Tafuta

Injili ya Yesu Injili ya Yesu  

Dominika ya 24 Mwaka C:Huruma ya Mungu ni ya milele

Habari njema ni hii,pamoja na makosa na dhambi zake zote,mwana mpotevu alipojichunguza moyoni,alijutia maovu yake na njia yake mbaya,akaamua kurudi kwa Baba yake na kuomba msamaha.Matunda ya toba yake ni msamaha na kufanywa tena mwana katika familia.Hii inatuonyesha kuwa huruma ya Mungu ni ya milele na upendo wake kwetu sisi wanae ni mkubwa kiasi kwamba,hakuna dhambi ambayo Mungu hawezi kuisamehe isipokuwa ya kufuru kwa Roho Mtakatifu, yaani kukata tamaa.

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 24 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe mkuu wa masomo ya dominika hii ni kuwa; Huruma ya Mungu ni ya milele. Mungu daima yuko tayari kumsamehe mkosefu anayetubu, na anafurahi kusamehe, na furaha ya kweli kwa mwanadamu imo katika kung’amua kwamba amesamehewa na Mungu, baada ya kukiri na kutubu makosa yake, na hivyo anakuwa na amani tele moyoni mwake. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii unasema hivi; “Ee Bwana, uwape amani wakungojao, ili watu wawasadiki manabii wako; usikilize sala ya mtumwa wako, na ya taifa lako Israeli” (Taz. 27:30-28:1-7). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu uliye Mwumba na Mwongozi wa vitu vyote, ututazame, utuwezeshe kukutumikia kwa moyo wote, ili tupate baraka ya huruma yako”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Kutoka (Kut 32:7-11, 13-14). Somo hili linasimulia uasi wa wana wa Israeli kwa kujiharibu nafsi zao, na kupotoka kwao kwa kuiacha njia aliyowaamuru Mungu, wakajifanyizia ndama ya dhahabu, wakaiabudi na kuitolea dhabihu kama miungu yako. Kwa tendo hili waliivunja amri ya kwanza ya Mungu – “Ndimi Bwana Mungu wako usiwe na miungu mingine” (KKK 2084-2141), wakavunja na Agano walilofanya Naye chini ya mlima Sinai baada ya kuwatoa utumwani Misri (Kut 20:2-6). Kwa kutenda dhambi hii, Mungu aliazimia kuwaangamiza na kuunda taifa jingine jipya. Musa alichukua jukumu la kikuhani na kinabii, akaliombea msamaha Taifa lake, akitumaini katika upendo wa Mungu na huruma yake kuu. Kwa sala na maombi ya Musa, Mungu aliwasamehe wana wa Israeli, akaghairi kuwaangamiza. Ujumbe kwetu ni huu; tukitambua, tukajuta na kukiri dhambi zetu, Mungu Baba yetu ni mwenye huruma atatusamehe na kututakasa na uovu wetu wote.

Ngano
Ngano

Ni katika muktadha huu wimbo wa katikati unasema hivi; “Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu. Ee Mungu, unirehemu, sawa sawa na fadhili zako. Kiasi cha wingi wa rehema zako, uyafute makosa yangu. Unioshe kabisa na uovu wangu, na dhambi yangu i mbele yangu daima. Ee Mungu, uniumbie moyo safi, uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu. Usinitenge na uso wako, wala roho yako takatifu usiniondolee. Ee Bwana, uifumbue midomo yangu, na kinywa changu kitazinena sifa zako. Dhabihu za Mungu ni roho iliyovunjika, moyo uliovunjika na kupondeka, Ee Mungu, hutaudharau (Lk. 15:18; Zab. 51:1-2, 10-11, 15, 17).

Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Timoteo (1Tim 1:12-17). Huu ni waraka wa kichungaji aliomwandikia Timoteo Askofu wa Efeso, akimtia moyo akijua wazi kuwa atapata magumu katika kuihubiri Injili, waamini wataweza kukata tamaa watakapokumbana na madhulumu na mateso, mashaka na wasiwasi vitatawala, migawanyiko itatokea. Lakini asiogope kwani Kristo Yesu yuko pamoja naye. Mtume Paulo anasisitiza juu ya huruma ya Mungu na furaha aipatayo mdhambi anaposamehewa, yeye akiwa ni mfano hai. Hivyo anamshukuru Mungu kwa kumsamahe kwa njia ya Kristo dhambi zake alizozifanya ambazo zilikuwa ni matokeo ya ujinga, na kutokuwa na imani sahihi. Lakini kwa neema na upendo wa Kristo aliweza kuongoka akiwa njiani kuelekea Damasko kuwakamata, kuwatesa na kuwaua wafuasi wa Kristo. Hivyo maisha yake yalibadilika na kuwa ya furaha kwa kukiri na kutubu makosa yake na kuanza maisha mapya. Hivyo anatutia moyo kuwa kama Mungu aliweza kumsamehe yeye aliyekuwa mtesi wa Kanisa, na kumfanya kuwa mtume; basi yeyote yule anayetubu makosa yake atapokea msamaha. Nasi tusiwe na mashaka juu ya huruma ya Mungu ili kwayo tupate uzima wa milele, kwake yeye aliye mfalme wa milele, asiye kufa, asiyeonekana, yaani Mungu Baba. Yote ni kwa heshima na utukufu wake milele na milele. Amina (1Tim 1:17).

Mungu anafurahi kwa mtoto anayerudi na kutubu
Mungu anafurahi kwa mtoto anayerudi na kutubu

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 15:1-32). Sehemu hii inaweka bayana huruma ya Mungu isiyo na mipaka kwa kutumia mifano mitatu; Kondoo aliyepotea (Lk 15:4-7), shilingi iliopotea (Lk 15:8-10), na Mwana mpotevu (Lk 15:11-32), ikisistiza juu ya furaha ilivyo kuu mbinguni, mkosefu anapotubu na kumrudia Mungu. Mifano hii Yesu anaitumia kuwafundisha Mafarisayo na Waandishi – na wote wale katika nyakati zetu – kwa kuwa na chuki kwa wakosefu na wadhambi, na kumhukumu Yesu na mitume wake wa kipindi hicho na sasa, kwa kuwapokea na kushiriki nao chakula. Tunasoma hivi; “Watoza ushuru na wote wenye dhambi walikuwa wakimkaribia wamsikilize. Nao Mafarisayo walimnung’unikia Yesu wakisema; “Mtu huyu huwakaribisha wenye dhambi na kula nao” (Lk 15:1-2).

Bwana ni mchungaji wa Kondoo na kumtafuta anayepotea
Bwana ni mchungaji wa Kondoo na kumtafuta anayepotea

Mifano miwili ya mwanzo, yaani kondoo aliyepotea na shilingi iliopotea, inasisitiza jinsi Mungu anavyowatafuta wanawe waliopotea. Hivyo, asili ya fumbo la ukombozi wetu ni Mungu mwenyewe. Nasi tunaaswa kuwatafuta na kuwasamehe waliotukosea, kwa maana msamaha huanza kutolewa na aliyekosewa. Na mfano wa Baba mwenye huruma kwa mwanae aliyepotea unasisitiza namna Mungu anavyoheshimu uhuru wa kila mwanadamu. Mungu hatushurutishi kutambua makosa yetu, kuyajutia, kuyakiri, wala kurudi kwake na kuomba msamaha. Lakini kwa saburi anatusubiri turudi na kusema nimekosa nihurumie, naye daima anamsamehe na kumfanya tena mtoto wake kwa kumkaribisha katika karamu ya uzima wa milele, kila anayetubu na kuomba masamaha, bila kuangalia idadi ya makosa yake. Ni wazi makosa ya mwana mpotevu ni mengi na mazito, lakini alisamehewa yote. Alidai urithi kwa baba yake wakati angali hai. Hii ni sawa na kusema: “Baba utakufa lini? Baba kwanini unachelewa kufa? Baba huoni kuwa mda wako wa kuishi umeisha, kwa nini unaendelea kutuzibia riziki yetu?” Pili aliuza urithi wake, na hivyo kuihujumu familia yake kwa kutoiachia urithi tena, na kuinyima huduma yake. Tatu alikwenda nchi ya mbali, ndiyo kusema dhambi inamfanya mdhambi kujitenga na Mungu, na sio Mungu kujitenga na mdhambi. Tunapotenda dhambi tunajitenga na Mungu, tunakuwa mbali naye. Matokeo yake tunakuwa gizani, tunakuwa na huzuni na masikitiko, furaha na amani vinatoweka moyoni, ndio mwanzo wa kuukosa uzima wa milele.

Baada ya kuishiwa urithi na mali zote, mwana mpotevu alijishikamanisha na mtu tajiri, na kufanywa mtumwa wa kulisha nguruwe, mnyama najisi, mchafu, haramu kwa wa Isaraeli (Walawi 11:17, Kumb 14: 8). Hii ni hatua ya kutisha kabisa kutoka kuwa mwana – mtu huru –hadi kuwa mtumwa. Hii ni sawa na kuwa chini ya himaya ya shetani, ambaye daima anatuhadaa kwa kutushawishi kutenda dhambi kwa ahadi zake nzuri na za kuvutia. Lakini baada ya kutenda dhambi, ahadi zake hutoweka, badala raha, anatulipa aibu, mateso na mahangaiko. Habari njema ni hii, pamoja na makosa na dhambi zake zote, mwana mpotevu alipojichunguza moyoni, alijutia maovu yake na njia yake mbaya, akaamua kurudi kwa Baba yake na kuomba msamaha. Matunda ya toba yake ni msamaha na kufanywa tena mwana katika familia. Hii inatuonyesha kuwa huruma ya Mungu ni ya milele na upendo wake kwetu sisi wanae ni mkubwa kiasi kwamba, hakuna dhambi ambayo Mungu hawezi kuisamehe isipokuwa ya kufuru kwa Roho Mtakatifu, yaani kukata tamaa na kushindwa kuomba msamaha.

Kwa upande mwingine yule mwana wa pili – mkubwa, naye tunaweza kusema kuwa alipotea, lakini ndani ya nyumba kama shilingi. Kwa kiburi, chuki na wivu anamkataa ndugu yake kwa kukataa kufurahi pamoja na Baba yake. Kila mmoja ajiulize yeye ni yupi, aliyepotea ndani ya nyumba kama shilingi, au aliyepotea nje ya nyumba kama kondoo nyikani? Kanisa ni jumuiya ya wenye dhambi waliosamehewa. Je, sisi nasi hatupo kama kijana wa pili? Je hatuwatengi na kuwalaani waliovunjika moyo kwa dhambi zao? Tukumbuke daima kuwa dhambi inatufanya kuwa watumwa. Lakini ni huruma ya Mungu tu ndiyo inayoweza kutuweka huru na kutufanya wanae tena. Zaidi sana simulizi hili linatufundisha kuwa kila mwanadamu ana makosa na dhambi zake, anapotea kwa namna yake. Lakini hatupaswi kukata tamaa tunapokosea na kuangua dhambini, bali tuzingatie moyoni ukuu wa upendo na huruma ya Mungu Baba, tujirudi na kujisemea moyoni; Nitaondoka nitakwenda kwa niliyemkosea, baba, mama, mke, mume, dada, kaka, familia, ndugu, jamaa au rafiki na kumwambia nisamehe nimekosa. Kisha tumgeukie Mungu na kumuomba msamaha, Naye daima anatungoja, kwa upendo kutupokea, kutukumbatia na kutufanyia sherehe.

Dominika ya 24 ya mwaka C

Tumwombe Roho Mtakatifu atujalie neema zake ili nasi tutambue mwito wa kuomba msamaha kwa Mungu na kwa ndugu zetu, ili tuweze kuishi kwa amani na furaha hapa duniani na kushirikishwa ya mbinguni baada ya Mungu kumtuma mjumbe wake – kifo – kuja kutuita. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi akituombea; “Ee Bwana, uridhike na dua zetu; uipokee kwa wema dhabihu yetu sisi watumishi wako, ili kitu alichokutolea kila mmoja wetu kwa heshima ya jina lako, kitufae sote kwa wokovu”. Na katika sala baada ya komunyo anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii anasali; “Ee Bwana, tunakuomba nguvu ya neema zako za mbinguni itujaze mwili na roho, ili tusitawaliwe na tama zetu, ila tu na nguvu hiyo”. Na hili ndilo tumaini letu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika XXIV Mwaka C
11 Septemba 2025, 16:30