Tafuta

Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Pasaka: Yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Waamini wanaitwa na kutumwa kuwa ni mashuhuda wa Fumbo la Pasaka: Yaani: Mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu.   (@Vatican Media)

Tafakari Dominika ya Tatu ya Pasaka Mwaka C: Mashuhuda wa Fumbo la Pasaka

Kristo mfufuka anawatokea baada ya ufufuko wake mara kadhaa, na anawapa amani, anawaondolea hofu na mashaka. Kisha anawakumbusha wito wao wa kwanza, kuwa wavuvi wa watu kwa njia ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, maisha ya ushuhuda wa Imani, kufundisha na kuwabatiza, watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa. Mtume Petro, licha ya kuwa hapo Mwanzo alimkana Bwana wake, anaimarishwa na anapewa jukumu la kuwa kiongozi mkuu wa Kanisa.

Na Padre Bonaventura Maro, C.PP.S., -Kolleg St. Josef, Salzburg, Austria.

Utangulizi: Wapendwa Taifa la Mungu, leo ni Dominika ya Tatu ya Pasaka Mwaka C wa Kanisa. Liturujia ya Neno la Mungu katika Dominika hii ya tatu ya Pasaka yatutafakarisha juu ya, “Kristo Yesu mfufuka, chanzo cha upya wa maisha na utume wa wafuasi wake” Mitume wa Bwana wetu Yesu Kristo mara baada ya Yesu kuteswa na kufa Msalabani, walitawanyika, walipoteza matumaini, walijawa na hofu na mashaka. Wengine wakaanza kurudi katika shughuli zao walizokuwa wanafanya hapo Mwanzo. Kristo mfufuka anawatokea baada ya ufufuko wake mara kadhaa, na anawapa amani, anawaondolea hofu na mashaka. Kisha anawakumbusha wito wao wa kwanza, kuwa wavuvi wa watu kwa njia ya kutangaza Habari Njema ya Wokovu, maisha ya ushuhuda wa Imani, kufundisha na kuwabatiza, watu wa kila kabila, lugha, jamaa na taifa. Mtume Petro, licha ya kuwa hapo Mwanzo alimkana Bwana wake, anaimarishwa tena na anapewa jukumu la kuwa kiongozi mkuu wa kundi la Kristo. Kwa njia ya Roho Mtakatifu ambaye walimpokea siku ya Pentekoste, Mitume wanaanza tena kwa nguvu na ari kazi ya kuwa wavuvi wa watu. Wanamtangaza Kristo kwa ujasiri hata kuwa tayari kuteseka na watakufa kifo dini kwa ajili ya Injili. Sisi sote kwa njia ubatizo wetu, tunaalikwa kuacha maisha ya zamani na kuanza maisha mapya, kuishi maisha ya ushuhuda kwa njia ya Imani, maneno na matendo yetu, na kushiriki kazi ya kuwa wachungaji kila mmoja katika wito ambao Kristo amemwitia katika Kanisa. Kanisa limebaki imara chini ya Kristo, na li wazi kuwapokea watu wote.

Wavuvi wa watu
Wavuvi wa watu   (ANSA)

Somo la Injili: Ni Injili ya Yn 21:1-19. Ndugu wapendwa, somo la Injili Takatifu, Kristo anawatokea Mitume wake katika Bahari ya Tiberia. Ni Mitume saba kati ya Mitume wake kumi na mmoja ambao baada ya Yesu kuteswa, kufa na kuzikwa, walipoteza matumaini na kurejea katika kazi na maisha yao ya zamani, wanakwenda kuvua Samaki. Katika kazi yao ya kawaida, kazi ya kuvua samaki, Kristo Mfufuka anawatokea na kuwapa kazi kubwa isiyo ya kawaida, ya kuwa wavuvi wa watu. Kristo anawaalika kufungua kinywa, ishara ya ukarimu wa Kristo katika karamu ya Ekaristi, anawaimarisha Mitume wake kisha kuwapa kazi. Ni kazi ya kuwa wavuvi wa watu kwa njia ya kuhubiri Injili, kubatiza na kuwafanya watu kuwa wafuasi wa Kristo. Kanisa li wazi kuwapokea watu wote, na kwa kuwa li chini ya Kristo, daima litabaki imara na katika umoja, mithili ya jarife lile kubwa ambalo licha ya kuwa na Samaki wengi wa kila aina halikupasuka. Mtume Petro ambaye licha ya kwamba hapo Mwanzo alimkana Bwana wake mara tatu, anakabidhiwa wajibu mkubwa na Kristo wa kuwa kiongozi na mchugaji wa kundi la Kristo. Kristo anamtabiria Mtume Petro kwamba, kazi hiyo haitakuwa rahisi. Itampasa kupitia mateso, madhulumu, hata kufa kifo dini kwa ajili ya Bwana wake. Ndivyo ilivyokuwa pia kwa Mitume wengine wote isipokua mtume Yohane. Katika Somo hili la Injili Dominika ya Tatu ya Kipindi cha Pasaka tuna mafundisho saba ya kujifunza. Kwanza: Kristo Mfufuka anawapa matumaini mapya wafuasi wake, wanaacha maisha ya kale, wanaanza maisha mapya.

Mashuhuda wa Fumbo la Pasaka; Mateso, kifo na Ufufuko wa wafu
Mashuhuda wa Fumbo la Pasaka; Mateso, kifo na Ufufuko wa wafu   (@VATICAN MEDIA)

Mitume wa Yesu baada Yesu kuteswa na kufa ya walikata tamaa. Waliona hakuna tumaini tena na hivyo wakaamua kurudi katika maisha na kazi zao ambazo walizokuwa wakizifanya hapo mwanzo kabla hawajaitwa na Kristo ambapo wengi wao walikuwa ni wavuvi. Kristo Mfufuka anawatokea katika Bahari ya Tiberia. Katika hali hiyo ya mkato wa tamaa Yesu anawatokea na anawapokea tena na anawapa utume mpya. Ndugu mpendwa kuna nyakati katika maisha yetu tunapoteza matumaini kabisa. Pengine hali fulani tunazopitia katika maisha tunaona kama hakuna tumaini tena mbele. Tunahisi ukavu rohoni, imani inatetereka, matumaini yanafifia na kuona mbele hakuna njia tena. Kristo mfufuka anatokea kwetu kila siku kama alivyotokea kwa hawa mitume wake pale katika bahari ya Tiberia. Anatokea katika hali zetu za kawaida kabisa, hivyo hivyo anatuuliza swali lile lile alilowauliza mitume, Wanangu, mna kitoweo?Maneno haya ni maneno yanayoonesha mapendo ya kibaba, Kristo anayewajali na kuguswa na mahitaji ya mitume wake katika ukawaida wa hali zao. Sisi pia, mara zote tunapokata tamaa tusikie sauti hii ya ya upole ya Kristo mfufuka anayetuuliza, mwanangu, una amani? Una furaha moyoni? Familia yako ina amani?  Una matumaini na imani thabiti kwangu? Unaamini nguvu yangu itendayo kazi ndani mwako? Unaamini ninao uwezo wa kubadili historia yako, kuyabadili maisha yako nawe ukawa mpya tena? Unaamini nilikufa na kufufuka kwa ajili yako mwanangu mpendwa sana?  Haya ni maswali anatuuliza Yesu kila mara anapokuja kwangu mimi na wewe. Nasi tupate wasaa wa kumuuliza maswali, kumshirikisha hali zetu mbalimbali tunazopita, Yesu ni rafiki mwema, sio sisi tunamtatufa bali ni yeye aliyekuja kwangu mimi na wewe. Ninawaombea ndugu wapendwa, Kristo aseme nanyi, aseme na mioyo yenu katika hali zote. Awe faraja na kitulizo chetu sote hasa pale tunapopita katika bonde la uvuli wa mauti, tunapopita katika nyakati za giza, nyakati ngumu za kukatisha tamaa, tuone mwanga wa Kristo mfufuka ndani ya mioyo yetu.

Wito wa kwanza: Kutangaza Habari Njema ya Wokovu
Wito wa kwanza: Kutangaza Habari Njema ya Wokovu   (@Vatican Media)

Pili: Maisha na utume wetu unazaa matunda tunapoambatana na Kristo. Somo la Injili Takatifu latueleza kuwa, Mitume wakiongozwa na Petro walitoka kwenda kuvua samaki. Wanakwenda kuvua samaki lakini ndani mwao mawazo yao bado ni juu ya mambo yaliyotokea, kuhusu mateso na kifo cha Bwana na mwalimu wao. Wanakwenda bila matumaini, walishajikatia tamaa kabisa. Walipanda chomboni na usiku ule, pasi na matumaini tena kwa Kristo, hawakupata kitu chochote (Yn 21:3). Lakini asubuhi kulipokucha, Yesu alisimama ufuoni, akawaamuru walirushe jarife upande wa kuume wa chombo. Kwa Neno hili la Kristo walipata samaki wengi. Ndugu wapendwa, maisha yetu, utume wetu bila Yesu hatuwezi kufanikiwa kuzaa matunda. Mitume walikwenda bila Imani kwa Yesu ambaye kila mara aliwawezesha katika mambo mengi. Waliamini katika jitihada zao, waliamini katika ujuzi, akili na maarifa yao ya hapo mwanzo. Hii yatufundisha kuwa, akili, vipaji, karama, nguvu na uwezo wetu si kitu kama hatuongozwi na Neno la Kristo katika kufanikisha utume wetu katika maisha yetu sisi wafuasi wa Kristo. Hatuwezi kufanikiwa katika kazi zetu za kila siku, katika utume wetu tusipomruhusu Kristo aende nasi katika chombo chetu. Tusipomsikiliza Kristo akitufundisha ni wapi tutupe jarife ili tupate Samaki wengi. Kumbe twapaswa kila mara kusikiliza Neno la Kristo na kumpokea akae nasi katika vyombo vyetu. Akae katika familia zetu ili ziwe na amani na utulivu, akae katia nchi yetu ili iwe kielelezo cha haki, umoja, utu, uwajibikaji na amani ya kweli, akae katika jumuiya zetu ili ziwe vitalu vya upendo, huruma na mshikamano wa kweli. Mruhusu Yesu atembee nawe katika chombo chako, nawe utapata Samaki wengi.

Maisha mapya katika Roho Mtakatifu
Maisha mapya katika Roho Mtakatifu   (@VATICAN MEDIA)

Tatu: Kanisa li wazi kuwapokea watu wote, katika umoja na ushirika limesimama imara chini ya Kristo Mchungaji wetu. Mwinjili Yohane anatuambia kuwa, Mitume, kwa njia ya Neno la Kristo waliweza kupata Samaki wapatao mia Hamsini na watatu, hata hivyo, jarife (wavu) halikupasuka. Kwa nini mwijili Yohane anatupatia idadi hii ya Samaki ambao Mitume walipata? Mtakatifu Yeronimo, Mtaalamu wa Maandiko Matakatifu anatuambia kuwa, katika tamaduni za wagiriki, waliamini ya kuwa katika Bahari kulikua na aina 153 ya Samaki. Idadi hii ya Samaki yatuonesha kuwa utume wa Mitume hawa wa Yesu, utume wa Kanisa ni kuwakusanya watu wote. Wavu huu ambao licha ya kuwa na Samaki wengi haukupasua ni ishara ya uimara na umoja wa Kanisa ambalo licha ya kuwa na utofauti huu mkubwa wa watu, wema na wabaya bado limebaki imara kwa kuwa limejengwa juu ya mwamba imara, ndiye Kristo Mfufuka. Ndugu wapendwa, Kazi ya mitume ilikua ni kutangaza Habari Njema ya Injili kwa watu wa mataifa yote, na kuwabatiza na kuwafanya kuwa wanafunzi wa Kristo. Lipo wazi kuwapokea wote. Kanisa hili ni mali ya Kristo, licha ya tofauti zote hizo bado litaendelea kubaki imara. Tunapoombea umoja wa kanisa tunaombea pia umoja katika ngazi ya familia na jumuiya zetu. Tunaombea utayari wa kupokeana katika tofauti zetu, kuchukuliana kwa upole na kusaidiana ili sote tuweze kuupata uzima wa milele. Fotauti zetu zisiwe chanzo cha utengano bali sote tuwe na umoja kama Mungu wetu alivyo katika umoja na Mwana na Roho Mtakatifu.

Ukarimu wa Kristo Yesu katika Ekaristi Takatifu
Ukarimu wa Kristo Yesu katika Ekaristi Takatifu   (@VATICAN MEDIA)

Nne: Kristo Mkarimu anatulisha, anatuimarisha kwa Ekaristi Takatifu, kisha kututuma. Mara baada ya Mitume kuvuta jarife lilokuwa limejaa Samaki, Yesu anawaalika kufungua kinywa. Palikuwako na moto wa makaa na juu yake paemetiwa Samaki na mkate. Samaki na mkate ni ishara ya Ekaristi Takatifu, Kristo anayeendelea kila mara kuwalisha na kuwamirisha Mitume wake. Mitume hawakuthubutu kumwuliza wakijua ya kuwa ni Bwana. Mara baada ya tukio hilo, anawatuma Mitume wake, akimchagua Petro kuwa kiongozi na mchungaji wa kondoo wake. Ndugu wapendwa, Kristo mkarimu anatulisha kwa Ekaristi Takatifu. Yeye ndiye mwezeshaji na mtoaji wa ukarimu wote. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, tunapata nguvu na afya rohoni ya kusonga mbele katika utumishi wetu kwa Mungu na kwa ndugu zetu. Uwepo wa Kristo kati ya Mitume wake uliwapa nguvu ya kuvumilia na kuendelea mbele kwa Imani na matumaini kumtangaza Kristo kama tunavyoelezwa katika kitabu chote cha Matendo ya Mitume. Yesu yupo nasi mpaka utimilifu wa dahari. Tujongee kwake kila siku, tujipatie nguvu na afya rohoni mwetu ili tuwe imara katika kuendelea kumtumikia yeye. Yupo kati yetu katika maumbo ya mkate na divai, yupo daima katika Tabernaklo Takatifu, tuzungumze naye, tumshirikishe changamoto zetu mbalimbali ili atuimarishe na kutupa nguvu ya kuendelea kumshuhudia kwa maneno na kwa Matendo yetu. Tuanze na Mungu kila siku ya maisha yetu, na tumalize na Mungu. Tumpe nafasi tumpe muda atembee nasi.

Kristo Yesu anaendelea kukutana na waje wake katika Neno na Ekaristi
Kristo Yesu anaendelea kukutana na waje wake katika Neno na Ekaristi   (Vatican Media)

Tano: Kristo anamwimarisha Petro, anakuwa mpya tena katika imani matuamini na mapendo yake kwa Kristo. Kukutana kwa Petro na Kristo katika bahari ya Tiberia kwatueleza tendo la kukiri Imani la Mtume Petro ambaye hapo mwazoni alimkana Yesu mara tatu mbele ya baraza. Jibu lake la, Ndiyo Bwana, laonesha tendo la kukiri tena Imani na mapendo yake kwa Kristo. anamhoji mara tatu kusisitiza umuhimu wa mapendo ya Petro kwa Kristo akitegemewa kuwa kiongozi wa Mitume wengine. Lakini Neno “Upendo” lina maana tofauti katika mara hizi tatu ambazo Kristo alimhoji Petro.  Kwa mara ya kwanza na ya pili, Kristo anamuuliza, “Simoni wa Yohane, wewe wanipenda kuliko hawa? Neno Upendo hapa ni “Agape”, na huu ni upendo wa kimungu, kumaanisha, Petro uko tayari kunipenda hata kuutoa uhai wako? Petro hakuwa na upendo huu kwa kuwa alikwisha mkana Bwana wake. Hivyo Petro anajibu, “Phileō” yaani upendo wa kindugu tofauti na alichoulizwa na Kristo. Na kwa mara ya tatu, Yesu anamhoji, Simoni wa Yohane wanipenda? Neno analotumia Yesu hapa ni “Phileō” badala ya “Agape” akimuuliza Petro, unanipenda hivyo hivyo kama rafiki, kama ndugu? Petro analia machozi kwa kuwa Kristo amempokea tena licha ya kwamba yeye alimkataa na kumkana hapo Mwanzo. Utimilifu wa upend wa kimungu “Agape” utatimia kwa Petro kufa kifo dini kwa ajili Kristo hapo baadaye. Ndugu wapendwa, Yesu alimpokea Petro vile alivyo, na ndivyo Yesu anavyotupokea sisi sote. Anatuimarisha, anatutakasa na kutupa kazi ya kuwa wachungaji wa kondo wake. Kila mmoja apaswa kujibu swali hili la Kristo binafsi, kwamba, F, unanipenda kuliko hawa? Yesu hamlaumu Petro wala hamwaibishi bali anampokea na kumwimarisha na kumpatia wajibu mpya wa kulichunga kundi lake. Yesu anatupokea vile tulivyo. Katika madhaifu yetu anatukamilisha ili tuweze kustahili kuwa wafuasi wake kweli. Ni nafasi yakuulizana pia sisi kwa sisi ni kwa kiasi gani tunapendana? Baba ni nafasi ya kumuuliza mkeo, je wanipenda, Mama ni nafasi ya kumuuliza mume wako, je wanipenda? Mim kam padre, ninaupenda utume wangu kwa moyo? Nimampenda Kristo kweli aliyeniweka kuwa mhudumu wa mambo matakatifu katika kanisa lake? Vivyo hivyo Watoto kwa wazazi. Yesu anatukumbusha kuchuliana kama tulivyo na kupokeana katika madhaifu yetu, na kusaidiana ili tuendelee kukamilishana katika mapendo ya kweli.

Kristo Yesu anaendelea kukutana na waja wake katika NENO
Kristo Yesu anaendelea kukutana na waja wake katika NENO   (@Vatican Media)

Sita: Tunapoanguka katika ufuasi wetu kwa Kristo sio mwisho wa safari. Petro alipomkana Yesu mara tatu haikua mwisho wa historia yake. Yesu hakumwaibisha, Yesu hakumhukumu, Yesu anampa nafasi nyingine ya kuonesha mapendo yake ya kweli katika ufuasi wake mara baada ya kuimarishwa tena baada ya ufufuko wa Kristo.  Ndugu wapendwa, Yesu anashuka kila mara kutuinua tena pale tunaposhindwa katika utumishi wetu. Anatupa neema ya kutambua udhaifu wetu na kufanya majuto na mageuzi ya kweli katika ufuasi wetu. Mara nyingi tunaanguka katika ufuasi wetu kwa Kristo, Kristo bado anatupa nafasi ya kuendelea kuonesha kuwa anatupenda na sisi tunampenda na tuna shauku bado ya kutaka kuendelea kumtumikia. Tumwombe Kristo Yesu kama alivyomwinua Petro, licha ya udhaifu wake bado akamwimarisha, atuinue na kutuimarisha na sisi hasa pale tunapomwacha Bwana kwa sababu mbalimbali, pale tunaposhindwa kuwa waaminifu katika ndiyo yetu kwa Kristo, atupe moyo wa kuamka tena na kusonga mbele.

Waamini wasimame imara kulinda imani yao!
Waamini wasimame imara kulinda imani yao!   (@Vatican Media)

Saba: Kumfuasa Kristo yahitaji kujitoa sadaka. Mtume Petro anatabiriwa kufa kifo dini. Ufuasi wake kwa Kristo uliambatana na mateso na kifo, yeye pamoja na Mitume wengine isipokua Mtume Yohane. Kumbe hakuna ufuasi wa kweli bila sadaka na Msalaba. Ndugu wapendwa, ufuasi wetu kwa Kristo unaambatana na msalaba. Tukimfuata Kristo twapaswa kuelewa daima kwamba njia yake ndio njia yetu sote. Kumbe nyakati mbalimbali tunapopitia katika mateso na changamoto, tujipe moyo kwamba, Kristo alishinda, nasi tutashinda kwani tupo na Kristo, anayetutia nguvu. Somo la 1: Ni kitabu cha Matendo ya Mitume Mdo 5:27b-32, 40b-41. Mitume wa Yesu baada ya Pentekoste walianza kwa nguvu kumtangaza Kristo Mfufuka pasi na hofu na mashaka tena. Injili ikaanza kuenea kwa kasi katika Yerusalemu na baadaye hata nje ya Yerusalemu. Matokeo yake wanaitwa katika Baraza ya Wayahudi, Sanheldrin na kuonywa kutokuhubiri wala kusema tena juu ya habari ya Kristo Mfufuka. Mtume Petro, ambaye alipewa jukumu na Bwana wetu Yesu Kristo kuwa kiongozi, mchungaji na mlinzi wa kundi la Kristo anasimama kwa ujasiri kuzungumza kwa niaba ya Mitume. Petro hapepesi macho katika kuhubiri ukweli juu ya habari za Kristo Mfufuka akisisitiza kua wao ni mashahidi wa yale yote aliyoyatenda Kristo. Ndugu zangu katika somo hili la kwanza tuna mambo mawili ya kujifunza. Kwanza: Roho Mtakatifu aliwaimarisha Mitume, anatuimarisha nasi sote kumshuhudia Kristo Mfufuka. Mtume Petro pamoja na Mitume wengine baada kumpoke Roho Mtakaifu walikua na ujasiri wa kusimama na kumshuhudia Kristo tofauti na ilivyokua hapo mwanzoni. Tunaelezwa katika somo la Injili wengi walikata tamaa baada ya Yesu kufa lakini somo hili la matendo ya Mitume latueleza nguvu mpya waliyoipata Mitume baada ya pentekoste ya kumkiri Kristo Yesu na kusema ukweli bila kuogopa.

Kristo Mfufuka ni chemchemi ya matumaini mapya
Kristo Mfufuka ni chemchemi ya matumaini mapya   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ndugu wapendwa, sisi kama wabatizwa twapaswa kusimamia kwa maneno na kwa matendo yetu kweli ya Imani yetu. Twapaswa kuwa imara katika Imani yetu kwa kiishi kweli imani kwa matendo. Mara kadhaa tunaogopa kusema ukweli na kuishi vyema Imani yetu kwa kuogopa mateso, hasara, fedheha, kupoteza marafiki, kazi nk. Mitume walisimama na Injili, hawakusita kumtangaza Kristo hata walipotishwa kupigwa na kuteswa. Je mimi nipo imara kusimamia Imani yangu kwa maneno na kwa matendo yangu? Yesu atusaidie ili tumshuhudie bila hofu kwa maneno, kwa imani na kwa matendo yetu. Pili: Mitume walifurahi kushiriki mateso pamoja na Kristo, nasi yajapo mateso kwa sababu ya Kristo, tuwe tayari kuvumilia. Mitume mara baada ya kupigwa kwa sababu ya Imani yao, walifurahi kwa kuwa walishiriki mateso pamoja na Kristo. Hawakakukata tamaa wala hawakusita katika kuendelea kumtangaza Kristo. Kristo alimtabiria Petro kifo dini na hivyo walikufa pia Mitume wengine kwa kumshuhudia Kristo. Ndugu wapendwa, Kristo mfufuka anatupa nguvu ya kuunganisha mateso yetu na mateso yake. Tunapata mfano kutoka kwake yeye aliyeteseka, aliyedhulumiwa, aliyebeba msalaba na kuuwawa bila kosa, tunapata nguvu kwamba, kwa njia ya misalaba yetu, tutamwona Mungu. Tunaalikwa kuunganisha mateso yetu na mateso ya Kristo, huenda nimepitia katika magonjwa yasiyotibika, au ninapitia katika changamoto nyingine mbalimbali, Kristo anatupa nguvu na sababu ya kuendela kuwa imara.

Kristo Mfufuka
Kristo Mfufuka   (AFP or licensors)

Somo la Pili: Ni kitabu cha Ufunuo wa Yohane 5:11-14. Mwandishi wa kitabu hiki, Mtume Yohane, aliwaandikia Wakristo waliokuwa wakiteseka katika kisiwa cha Patmos katika Asia ndogo, ili kuwapa moyo na kuwaimarisha Imani yao katika nyakati ngumu utumwa na mateso kutoka kwa watawala wa Kirumi. Somo hili lamwelezea Kristo Mwanakondoo aliyejitoa sadaka kwa ajili yetu sote astahili sifa na heshima ya pekee. Tunaadhimisha sadaka hii ya Kristo ambayo kwayo imetupatia sisi ukombozi wa milele katika Adhimisho la Misa takatifu, ambapo tunaungana na viumbe vyote vya mbinguni kumtukuza Mungu kwa zawadi ya ukombozi kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Ni kwa njia ya sadaka yake sisi sote tumefanywa upya, tumeimarishwa na kutumwa kuwa mashuda wake katika ulimwengu mzima. Hitimisho: Sisi sote kwa njia ubatizo wetu, tunaalikwa kuacha maisha ya zamani na kuanza maisha mapya, kuishi maisha ya ushuhuda kwa njia ya Imani, maneno na matendo yetu, na kushiriki kazi ya kuwa wachungaji kila mmoja katika wito ambao Kristo amemwitia katika Kanisa. Kanisa limebaki imara chini ya Kristo, na li wazi kuwapokea watu wote.

Tafakari D3 Pasaka
03 Mei 2025, 15:33