Tafuta

Wanaitwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili bila woga wala wasi wasi. Wanaitwa kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili bila woga wala wasi wasi. 

Tafakari Dominika ya Tatu ya Pasaka! Mashuhuda wa Ukweli

Waamini wanaalikwa kumtangaza Kristo Mfufuka bila hofu kama walivyofanya Mitume wakisema; “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.” Ili tuweze kuwa na ujasiri huu yatupasa kumtumainia Roho Mtakatifu ili atujalie nguvu na ujasiri wa kutangaza habari za ufufuko wa Kristo na za mafundisho yake bila woga. Ndivyo ilivyokuwa kwa Mitume ambapo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu walimshuhudia Kristo mfufuka, na mafundisho yao ya kijasiri yaliwatia woga viongozi!

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 3 ya Pasaka, mwaka C wa Kiliturujia katika Kanisa. Masomo ya dominika hii yanatutaka tuwe watii kwa Mungu katika kuiishi na kuishuhudia imani yetu kwa Kristo Mfufuka bila kuogopa mamlaka ya kidunia kwa maana ufufuko wake ni tunda la utii wake kwa Mungu Baba kwa Yeye kukubali kufa msalabani ili kutukomboa sisi. Ni katika tumaini hili Mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, watu wako na waone furaha siku zote kwa ajili ya kutiwa nguvu mpya roho zao. Kwa vile sasa wanafurahi kwa kurudishiwa ile heshima ya kuwa wana wako, waitazamie ile siku ya kufufuka kwao, wakitumaini kupewa pongezi”. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika unatualika kufurahi ukisema; “Mpigieni Mungu kelele za shangwe, nchi yote, imbeni utukufu wa jina lake. Tukuzeni sifa zake, aleluya (Zab. 66:1-2)  Somo la kwanza ni la kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo. 5:27b-32,40b-41). Somo hili linatutaka kumshuhudia Kristo Mfufuka bila hofu kama walivyofanya Mitume wakisema; “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.” Ili tuweze kuwa na ujasiri huu yatupasa kumtumainia Roho Mtakatifu ili atujalie nguvu na ujasiri wa kutangaza habari za ufufuko wa Kristo na za mafundisho yake bila woga. Ndivyo ilivyokuwa kwa Mitume ambapo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu walimshuhudia Kristo mfufuka, na mafundisho yao ya kijasiri yaliwatia woga viongozi na wakuu wa wayahudi wakajawa mashaka na hofu nyingi kwamba watu wangeweza kulipiza kisasi kwa kosa lao la kumuuua Kristo bila kosa wala hatia yoyote. Hivyo walitumia nguvu nyingi sana kuwanyamazisha bila mafanikio. Ndiyo maana Kuhani Mkuu akiwaonya Mitume anasema hivi: “Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina la mtu huyu? Tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu.”

Waamini wanaalikwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo kwa maisha yao
Waamini wanaalikwa kumtangaza na kumshuhudia Kristo kwa maisha yao

Lakini msimamo wa Mitume ulibaki ule ule wakisema; “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.” Wakasisitiza kusema; “Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimuua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio.” Baada ya ushuhuda huu mitume walipigwa sana na kuamuriwa kuacha kumtangaza Kristo. Lakini wao walifurahi sana kwa kuwa waliaibishwa kwa ajili ya Kristo. Hivyo habari za Yesu Kristo mfufuka ziliendelea kuenea kama moto wa kiangazi. Basi nasi yatupaswa kumtii Mungu na sio wanadamu ili tuweze nasi kuibuka washindi na kuingia katika uzima wa milele. Maana Mungu akiwa upande wetu hakuna wa kututisha wala wa kushindana nasi na kutushinda. Ni katika muktadha huu wimbo wa katikati unasema hivi; “Ee Bwana, Mungu wangu, nalikulilia ukaniponya. Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua, wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu. Umeniita nafsi yangu, Ee Bwana, kutoka kuzimu, umenihuisha na kunitoa miongoni mwao washukao shimoni. Mwimbieni Bwana zaburi, enyi watauwa wake, na kufanya shukrani kwa kumbukumbu la utakatifu wake. Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo, katika radhi yake mna uhai. Huenda kilio huja kukaa usiku, lakini asubuhi huwa furaha. Ee Bwana, usikie, unirehemu, Bwana, uwe msaidizi wangu. Uligeuza matanga yangu kuwa machezo; Ulinivua gunia, ukanivika furaha. Ee Bwana, Mungu wangu, nitakushukuru milele” (Zab. 30:1, 3, 5, 10-12). Hivi ndivyo inavyokuwa kwao wamtumainiye Mungu wa kweli.

Imewapasa waamini kumtii Mungu kuliko wanadamu!
Imewapasa waamini kumtii Mungu kuliko wanadamu!

Somo la pili ni la Kitabu cha Ufunuo wa Yohane (Ufu. 5:11-14). Somo hili linatueleza kuwa Mwanakondoo aliyejitolea kuwa sadaka kwa ajili yetu, Yesu Mfufuka, anastahili sifa na heshima ya pekee. Kwa kumhimidi yeye, viumbe vyote vya mbinguni na duniani vinashiriki utukufu wa huyo Mwana Kondoo na heri ya mbingu. Injili ni ilivyoandikwa na Yohane (Yn. 21:1-19). Sehemu hii ya Injili inatueleza mambo makuu matatu: Yesu mfufuka kujidhihirisha kwa Mitume wakivua samaki; Yesu kuwaalika wanafunzi kufungua kinywa kwa kula samaki na mkate wa kuokwa, ishara ya Ekaristi Takatifu, na Yesu kumkabidhi Simoni Petro Kanisa lake kuwa mchungaji mkuu. Mambo haya yanafanyika Yesu mfufuka alipowatokea mara ya tatu wanafunzi wake wakiwa wamerudi katika kazi yao ya awali kabla ya kuwaita, kazi ya kuvua samaki. Petro anakabidhiwa kanisa baada ya kuulizwa swali mara tatu, Simoni wa Yohane wanipenda. Baada ya Petro kujibu kwa mfadhaiko mara ya tatu Bwana wewe wajua kuwa na kupenda, Kristo alimpa mamlaka ya kuliongoza Kanisa lake alilolianzisha Mwenyewe kwa kumpa madaraka na mamlaka kamili juu ya Kanisa. Yesu anatimiza kile alichomwahidi Petro baada ya kukiri ukuu wake akisema; “Wewe ndiwe Kristo mwana wa Mungu aliye hai” (Mt 16:16).  Naye Yesu alimwambia: “wewe ndiwe Petro na juu ya mwamba huu nitalijenga kanisa langu” (Mt 16:18). Mamlaka na madaraka haya anayapokea kila Baba mtakatifu, halifa wa mtume Petro anapochaguliwa kadiri ya mapokeo ya Kanisa.

Hayati Papa Francisko alikuwa ni shuhuda wa huruma ya Mungu
Hayati Papa Francisko alikuwa ni shuhuda wa huruma ya Mungu   (ANSA)

Katika somo hili tunajifunza kuwa imani kwa Yesu Mfufuka ni zawadi kutoka kwa Mungu naye huwapatia wanyofu na wanyenyekevu wa moyo ambao wako tayari kuipokea kwa upendo. Ni kutokana na upendo wake kwa Yesu, Yohani alikuwa wa kwanza kumtambua Yesu mfufuka. Tunasoma hivi; “Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro; “Ndiye Bwana” (Yn 21:7). Kwa upande mwingine Petro alipoona mambo ya Ufufuko wa Yesu hayaeleweki aliwaambia ndugu zake; “Naenda kuvua samaki” kwa maana alichokitegemea hakukiona hivyo aliamua kurudia maisha yake ya zamani. Baada ya mfungo wa Kwaresima na Pasaka, tumeamua kuanza maisha mapya. Lakini matatizo bado yanaendelea, tusipokuwa na Imani katika ufufuko tunaweza kujikuta tumerudi tulikotoka. Ndivyo ilivyokuwa kwa Waisraeli, walipotolewa Misri wakapigwa njaa jangwani wakamnung’unikia Mungu wakisema; “Afadhali tungekufa Misri kwenye masufuria ya nyama” (Hes.14:4). Sisi tukumbuke kuwa ingawa maisha ya ukristu yana mateso, lakini mwisho wake ni uzima wa milele. Kwa Ubatizo na kwa Kipaimara tumepokea kutoka kwa Roho Mtakatifu paji la uimara. Tutumie paji hili kuilinda imani yetu kwa Kristo mfufuka kwani anastahili yeye Mwana-Kondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri, hekima na nguvu, heshima na utukufu. Baraka na heshima, utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, hata milele na milele. Basi tujitahidi kuwa mashuhuda wa ufufuko wa Kristo Yesu kwa kuukubali ukweli huu kuwa chanzo cha matumaini yetu kuwa baada ya maisha ya hapa duniani tutavikwa furaha ya uzima wa milele mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana tunakuomba dhabihu za Kanisa lako linalofanya shangwe. Na kama ulivyolifanya lifurahi sana sasa, ulijalie pia furaha ya milele”. Na katika sala baada ya komunyo anahitimisha maadhimisho ya dominika hii akisali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba utuangalie kwa wema sisi taifa lako. Utujalie tufufuke na miili mitukufu, sisi ambao umependa kutufanya wapya kwa mafumbo haya ya milele”. Na hili ndilo tumaini letu. Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika 3 Pasaka C
02 Mei 2025, 16:14