Tafuta

2025.10.01 Mwenyeheri Peter To Rot azungumziwa na Askofu Mkuu Rochus Josef Tatamai MSC. 2025.10.01 Mwenyeheri Peter To Rot azungumziwa na Askofu Mkuu Rochus Josef Tatamai MSC.  (© Fr. Zdzislaw Mlak SVD in PNG)

Mwanafamilia wa Mwenyeheri Peter To Rot,azungumzia juu ya Maisha yake

Askofu mkuu Rochus Tatamai,mjukuu wa Mwenyeheri Peter To Rot,asimulia maisha ya shahidi huyu wa kikatoliki wa Papua New Guinea, akisisitiza kuwa imani ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku kwa njia ya sala, Misa,na kuwasaidia jirani zetu.

Na Sr. Christine Masivo, CPS – Vatican.

Wakati tunatarajia kutangazwa kuwa Mtakatifu kwa Mwenyeheri Peter To Rot tarehe 19 Oktoba 2025, Askofu Mkuu Rochus Josef Tatamai, MSC, wa jimbo kuu la Rabaul, nchini Papua New Guinea, alizungumza na Vatican News kuhusu urithi wa mfia imani, ambaye  alisema ni wa kibinafsi na wa kiroho. Mwenyeheri Peter To Rot alikuwa Katekista kijana aliyeuawa kwa ajili ya imani yake nchini Papua New Guinea wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia na Wajapan mwaka 1945. Askofu mkuu Tatamai alisema wakati wa utoto wake alisikia historia za ujasiri na imani za babu yake. "Tangu utotoni, nilihisi uwepo wake nyumbani kwetu," Askofu Mkuu wa PNG alisema.

Familia na Imani

Peter To Rot alizaliwa mwaka 1912, alikuwa mtoto wa tatu kati ya watoto wanne katika familia katika kijiji cha Rakunai. "Ndugu zake walikuwa Theresa IaVarpilak, Josef Tatamai, na Gabriel Telo. Wazazi wao, Angelo Topuia na Maria Iatumul, walikuwa wa kwanza kubatizwa na kuwa Wakatoliki, na familia nzima ilibatizwa na Wamisionari wa Moyo Mtakatifu, katika Jumuiya yetu," Tatamai alisema. Kadhalika Askofu Mkuu alielezea kwamba uhusiano wake na Mwenyeheri Peter To Rot, unaanzia kwa babu yake, Yosefu  Tatamai, kaka yake mkubwa wa  Peter To Rot. "Wazazi wangu na babu zetu walituambia kuhusu kujitolea kwa Peter To Rot kwa Mungu na jumuiya, bila kuyumbayumba. Haikuwa historia tu, alikuwa ni mfano wa kweli kwa wote," alisema. Babu yake Askofu Mkuu Tatamai alipenda sana kwamba siku moja kutakuwa na Padre katika familia, na wazee wa Kijiji walikumbuka sana haya maneno siku ambayo Rochus Tatamai alipokuwa Padre.

Msukumo wa Peter To Rot

“Maisha yake yalinifundisha kwamba imani si jambo la kufikirika, tunaishi Imani hii wakati mwingine katika mazingira magumu.” Alieleza na kuongeza “Ujasiri wa Peter To  Rot, kama babu yangu, kupitia historia  nilizosimuliwa, hunitia moyo kutumikia kujitolea kuitumikia Kanisa.” Huko Papua New Guinea, kama ilivyo katika tamaduni zingine, ni kawaida kuwaita wajomba kama "babu."” Kwa njia hiyo “kuwa Padre na baadaye Askofu Mkuu ilikuwa na changamoto zake, kila wito una matatizo yake,” alithibitisha Askofu Mkuu Tatamai. “Kulikuwa na wakati ambao nilikuwa na mashaka kuhusu kuwa tayari kuifanya kazi ya Mungu. Lakini siku zote nilirudi kwenye kielelezo cha babu yangu, ambaye alisimama imara hata aliponyanyaswa kwa ajili ya Kristo. Ujasiri huo ulinitia nguvu.”

Imani katika Kanisa

"Imani ni chanzo cha utambulisho na nguvu ya kikristo," Askofu Mkuu Tatamai alisisitiza. "Ningependa kuwatia moyo vijana kutafuta ushuhuda kwa kuishi imani yenu kwa ujasiri na uadilifu. Tunaishi katika ulimwengu uliojaa mambo ya kukanganya, lakini imani italeta uwazi na sababu katika maisha." Huduma ya Askofu Mkuu ina uhusiano wa kina na jumuiya yake. "Kazi ya kichungaji ni kusikiliza na kutembea na watu katika furaha na shida zao," alielezea. "Jukumu langu ni kuwa mtumishi wa wote na kuwasaidia wengine kuwa na tumaini hasa wakati ngumu. Maisha ya To Rot yananikumbusha kwamba, kuwatumikia wengine kwa upendo ndiyo njia kweli ya kuishi imani yangu. Maamuzi ninayofanya, homilia zangu  na  matendo ya huruma katika maisha yangu yanaadhihirishwa na ushuhuda wake. Yeye ni mfano mwema wa kuigwa, ninahisi kuwa na jukumu la kuishi kwa uhalisi, ili historia yake iendelee kuwatia moyo wengine.”

Padre kutoka ka familia ya To Rot

Askofu Mkuu alizungumzia pia juu ya nchi kuadhimisha miaka 50 ya uhuru, akisema, "Mungu mwenyewe anaibariki nchi yetu kwa neema na zawadi nzuri ya uhuru wetu kwamba kila mtu anapaswa kuishi maisha ya utakatifu hasa kuishi maisha ya kikristo. Aliwahimiza wanafamilia kuzingatia kuishi maisha ya familia kwa uadilifu. “Mtoto anayezaliwa katika familia hupafuta ushauri kutoka kwa wazazi. Mume na mke wanapaswa kuwa kielelezo cha kuigwa katika kuendeleza maisha ya familia, kuwafundisha watoto kusali, kusoma Biblia, na kudumisha imani kama watakatifu, kushika imani ya Kikatoliki, na kuwa kichocheo kwao kwa kuishi sakramenti.”

Matumaini ya siku zijazo

Askofu mkuu Tatamai alitafakari juu ya matumaini yake ya siku za usoni akisema, “ningepeda kuona Kanisa ambalo wanaishi imani kwa ujasiri, jumuiya zinasaidiana, na vijana wanahamasishwa kuwa viongozi wanaojikita katika upendo na huduma. To Rot anatufunza kuwa sote tunaweza kuishi utakatifu kwa misngi wa imani. Askofu Mkuu, alisisitiza kwamba  Mwenyeheri Peter To Rot sio kumbukumbu ya kihistoria tu bali ni mfano wa kutuongoza katika njia ya imani na wale tunaowahudumia. Kwa kuhitimisha alibainisha: "Ni zawadi na jukumu letu sote," alimalizia kwa kusema. "Zawadi kwa sababu anatupatia matumaini, na jukumu linalotuita kuishi kwa uaminifu, ili wengine waweze kuhamasishwa kufanya vivyo hivyo. Kanisa lote linapojiandaa kusherehekea Peter To Rot kuwa Mtakatifu, atakuwa si tu  Mtakatifu wa jadi,  bali pia wa siku zijazo na anatufunza kuwa,  kufa kwake kama shahidi wa imani ni ishara tosha ya kuishi maisha ya Kikristo.”

Mwenyejeri To Rot atatangazwa kuwa Mtakatifu 19 Oktoba
13 Oktoba 2025, 11:37