Polisi lilisema “kumshilikilia mtu mmoja mkazi wa Kurasini, Rauli Mahabi kuhusiana na tukio hilo na kwamba mahojiano na uchunguzi zaidi unaendelea ili kuchukua hatua kali na haraka dhidi ya waliohusika.”