Tafuta

Yesu alimwambia Zakayo telemka chini,leo ninaingia nyumbani kwako." Yesu alimwambia Zakayo telemka chini,leo ninaingia nyumbani kwako." 

Dominika ya 31 ya Mwaka C:Siku ya wokovu ni leo na umefika kwako!

Zakayo kumkaribisha Yesu nyumbani kwake, ukawa ndio mwanzo wa kubadili maisha yake, kuongoka kwake, ishara ya upendo wa Mungu kwa watu wote. Na baada ya kuongoka kwake alitangaza rasmi kuwa “nusu ya mali yake anawapa maskini na kama kuna yeyote aliyemnyang’anya na kumdhulumu atamlipa mara nne zaidi”.

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 31 mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe mahususi ni wokovu ni kwa ajili ya watu wote na kila mtu yuko huru kuupokea au kuukata, kwani kila mwanadamu amejaliwa akili, utashi na uhuru kamili. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema hivi: “Wewe Bwana usiniache, Mungu wangu, usijitenge nami, ufanye haraka kunisaidia, ee Bwana wa wokovu wangu” (Zab. 38 :21-22). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali hivi: “Ee Mungu Mwenyezi na mwenye huruma, wawajalia waamini wako neema ya kukutumikia vema na kwa uchaji. Tunakuomba utuwezeshe kukimbilia ahadi zako pasipo kukwaa.”

Somo la kwanza ni la kitabu cha Hekima ya Sulemani (Hek. 11:22-12:2). Huruma ya Mungu ni kwa watu wote na viumbe vyote, ndio ujumbe mkuu. Hii ni kwa sababu ya upendo wake Mungu usio na kipimo kwa vitu vyote alivyoviumba, maana roho yake isiyoharibika imo katika vyote. Yeye anawahurumia watu wote, na kwa sababu anao uweza wa kutenda mambo yote, anawasahihisha kidogo kidogo wale wanaokengeuka kutoka katika njia njema, akiwaonya, na kuwakumbusha makossa yao, ili waache ubaya wao, na kurudi katika njia ya haki na kweli. Lakini wasipotubu mwisho wao ni kuangamia milele. Nasi tukianguka katika dhambi, tumrudie na kumlilia, Naye kwa upendo wake mkuu, atatuhurumia na kutusamehe.

Ni katika tumaini hili zaburi ya wimbo wa katikati inasema hivi; “Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza, na kulihimidi jina lako milele na milele. Kila siku nitakuhimidi, na kulisifu jina lako milele na milele. Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema. Bwana ni mwema kwa watu wote, na rehema zake zi juu ya viumbe vyake vyote. Ee Bwana, viumbe vyako vyote vitakushukuru, na wacha Mungu wako watakuhimidi. Waunena utukufu wako, na kuuhadithia uweza wako. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote, na mamlaka yako ya vizazi vyote. Bwana huwategemeza wote waangukao, huwainua wote walioinama chini” (Zab. 145:1-2, 8-11, 13-14).

Somo la pili ni la waraka wa pili wa Mtume Paulo kwa Wathesalonike (2Thes. 1:11-2:2). Ni mawaidha ya kutia moyo na kutuimarisha katika imani tunapokumbana na madhulumu, mateso na mafundisho ya uongo kuhusu kuja kwa Yesu mara ya pili. Ni kweli kuwa Kristo atarudi kuwafariji wanaomwamini, kuwachukua na kuwapeleka mbinguni, na waovu adhabu yao ni moto wa milele. Lakini siku hiyo ya hukumu, haifiki mara moja kwa wote, bali inampata kila mmoja kwa wakati wake. Hivyo hakuna sababu ya kufadhaika na kuhuzunika, kuacha kufanya kazi za maendeleo, tukiisubiri siku hiyo. Bali tuendelee kuishi vyema maisha yetu ya kila siku tukifanya kazi ili tujipatie mahitaji yetu. Mtume Paulo anasisitiza kufanya kazi kwa sababu wapo waliacha kufanya kazi kwa kuamini kwamba Kristo angerudi upesi kuwachukua. Nasi tunaonywa tusidanganyike na mafundisho hayo ya uongo, tufanye kazi kwa bidii, huku tukisali na kukesha kwa kutenda matendo mema, ili Bwana atakapomtuma mjumbe wake, dada kifo, atukute tu tayari kuingia katika ufalme wa mbinguni.

Yesu na Zakayo mtoza ushuru.
Yesu na Zakayo mtoza ushuru.

Injili ni ilivyoandikwa na Luka (Lk. 19:1-10). Nayo inahusu simulizi la kuongoka kwa Zakayo, jina lake likiwa na maana ya “msafi” – “mtu wa haki”. Huyu ni mtoza ushuru, mkuu wa watoza ushuru, mtu tajiri, mfupi wa kimo, Myahudi aliyefahamika kuwa ni mdhambi kwa sababu ya kazi yake ya kutoza ushuru, akishirikiana na utawala wa kirumi kuwanyonya na kuwanyanyasa watu wa taifa lake. Ni katika muktadha huu watoza ushuru wote walichukuliwa kuwa ni wadhambi, wala rushwa, kwa kuwatoza ushuru zaidi ya kiasi kilichowekwa. Ndiyo maana walipomuuliza Yohane Mbatizaji “na sisi, je, tufanye nini”? Aliwaambia; “msitoze zaidi ya kiasi kilichowekwa” (Lk.3:12-13).

Zakayo alikuwa na hamu ya kumuona Yesu. Hamu hii ilimfanya apande juu ya mkuyu sababu ya ufupi wa kimo chake. Lakini Yesu alipofika mahali hapo, aliinua macho, akamuona, akamuita kwa jina lake, akamwambia shuka upesi leo hii nitakuwa nyumbani kwako.  Yesu anakuwa wa kwanza kumuona Zakayo, kabla ya yeye aliyetaka kumuona, kumuona, kwa maana Yeye amekuja kutafuta na kuona kilichopotea akiokoe. Hamu ya Zakayo kumuona Yesu, haikuishia tu kumuona, bali kuingia nyumbani kwake na kukaa naye. Na watu walipoona hivyo walinung’unika, wakisema; “Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi”. Ndipo Kristo akatangaza lengo la kuja kwake, wokovu kwa watu wote, kutafuta kilichopote na kukiokoa.

Zakayo kumkaribisha Yesu nyumbani kwake, ukawa ndio mwanzo wa kubadili maisha yake, kuongoka kwake, ishara ya upendo wa Mungu kwa watu wote. Na baada ya kuongoka kwake alitangaza rasmi kuwa “nusu ya mali yake anawapa maskini na kama kuna yeyote aliyemnyang’anya na kumdhulumu atamlipa mara nne zaidi”. Tendo hili la kulipa mara nne zaidi ni ishara ya toba na wongofu wa ndani, unaomsukuma mtu kutenda zaidi ya madai ya kisheria kwa wadhambi waliotubu; “Ndipo atakapoungama dhambi zake alizozifanya, naye atarudisha kwa hatia yake, kwa utimilifu wake, tena ataongeza juu yake sehemu ya tano na kumpa huyo aliyemkosea” (Hes 5:7; Wal 6.5) au kulipa mara mbili zaidi (Kut. 22:4). Kulipa mara nne zaidi ilikuwa ni dalili wazi ya yeye kuongoka, kwa maana kuongoka kuliko kwa kweli kunaendana na kuona uchungu kwa makosa uliyofanya na madhara uliyo sababisha kwa wengine na kuamua kuyasahihisha yale unayoweza, na yale usiyoweza unaonyesha toba ya kweli kwa kwa kutenda matendo ya huruma.

Zakayo aliyatenda haya yote kuonesha kuwa yeye sasa ni kiumbe kipya. Ndiyo maana Yesu alitangaza kuwa; “Leo wokovu umefika nyumbani humu...Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea” (Lk 19:10). Hii ndiyo maana ya mfano wa kondoo aliyepote (Lk.15:4-7), na kutimia kwa utabiri wa Nabii Ezekieli unaosema; “Nami Nitawatafuta kondoo waliopotea na kuwarudisha katika zizi. Nitawafunga waliojeruhiwa na kuwatia nguvu waliodhaifu…Nitalichunga kundi kwa haki” (Ez. 34:16). Ndiyo kusema mara baada ya kuongoka kwake, akalisikia Neno la Mungu, Zakayo alianza mara moja kuliishi na kuweka katika matendo mafundisho haya Yesu; “Basi toeni sadaka vile mlivyo navyo, na vitu vyote vitakuwa safi kwenu” (Lk 11:41). “Uzeni mali zenu mkawape maskini. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, mkajiwekee hazina mbinguni isiyokwisha, mahali ambapo mwivi hakaribii wala nondo haharibu. Kwa maana hazina yako ilipo, ndipo na moyo wako utakapokuwa pia” (Lk 12:33-34). “Nenda ukauze kila kitu ulicho nacho, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni. Kisha njoo, unifuate” (Lk 18:22).

Nasi tuige mfano wake, tulipodhulumu turudishe mara nne, kama hatuweze kurudisha bila kusababisha madhara zaidi, basi tutende matendo ya huruma, tuwasaidie wahitaji kwa mali ya dhuluma, naye Mungu atapendezwa na kutustahilisha kuingia katika uzima wa milele kwa sadaka na majitoleo hayo. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi: “Ee Bwana, sadaka hii tunayokutolea iwe dhabihu safi mbele yako, ituletee na sisi huruma yako”. Na katika sala baada ya kuomunyo akihitimisha maadhimisho haya anasali: “Ee Bwana, tunaomba neema yako izidi kutenda kazi ndani yetu, na tena ituweke tayari kupokea ahadi za sakramenti hizi zilizotuburudisha”. Hii iwe ndiyo hamu ya mioyo yetu itakayotimia tutakapoingia katika uzima wa milele mbinguni.

Tumsifu Yesu Kristo.

Tafakari ya Neno la Mungu
31 Oktoba 2025, 17:25