Dominika ya 27 ya Mwaka C:Nguvu ya imani na utumishi wa upendo
Na Padre Paschal Ighondo –Vatican.
Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 27 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe mkuu unahusu umuhimu wa imani katika maisha yetu. Imani kwa Mungu inatufanya tuwe daima upande wake, na Mungu kuwa upande wetu. Naye akiwa upande wetu hatupaswi kuogopa chochote, maana hakuna kitakachotushinda, kwani Yeye ni muweza wa yote. Ni katika muktadha huu wimbo wa mwanzo unasema hivi: “Ee Bwana, ulimwengu wote u katika uwezo wako, wala hakuna awezaye kukupinga ukipenda. Wewe umeumba yote, mbingu na nchi, na vitu vyote vya ajabu vilivyomo chini ya mbingu; ndiwe Bwana wa yote” (Esta 13:9, 10-11). Naye kwa upendo wake mkuu kwetu, anatujalia hata tusiyoomba. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya Mwanzo anasali hivi: “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, unatujalia kwa wema wako mkuu mema mengi kupita yale tunayoomba na kutamani. Utushushie huruma yako, utusamehe makosa yanayotuletea hofu moyoni, utuongezee na hayo tusiyothubutu kuomba”.
Somo la kwanza ni la kitabu cha Habakuki (Hab 1:2-3; 2:2-4). Kitabu hiki kimeandikwa kwa mtindo wa mazungumzo kati ya Mungu na Nabii Habakuki. Huyu alikuwa kutoka ukoo wa Yuda wa kabila la Lawi (Hab.1:1;3:1), aliyeishi kipindi kimoja na manabii Yeremia, Sefania na Nahumu (625-612KK). Wakati Nahumu akitangaza kuanguka kwa utawala wa Ashuru, makao makuu yake yakiwa mji wa Ninawi, kama adhabu toka kwa Mungu kwa uonevu na udhalimu wao, Habakuki alitangaza kukua na kuinuka kwa utawala wa Wakaldayo, Babilonia, unaokuja kuwaadhibu viongozi waovu wa ufalme wa Yuda, na wakati Sefania akiwaonya watu wa Yuda waache kuabudu sanamu na wamrudie Mungu, Yeremia anatangaza kuangamizwa kwa Yerusalemu kwa sababu ya dhambi za watu wake.
Ni katika mazingira haya Habakuki anamlalamikia Mungu kwa kuwaacha viongozi waovu na wenye dhambi kunawiri kama mfalme wao Yehoakimu aliyekuwa akiishi kwa anasa na starehe, huku watu wake maskini tena walio waadilifu, wakinyonywa na kuteswa na matajiri bila mtetezi. Naye Mungu hasikii kilio na maombi ya watu wake na ya nabii akimuomba awaokoe kutoka mikono ya adui zao. Hivyo anamuuliza, ni kweli wametenda dhambi, lakini, Je, adui zao ni wema kuliko wao hata anawaacha wawatese? Mungu anamjibu kwamba Wakaldayo walioishi Babilonia, Iraq ya sasa, wangekuja kuwaadhibu watu na viongozi waovu. Habakuki hakuelewa kwamba Mungu angeweza kuwatumia Wakaldayo, walio waovu kuliko Wayahudi waovu, ili kutekeleza hukumu dhidi yao. Mungu alimjibu kuwa Wakaldayo watatumika kuwaadhibu waovu ili wajirudi, waache uovu wao. Lakini pia wakaldayo nao watahukumiwa, kama watabaki katika uovu wao, na hatimaye haki itatawala na mtu mwadilifu ataishi kwa imani yake, akijikabidhi kwa Mungu muweza wa yote, akiisikiliza sauti yake na kutenda anayoamuru.
Kumbe Mungu anaweza kuwatumia waovu kuwaadhibu waovu, ili waache uovu wao na kurudi katika njia ya kweli. Nao waovu wakiisha kutimiza kusudi lake, wataadhibiwa kwa adhabu kubwa zaidi kama nao hawataacha uovu wao na kuenenda katika haki na kweli. Ni katika muktadha huu, zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; Njoni tumwimbie Bwana, tumfanyie shangwe mwamba wa wokovu wetu. Tuje mbele zake kwa shukrani, tumfanyie shamgwe kwa zaburi. Njoni, tuabudu tusujudu, tupige magoti mbele za Bwana aliyetuumba, kwa maana ndiye Mungu wetu, na sisi, tu watu wa malisho yake, na kondoo za mkono wake. Ingekuwa heri leo msikie sauti yake! Msifanye migumu mioyo yenu; kama huko Meriba; kama siku ile ya Masa jangwani, hapo waliponijaribu baba zetu, wakanipima, wakayaona matendo yangu” (Zab. 95:1-2, 6-9).
Somo la pili ni la waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Timoteo (2Tim 1:6-9, 13-14). Ujumbe ni kutokuionea haya imani yetu kwa Kristo, hata katika magumu kwa imani hii ina nguvu na uweza wa Mungu ambao haushindwi na chochote. Paulo aliamini juu ya hili, hivyo licha ya kuwa yuko gerezani, alimtia moyo Timoteo abaki imara na kuendelea kuihubiri Injili mpaka kieleweke. Nasi tunapaswa kuishuhudia imani hii tuliyoipokea kwa njia ya ubatizo na kwa kuwekewa mikono na wazee wa Kanisa, tukampomkea Roho Mtakatifu kwa sakramenti ya kipaimara, na tunaendelea kuimarishwa kwa Neno la Mungu, kutiwa nguvu kwa Ekaristi Takatifu, Mwili na Damu ya Kristo. Hivyo tusione haya kuishuhudia imani yetu kwa Kristo, bali tuishuhudie hata katika mateso na madhulumu, tusife moyo wala kuogopa cho chote. Kwa maana nguvu ya Roho Mtakatifu tuliyoipokea sio “roho ya woga, bali ya nguvu na ujasiri. Zaidi sana tuwafariji na kuwatia moyo wanaoteseka kwa ajili ya kuitangaza Injili ili nao wasife moyo, wala kurudi nyuma, bali wasonge mbele daima.
Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk. 17: 5-10). Ujumbe mkuu ni huu; nguvu ya imani ni utumishi kwa upendo. Yesu anatoa fundisho hili baada ya ombi la mitume kuongezewa imani. Licha ya kuwa hatuambiwa kwa nini mitume waliomba kuongezewa imani, lakini Yesu hawaongezei imani, bali jibu lake kwa ombi lao linaonesha kuwa mitume hawakuwa na imani hata kidogo, kwani wangekuwa nayo hata kama ni ndogo kama chembe ya haradali, ingewatosha kufanya mambo makubwa. Hii inatufundisha kuwa imani hata kama ni ndogo kiasi gani, inaweza kufanya mambo yasiyowezekana yakawezekane, kwa maana nguvu yake haitegemei uweza wa mtu, bali katika uwezo wa Mungu usioshindwa lolote. Hivyo imani haitegemei nguvu za mtu, bali kwa mtu kuweka tumaini lake lote kwa Mungu muweza wa yote, ambaye kwake hakuna lisilowezekana. Na imani inayofanana na chembe ya haradali, ni imani iliyojisimika katika unyenyekevu, haina kiburi wala majigambo, imejaa moyo wa shukrani, inatambua umuhimu, thamani, na mahitaji ya wengine, na kuwahudumia.
Ni katika muktadha huu Yesu anatoa mfano wa mtumwa asiye na faida, kwa tajiri wake. Lengo sio kuhalalisha ukatili, kukosa moyo wa huruma na shukrani kwa tajiri, ambaye mtumwa wake, mara baada ya kurudi kutoka shambani, amechoka na ana njaa, badala ya kumkaribisha ale na kupumzika, anamtaka amwandalie yeye chakula, amhudumie ale na kunywa kwanza, akishiba yeye ndipo amruhusu mtumwa wake ale na kunywa. Lengo ni kuonesha mahusiano yetu na Mungu, kuwa sio ya bwana na mtumwa, bali ni kama ya Bwana na Bibi Arusi, uhusiano unadai kila mmoja kujitoa kwa upendo na hiari bila kujibakiza, tena bila kutafuta faida binafsi. Hivyo hatupaswi kuiishi imani yetu kwa hofu na mashaka kama watumwa, bali watu huru, wanaofanya yote kwa upendo na uhuru kamili, bila shuruti yo yote. Ni katika mazingira na ufahamu huu, katika hitimisho la simulizi hili Yesu, anasema; “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya” (Lk 17:10). Huu ndio moyo wa kujitoa wazima wazima tukitumikiania kwa furaha na upendo sisi kwa sisi, kwa unyenyekevu, bila kutafuta maslahi binafsi. Ni kwa kufanya hivyo tutaweze kuishi pamoja kwa amani, utulivu na furaha maisha ya hapa duniani, tukiakisi tutakavyoishi milele yote mbinguni. Basi tumruhusu Roho Mtakatifu atawale maisha yetu, atufundishe na kutuongoza vyema, ili tuweze kutambua mpango na makusudi ya Mungu katika maisha yetu, kama alivyotuahidi Kristo Yesu aliposema; “Atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza kwenye kweli yote” (Yn 16:13).
Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi: “Ee Bwana, tunaomba uzipokee sadaka zilizowekwa kwa amri yako. Upende kutujaza neema za ukombozi wako kwa mafumbo haya matakatifu, tunayoadhimisha kwa mujibu wa utumishi wetu”. Na katika sala baada ya komunyo anasali; “Ee Mungu Mwenyezi, utujalie sakramenti hizi tulizopokea zizidi kutuburudisha na kutusitawisha, tupate kuwa na uzima wake yeye tuliyempokea”. Basi tuziruhusu neema za sakramenti tunazozipokea kufanya kazi ndani mwetu kwa sifa na utukufu wa Mungu, ili kwazo tuweze kutakatifuzwa na mwisho kuufikia uzima wa milele mbinguni. Lakini wanaofaidika nazo ni wale wanaoamini kuwa katika mafumbo ya Mkate na Divai, yumo Kristo Yesu mzima. Na hili ndilo tumaini letu.
Tumsifu Yesu Kristo.