Tafuta

Askofu Pisa,Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Tanzania(TEC),wakati wa Misa ya Jubilei miaka 100 ya Seminari Kuu ya Tabora. Askofu Pisa,Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Tanzania(TEC),wakati wa Misa ya Jubilei miaka 100 ya Seminari Kuu ya Tabora. 

Tanzania:TEC:Kanisa kujitambulisha kwa maskini&tuzingatie misingi ya Mafundisho yake!

Katika mahubiri ya Rais wa TEC,wakati wa Jubilei ya miaka 100 ya Seminari Kuu ya Kipalapala,Tabora,alijikita na mambo III:Shukrani kwa Mungu kwa zawadi ya Seminari. Pili:Kukumbuka tulikotoka,Maaskofu,watawa,waamini,waseminari,kwa kurudi kwa Mungu na kukiri Imani yetu.Tatu:Uchaguzi:"Sheria za Kanisa ni wazi na zinajulikana:Ni marufuku mapadre na watawa kushiriki kampeni za siasa,hiyo ni pamoja na uvaaji wa sare za chama chochote cha kisiasa."

Na Sarah Peraji, Tabora -Tanzania na Angella Rwezaula-Vatican.

Baada ya maandalizi ya mwaka mzima wa tukio kuu la kijubilei la Miaka 100 ya Seminari Kuu ya Tabora, nchini Tanzania, hatimaye ilifika kilele chake kwa adhimisho la   Misa Takatifu iliyoongozwa na Mwadhama Protase Kardinali Rugambwa, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Tabora katika Viwanja vya Seminari  kuu hiyo, tarehe 25 Septemba 2025, ili kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa mambo makuu aliyotenda kwa miaka hii 100 ya Seminari hiyo, na ambayo imewafunda viongozi wengi wa  Kanisa, lakini pia hata wa kijamii. Katika mahubiri yalioongozwa na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania,  Askofu Wolfgang Pisa, OFM,Cap, na Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi,  alijikita juu ya mambo makuu matatu.

Misa ya Jubilei miaka 100 ya Seminari Kuu ya tabora
Misa ya Jubilei miaka 100 ya Seminari Kuu ya tabora
Maadhimisho ya Miaka 100 ya Seminari Kuu Tabora,Tanzania
Maadhimisho ya Miaka 100 ya Seminari Kuu Tabora,Tanzania

Kwanza kabisa shukurani, kwa Mwenyezi Mungu, kwa kuwezesha safari hiyo miaka 100 ya Seminari, akitazama Somo la Kwanza lililosomwa kutoka Kitabu cha Walawi, na pia  kukumbuka suala la Jubilei linalosikika katika Kitabu cha Kumbu kumbu ya Torati. Askofu alielezea juu ya historia ya Seminari yenyewe, hadi kufikia miaka 100. “Shukrani kwa Wamisionari wa Afrika” wajulikanao White Fathers.  Na kwa njia hiyo akasema:  “Jubilei ni Mwaka wa Shukrani. Ni Mungu anayetekeleza yote kwa sababu haya si mastahili yetu.” “Katika Kitabu cha Walawi aliongeza "kinabainisha kuwa “Ni Mungu anayetekeleza yote.” Kuondoka kwa waseminari, hakufanyi kuyumbisha Seminari, bali inaendelea, kwa sababu ni Mungu mwenyewe anayejua.” Katika Injili iliyosomwa kuhusu Mkoma aliyeponywa, Askofu Pisa alisema, hiyo inasisitiza  kwamba : “Tupaze Sauti zetu  na tumshukuru Mungu, kama Mkoma alivyopaza sauti  yake na  hivyo tuunganishe sauti zetu na kumshukuru Mungu”… wote walipaza sauti na kwa mdundo wa ngoma…

Kardinali Rugambwa wakati wa Ibada ya Misa ya Jubilei
Kardinali Rugambwa wakati wa Ibada ya Misa ya Jubilei

Askofu Pisa alijikita kuelezea sehemu ya Pili kuhusu: “Kukumbuka tulikotoka, ” hasa kwa kutazama Wajubilei, daima kwa Wana wa Israeli, Wayahudi kwenye mali zao, na kwamba: “tunaalikwa kurudi katika familia zetu. Je ukoo wetu ni upi, familia yetu ni ipi? Kwa hiyo tunakumbushwa kurudi katika milki zetu. Tunaalikwa kurudi mahali  tuliko toka, katika Mwaka huu wa Jubilei. Na zaidi katika Jubilei Kuu ya Matumaini.” Rais wa TEC alikazia kusema: “Ni Bahati iliyoje kwa Seminari Kuu ya Tabora kuadhimisha miaka 100 katika Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Matumaini 2025. Katika mmantiki hiyo alitoa ushauri kuwa: “Turudi, nyuma kwa kutazama mema mengi yaliyotokea. Na zaidi mabadiliko yaliyofikiwa hadi sasa.” Aliwapongeza “wana Kipalapala kuboresha mazingira ya Seminari kuwa katika hali nzuri wakati wa  kusheherekea Jubilei hiyo.”

Walimu na Walezi wa Seminari Kuu ya Tabora
Walimu na Walezi wa Seminari Kuu ya Tabora

Na hiyo alendelea, "kama sisi ni wabatizwa, wakatoliki, mapadre, Maaskofu, watawa, waamini, waseminari, turudi kwa Mungu wetu. Kama Wakristo, tukiri Imani yetu,  kuamini Mungu mmoja katika nafsi Tatu… “nina sadiki kwa Yesu Kristo ambaye alikufa kwa ajili yetu, na ambaye Kanisa linaendelea kutangaza imani hiyo ya Ukweli wa Kanisa Katoliki.”  Askofu Pisa, alikazia kusema kuwa lazima, “Kuhubiri Injili, bila kuipunguza, kwa kufikiria kwamba itaendana na jinsi watu wanavyotaka.” Alihamasisha “kusali sala” na kufanya “Ibada kuu kwa Mama Bikira Maria.”

“Kanisa linapaswa kujitambulisha kwa wale walio maskini. Injili, siku zote si  kutatua matatizo, tuhubiri Msalaba, kuna hatari ambayo tunaweza kupunga Injili.  Askofu Pisa alitoa mifano ya kibiblia katika kitabu cha Pili cha Makabayo, 6,18-20; Wana wa Makabayo walipingana na waliotaka kuharibu Mila na tamaduni za Wayahudi, katika muktadha huo, Askofu Pisa alielezea hata sababu za kutaka kudhoofisha Kanisa. Kwa namna hiyo kudhoofisha walio wakubwa, huku akitaja kwamba hata walio altareni, wanaweza kudhoofika  na kuendelea hadi ngazi ya chini. Aliuliza maswali hata Masisita kwamba: “je wanatuchukua namba ngapi au waseminari katika kile kiitwacho: (Soft exposition)…(yaani  inayoweza kueleweka kama matumizi  laini au utumiaji wa mbinu za upole au za hila ndani ya muktadha wa kidini katika kuepuka migogoro.) Askofu Pisa, alitoa mfano kuhusu Mtakatifu Agostino ambaye anaelezea kwamba: “wachungaji wawatie moyo walio dhaifu: “Mchungaji huyu ndiye ambaye, kwa maneno na mfano, hutia ujasiri katika mioyo ya waamini, akiwaambia kwamba Bwana aliteseka na kuvumilia kwa ajili yao, akiwahimiza wasijitenge na imani.”

Injili Siku zote si kutatua matatizo,katika mahubiri ya Askofu Pisa,Rais wa TEC.
Jubilei ya Miaka 100 ya Seminari Kuu Tabora,Tanzania
Jubilei ya Miaka 100 ya Seminari Kuu Tabora,Tanzania

Na sehemu ya Tatu ilijikita kuhusu suala la uchaguzi, unaotarajia mwezi ujao Oktoba 2025. Askofu Pisa alisema, “Sheria za Kanisa ni wazi na zinajulikana.” Kwa njia hiyo kama mwakilishi wa Baraza zima la Maaskofu Katoliki nchini Tanzania (TEC) alipiga marufuku kwa mapadre, watawa na waseminari na wale wote waliowekwa wakfu kujihusisha na kampeni za kisiasa au kutambulishwa na chama chochote cha kisiasa kama washiriki wao. Aidha, marufuku hiyo inajumuisha kuvaa sare za vyama vya siasaKatika mahubiri hayo Askofu Pisa alilaani vikali tabia ya baadhi ya wanasiasa wanaopita kwenye nyumba za watawa na taasisi za Kanisa kwa lengo la kuwarubuni watu, wakiwemo watawa, ili ionekane kuwa wanawaunga mkono wao au vyama vyao vya siasa.

Askofu Pisa akiwasha Mshumaa
Askofu Pisa akiwasha Mshumaa

“Ni dhambi na kosa kubwa kumrubuni mtu ambaye hana uelewa wa jambo unalomtaka alifanye. Mnamkamata mnovisi au mtawa ambaye hata radio hasikilizi, taarifa hasomi, unamsomba tu na kumshirikisha kwenye jambo ambalo halielewi, hiyo ni dhambi. Marufuku!” alisisitiza. Askofu Pisa alisisitiza kuwa “katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu, viongozi wa Kanisa wakiwemo mapadre, watawa wa kike na kiume wanapaswa kufahamu na kuheshimu nafasi zao.” Alieleza kuwa “Sheria za Kanisa (Sheria za Kanoni) zimeweka bayana kuwa viongozi wa Kanisa hawapaswi kuhusishwa na kampeni au vyama vya siasa kwa namna yoyote ile,”( Rej Kifungo cha Sheria za Kanisa za Canon 672).

Waseminari wa Kipalapala wakati wa misa
Waseminari wa Kipalapala wakati wa misa

“Mapadre, watawa na waseminari hawapaswi kushiriki kampeni au kuvaa sare za vyama vya siasa. Ni marufuku kubwa kwa yeyote miongoni mwenu kuonekana kwenye kampeni. Hatutakiwi kuwa huko kabisa,” alieleza kwa msisitizo. Askofu Pisa pia alitangaza marufuku mahsusi kwa waseminari kuvalia mavazi ya chama chochote cha siasa  iwe ni fulana, kofia au aina nyingine ya vazi lenye alama ya kisiasa hata katika mazingira ya kawaida kama michezo au hata kulala nayo. “Ni marufuku kwa waseminari kuvaa T-shirt au kofia ya chama cha siasa, iwe ni kwa michezo, kulala nayo usiku au popote pale hata kama mgombea ni ndugu yako. Msilete unajisi Kanisani! Hiyo ni marufuku,” alisema kwa ukali.

Maaskofu Tanzania
Maaskofu Tanzania

Kabla ya uchaguzi fanya mang'amuzi

Askofu Pisa aliwahimiza waamini kutafakari kwa kina kabla ya kushiriki uchaguzi, huku akisisitiza kuwa uamuzi wa kumpigia kura mgombea fulani unapaswa kufanywa kwa dhamiri safi na yenye uelewa wa kutosha. “Tuachane na dhamiri potofu. Dhamiri yako inapaswa kuongozwa na ukweli na haki. Soma Neno la Mungu, zingatia Amri za Mungu, kisha fanya sala. Ihoji dhamiri yako ndipo ufanye uamuzi wako,” alielekeza.  Katika kuhitimisha mahubiri hayo, Askofu Pisa aliwakumbusha waamini wote kuhusu umuhimu wa kutafuta upatanisho na huruma ya Mungu, hasa katika kipindi hiki cha Mwaka wa Mahujaji wa Matumaini. Alitumia nafasi hiyo pia kuomba msamaha kwa niaba ya Kanisa kwa mapungufu yoyote yaliyotokea katika maandalizi au maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 100 ya Seminari ya Kipalapala. “Katika Mwaka huu wa Mahujaji wa Matumaini, tujitahidi kutafuta huruma ya Mungu na kuzingatia misingi ya kweli ya mafundisho ya Kanisa Katoliki,” alihitimisha.Jubilei ya Miaka 100 ya Seminari Kuu ya Kipalapala

Salamu:  Ujumbe wa pongezi kutoka Vatican

Mara baada ya Misa Takatifu, ilifuatiwa salamu mbali mbali, na kwa njia hiyo katika ujumbe kutoka Vatican ulisomwa na Katibu wa Balozi wa Vatican nchini Tanzania. Kwa njia hiyo alisema kuwa Kanisa la Tanzania limepongezwa kwa mafanikio ya Seminari hiyo kwa miaka 100 na kwamba mafanikio hayo ni uthibitisho wa imani ya kina na uongozi thabiti wa Kanisa. Ujumbe huo pia uliwapongeza waseminari wanaoendelea na safari ya wito wa kipadre na kuwatia moyo waendelee kwa unyenyekevu, bidii na maombi. Vatican imeikabidhi Tanzania kwa Mama Bikira Maria ili aendelee kuombea amani, mshikamano na umoja wa Taifa.

Katibu wa Balozi wa Vatican nchini Tanzania
Katibu wa Balozi wa Vatican nchini Tanzania

Historia fupi ya Seminari Kuu ya Kipalapala

Katika maadhimisho hayo ya kihistoria Askofu Pissa alieleza historia ya Seminari Kuu ya Kipalapala tangu ilipoanzishwa mwaka 1925. Seminari hiyo imesomesha wanafunzi 3,548 na kutoa mapadri 1,540, wakiwemo maaskofu 43 akiwemo Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo Askofu Mstaafu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam. Kipalapala ni seminari iliyoanzishwa na Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers) na imetoa mchango mkubwa katika kueneza Injili na malezi ya viongozi wa Kanisa nchini. Seminari ya kwanza ilianzishwa Ushirombo mwaka 1908 chini ya usimamizi wa Mtakatifu Karoli Borromeo. Ilihamishiwa Itaga, Tabora mwaka 1922, na hatimaye mwaka 1925 ikahamia Kipalapala ambako inaendelea hadi leo. Ilielezwa kuwa uamuzi wa kuhamia Tabora ulifanywa baada ya changamoto za usafiri na usambazaji wa vifaa kutoka makao makuu ya Vikarieti. “Tabora ilifaa zaidi kutokana na urahisi wa mawasiliano,” alisema. Mbali na kutoa mapadri, Askofu Pisa alisema seminari hiyo imechangia kutoa viongozi wengi wa kijamii waliopitia mafunzo ya Kipalapala lakini hawakufikia Daraja Takatifu. lakini wamekuwa baraka kwa taifa,” alisema. Alikumbusha pia ‘Wimbi la MV Kiparapara’, maarufu kwa kuwakatisha waseminari wengi masomo yao. Hata hivyo, alisisitiza kuwa changamoto hizo hazikuweza kuitikisa misingi ya seminari hiyo. Alihitimisha kwa kutoa wito: “Tuendelee kushika mafundisho ya Kanisa kwa uaminifu, tukiwa na moyo wa toba, sala, na upendo wa kweli wa Injili ya Kristo.

Walei ambao walisomea Seminari Kuu ya Tabora
Walei ambao walisomea Seminari Kuu ya Tabora

Gombera wa Kipalapala aeleza mikakati ya Maendeleo Mapya

Gombera wa Seminari hiyo, Padre Herman Kachema, baada ya kuwashukuru Maaskofu, kamati ya maandalizi na wote waliofanikisha sherehe hiyo, alieleza kuwa Kamati ya Maadhimisho ya Jubilei sasa imegeuka kuwa Kamati ya Maboresho. “Tunaelekea katika ujenzi wa ukumbi mpya kwa heshima ya Wamisionari wa Afrika, nyumba ya waseminari, Ofisi za Taasisi ya Utafiti wa Kichungaji, na nyumba za kisasa za mapadri,” alisema. Miradi hiyo inalenga kutoa mazingira bora ya malezi, masomo, na huduma kwa Kanisa na jamii kwa ujumla.

Gambera wa Seminari Kuu ya Tabora Tanzania
Gambera wa Seminari Kuu ya Tabora Tanzania

Padre Kitima: Kipalapala Chanzo cha Mawazo ya Vyuo Vikuu vya Kanisa

Katibu Mkuu  TEC, Padre Charles Kitima, alisema kuwa Kipalapala imekuwa kitovu cha maamuzi makubwa ya Kanisa, yakiwemo Azimio la 1995 la kuanzisha shule na vyuo. Alisema seminari hiyo ilikuwa chimbuko la shule kama Mtakatifu Francis (Pugu) na Mtakatifu  Maria (Kilakala), pamoja na vyuo vikuu vya Kanisa Katoliki nchini. Alisema pia kwamba mchango wa seminari hiyo katika sekta ya uchapishaji ni mkubwa, kwa kuwa ndio chimbuko la Tanzania Mission Press (TMP), kiwanda cha kwanza cha uchapishaji nchini kilichoendeshwa na Kanisa.

Utoto Mtakatifu wa Kimisionari katika Jubilei
Utoto Mtakatifu wa Kimisionari katika Jubilei

Wamisionari wa Afrika: Tunaimba Wimbo wa Maria

Mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Afrika (White Fathers) nchini Tanzania, naye alieleza furaha ya Shirika hilo kuona mbegu waliyopanda miaka 100 iliyopita inaendelea kuzaa matunda. “Tunaimba wimbo wa Maria: ‘Bwana amenitendea makuu’. Kwa mioyo yenye shukrani tunamshukuru Mungu,” alisema. Alisema Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 ya Seminari ya Kipalapala si tu yalikuwa kumbukumbu ya kihistoria, bali pia mwito wa kuendeleza usafi wa imani, kudumisha malezi bora ya kiroho na kuilinda nafasi ya Kanisa katika jamii, bila kuingizwa kwenye mitego ya kisiasa.

Mwamisionari wa Afrika
Mwamisionari wa Afrika

 

27 Septemba 2025, 10:03