Tafuta

Neno la Mungu:Yesu anasisitiza hatari ya utajiri kwa maisha ya kiroho na ya utakatifu ikitumika vibaya. Neno la Mungu:Yesu anasisitiza hatari ya utajiri kwa maisha ya kiroho na ya utakatifu ikitumika vibaya.  

Dominika ya 25 Mwaka C:Mali ya dunia na Ufalme wa mbinguni

Katika Dominika hii tumwombe Mungu afungue macho ya mioyo yetu ili tupate kuelewa na kutambua tunavyopaswa kuvitumia vitu vya kidunia kwa sifa na utukufu wake,ili Yeye mwenyewe atustahilishe kuingia katika utukufu wake mbinguni mda utakapofika.Kwa nguvu zetu hatuwezi,tunahitaji kujivika unyenyekevu ili neema za Mungu zitusaidie.

Na Padre Paschal Ighondo –Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 25 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Masomo ya Dominika hii yanatuelekeza kutumia vizuri mali za duniani kwa kuwahudumia wanaohitaji msaada wetu, ili tujijengee muunganiko na Mungu wetu aliye Mtakatifu sana. Tukifanya hivyo kila tunapomlilia na kuomba msaada wake daima atatusikiliza, na zaidi sana atatustahilisha kuingia katika uzima wa milele mbinguni. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii unasema; “Bwana asema: Mimi ni wokovu wa watu wangu. Wakinililia katika taabu yo yote nitawasililiza, nami nitakuwa Bwana wao milele”. Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, umeziweka katiba zote za sheria takatifu, katika amri ya kukupenda wewe na jirani. Utuwezeshe kuzishika amri zako, tupate kustahili kuufikia uzima wa milele”.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Amosi (Amo 8:4-7). Somo hili linahusu maonyo na utabiri wa adhabu kwa matajiri wa Samaria kwa kuwanyonya maskini na fukara. Amosi aliyekuwa mchungaji wa kondoo kutoka Ufalme wa Yuda miaka 750 KK, aliitwa na Mungu kuwa Nabii katika ufalme wa Samaria wakati wa utawala wa Yeroboam II, kipindi ambacho Israeli ilikuwa imestawi kiuchumi, na kukua kwa uovu, kwani ni watu wachache tu, matajiri, ndio walionufaika na maendeleo hayo, na watu walio wengi, maskini na fukara, walinyonywa na kuteseka mno (Amo 5:7-13, 6:1-7). Hii ni kwa sababu matajiri walijikita zaidi katika biashara, wakazifanya mali kuwa miungu yao, wakamuacha Mungu wa kweli, wakaacha kusali na kumwabudu Mungi, wala hawakuiheshimu tena siku ya Sabato. Ni katika mazingira haya sheria iliwekwa kukataza watu kufanya biashara siku ya Sabato na siku ya kwanza ya mwezi. Ndio maana katika somo hili matajiri na wafanya biashara wanalalamika wakisema; “Sabato itapita lini na mwezi mpya utaisha lini ili tuweze kufanya biashara?”

Na katika biashara zao waliwalaghai na kuwaibia wanunuzi kwa kupunguza vipimo vya mizani, walinunua mazao na vitu vingine kwa bei ndogo na baadae kuuza kwa bei za juu zaidi kuliko thamani ya vitu vyenyewe. Katika mazingira hayo, maskini waliishi kwa mikopo yenye riba kubwa, licha ya kuwa sheria ilikataza kukopesha kwa riba ikisema; “Ukimkopesha fedha mtu yeyote, miongoni mwa watu wangu walio maskini…usimtoze riba…ndugu yako Mwisraeli usimtoze riba, naye Mungu wako atakubariki katika kazi zako…” (Kut 22:24-25; 23:20). Sheria hii haikufuatwa. Maskini walitozwa riba kubwa, na waliposhindwa kulipa walinyang’anywa vitu vyao hata mashamba, na wasio na kitu, walifanywa watumwa kwa kuuzwa na kununuliwa kwa bei ndogo inayolinganishwa na jozi ya viatu. Mungu kwa kinywa cha Nabii Amosi analaani mambo haya na kutangaza adhabu akisema; “Na hasira yangu itawaka, nami nitawaueni kwa upanga, wake zenu watakuwa wajane na watoto wenu yatima”. Adhabu hii ilitimia kwa Samaria kuvamiwa na Asiria na watu wake kuchukuliwa mateka.

Hali ya kipindi cha Nabii Amosi haiko tofauti sana na nyakati zetu, ambapo baadhi ya viongozi na matajiri wanakula na kunywa na kujinenepesha kwa jasho la maskini. Mungu anasema, hakika msipotubu, mkaacha ufisadi wenu, na kuwatendea haki wengine, adhabu inawajia, mtateseka na kufa katika uovu wenu, mtakiona cha moto mngali duniani, na baada ya kufa mtaingia katika moto wa milele. Na maskini Mungu atawatunza kwa mkono wake wenye nguvu, usioshindwa lolote. Ni katika muktadha huu wimbo wa katikati unasema hivi; “Msifuni Bwana anayewakweza maskini. Aleluya! Enyi watumishi wa Bwana, sifuni, lisifuni jina la Bwana. Jina la Bwana lihimidiwe, tangu leo na hata milele. Bwana ni Mkuu juu ya mataifa yote, na utukufu wake ni juu ya mbingu. Ni nani aliye mfano wa Bwana, Mungu wetu aketiye juu; Anyenyekeaye kutazama mbinguni na duniani? Humwinua mnyonge kutoka mavumbini, na kumpandisha maskini kutoka jaani. Amketishe pamoja na wakuu, naam, pamoja na wakuu wa watu wake (Zab. 113:1-2, 4-8).

Somo la Pili ni la waraka wa kwanza wa mtume Paulo kwa Timoteo (1Tim 2:1-8). Ujumbe mkuu katika somo hili unahusu sala ya kiliturujia katika Kanisa. Kwanza, lengo la sala hii ni kwa ajili ya kutimia kwa mapenzi ya Mungu ya watu wote kuokolewa kwa njia ya Yesu Kristo, aliyejitoa mwenyewe kuwa ukombozi kwa ajili ya wote. Pili, sala ya kiliturujia ni kwa ajili ya watu wote; raia, viongozi wa kisiasa, kiserikali, wafalme na wenye mamlaka, ili waweze kuwaongoza watu kwa upendo, haki, utulivu na amani. Sala hii haibagui viongozi, hata wale wa kiimula, ili waweze kuongoka na kutenda haki kwa watu wote. Itakumbukwa kuwa kipindi Mtume Paulo anaandika waraka huu, Nero, mtu katili na muovu, ndiye alikuwa kiongozi wa utawala wa kirumi. Tatu, sala ya kiliturujia katika Kanisa inapaswa kukiri imani ya kuwa; “Mungu ni mmoja, na mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu ni mmoja, Mwanadamu Kristo Yesu”. Na mwisho anatoa mwongozo namna sala ya kiliturujia katika Kanisa inavyopaswa kuwa; iongozwe na wanaume kila mahali, wakiinua mikono iliyotakata, isiyo na dhambi, pasipo hasira wala malumbano. Basi nasi tuwe kweli watu wa sala, tusali daima kwa ajili ya wokovu wetu binafsi, na wa watu wote hasa viongozi wa kisiasa, na kiserikali ili waweza kutuongoza kadiri ya amri, maagizo na mpango wa Mungu Baba yetu.

Injili ilivyoandikwa na Luka (Lk 16: 1-13). Sehemu hii ya Injili inahusu mafundisho ya maisha ya kijamii, mhusika mkuu akiwa ni Karani dhalimu na mwerevu. Katika fundisho hili Yesu anasisitiza hatari ya utajiri kwa maisha ya kiroho na ya utakatifu ikitumika vibaya. Hivyo anatuasa namna ya kutumia vyema mali za kidunia ili kwazo tustahilishwe kuupata uzima wa milele. Tukirejea historia ya wana wa Israeli, mara tu walipofika nchi ya ahadi, Bibilia inasimulia kuwa kila kabila na familia iligawiwa ardhi yake (rej. Yoshua 13:1-21:45). Lakini baadae, wapo waliouza ardhi yao, hivyo kukatokea matabaka kati ya wamiliki na wasiomiliki ardhi. Hivyo likatokea tabaka la maskini, waliobaki kuwa vibarua kwa matajiri ili wajipatie posho ya siku (rej. Mt 20:1-16), au kufanya kazi kwenye mashamba kwa makubaliano ya kugawana mavuno na wenye mashamba, na wengine waliwekwa kuwa makarani au mawakili, ili kukusanya ushuru kutoka kwa waliokodi mashamba (rej. Mt 21:33-46, Lk 20:1-19). Sasa miongoni mwa mawakili walikuwepo waovu na mafisadi, waliohujumu mali za matajiri waliowaajiri kwa rushwa, au kutoza kodi kubwa zaidi ya ilivyowapasa.

Ni katika mazingira haya, wakili dhalimu anayesimuliwa, alipojulikana kwa udhalimu wake, na akapata taarifa ya kufukuzwa kazi, hakukiri makosa yake wala kuomba msamaha, bali alifanya ufisadi zaidi kwa kuwarubuni wadeni wa bwana wake, na kula rushwa kwao kwa kupunguza hesabu za madeni yao, ili akifukuzwa kazi waweze kumhifadhi kwa ukarimu wake wa kifisadi, akifahamu wazi madhaifu yake kuwa hana uwezo wa kulima, na kuomba anaona haya. Cha kushangaza ni kuwa, Bwana wake alimsifu, sio kwa udhalimu bali kwa alivyotenda kwa busara, akijiandalia mazingira ya kuishi baada ya kufukuzwa kazi. Na Yesu anashauri kuiga mfano wa wakili huyu dhalimu. Hii haina maana kuwa anatushauri nasi tuwe wadhalimu. Hapana! Bali anatusihi kuwa mbinu na muda, hekima na busara, tunazotumia kwa mambo ya kidunia kama vile kutafuta mali, tuzitumie katika kuutafuta ufalme wa mbinguni.

Yesu anatumia misemo mbalimbali kufikisha ujumbe huu. Kwanza anasema; “Jifanyieni marafiki kwa mali ya udhalimu, ili zitakapowaishieni, wawapokee katika makao ya milele” (Lk 16:9). Maana yake tutumie mali tulizozipata kwa dhuluma, kujenga urafiki na Mungu na watu kwa namna inayofaa, ikiwa ni pamoja na kuwarudishia tulio wadhulumu na kusahihisha madhara tuliyo wasababishia, na kama haiwezekani kuzirudisha na kusahihisha madhara tuliyo sababisha, basi tuzitumie kutenda matendo ya huruma, kuwasaidia wahitaji na maskini, au kuziwekeza kwa maendeleo ya kijamii, kwa kujenga fursa na nafasi za ajira kwa wahitaji, tukifuata mfano wa Zakayo, ambaye kwa kufanya hivyo, wokovu uliingia nyumbani kwake (rej. Lk. 19:1-10). Kwa maana ni katika kutenda haya tunajenga urafiki na Mungu na watu watakao shuhudia na kuthibitisha uwakili wetu wa rasilimali za kidunia, kwamba tulizitumia kwa ukarimu kwa kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwavika walio uchi, kuwahudumia wagonjwa na wafungwa (rej. Mt 25:34-40), hivyo mjumbe wa Mungu, dada yetu kifo, atakapotuita tukatoe hesabu za uwakili wetu, tutaweza kustahilishwa kuingia katika uzima wa milele mbinguni.

Yesu anasisitiza kuwa kuaminiwa na kukabidhiwa mambo makubwa kunatokana na kuonesha uaminifu kwa yale madogo. Mali za duniani ni mambo madogo sana mbele ya “uzima wa milele”, ambao Mungu anawatunukia wale walioonesha uaminifu kwa mambo madogo, yaani mali za kidunia, ambazo sio zetu, ni za Mungu, naye atawapa wengine baada ya kifo cha aliyekuwa amezikabidhiwa, naye hataweza kuzichukua. Kumbe sisi ni mawakili tu, kwani duniani hatukuja na kitu cho chote, na hatutaweza kutoka na kitu cho chote (rej. 1Tim 6:7), tena hatuwezi kudumu katika fahari ya vitu tulivyo navyo (rej. Zab 49). Kilicho chetu kipo mbinguni na tutakikabidhiwa kama tumekuwa mawakili wema kwa yale ya duniani. Kisha akasema; “Hakuna mtumishi awezaye kuwatumikia mabwana wawili, kwa maana atamchuki huyu na kumpenda mwingine. Au ataambatana na mmoja na kumdharau mwingine. Hamwezi kutumikia Mungu na mali” (Lk 16:13). Msisitizo hapa ni kuwa kila tunachokifanya, tukifanye kwa uaminifu kwa sifa na utukufu wa Mungu, na sio kwa sifa na utukufu wetu.

Basi tumwombe Mungu afungue macho ya mioyo yetu ili tupate kuelewa na kutambua tunavyopaswa kuvitumia vitu vya kidunia kwa sifa na utukufu wake, ili Yeye mwenyewe atustahilishe kuingia katika utukufu wake mbinguni mda utakapofika. Kwa nguvu zetu hatuwezi, tunahitaji kujivika unyenyekevu ili neema za Mungu zitusaidie. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anatuombea akisali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba uwe radhi kuzipokea dhabihu zetu sisi taifa lako; utujalie kupata katika sakramenti takatifu hayo tunayoungama kwa imani”. Na katika sala baada ya Komunyo anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii anasali; “Ee Bwana, sisi unaotuburudisha kwa sakramenti zako, utuinue kwa msaada wako wa siku zote, tupate matunda ya ukombozi kwa njia ya mafumbo yako na mwenendo wetu mwema”. Na hili ndilo tumaini letu, kuishi vyema hapa duniani, ili tupate kustahilishwa kuingia katika uzima wa milele mbinguni.

Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari ya Dominika 21 Septemba 2025
19 Septemba 2025, 14:26