Tafakari Dominika ya Tatu ya Pasaka Mwaka C : Mashuhuda wa Ufufuko
Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.
UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio vatican leo, Mitume wanakamatwa na kuonywa wasihubiri tena kwa jina la Yesu, lakini wana jibu moja la msingi: “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.” Hili ni tamko la imani ya kweli – ujasiri wa kushikilia ukweli wa Kristo hata mbele ya mateso. Papa Fransisko, kwa maisha yake ya unyenyekevu na sauti ya kinabii, alisimama imara dhidi ya udhalimu, rushwa, uharibifu wa mazingira na ukosefu wa haki, akiwakumbusha waumini kuwa Injili ni mwanga wa matumaini hata kwa waliokataliwa. Katika mwaka huu wa Jubilei, tunaitwa tuwe Mashuhuda wa matumaini – si kwa maneno tu bali kwa matendo yenye ujasiri kama mitume na kama alivyokuwa Hayati Papa Francisko. Na hii ndiyo tabia yake, naye hutenda hivi siku zote, akikuongoza tofauti basi sio Yeye, tukifanya tofauti yanakuwa yetu, si yake… daima anatuongoza kumtii Mungu na Kristo wake na katika hili tunajua kuwa yumo ndani yetu, huyo ndiye Roho wa Bwana akitenda kazi ndani ya Mitume wa Kristo kwa ushuhuda ulio kamili. Utii ni dada ya unyenyekevu, pacha wa usikivu na shauri muhimu la Kiinjili… huo ni bora kuliko dhabihu (1Sam 15:22), anayekosa kutii ni raia katika utawala wa Ibilisi na mwanachama katika umoja usioeleweka… Katika kutii tunapata kuaminika, kupendwa na kubarikiwa na Mungu “basi mtiini Mungu, mpingeni shetani naye atawakimbia” (Yak 4:7)… tuone leo kuwa utii inakuwa fadhila ya muda wote yaani mazoea yenye kutujengea tabia njema, Mtakatifu Petro na wenzake waliona neno hili katika Roho Mt wakasema “..imetupasa kumtii Mungu na sio wanadamu” alleluia!
UFAFANUZI: Zaburi hii ni wimbo wa shukrani kwa Mungu aliyebadilisha kilio kuwa furaha. Katika maisha ya Baba Mtakatifu Francisko, tunaona namna alivyotumia mateso na changamoto kama jukwaa la kutangaza faraja ya Mungu. Alituasa mara kwa mara kuwa Kanisa ni hospitali ya dharura, si kwa wakamilifu, bali kwa waliojeruhiwa – na hiyo ndiyo mantiki ya matumaini ya Kikristo: kwamba Mungu hutubadilishia machozi kuwa tabasamu. Tunapomshukuru Mungu kwa ushindi wa Pasaka, Kristo akiendelea kujidhihirisha kwa wanafunzi wake ili kuwaimarishia imani yao, tuombe neema ya kumsikia na kumtii Mungu, utii wetu udhihirike katika kuwa mashahidi wa Kristo tukihubiri kwa Jina lake wakati utufaao na usiotufaa, tukaripie, tukemee na kuonya kwa uvumilivu na mafundisho (1Tim 4:2)… ndio, zipo nyakati ngumu na za hatari kabisa… katika somo I (Mdo 5:27b-32, 40b-41) Mitume Petro na wenzake wameaibishwa kwa viboko na masimango mengi kwa ajili ya Jina la Bwana, wanatukumbusha sote, kila mmoja katika nafasi yake tangu Familia, JNNK, Kigango, Parokia… kuwa kumtii Mungu kwa matendo ni sadaka inayoumiza lakini inayolipa zaidi kwao wavumiliao kwa vile “mkikubali na KUTII mtakula mema ya nchi” (Isa 1:19).
Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu… utii huo unaonekana katika somo II (Ufu 5:11-14) tunapofafanuliwa juu ya kusali, kusifu na kuabudu vema mbele ya kiti cha enzi… tuone hivi leo maisha yetu yanampa Mungu sifa na utukufu wake.. fikra zetu, maneno, matendo na kila kitu chetu viungane na vinywa vya majeshi ya mbinguni pamoja na wale wenye uhai wanne, na wale wazee 24 na vya wataua wote duniani kumtukuza Mungu kwa sauti moja kusema “baraka na heshima na utukufu na uweza una Yeye aketiye juu ya kiti cha enzi hata milele na milele” (5:13), huyo ni Mwanakandoo wa sadaka anayejidhihirisha kando ya bahari akitwaa na kuwapa mkate na samaki… tumuabudu fudifudi Mungu katika Ekaristi Takatifu. Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu… hili linawezekana kwa kuliamini Jina tukufu la Kristo akituamuru katika somo la Injili (Yn 21:1-19) kutupa jarife upande wa kuume wa chombo ili kupata samaki… mkono wa kuume ni ishara ya nguvu, neema na wokovu wa Mungu… katika hili samaki wanaopatikana ni watu wa Mungu anaotamani tuwalete kwake kwa njia ya utume wetu wa kikristo, Je tunashiriki vema uvuvi huu muhimu? tusiogope, yupo ufuoni akiongoza yote kwa nguvu na upole, tufanye yote ndani ya uwezo wetu na yanayobaki atakamilisha Yeye mwenyewe. Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu… tunaweza kuiishi fadhila hii ya utii kwa kumtambua Kristo tukisema na Mtakatifu Yohane “…ndiye Bwana” (Yn 21:7)… tumpokee kwa mioyo safi katika Ekaristi Tak tukimshukuru vipaji vya mkate na divai na kwa mazuri tunayofaulu kufanya na kumuachia changamoto za kila siku katika uwezo wake mwenyewe… anatupenda, hatuachi katika dhiki bali anatualika daima mezani pake, “Njoni mfungue kinywa” (21:12), ni heri ilioje kushiriki ‘kifungua kinywa’ na Mfalme Mkuu kama huyo!
Katika Injili hii, Yesu anamrejesha Petro katika utume wake kupitia maswali matatu ya upendo: “Je, wanipenda?” Huu ni mwaliko wa toba na upyaisho wa matumaini. Papa Fransisko alikuwa daima na ujumbe wa rehema – kwamba hakuna aliye mbali sana na huruma ya Mungu. Petro anapokiri upendo wake, anapewa jukumu la kulisha kondoo – nasi pia tunapoitikia upendo wa Kristo, tunaitwa kuwa vyombo vya matumaini kwa wengine. Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu… hili lionekane pia katika utendaji wetu wa kimisionari tukitenda yote “pamoja na Petro, na chini ya Petro” (Cum Petro et Sub Petro) ambaye leo ameungama mara tatu kumpenda Bwana wake kuliko wote (21:15-17)… Kanisa la Kristo ni la kihairakia, tunapomtii Mungu leo tuyasikie na kuyashika mafundisho ya Kanisa lake vile “magisterio” inaagiza, huenda kuna mambo hayatuvutii wala hayatunogei ndani ya Kanisa, mengine tunayaona hapa na pale tungetamani na sisi tufanye, Petro anaposema hapana basi iwe HAPANA, iwe ni kuhusu imani, maadili au matendo ya waamini, desturi za kusali na kuabudu, sadaka ya Misa, sakramenti na visakramenti, uhalifa wa Papa na ushirika wa watakatifu, haya yote ni katoliki na katoliki lazima yabakie… Petro yupo Parokiani katika nafsi ya Paroko, tumsikie na tumsikilize kwa utii na unyenyekevu, tukishauri, kujadiliana na kuchangia kikristo, tuenende pamoja na Petro na chini ya Petro, pamoja na waandamizi wa Pertro, waliopo kwenye Kanisa mahalia. Ipo amani ipitayo amani zote katika kumtii Mungu, Mungu ni Mungu, Yeye pekee anastahili heshima yangu, tumaini langu ni kwake, kwake tuu, nami nitamtii daima… pumziko langu, faraja yangu na amani yangu si popote isipokuwa kutuimiza mapenzi yake katika utii kamili, amina.
Katika Dominika hii ya Pasaka, tunakumbushwa kuwa tumaini ni zawadi kutoka kwa Mungu, lakini pia ni wajibu wetu kwa wengine. Tunaalikwa: kuwa mashahidi jasiri kama mitume, kutoa faraja kwa waliovunjika moyo, kumtukuza Mwanakondoo kama sababu ya matumaini yetu, na kujibu upendo wa Kristo kwa huduma na huruma. Papa Francisko alituonyesha kwamba matumaini ya Kikristo ni hai – yanatendeka katika utume, huduma, na kujitoa kwa wengine. Katika Jubilei hii ya Matumaini, na tuombe neema ya kufufuliwa katika matumaini, tukitembea katika njia ya upendo, haki, na rehema. Tusikate tamaa kamwe! Yesu yuko hai na anatembea pamoja nasi.” Aleluya.