Tafuta

Mzee Cleopa David Msuya amefariki dunia tarehe 7 Mei 2025 Jijini Dar es Salaam na kuzikwa nyumbani kwake Usangi, Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro Mzee Cleopa David Msuya amefariki dunia tarehe 7 Mei 2025 Jijini Dar es Salaam na kuzikwa nyumbani kwake Usangi, Wilaya ya Mwanga Mkoani Kilimanjaro 

Wasifu wa Hayati Cleopa David Msuya! Shujaa wa Tanzania

Rais Samia Suluhu Hassan ameongoza viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, familia na maelfu ya wananchi katika maziko ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Cleopa David Msuya aliyefariki mnamo Mei 7 Mwaka 2025 kwa ugonjwa wa moyo wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mzena, iliyoko jijini Dar es Salaam na maziko yamefanyika nyumbani kwake Usangi wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro Mnamo Mei 13 mwaka 2025.

Sarah Pelaji, - Vatican

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassan ameongoza viongozi mbalimbali wa Chama na Serikali, familia na maelfu ya wananchi katika maziko ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Kwanza wa Tanzania Hayati Cleopa David Msuya aliyefariki mnamo Mei 7 Mwaka 2025 kwa ugonjwa wa moyo wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Mzena, iliyoko jijini Dar es Salaam na maziko yamefanyika nyumbani kwake Usangi wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro Mnamo Mei 13 mwaka 2025. Akiwa mwamini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri la Tanzania, KKKT Askofu Mkuu Malasusa ameongoza ibada ya mazishi ya   Hayati Cleopa Msuya katika Usharika wa Usangi Kivindu. Askofu Dkt. Alex Gehaz Malasusa wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ambaye pia ni Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania katika mahubiri yake amesema viongozi wengi wamepoteza unyenyekevu kwa watu wanaowahudumia huku akisema wengine wanashindwa kutumia vizuri ndimi zao. Amesema Hayati Cleopa Msuya alitumia vyema muda wake na kuwaweka watu aliokuwa anawahudumia kuwa kipaumbele chake. “Tukijua kwamba hapa ulimwenguni tunaishi kwa kitambo kidogo hivyo tuishi kwa kuwajali wengine. Ushuhuda wa Mzee Msuya unanishangaza sana kwani wengi walio na nafasi za juu kama alizoshika yeye na wengi wa nafasi za chini yake wote wanamsifu sana. Hawa wa chini ndiyo tulio wengi viongozi tunashindwa kwa sababu hatuongozi kwa kuwapa vipaumbele watu wetu. Mzee Msuya anaitwa “Baba wa Mwanga” si kwa sababu ya uzee bali kwa alama ya upendo, utumishi na unyenyekevu kwa wale walio chini yake. “Mungu akitupa nafasi tulizonazo ili tuwaangalie wa chini ni kwasababu walio juu ni wachache hivyo tuna wajibu wa kuwafanya walio wengi chini yetu watabasamu,” amesema.

Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania wakati wa maombolezi ya Mzee Msuya
Rais Samia Suluhu Hassan wa Tanzania wakati wa maombolezi ya Mzee Msuya

Job Msuya, Mtoto wa Mzee Cleopa David Msuya amesema, Baba yake Mzazi Mzee Msuya alitoa kipaumbele cha pekee kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Januri 4, 2025 ilikuwa ni siku yake ya kuzaliwa, katika maadhimisho haya, aliagiza kama sehemu ya kumbukumbu yake endelevu kijengwe Chuo Kikuu Mwanga cha "Brain Power Technology, au IT pamoja na Benki ya Hakika Mwanga Bank. Mambo haya yawe ni kumbukumbu kwa Wilaya ya Mwanga, Mkoani Kilimanjaro. Job Msuya anasema, katika umri wake wa miaka 54 kikubwa alichojifunza kutoka kwa Baba yake Mzazi ni kujipambania katika maisha na kutafuta kile kilicho chako: Hakuwa ni mtu rahisi kutoa fedha kwa watoto wake.

Hayati Cleopa Msuya aliwafundisha watoto wake kujitegemea
Hayati Cleopa Msuya aliwafundisha watoto wake kujitegemea

Katibu Mkuu Utumishi Juma Mkumi ameeleza wasifu wa Hayati Cleopa Msuya kwa namna alivyolitumikia taifa la Tanzania katika ngazi mbalimbali za Serikali, Chama cha Mapinduzi CCM na jamii. Juma Mkumi alieleza kuwa, Hayati Cleopa Msuya alizaliwa tarehe 4 Januari 1931 katika kijiji cha Chomvu, kata ya Chomvu, tarafa ya Usangi, wilaya ya Mwanga mkoani Kilimanjaro. Ni mtoto wa tano kati ya watoto 9 wa Marehemu Mzee David Kilenga Msuya. Alisoma Elimu ya Msingi Kivindu kati ya mwaka 1939 -1942. Alisoma elimu ya Kati Usangi mwaka 1943. Alisoma elimu ya sekondari katika sekondari ya Old Mosh mwaka 1944 na kuhitimu kidato cha nne mwaka 1949. Aliendelea na elimu ya sekondari ya “Adavanced Level” Tabora mwaka 1950 na kuhitimu kidato cha sita mwaka 1951 kuzawadia cheti kutoka Chuo Kikuu cha Cambridge, Uingereza. Alijiunga na Elimu ya Chuo Kikuu cha Makerere nchini Uganda mwaka 1952 ambako alisoma na akahitimu na kutunukiwa shahada ya kwanza ya Sanaa, Sayansi ya siasa sayansi ya sanaa na Jiografia mwaka 1955.  Hayati Cleopa David Msuya alijiunga na utumishi wa serikali na kutekeleza kazi na nyadhifa mbalimbali kama ifuatavyo: Mwaka 1961-1964 alikuwa Naibu Kamishina wa Maendeleo ya Jamii katika Serikali ya Tanganyika. Mwaka 1964-1965 alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii na Utamaduni wa Taifa. Mwaka 1965-1967 alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Makazi na Maendeleo ya Maji. Mwaka 1967-1970 alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi na Mipango. Mwaka 1970-1972 alikuwa Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Hazina.

Askofu mkuu Dkt Alex Malasusa akiongoza Ibada ya Mazishi ya Mzee Msuya
Askofu mkuu Dkt Alex Malasusa akiongoza Ibada ya Mazishi ya Mzee Msuya

Hayati Cleopa David Msuya alijiunga na utumishi wa kisiasa kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge na Waziri katika wizara mbalimbali ikiwemo, Mwaka 1972 -1975 aliteuliwa kuwa Mbunge wa Mwanga Mkoa wa Kilimanjaro na Waziri wa Fedha. Mwaka 1975 -1980 aliteuliwa kuwa Mbunge wa Mwanga na Waziri wa Viwanda. Mwka 1980-1983 aliteuliwa kuwa Mbunge wa Mwanga na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwaka 1983 -1985 aliteuliwa kuwa mbunge wa Mwanga na aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha. Mwaka 1985-1990 aliteuliwa kuwa Mbunge wa Mwanga na Waziri wa Fedha, Uchumi na Mipango. Mwaka 1990-1994 aliteuliwa kuwa mbunge wa Mwanga na Waziri wa Viwanda na Biashara. Mwaka 1994-1995 alikuwa Makamu wa Kwanza wa Rais na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwaka 1995-2000 alikuwa mbunge wa Jimbo la Mwanga.Mnamo tarehe 29 Oktoba mwaka 2000 alitangaza kung’atuka kama mbunge wa Jimbo la Mwanga na kustaafu Utumishi wa umma na kisiasa. Hayati Cleopa Msuya alikuwa mwanachama hai wa TANU mwaka 1964-1977 na alikuwa mmoja wa waasisi wa Chama cha Mapinduzi kilichozaliwa Mnamo Tarehe 5 Februari mwaka 1977. Alishika nyadhifa mbalimbali katika utumishi wa Chama ambapo mwaka 1982-1992 alikuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi CCM. Mwaka 1992-1995 alikuwa Mjumbe wa Kamati Ku una Halmashauri ya CCM. Mwaka 1995 katika uchaguzi wa awali ndani ya Chama cha Mapinduzi alichaguliwa kuwa mmoja wa wagombea watatu wa kuwania nafasi ya Urais uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria mazishi ya Mzee Msuya
Baadhi ya viongozi waliohudhuria mazishi ya Mzee Msuya

Mwaka 2012-2014 aliendelea kushika nafasi muhimu za Chama katika ngazi ya Wilaya ya Mwanga na mkoa wa Kilimanjaro. Wakati huo alikuwa ameshatangaza kung’atuka shughuli za ubunge na za serikali hivyo aliamua kurudi nyumbani kwao Mwanga Kilimanjaro kutumikia wananchi. Hayati Cleopa Msuya alifanya kazi mbalimbali za huduma na uongozi ambapo mwaka 1983 -1990 aliongoza timu ya Serikali iliyoandaa kusimamia programu ya maboresho na kufufua uchumi wa Tanzania. Mwaka 1994-2012 alikuwa Mwenyekiti wa “Community Development Trust Fund.” Mwaka 2007-2021 alikuwa Mkuu wa Chuo Kikuu cha Ardhi Dar es Salaam. Mwaka 2004- 2019 alikuwa Mwenyekiti wa Kilimanjaro Development Forum. Mwaka 2007 -2021 alikuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Tanzania Brueries ltd. Mwaka 2014 Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga ilimpatia heshima ya kumuita Baba wa Mwanga. Hayati Cleopa Msuya alifanya pia kazi katika taasisi za kikanda na kimataifa ambapo kama Katibu Mkuu na Waziri aliwakilisha nchi ya Tanzania katika taasisi za kikanda na Kimataifa kuongoza kundi la Afrika katika Caribian na Pacific na Jumuiya ya Ulaya. Aliwakilisha Tanzania katika Afrika Mashariki Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, Tume ya Uchumi ya Umoja wa Mataifa Afrika na eneo maalumu la biashara la Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika. Pia alijenga ushirikiano na dunia na taasisi nyingine za kifedha na hazina akiwa Waziri wa Fedha.

Mzee Malecela akiwa katika majonzi makubwa kwa kifo cha Mzee Msuya
Mzee Malecela akiwa katika majonzi makubwa kwa kifo cha Mzee Msuya

Alikuwa pia na uzoefu katika Maendeleo ya kiuchumi na kujikita zaidi na maendeleo ya kilimo, vijiji na maendeleo ya jamii. Pia alijikita zaidi na usiamamizi wa Fedha na Umma, Uendelezaji wa viwanda na biashara hususani uanzishwaji wa vyuo vya ufundi VETA na mafunzo ya ujasiriamali na uendelezaji wa viwanda vidogo vidogo yaani SIDO. Pia alishiriki majadiliano ya kikanda na matengemano ya kiuchumi na mipango ya usimamizi wa uchumi. Baada ya kumaliza shughuli za kiserikali aliwekeza nguvu zake katika kilimo, maendeleo ya jamii, fedha na uwekezaji. Hayati Cleop David Msuya alipata nishani mbalimbali ikiwemo nishani ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Nishani ya Mwenge wa Uhuru Daraja la II mwaka 1961 hadi 2011. Alipata hati ya Heshima ya Muungano Daraja la I mwaka 1964 na 2014. Alikuwa mwamini wa KKKT na alipendelea kufanya ibada kutokana na taratibu za Kanisa hilo na Neno la Mungu. Katika maisha ya familia alimuoa Bi. Rhoda Christopha Mshana mnamo Januari 11 mwaka 1959 ambaye alifariki Agosti 1 mwaka 2005. Alijaliwa kupata watoto sita ambapo wanne ni wa kiume na wawili wa kike na wajukuu 10. Mhe. Cleopa Msuya enzi za uhai wake alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa moyo na kupata matibabu katika hospitali mbalimbali ikiwemo ya Mzena na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Dar es Salaam. Alikuwa pia akipatiwa matibabu ya kina nchini Uingereza mwaka 2022. Alifariki Mei 7 mwaka 2025 akiwa na umri wa miaka 94 katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu. Viongozi wengine walioshiriki katika maziko hayo ni Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi, Makamu wa Rais Dk Philip Mpango, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nnne Mheshimiwa Jakaya Kikwete, Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson, Katibu Mkuu CCM Dk Emmanuel Nchimbi, Mkuu wa Jeshi la Polisi IGP Camillus Wambura, Waziri Mkuu Mstaafu John Maleceala, Waziri Mkuu Mstaafu Fredrick Sumaye na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali.

Wasifu wa Cleopa Msuya
14 Mei 2025, 17:18