Tafuta

Dominika ya 26 ya Mwaka C.Tajiri na maskini. Dominika ya 26 ya Mwaka C.Tajiri na maskini. 

Dominika ya 26 ya Mwaka C:Mali ya duniani ni kwa ajili ya wote

Basi tuwe wepesi wa kuona mahitaji ya wenzetu,kuwasaidia na kuwahudumia kulingana na utajiri wa vipaji alivyotujalia Mungu,kwa upendo na bila dharau.Kipaji ulicho nacho kisikufanye umdharau asiye na kama cha kwako.Daima tusaidiane ili kukamilishana pale ambapo hatujajaliwa kipaji kimoja au kingine.

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 26 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Fundisho kuu katika masomo ya dominika hii – kwanza ni hili; Kujikusanyia na kujirundikia mali kwa njia isiyo halali ni sumu kwa maisha ya kiroho na hukumu yake ni moto wa milele. Pili, tajiri na masikini, wote ni wana wa Mungu, wameumbwa kwa sura na mfano wake, kwa lengo la kumjua, kumpenda, kumtumikia na mwisho wafike kwake mbinguni. Hivyo wanapaswa kusaidiana katika maisha ya hapa duniani, ili baadae wakaishi pamoja mbinguni. Matajiri kwa namna ya pekee, wanatakiwa kuwasaidia maskini kwa upendo katika mahitaji yao na kuwatendea kwa haki kama Mungu anavyotundea sote kwa haki. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unaofungua maadhimisho ya dominika hii unasema; “Ee Bwana, yote uliyotutendea, umeyatenda kwa haki, kwa kuwa sisi tumetenda dhambi, wala hatukuzitii amri zako. Ulitukuze jina lako na kututendea sawa sawa na wingi wa huruma zako” (Dan. 3:31, 29, 30, 43, 42). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi; “Ee Mungu, wewe unaonyesha enzi yako kuu hasa kwa kusamehe na kuhurumia. Utumwagilie daima neema yako, tupate kuzishiriki baraka za mbinguni, sisi tunaokimbilia ahadi zako.”

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Amosi (Amos 6:1, 4-7). Sehemu hii ya somo hili inahusu makemea ya tabia ya kujilimbikizia mali kwa matajiri na mishahara mikubwa kwa viongozi huku wakiwanyanyasi maskini na kuwaacha wakiteseka kwa kukosa mahitaji yao muhimu, wakifikiri kuwa utajiri wao ni alama ya baraka na neema za Mungu kwa wema wao, na maskini wamelaaniwa kwa maovu yao. Nabii Amosi anakemea tabia hii na kuwataka viongozi waliopewa kibali cha kuwaongoza watu, wazingatie misingi ya haki na amani, kutokomeza rushwa mahakamani, na udanganyifu wa wafanya biashara wanaogushi vipimo vya uzito na ujazo wa bidhaa walizouza na kununua. Na kama wataendelea kula raha, anasa na tafrija kwa jasho la maskini, adhabu kutoka kwa Mungu itawafikia. Na kwa kuwa walikaza shingo, hawakutaka kubadilika, hukumu iliwaangukia, adhabu ilitimia mwaka 722KK, kwa jeshi la Assiria chini ya Sargon II, kuivamia na kuiangamiza Samaria na kuwachukua watu wake mateka, na kuwafanya watumwa katika mashamba ya Mesopotamia.

Hata nyakati zetu, wapo matajiri na viongozi wenye mamlaka halali, ambao badala ya kutimiza nyajibu zao halali, wao wanajishikamanisha na matajiri, wanakula starehe na anasa kwa damu na jasho la maskani. Watambue kuwa kwa kufanya hivyo wanapotea uhalali wa mamlaka waliyopewa kwa halali. Na Mungu anasema; msipobadilika, mkaacha udhalimu wenu, mkatubu, mkaomba msamaha na kuanza kutenda haki, adhabu yenu inawajia hapa duniani na baada ya kifo katika moto wa milele. Na utajiri mliojikusanyia kwa hila, kwa kuiba au kuwanyang’anya wengine kwa nguvu, hata kwa kuua, kwa kufanya biashara zisizo halali kama kuuza dawa za kulevya, biashara haramu za binadamu, kuwadhulumu wajane na yatima urithi wao, kuuza au kutumia vibaya mali za umma kwa ufisadi, na rushwa, kutumia vibaya vyeo na mamlaka mliyopewa kwa kutunga na kutumia sheria zisizo halali wala za haki, ili kuwakandamiza na kuwaibia wanyonge na kuwanyamazisha watetezi wa wanyonge, utakuwa ni ushahidi wa hukumu yenu ya mwisho, na adhabu yake ni moto wa milele.

Dominika ya 26 ya mwaka C
Dominika ya 26 ya mwaka C

Ushauri ni huu, ni vyema kila mara kujichunguza dhamiri mbele za Mungu kwa kujiuliza; Je, mali nilizonazo hazijalowa, hazinuki, au hazina uvundo wa damu, jasho, machozi, au njaa ya maskini, wanyonge, wajane na yatima? Kumbuka daima kuwa hawa mtetezi wao ni Mungu ambaye haachi kamwe machozi, jasho, au damu yao imwagike na kupotea bila kulipwa. Ni katika muktadha huu, wimbo wa katikati unasema hivi; “Ee nafsi yangu, umsifu Bwana. Bwana huishika kweli milele, Huwafanyia hukumu walioonewa. Huwapa wenye njaa chakula, Bwana hufungua waliofungwa. Bwana huwafumbua macho waliopofuka, Huwainua walioinama. Bwana huwapenda wenye haki, Huwahifadhi wageni. Bwana huwategemeza yatima na wajane, bali njia ya wasio haki Huipotosha. Bwana atamiliki milele, Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi” (Zab. 146:1, 6-10).

Somo la pili ni la waraka wa kwanza wa Mtume Paulo kwa Timoteo (1Tim 6:11-16). Somo hili ni hitimisho la barua ya kwanza ya kichungaji ya Mtume Paulo kwa Timoteo. Katika kutoa mawaidha yake ya kichungaji, Mtume Paulo anaweka msisitizo katika umuhimu wa kuiungama na kuishuhudia Imani aliyoishuhudia Yesu mwenyewe mbele ya Pilato, alipokiri ukuu wa fumbo la ufalme wake akisema; “Mimi ni mfalme. Kwa ajili ya hilo nilizaliwa, na kwa ajili ya hili nilikuja ulimwenguni, ili niishuhudie kweli. Mtu ye yote aliye wa kweli husikia sauti yangu” (Yn 18:37). Na huu ndio ujumbe wa kikristo, imani kwa Kristo Yesu, imani yenye matumaini katika kujidhihirisha kwake, na upendo katika kuilinda bila hila wala doa lolote. Msingi wa yote katika kuiungama imani hii ni Kristo Yesu mwenyewe. Na mwenendo na tabia ya kila mkristo, inapaswa kujengwa katika kutenda haki kwa wote, na kuishi kwa uadilifu, utauwa, imani, upendo, saburi na upole; yote kwa ajili ya uzima wa milele.

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk 16:19-31). Sehemu hii ya Injili ni mafundisho ya ya Yesu kuhusu maisha ya kijamii ambayo yamejikita katika mzizi wa dhambi ya uchoyo, unaopelekea upofu wa kutokuona na kutokujalia mateso na mahangaiko ya wengine hasa maskini na wagonjwa, hata walio karibu nasi. Fundisho hili Yesu analitoa kwa simulizi la Tajiri asiyetajwa jina lake, kwa maana hakufanya lolote zaidi ya kuvaa “nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula siku zote kwa anasa”, na maskini Lazaro, jina lake likiwa na maana ya Mungu anasaidia. Fundisho kuu katika simulizi hili ni kuwa; mda wa kusaidiana ni sasa tungali bado hai, mda utafika ambapo hatutaweza kufanya hivyo, kwani baada ya kifo, katika ulimwengu ujao, tutatenganishwa na shimo kubwa, tusiweze kusaidiana sisi kwa sisi, msaada pekee utakaobaki ni faraja ya Mungu kwa walioteseka, na mateso kwa waliokosa huruma kwa wengine walipokuwa wanateseka na wao wakila raha. Ni katika maudhui haya, Yesu anatoa mawaidha ya namna ya kutumia mali za dunia hii vizuri, ili kwazo tustahilishwe kuingia katika uzima wa milele mbinguni, ambapo Mungu atafuta kila chozi kwa wanae kama kwa Lazaro aliyepokelewa katika furaha ya uzima wa milele na kufarijiwa. Kinyume chake ni kuingia katika moto wa milele kama tajiri aliyehukumiwa na kutupwa katika moto wa milele, kwa kuwa alipokea na kula mema ya dunia bila kuwajali wengine.

Ifahamike kuwa hukumu ya tajiri haikusababishwa na yeye kuwa na mali, kuvaa na kula vizuri, bali kwa kutokujali mahitaji ya wengine, maskini na wagonjwa kama Lazaro. Hii ni dhambi ya kutokutimiza wajibu wa kutenda mema. Tabia hii ni chukizo kubwa kwa Mungu aliyeumba vitu vyote kwa ajili ya wote, na adhabu yake ni moto wa milele, ambapo katika hukumu yake bila shaka aliambiwa; Ondoka wewe uliyelaaniwa, nenda kwenye moto wa milele alioandaliwa ibilisi na malaika zake. Kwa maana nilikuwa na njaa hakunipa chakula, nilikuwa na kiu hakuninywesha, nilikuwa mgeni hakunikaribisha, nilikuwa uchi hakunivika, nilikuwa mgonjwa hakunitunza, na nilikuwa gerezani, hakuja kunitembelea (rej. Mt. 25:41-44). Kumbe mali binafsi isipozingatia manufaa ya Umma na hasa wahitaji, itatuhukumu siku ya mwisho. Ni katika muktadha huu Mtakatifu Clementi wa Alexandria anasema hivi; “utajiri si mbaya katika wenyewe, uadilifu wake unategemea katika matumizi yake. Mtu tajiri anayefanya matumizi mazuri ya utajiri wake na kuwasaidia wengine ni bora kuliko maskini ambaye katika maisha yake anatamani kupata utajiri hata kwa njia zisizo halali”.

Lakini kwa nini mtu ahukumie kwa mali aliyoitokea jasho? Ni kwa sababu kila kilichoumbwa na Mungu ni kwa ajili ya manufaa ya wote, yaani umma. Ingawa tuna haki ya kumiliki mali binafsi, tunapaswa kufanya hivyo kwa ajili ya manufaa ya umma, kwani mali binafsi ni mali ambayo mtu anachukua sehemu ya mali ya umma kihalali na kuifanya binafsi, ili azalishe kwa manufaa ya umma. Hivyo, kuwasaidi wahitaji si jambo la hiari ni wajibu. Mtakatifu Paulo VI, Papa, katika waraka wake wa Populorum progressio – maendelo ya watu – anasema; “Hakuna mtu mwenye haki ya kutumia vitu vya ziada, wakati wengine hawana mahitaji muhimu”. Naye Mtakatifu Ambrosi anasema: “Unapompa maskini kitu, humpatii kilicho chako, bali unamrudishia kilicho chake, kwani mali ya dunia hii ni yetu sote.” Kumbe yote tuliyojaliwa na Mungu, tunapaswa kuyatumia kwa mafaa ya wengine wenye kuhitaji tena kwa upendo. Matokeo ya kuziba masikio yetu kwa kilio cha wahitaji, ni hukumu ya moto wa milele. Kumbe hata utajiri uliopatikana kwa njia halali, usipotumika kuwasaidia wahitaji utatumika kutuhukumu kama ilivyotokea kwa tajiri kwenye simulizi la Injili.

Kuwepo kwa matabaka baina ya matajiri na maskini duniani ni kinyume na mpango wa Mungu. Hivyo kujirundikia mali za ziada usizozitumia, au kujimilikisha eneo kubwa la ardhi, hata kama ni halali kisheria, kama huviwekezi ulivyonavyo ili kutoa ajira, au kuleta maendeleo kwa manufaa ya umma, na hivyo unakuwa sababu ya umma kukosa mahitaji msingi ya maisha, ujue na utambue kabisa kuwa unatenda dhambi kubwa ya mauti. Lakini pia ni dhambi ya mauti kujitafutia mali kwa kuharibu manzingira. Tena ni dhambi ya mauti kuchagua viongozi kwa upendeleo kwa manufaa binafsi, ukijua kabisa unayemchagua hana sifa za kiongozi bora, wala nia, wala malengo ya kuwasaidia raia, hasa maskini, wanyonge na wahitaji, kutoa ushahidi wa uongo ili kumnyang’anya mwingine haki yake, au kutokufanya mambo hata kama ni madogo na yako ndani ya uwezo wako kama vile kuwafariji wanaoteseka, mfano waliofiwa, kuwatembelea wagonjwa na wafungwa, na kuwatetea wanaodhulumiwa. Ujue, utahukumiwa.

Tajiri anayesimuliwa katika Injili baada ya ombi lake la kusaidiwa na maskini Lazaro kupitia kwa Babu Ibrahimu kugonga mwamba, anaomba ndugu zake wasaidiwe ili nao wasije wakapatwa na mateso yale yale baada ya maisha yao ya hapa duniani. Kila mtu ni ndugu ya huyu tajiri, na tunao Musa na manabii wa nyakati zetu. Je tunawasikiliza wanapotufundisha na kutuonya tunapokengeuka katika maisha ya kiroho na kimaadili? Tunapoambiwa tuwatendee wengine kwa haki na kuwajali katika mahitaji yao, tunafanya hivyo? Tukumbuke kuwa maskini ni mtu yeyote anayehitaji msaada katika jambo lolote lile. Na kuwa tajiri haimaanishi tu kuwa na vitu vingi. Kila mtu ni tajiri na maskini kwa namna moja au nyingine, kwa maana Mungu amemjalia kila mtu karama nyingine na kumnyima nyingine. Vipawa na vipaji alivyotujalia Mungu tunapaswa tuvitumie siyo kwa manufaa binafsi tu, bali pia kwa ajili ya wengine, na tusipofanya hivyo, tutahumukiwa kwa hilo.

Basi tuwe wepesi wa kuona mahitaji ya wenzetu, kuwasaidia na kuwahudumia kulingana na utajiri wa vipaji alivyotujalia Mungu, kwa upendo na bila dharau. Kipaji ulicho nacho kisikufanye umdharau asiye na kama cha kwako. Daima tusaidiane ili kukamilishana pale ambapo hatujajaliwa kipaji kimoja au kingine. Tumepewa bure kwa upendo, tutoe bure kwa upendo kama antifona ya Komunyo inavyosema; “Katika hili tumelifahamu pendo la Mungu, kwa kuwa yeye aliutoa uhai wake kwa ajili yetu; imetupasa na sisi kuutoa uhai wetu kwa ajili ya hao ndugu (1Yn. 3:16). Tumwombe Mungu atujalie neema na baraka zake, ili tuweze kuwasaidia wanaohitaji msaada wetu kwa haki na usawa. Ni katika muktadha huu sala ya kuombea dhabihu inasema hivi; “Ee Mungu mwenye huruma, ukubali dhabihu yetu hii ikupendeze, nayo itufungulie chemchemi ya baraka zote”. Na mama Kanisa katika sala baada ya komunyo anapohitimisha maadhimisho ya dominika hii anatuombea hivi; “Ee Bwana, fumbo hili la mbinguni lituponye mwili na roho, tupate kuurithi utukufu pamoja na Mkombozi, ambaye tunamsikitikia tunapohubiri kufa kwake”. Na hili ndilo tumaini letu.

Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari Dominika ya 26 Mwaka C
26 Septemba 2025, 08:49