Tafuta

Kumbukumbu ya Miaka 26 tangu alipofariki dunia Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere: Tanzania imejengwa juu ya misingi ya haki, amani, majadiliano, heshima na haki msingi za binadamu. Kumbukumbu ya Miaka 26 tangu alipofariki dunia Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere: Tanzania imejengwa juu ya misingi ya haki, amani, majadiliano, heshima na haki msingi za binadamu. 

Maadhimisho ya Kumbukumbu ya Mwl J.K. Nyerere: Haki Na Amani Nchini Tanzania

Uchaguzi mkuu ni tukio muhimu; wito kwa watanzania kujikita katika majadiliano kwa kukazia ukweli na uwazi, umoja na mshikamano wa Kitaifa; thamani ya uhai, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watanzania waendeleze urithi wa Mwalimu na kwamba, amani ni jukumu la wote. Maaskofu wamekazia kuhusu: Heshima kwa uhai wa mwanadamu ulindwe. Watanzania washiriki Uchaguzi Mkuu wakiongozwa na dhamiri hai. Ujumbe umetolewa tarehe 14 Oktoba 2025.

Na Sarah Pelaji, Dar Es Salaam

Kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025: TUME ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), imetoa ujumbe maalum unaohusisha tafakari ya kina juu ya mustakabali wa Taifa, hasa katika kipindi ambacho Watanzania wanamkumbuka Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, na kuelekea Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29 mwaka 2025. Uchaguzi mkuu ni tukio muhimu; wito kwa watanzania kujikita katika majadiliano kwa kukazia ukweli na uwazi, umoja na mshikamano wa Kitaifa; thamani ya uhai, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Watanzania waendeleze urithi wa Mwalimu na kwamba, amani ni jukumu la watanzania wote. Maaskofu wamekazia kuhusu: Heshima kwa uhai wa mwanadamu ulindwe. Watanzania washiriki Uchaguzi Mkuu wakiongozwa na dhamiri hai. Ujumbe huo umetolewa tarehe 14 Oktoba, 2025 ikiwa ni miaka 26 tangu kufariki kwa Mwalimu Nyerere, ukisisitiza kwamba haki, amani, umoja na utu wa binadamu ndizo nguzo kuu alizoacha kama urithi kwa Taifa. Katika ujumbe huo uliosainiwa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki na Amani TEC Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki Dar es Salaam, Yuda Thadaeus Ruwa’ichi, OFM Cap imewakumbusha Watanzania kwamba Tanzania imejengwa juu ya misingi ya amani, majadiliano na heshima kwa haki za binadamu.

Kumbukizi ya Miaka 26 tangu Mwl. J.K. Nyerere alipofariki dunia.
Kumbukizi ya Miaka 26 tangu Mwl. J.K. Nyerere alipofariki dunia.

Umeeleza kuwa Uchaguzi Mkuu ni tukio muhimu linalotoa nafasi ya kuimarisha misingi hiyo na si muda wa mgawanyiko bali wa umoja na tafakari ya kina juu ya mustakabali wa Taifa. Akiwasilisha ujumbe huo, Askofu Mkuu Ruwa’ichi alisema kuwa ni wajibu wa kila raia kuhakikisha kwamba anatumia haki yake ya kupiga kura kwa kuongozwa na dhamiri safi, yenye hofu ya Mungu na iliyojengwa juu ya ukweli. “Dhamiri hai na safi ndiyo inayoongoza mtu kufanya maamuzi sahihi, bila kurubuniwa kwa vitisho au rushwa,” amesema, huku akitoa wito kwa wananchi kuepuka kugawanywa kwa misingi ya itikadi za kisiasa, ukabila au dini. Amesisitiza kuwa viongozi wanaogombea nafasi za uongozi wanapaswa kuwa mfano wa amani na kuheshimu utu wa kila mwanadamu. Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ibara ya 3 na 5, inayoweka bayana kuwa, mamlaka ya kuongoza hutolewa na wananchi, hivyo viongozi wanaopata dhamana wanapaswa kuilinda, kuihudumia na kuijenga jamii kwa misingi ya haki, uadilifu na utumishi kwa umma.

Askofu mkuu Yuda Thaddei Ruwaichi, Tume ya Haki na Amani, TEC
Askofu mkuu Yuda Thaddei Ruwaichi, Tume ya Haki na Amani, TEC

Wito wa Majadiliano na Ushirikiano: Katika ujumbe huo, Maaskofu wamesisitiza umuhimu wa mazungumzo kati ya wadau wa siasa kama njia kuu ya kusuluhisha tofauti na kuimarisha demokrasia. Wamesema kuwa Tanzania ina historia nzuri ya maridhiano na umoja, hivyo ni muhimu kwa viongozi wa serikali na vyama vya siasa kuendeleza utamaduni wa kusikilizana badala ya kupuuzana. “Wanasiasa kupitia vyama na serikali kaeni mzungumze ili kuwahakikishia watu haki zao. Nguvu ya wananchi ipo kwenye hoja na serikali kupokea mawazo ya wananchi ni ishara ya nguvu ya utawala unaojengwa juu ya uwazi na ukweli,” ujumbe huo unasema. Ujumbe huo umesisitiza kuwa kilio cha raia ni sehemu ya ujenzi wa taifa na serikali inapoonesha utayari wa kusikiliza, hujenga imani ya wananchi na kuimarisha amani ya kudumu.

Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere
Mtumishi wa Mungu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere

Thamani ya Uhai, Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu: Tume hiyo imesisitiza kwamba uhai wa mwanadamu ni zawadi takatifu, hivyo unapaswa kulindwa na kuthaminiwa na kila mmoja ndani ya jamii. Wamenukuu Maandiko Matakatifu mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, hivyo hakuna mwenye mamlaka ya kuuondoa uhai wa mtu mwingine. Ingawa ujumbe umeangazia hitaji la kulinda utu wa binadamu, Tume hiyo pia imetoa matumaini kwamba Tanzania itaendelea kudumisha utulivu na kuheshimu haki za kila raia. Tume hiyo ya Haki na Amani TEC imekemea matukio ya utekaji ambayo yanasababisha kupotea kwa haki msingi za binadamu hasa haki ya kuishi. Aliisisitiza serikali kuhakikisha usalama na haki ya kuishi kwa wananchi wote, akibainisha kuwa uchaguzi ujao utakuwa na maana tu endapo viongozi watakaochaguliwa watakuwa tayari kulinda na kutetea uhai wa binadamu kwakuwa wao ndiyo waliopewa dhamana ya kulinda maisha ya Watanzania. Imesisitiza kuwa ushirikiano kati ya vyombo vya dola, viongozi wa dini na wananchi unaweza kuimarisha zaidi amani nchini.

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania

Kuendeleza Urithi wa Mwalimu Nyerere: Maaskofu wamesema kuwa kumbukizi ya Mwalimu Nyerere inapaswa kuwa chanzo cha kutafakari na kujifunza. Mwalimu alitanguliza mbele uzalendo, utu, umoja na amani kama nguzo za taifa. “Tutamuenzi Baba wa Taifa iwapo tutaendeleza mazungumzo yenye kujenga, kuheshimiana na kutanguliza maslahi ya Watanzania wote,” wamesema. Tume hiyo imewataka Watanzania kutumia kipindi hiki kuelekea uchaguzi kama nafasi ya kuimarisha udugu, upendo na mshikamano, badala ya kujenga uadui. Wamewakumbusha wananchi kuwa uchaguzi si vita, bali ni sehemu ya safari ya taifa kuelekea maendeleo na haki kwa wote.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere: Uzalengo, Utu, Umoja na Amani
Mwalimu Julius Kambarage Nyerere: Uzalengo, Utu, Umoja na Amani

Tanzania ya Amani ni Jukumu Letu Sote: Wakihitimisha ujumbe wao, Tume hiyo imesema kuwa historia ya chaguzi za Tanzania tangu mwaka 1962 imejengwa juu ya misingi ya amani na maridhiano. Wananchi na viongozi wote wanapaswa kuendelea kuilinda historia hiyo kwa kuweka mbele maslahi ya Taifa. “Tunaomba kila Mtanzania, awe kiongozi au raia wa kawaida, aheshimu dhamiri yake, azingatie ukweli na atangulize amani katika kila hatua. Tanzania ni yetu sote na amani yake ni urithi wa thamani tuliouachiwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere,” Askofu Ruwa’ichi amesema.

Nyerere Say 2025
16 Oktoba 2025, 16:48