Maaskofu wa Kenya waomboleza Raila Odinga:Kiongozi jasiri na bingwa wa haki”
Na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.
Baraza la Maaskofu Katoliki wa Kenya (KCCB) limetoa rambirambi kwa Mheshimiwa Dkt William Samoei Ruto, Rais wa Jamhuri ya Kenya, kwa Mama Ida Odinga na familia nzima ya Odinga, na kwa wananchi wote wa Kenya, kwa niaba ya Kanisa Katoliki nchini Kenya.
"Tunaungana na Wakenya wote kuomboleza kwa kumpoteza kiongozi shupavu na aliyejitolea, alitetea bila kuchoka demokrasia, haki za binadamu, na utawala wa sheria na mara nyingi akiwa katika hatari bila kuogopa," maaskofu walitoa ujumbe huo katika taarifa iliyotiwa saini na mwenyekiti wa baraza la Maaskofu, Maurice Muhatia Makumba, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu katoliki la Kisumu na Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya(KCCB).
“Wakati wa huzuni uunganisha wakenya wote katika roho ya upatanisho”
"Kujitolea kwake bila ubinafsi, uthabiti, na maono ya nchi isiyoyumba na yenye umoja itasalia kuwa urithi wa kudumu kwa vizazi vijavyo." Maaskofu waliikabidhi roho yake kwa Mungu, na kumuombea pumziko la amani, na kuwapa pole na kuwatakia faraja ya Mungu kwa familia, na nchi yote kwa ujumla wakati huu wa majonzi. "Tunapoikabidhi roho yake kwa Mungu, ambaye ni mwingi wa huruma, tunamwomba Mungu ampe pumziko la milele na kumlipa kwa kazi yake katika shamba la mizabibu la haki na amani," ujumbe ulibainisha. "Naomba wakati huu wa huzuni ya kitaifa uunganishe Wakenya wote katika roho ya upatanisho, ushirikiano na matumaini."
Urithi wa Ujasiri na Maono
Hayati Raila Odinga, mmoja wa watu mashuhuri wa kisiasa nchini Kenya, atakumbukwa kwa kupigania demokrasia, upinzani wake dhidi ya utawala wa kimabavu na kutetea haki za watu wanyonge na waliotengwa. Alikuwa ishara ya uvumilivu na umoja wa kitaifa, akihamasisha Wakenya wengi kuamini katika jamii huru na ya haki.
Ujumbe wa Maaskofu unaonyesha jukumu la muda mrefu la Kanisa Katoliki katika safari ya kidemokrasia ya Kenya, likisimama pamoja na watu katika matarajio yao ya haki, amani na upatanisho. “Mtakuwa mashahidi wangu” (Mndo 1:8), kauli mbiu ya Maaskofu inakumbusha, ikiwaalika Wakristo wote kushuhudia ukweli na matumaini, hasa katika nyakati za huzuni za kitaifa.