Padre Joseph Farrell ni Mkuu Mpya wa Shirika la Waagostinian
Vatican News
Padre Joseph Farrell kuanzia tarehe 9 Septemba 2025 ni Mkuu wa 98 wa Shirika la Mtakatifu Agostino, katika zaidi ya miaka 750 ya historia ya Waagostinian duniani. Alasiri hiyo walimchagua Ndugu waagostinian 73 wanaoshiriki Mkutano Mkuu wenye haki ya kupiga kura, waliounganika pamoja katika Mkutano Mkuu wa 188, ambao unaendelea jijini Roma katika Taasisi ya Kipapa ya Baba wa Kanisa Augustinianum.
![]()
Padre Joseph Farrell
Padre Farrell, ambaye kwa sasa alikuwa ni makamu wa Shirika na Msaidizi Provinsi ya Amerika Kaskazini, alipokea muhuri wa idhini kutoka kwa Padre Alejandro Moral Antón, ambaye amemaliza muhula wake wa pili, na kukubali jukumu lake jipya kama mkuu wa Shirika hilo. Alizaliwa tarehe 11 Julai 1963, huko Drexel Hill, Pennsylvania, Marekani, na amekuwa anashirikiana na Provinsi ya Mtakatifu Agostino huko Mtakatifu Thomas wa Villanova. Alihitimu Shule ya Utawala wa Biashara katika Chuo Kikuu cha Villanova mnamo 1985. Miaka sita baadaye, alipata Shahada ya Uzamili wa Taalimungu katika Chuo Kikii Kishirikishi cha Taalimungu huko Washington. Alifunga nadhiri za kwanza katika Shirika mnamo 1987 na za daima mnamo 1990.
Alipewa daraja la upadre mnamo tarehe 29 Juni 1991, katika Kanisa la Mama Yetu wa Shauri Jema, huko Bryn Mawr, Pennsylvania. Alihudumu katika parokia, shule, na vyuo vikuu, akijitofautisha kama Padre wa chuo kikuu na profesa msaidizi huko Villanova, Marekani. Mnamo 2013, aliteuliwa kuwa makamu wa Shirika hilo, akimsaidia Mkuu wa Shirika hili katika ziara za kisheria kwa jumuiya, mikutano ya shirika na majukumu mengine. Mnamo 2019, alichaguliwa tena kama Makamu wa Shirika katika Mkutano Mkuu wa kawaida. Katika jukumu hili, alishirikiana kikamilifu na tume kadhaa za kimataifa za Shirika hilo huku akitembelea jumuiya za Kiagostinian katika nchi mbalimbali.