Tafuta

Kila tarehe 14 ya kila mwaka ni Sherehe kubwa ya Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu. Kila tarehe 14 ya kila mwaka ni Sherehe kubwa ya Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu. 

Sherehe ya Kutukuka kwa Msalaba:Ujasiri wa Msalaba katika maisha ya kila siku!

Kila tarehe 14 Septemba ya kila mwaka Mama Kanisa anasherehekea Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu,Ukombozi wetu umeletwa kwa njia ya kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo msalabani.Kwa vile msalaba umekuwa ni kielelezo cha wazi juu ya ukombozi wetu,hatuna budi basi kuupatia heshima ya pekee,heshima inyostahili.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa radio Vatican Leo tunaadhimisha Sherehe ya Kutukuka kwa Msalaba. Tunapoadhimisha sikukuu hii ya kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu wa Bwana wetu Yesu Kristo, ni fursa kwetu sisi wakristo kutafakari juu ya ukombozi wetu. Ukombozi wetu umeletwa kwa njia ya kifo cha Bwana wetu Yesu Kristo msalabani. Kwa vile msalaba umekuwa ni kielelezo cha wazi juu ya ukombozi wetu, hatuna budi basi kuupa heshima ya pekee, heshima inyostahili. Somo la I: Numbers 21:4b–9 – Waisraeli waliopigwa na nyoka nusu_maisho, na walipopokea amri ya kuangalia nyoka wa shaba, waliokolewa. Somo la II: Filipo2:6–11 – Kristo, alijinyenyekeza kwa kufanana watu hadi kifo cha msalaba; Mungu akamwinua na kumpa jina kuu sana. Injili: Yohane 3:13–17 – Yesu alivyosemesha kwamba amepandishwa – kama nyoka wa shaba – ili kila amwamini apate uzima wa milele; alitumwa si kuhukumu, bali kuokoa

Mara nyingi watu wamekuwa wakitoa tafsiri mbalimbili juu ya msalaba wakimaanisha, mateso au magumu wanayopambana nayo katika maisha. Kwa mfano; kuumwa, kufiwa, kukataliwa, kuonewa, kunyimwa haki msingi, kukosa watoto, kushindwa katika jambo fulani, umaskini, kunyanyapaliwa, kutawaliwa, kukosa ajira, na mengine mengi tunayoyafahmu. Je hiyo ndiyo tafsiri sahihi juu ya Msalaba ya Bwana Wetu Yesu Kristo? Je sisi wakristo wakatoliki tunazo tafsiri hizo hizo juu ya msalaba mtakatifu ambao leo tunaadhimisha ushindi uliopatikanika juu ya msalaba huo? Nini basi maana ya msalaba huu wa Bwana Wetu Yesu Kristo kwetu sisi wakristo wakatoliki?

Msalaba Mtakatifu
Msalaba Mtakatifu

Maana ya Nyoka wa shaba alikuwa ishara ya ukombozi kwa waliojeruhiwa; hivyo Kristo amepandishwa ili watu waamini na kuokolewa. Katika maisha ya leo – wakati wa hofu, srress, vita: tumkumbuke Kristo kama mwanga wetu wa wokovu, si kitisho. Masomo yetu ya leo yanatupa picha halisi juu ya msalaba na umuhimu wake kwetu sisi wote na hasa kwa wale walio na jicho la imani. Katika somo la kwanza tunaona Waisraeli, wale walioumwa na nyoka wanaponywa kwa kumtazama nyoka wa shaba aliyetundikwa juu ya mti. Lakini katika somo la pili na Injili tunaelezwa pia Yesu anainuliwa na kufa kifo cha msalaba, naye amwaminiye hahukumiwi, asiyemwamini amekwisha kuhukumiwa, kwasababu hakuliamini Jina la Mwana pekee wa Mungu. (rej. Mt 3:18). Ndugu zangu, Waisraeli waliponywa si kwa sababu ya kumtazama tu yule nyoka wa shaba bali imani yao ndiyo iliyowaponya, kumbe leo Yesu anatueleza kuwa si kwa msalaba pekee tunakombolewa, bali kwa imani juu ya jina lake.

UFAFANUZI: Msalaba umepata maana na umuhimu wa pekee baada ya: mateso na kifo cha Yesu Kristo Msabalani. Kwa nini basi Yesu ilipasika kufa kifo cha msalaba? Wapendwa ndugu zangu, msalaba ni chombo, msalaba ni alama, lakini zaidi sana msalaba ni ishara ambayo kwa yenyewe tayari imebeba ukweli fulani. Kwa mara ya kwanza kihistoria, Warumi walitumia chombo hicho kwa lengo la kumuadhibu mtu mkosefu. Adhabu ilitolewa kwa kumning’iniza mtu huyo aliyekosa ili kutoa fundisho kwa wengine kutofanya uhalifu kama huo. Hivyo msalaba ulitumika kwa lengo hilo la kuwadhibia wakosefu wa makosa makubwa, ili kuwaonya wengine wasiweze kufanya kosa au makosa ya mtindo huo.

Katika “Spes non confundit” yaani matumahaini hayatayarishi, Hayati Papa Francisko aliita waamini kuwa ni mahujaji wa matumaini – waliojaa matumaini yenye nguvu ya msamaha, iliyoonyesha neema ya Mungu Katika Jubilee hii: Msalaba unakuwa mfano wa huruma endelevu kwa waliojeruhiwa: maskini, wakimbizi, walioathiriwa na vita. Ni kiini cha “mahujaji katika matumaini” – kutembea kwa imani na matumaini. Kwa mtazamo huo huo wa kuwaadhibu wavunja sheria kwa lengo la kuwaonya wengine, Bwana wetu Yesu Krsto kwa kutuhumiwa kuvunja sheria za kiyahudi kwa makusudi, alipata adhabu kama hiyo. Hivyo ilimpasa naye pia apate adhabu hiyo ya kifo cha  kutundikwa msalabani. Kwake Yeye  makosa yaliyopelekea kupata adhabu hiyo yalikuwa matatu: Alionekana kuwa na hatia ya kusema kwamba, angeliweza kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu. Kumbe Yesu alikuwa anazungumzia mwili wake mwenyewe (rej. Yh 2: 18). Kosa jingine kadiri ya sheria za kiyahudi ni kwamba, Yesu alijiita Masiha, wakati hakulingana na masiha waliyemtaka na kumsubiri wao, yaani masiha mkombozi wa kisiasa. Pia alitenda kosa linalo stahili adhabu hiyo kwa kujiita Mwana wa Mungu. Kwa Wayahudi hayo yalikuwa ni makosa makubwa, ambayo mweny kuyatenda alistahili kupewa adhabu ya kifo. Hivyo kwa makosa hayo kadiri ya wayahudi Yesu alisulubiwa msalabani.

Yesu alibeba Msalaba wake kwa ajili yetu
Yesu alibeba Msalaba wake kwa ajili yetu

Tafsiri ya kwamba Msalaba ni mateso, kuumwa, kufiwa, kukataliwa, kuonewa, kunyimwa haki msingi, kukosa watoto, kushindwa katika jambo fulani, umaskini, kunyanyapaa, kutawaliwa, kukosa ajira, na kadhalika, sio tafsiri sahihi kwa yule mkristo anayefahamu maana halisa ya msalaba. Papa Yohane Paulo II alisema, “Msalaba siyo ishara ya kifo, bali uzima; siyo ishara ya jambo la kuvunja moyo, bali matumaini; siyo ishara ya kushindwa, bali ya ushindi.” Hiyo ndiyo picha halisi ambayo wakristo tunapaswa kuwa nayo katika maisha yetu. Pamoja na kwamba tunafahamu kile tunachokifanya siku ya Ijumaa kuu pamoja na umuhimu wake, lakini bado wakatoliki tumeshutumiwa na wakristo wenzetu wa madhehebu mengine kwamba tunaabudu msalaba. Shutuma hizo zisiondoe ukweli tunaoufahamu sisi wenyewe wala zisitupe wasiwasi juu  ya ibada zetu na misingi sahihi ya imani yetu.

Ingawaje na wao pia, popote duniani wanaamini kuwa ukombozi wa mwanadamu umekuja kwa kifo cha Yesu Kristo msalabani, lakini bado wanashindwa kuelewa fumbo lililofichika juu ya msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Kuabudu ni tendo la kutukuza ambalo linaweza kufanyika kwa kitu au mtu yeyote yule. Lakini Mungu amekataza kufanya hivyo kwa vitu vingine zaidi yake Yeye mwenyewe. Yeye ndiye anayestahili kuabudiwa peke yake (rej. Mdo 17:28) “kwa kuwa ndiye anatuwezesha kwenda na kufanya chochote,” rejea pia Kumb 4:15, 15:42), sehemu ambazo Mungu ametukataza kuabudu kitu kingine chochote tofauti na Yeye.

Wakatoliki wanatambua na tunapaswa kujua siku ya Ijumaa kuu hatuabudu masalaba bali tunaabudu  WOKOVU uliotundikwa juu ya msalaba, yaani YESU KRISTO mwenyewe, kiebrania ‘Yeshua’ (Mwokozi). Kumbukeni maneno ya Padre au Shemasi anapowaalika waamini siku ya Ijumaa kuu akisema, “Huu ndio mti wa msalaba, ambao wokovu wa dunia umetundikwa juu yake, njooni tuuabudu.” Kwa maana hiyo basi tunachokiabudu sisi wakatoliki sio mti wa msalaba wala sanamu ile iliyotundikwa juu ya ule msalaba, bali tunamwabudu WOKOVU ambaye ndiye Yesu Kristo mwenyewe Mungu Mwana.

Msalaba katka maisha ya vijana
Msalaba katka maisha ya vijana

Tukumbuke pia, imani ya mwanadamu hukua hatua kwa hatua kama vile akili ya mtu inavyokua kutoka utoto, ujana hadi utu uzima. Mwanzoni kabisa waisraeli walikuwa kama watoto kiimani. Kumbuka Abrahamu alitoka kwenye nchi ya kipagani baadaye taratibu Mungu anamtoa kutoka katika utamaduni huo wa kuabudu miungu hadi kwenye kumwabudu Mungu mmoja. Kilele cha kumwabudu Mungu mmoja kinafikia pale mlimani sinai wanapopewa sheria. Kukua taratibu huko kwa imani ya waisrael ndiyo sababu inayofanya kuwepo tofauti ya nukuu za Mungu kukataza au kuruhusu kuabudu vitu au sanamu. Kama wakristo wakatoliki, hatuna budi kuona fahari juu ya msalaba, kwa vile tumekombolewa kwa njia ya msalaba ambapo Bwana wetu Yesu Kristo alitundikwa na akafa juu yake. Lengo la Yesu ni kutuletea wokovu. Tulistahili kupata adhabu hii ambayo yeye ameipata badala yetu. Kwetu msalaba ni ukombozi, msalaba ni sehemu ya maisha yetu na msalaba ni haki yetu. Hivyo kwa namna ya pekee Msalaba lazima uheshimiwe.

Ndugu zangu katika Kristo, yatupasa kutembea kifua mbele, huku tukijivunia Msalaba ambao ni ishara ya Kristo Mshindi. Tumwombe Mungu atujalie nguvu na ujasiri wa kumuungama, kumshuhudia na kumtangaza Bwana wetu Yesu Kristo aliyeteswa na kufa msalabani ili kuukomboa ulimwengu. Leo tunasherehekea Fumbo la Msalaba, taji la Kristo, si kitu cha aibu. Ametambazwa kwa kujitolea kwake – na sasa anatupa nguvu ya kuwa watunza wa matumaini katika dunia yenye giza. Katika Jubilee ya MatumainiTumaini linayooneshwa kwa macho – sio hisia, bali ushuhuda wa msalaba, upendo, na kukasirika kwa ajili ya wengine. “Kwa maana aliye juu, amempandisha.” (Fl 2:9.) Amani iangazie roho zetu, utiifu umuwelekee Kristo msalabani tu, kama chemchemi ya huruma na uzima wetu. Amina.

Msalaba
Msalaba
Tafakari ya Kutukuka kwa Msalaba
Samweli Abes
11 Septemba 2025, 16:45