Serminari ya Wamba yasimamishwa nchini Congo DR
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kitendo cha viongozi wa dini na baadhi ya walei kukataa kumpokea Askofu Emmanuel Ngona Ngotsi kuwa Askofu wa Jimbo la Wamba(kaskazini-mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo) kumepelekea uamuzi wa kusitisha malezi ya wasemina katika Jimbo hilo. Kwa mujibu wa taarifa kutoka Shirika la Kipapa la Habari za Kimisionari (FIDES) limebanisha kuwa, Askofu Ngona aliteuliwa kuwa Askofu wa Wamba kunako tarehe 17 Januari 2024, lakini hakuweza kumiliki jimbo hilo kutokana na kukataa kwa mapadre na waamini walei wengi wa kawaida. Licha ya majaribio kadhaa ya majadiliano yaliyoanzishwa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, Kitengo cha Uinjilishaji wa Kwanza na Makanisa Maalum, Ubalozi wa Vatican,na Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Congo(CENCO), hali hiyo haikupatiwa ufumbuzi.
Uamuzi Kutoka Baraza la Kipapa la Uinjilishaji
Ndiyo maana, tarehe 15 Aprili 2025, katika mawasiliano kwa Balozi wa Kitume nchini DRC, Mhashamu Askofu Mitja Leskovar, iliyotiwa saini na Kardinali Luis Antonio G. Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji, Kitengo cha Uinjilishaji wa Kwanza na Makanisa Maalum mwenye dhamana hiyo pamoja na Askofu Mkuu Fortunatus Nwachukwu, Katibu Mkuu wa Baraza la Kipapa hilo hilo, waliamua kusitisha malezi ya mapadre wajao katika jimbo hilo la Wamba.
Hali ni chungu la Jimbo la Wamba
Baada ya kukumbuka "hali chungu ya Jimbo la Wamba," Baraza la Kipapa la Uinjilishaji lilisema: "Kwa kuzingatia kwamba mazingira ya shida kama haya kwa sasa hayafai malezi ya mapadre wajao, na kwa hiyo hiyo Baraza hili, kwa kuzingatia ombi la mara kwa mara la Mheshimiwa, limeamua kusimamisha kwa muda shughuli zote za malezi katika Seminari ya Maandalizi, na Seminari Ndogo mwisho wa mwaka wa kitaaluma yaani tarehe 30 Juni 2025."
Waseminari wanataka kuendelea na malezi wanaweza kuomba kwa Maaskofu wa majimbo mengine
Askofu Sosthene Ayikuli Udjuwa, wa Jimbo la Mahagi-Nioka na Msimamizi wa Kitume wa Wamba, kisha alitangaza uamuzi wa Baraza la Kipapa Uinjilishaji. Kulingana na uamuzi huu, Askofu Ayikuli alikumbuka, "Waseminari wanaotaka kuendelea na malezi yao ya kipadre wanaweza kuwasiliana na maaskofu wengine wa Congo ambao wanaweza kuwakubali baada ya utambuzi ufaao. Kuhusu wafundaji na maprofesa wa seminari hizo mbili, ni lazima wagawiwe majukumu ya kihuduma isipokuwa malezi."