Tafuta

2021.12.28 Pace, colomba, ramo di ulivo

Dominika ya XXV,mwaka C:Amani na Huduma inajengwa kwa uaminifu na usafi wa Moyo!

Dominika ya 25,Mwaka C inatuita:tuwe viongozi wa matumaini,si kwa nguvu wala mali bali kwa sala,huduma na uaminifu.Amani iwe radhi ya Kristo,nayo ihuishe mioyo yenu"(Kol 3:15).“Ambaye ni mwaminifu katika kidogo,mwaminifu pia katika mengi.”(Lk 16:10).Amani,upendo,na uaminifu viondoe madaraka ya rushwa na mali, tuishi msingi wa tumaini la kweli kwa sababu Dunia inahitaji ili iponywe.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio vatican leo Dominika ya 25, Somo la I: Amosi 8:4–7, Mwenyezi Mungu analaumu wale wanaotoroka usiku, wakipelekea maskini, wakifanya biashara kwa udanganyifu. Somo la II: 1 Timotheo 2:1–8 – Mtume Paulo anahimiza sala, dua na shukrani kwa wote; hasa kwa viongozi, ili tuwe na maisha ya amani na utulivu wa kiroho. Injili: Luka 16:1–13 (Mfano wa msimamizi mwoga) ,Yesu anataka tuwe waaminifu kwa utimilifu wa mali, tukitambua kuhusu utayari wa moyo zaidi ya mali. Katika utulivu wa fikara Raisi Thomas Jefferson aliona neno hili zuri, ya kwamba “Uaminifu ni sura ya kwanza katika kitabu cha hekima”… Tafakari ya Dominika hii inaamsha ndani mwetu fadhila ya UAMINIFU katika mambo madogo na ya kawaida yanayopelekea tuzo katika ulimwengu ujao. Mungu anashtaki wazalendo wa maendeleo binafsi kwa uhakika; wale wanaowenyima maskini na kupoteza utu na haki. Katika dunia ya leo ya ubinafsi na hakikisho la namna ya uchaguzi, maandamano na matarajio ya mafanikio lazima  beresha uwazi na usawa   kwa manufaa ya wengine, Maisha ya KiKristo yanapinga aina yoyote ya ukandamizaji ni lazima tulinde utu wa wanyonge.

Nabii Amosi katika somo la Kwanza (8:4-7) anazungumzia “mtu anavyoweza kuiba”… aliishi mwaka 750 KK Israel ikiwa kileleni mwa mafanikio kiuchumi, kisiasa na kijamii. Mfalme Yeroboam II aliijenga sana Israel na kuipatia maendeleo makubwa. Hata hivyo masikini walipunjwa na sera za nchi ziliwabeba matajiri na wenye vyeo. Ndipo Nabii anaanza kutoa maonyo makali kwa mfalme na wanyonyaji wengine.  Kundi linalolaumiwa na Nabii ni la wale wanaowameza wahitaji na kuwakomesha masikini wa nchi, hao ni wale wanaowalangua wakulima wadogo kwa bei ndogo za mazao na wao kuuza ghali zaidi… wanatajirika kwa kuiba na kukandamiza. Nabii anaonya viujanjaujanja na vimbinumbinu vya udanganyifu akieleza wazi kuwa matendo yasiyo haki hayasahauliki mbele za Mungu na hivi ni lazima kuona tunauza na kununua kwa haki na sio kupanga bei za bidhaa kwa kujiamulia tu.

Injili leo (Lk 16:1-13) imebeba wazo hilo la maadili mintarafu kuiba kwa udanganyifu. Wakili dhalimu anaachishwa kazi sababu amekosa uaminifu. Katika kuwaza sana anajiuliza “nifanyeje? kulima siwezi, kuomba  aibu”… anapata wazo la kuwekeza kwa watu ili wampende na atakapofukuzwa kazi wamuhudumie na kumtunza.. Anamwita mdeni wa bosi wake na kumuuliza “wawiwani?” “vipimo 100 vya mafuta”, “haya kaa hapo chukua risiti andika 50.” Wadeni hawa wanafurahi sababu nao sio waaminifu kama meneja huyu na hakika hawawezi kumsahau na daima watataka kulipa fadhili hizi kwa kumsaidia naye katika matatizo yake.

Jambo la ajabu ni hili, Yesu anamsifu huyu wakili dhalimu kuwa ana busara. Je tumuige? Hapana... Kumsifu mtu haina maana ya kukubali alichofanya. Mwanasiasa mjanja aliyewapa sera za uhakika na kuwahadaa na kwa ujinga mkamchagua kisha akapotea asitimize alichoahidi anasifika sababu ana akili na wananchi wake ni wajinga ila hatumuigi katika uongo wake... Mfungwa mmoja alitoroka gerezani akifungua milango akitumia kiberiti cha gesi cha sigara, tunampongeza kwa uhodari wake lakini hatumuigi katika ujeuri huo... Mwizi anayefaulu kuiba benki sababu walinzi na wahudumu ni wazubavu ni mwerevu na ni mjanja zaidi lakini kamwe hatumuigi katika wizi wake. Walichofanya wafanyabiashara enzi za Nabii Amosi na alichofanya wakili huyu wa Injili ndicho tunachofanya sisi leo, mkulima masikini ananyonywa yeye ambaye nchi yake inategemea kilimo kwa zaidi ya 80% ana hali duni, walanguzi wanafaidi jasho na damu ya mtu huyu mnyonge na hakika wanatajirika... upungufu wa maadili.

Yesu anatuhimiza kuwa watumishi waaminifu. Msimamizi mwoga anajifunza kuwa na urahisi bila hila – “Ambaye mwaminifu katika kidogo, mwaminifu pia katika mengi.” Katika kazi, familia, uhusiano – usafi wa moyo, uaminifu na utunzaji wa mali, ni taaluma, sio ujanja.  Mahujajina watu wa matumaini lazia watangaze na kuimba haki, huruma, uaminifu, na huduma  Inamaanisha, Kupinga unyonyaji , Kuomba kwa ajili ya haki, Kuishi maisha ya uaminifu katika mali. Kughushi nyaraka na risiti imekuwa kawaida leo, wafanyakazi huungana kuwazunguka waajiri wao huku waajiri nao wakitumia fedha zao na nguvu nyingi kuwakandamiza wafanyakazi wao ili kulimbikiza utajiri. Mtu mmoja amesema nchi nyingi, hasa za kiafrika, zimeuzwa na ubadhirifu umeshamiri. Ina faida gani mali ya udhalimu? Yesu anasema leo shika moja, au Mungu au mali... ni ngumu kutumikia mabwana wawili, na hiyo ni tabia ya kikahaba. Ni amri ya Mwenyezi Mungu kwamba tusiibe... wizi ni mbaya, wizi haujengi, wizi huchafua na kunajisi, ni kinyume cha uaminifu na heshima, ni mapato ya tamaa. Labda tunaiba sababu ya ufukara na umasikini wetu lakini mbona hata matajiri bado wanaiba? daima fedha haitoshi na kamwe haitakaa itoshe.. Upo pia ugonjwa wa kuiba, “kleptomania” ambapo mtu anashindwa kudhibiti hisia za kuiba hasa vitu asivyovihitaji, wagonjwa hawa wakikosa cha kuiba basi hujiibia na kuficha vitu vyao wenyewe...

Wengine kuiba kwao ni mazoea, wanaibia taasisi, serikali, bank na wanawaibia watu... wapo wezi wadogo wa kuku na mkungu wa ndizi, nk, hawa hukamatwa, kupigwa sana na hata kuuawa... Halafu kuna wezi wakubwa, hawa ni watu wa heshima, hawadhaniwi, hawaguswi, hawatajwi... Tabia ya wizi huanza utotoni kwa vitu vidogo kama mboga hasa nyama, kalamu na daftari, halafu hukomaa na kuwa wizi mkubwa... Huko shuleni baadhi ya wanafunzi huibia wenzao sahani, vikombe, blanketi, shuka na masweta hivi ni lazima kujizatiti kwa sanduku ya bati na kufuli imara, hao ndio Taifa na Kanisa, baba na mama wa hapo kesho. Wapo wanaofanya magendo na uhujumu wa nyara za serikali (ndege wazuri, twiga, pembe za ndovu na faru, ngozi za thamani, madini)... kutolipa kodi, bidhaa zilizopita muda wake, kukosa ubunifu wa namna ya kuongeza mapato, miradi hewa na bajeti zisizonufaisha wanyonge... haya yanapewa maelezo mazuri na ya kuvutia lakini kiuhalisia hayana nafuu kwa watu walioumbwa na Mungu na kupewa dunia waitunze nayo iwanufaishe.

Kristo amesema “wana wa ulimwengu huwa na busara kuliko wana wa nuru...” ni kweli, laiti tungetumia akili na busara zetu zote kufoji risiti za kuingilia mbinguni, tungetumia muda mwingi kujilea na kujikuza kiroho, tungetumia nguvu nyingi na busara kwa maendeleo kuliko kunyonyana na kukamuana bila huruma halafu jamii yetu ingekuwa paradiso ya duniani... Mt. Ambrose Askofu anasema “Tusihesabu kama ni utajiri kile ambacho hatuwezi kuondoka nacho, hicho sio chetu, ni mali ya wengine”... Nayo Zaburi 49 yatubainishia “... hayo ndiyo yawapatayo wanaojiamini kipumbavu, ndio mwisho wa wale wanaojivunia mali zao, watakufa tu kama kondoo, kifo kitakuwa mchungaji wao, mwanadamu hatadumu katika fahari yake, atakufa tu kama mnyama”...

Mtakatifu Paulo analenga sala kama msingi wa maisha ya haki: “Kwa sababu hii mimi nimwelekeza...” Sala huimarisha ushirika, faraja na haki, na kuboresha jamii. Katika zama za machafuko, unyanyasaji na migogoro, suala la kisiasa na kijamii, sala yetu inafungua njia ya amani, si malalamiko wala vurugu....ikiwa ndio hivi basi utajiri wetu uwe ni vitu tutakavyoondoka navyo baada ya maisha ya hapa duniani yaani matendo mema ya huruma, upendo, maelewano, utu wema, kusaidiana, kuonyana kwa mapendo na saburi, ushauri mwema na maisha ya adili... Yote, amesema Mt Paulo katika somo II (1Tim 2:1-8), yaongozwe na dua, na sala, na maombezi, na shukrani kwa ajili ya watu wote kusudi fadhila hii ya UAMINIFU iliyo sura ya kwanza ya kitabu cha hekima ituongoze tustahilishwe kupata furaha za milele mbinguni, amina! Dominika ya 25, Mwaka C linatuita: tuwe viongozi wa matumaini, si kwa nguvu wala mali bali kwa sala, huduma na uaminifu. Amani iwe radhi ya Kristo, nayo ihuishe mioyo yenu...” (Kol 3:15) “Ambaye ni mwaminifu katika kidogo, mwaminifu pia katika mengi.” (Lk 16:10). Katika Jubilei ya Matumaini, tumaini letu linaota pale tunapokuwa watumishi waaminifu, wasalihishi, wa maombi na maskini wa moyo. Amani, upendo, na uaminifu viondoe madaraka ya rushwa na mali, tuishi msingi wa tumaini la kweli dunia inahitaji ili iponywe. Amina.

Tafakari ya Dominika ya XXV
19 Septemba 2025, 16:30