Siku kuu ya Watakatifu wote na Marehemu Wote
Na Shemasi George Francis Timalias - Chuo Kikuu cha Kipapa Antonianum.
Karibu ndugu msikilizaji wa Radio Vatican, katika tafakari hii, inayotugusa kwa karibu sana ambayo inakumbusha Siku Kuu ya Watakatifu wote, kila ifikako tarehe Mosi Novemba ya kila mwaka, lakini pamoja na Watakatifu, kuna ndugu zetu Marehemu wote waliotutangulia mbele ya haki ambapo Mama Kanisa, anatunapatia fursa ya kuwakumbuka kila ifikapo tarehe 2 ya mwezi Novemba na kuendelea hadi mwisho wa mwezi. Kwa hiyo tuanze tafakari hii, sehemu ya kwanza ya Watakatifu. Fundisho kuu tunalopata katika siku hii ya watakatifu wote ni msisitizo wa maisha yetu kuishia mikononi mwa Mungu aliyetuumba huko mbinguni. Kwa uhakika mafundisho ya Kanisa letu Katoliki yametueleza wazi kwamba tumeumbwa ili kumtumikia Mungu Muumbaji wetu, kumpenda na kumuabudu yeye peke yake na mwisho kufika kwake mbinguni(Rej.KKK 1721). Na heri hutufanya washiriki wa asili ya Kimungu (2 Pt 1:4) na uzima wa milele. Kwa hiyo, mwanadamu huingia katika utukufu wa Kristo na katika kufurahia maisha ya Utatu.
Hatua hii ya mwisho ya kufika kwake mbinguni ndiyo hatua ambayo wenzetu hawa ambao ni kundi la watakatifu wameifikia. Tuishi katika mlengo huo. Ni wazi waliishi katika dunia hii tuliopo na walishughulika na shughuli hizi hizi kwa hiyo hakuna kazi ambazo mpaka uwe katika hizo ndipo utakuja kuwa Mtakatifu. Kuna watakatifu maaskofu, mapadre, watawa, wakulima, waalimu, waandishi, waimbaji, mafundi wengine wengi. Kwa hiyo kila mmoja wetu anayo nafasi ya kutazama maisha ya Mtakatifu fulani aliye fanya kazi ambayo unaifanya sasa. Hilo liunganishwe pia na maisha ya sala, kutenda matendo mema na upendo mkubwa kwa wenzetu.
Kumpenda Mungu na kumtumikia kunajumuisha kufuata amri zake. Kumpenda Mungu kutaonekana katika matendo yetu, katika kuwajibika kwetu kwa muumba wetu. Kwa sisi wakatoliki basi ni kuungana na Kristo katika kuziishi sakramenti Takatifu zinazotuunganisha na Yeye. Tubatizwe, tufanye toba tunapomkosea, tumpokee katika Ekaristi Takatifu. “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele nami nitamfufua siku ya mwisho.” (Rej. Yh 6:54) Tuishi vema katika maisha ya viapo vyetu kila mmoja katika wito alio uchagua. Ndoa na viapo vyake, utawa na nadhiri zake pamoja na upadre kwa kuzingatia utii, useja na ufukara. Mababa wa Kanisa walio wengi wamefafanua kwamba, watakatifu tunaowasherehekea, sio kwamba waliishi kama Malaika, hapana.
Walikuwa na madhaifu yao ya kibinadamu isipokuwa kilichopelekea wao kuwa watakatifu ni bidii na jitihada zao katika kumtafuta Mungu, katika kuutafuta utakatifu, hata katika magumu walipambana wakiongozwa na shauku thabiti ya kufikia uzima wa milele. Hili liliambatana na kuilinda imani yao kila mmoja katika mazingira yake mpaka mwisho wa maisha yao hapa duniani. Kwa hiyo ni Mwaliko kwetu sote katika aina zote za maisha tunayoishi, katika mazingira yetu na hali zetu mbalimbali kwamba mlango uko wazi kufika Mbinguni na kupata uzima wa milele. Kwa hiyo kusherehekea siku kuu ya watakatifu wote ni kupongeza juhudi na bidii zao zilizo wafikisha kuwa watakatifu na pia kujifunza kutoka kwao ili kufuata mifano na nyayo zao nasi kuwa watakatifu siku moja kama walivyofanya wao.
Siku ya kukumbuka Marehemu wote tarehe 2 Novemba
Ndugu msikilizaji, kama nilivyotangulia kusema kumbu kumbu ya ndugu zetu waliotutangulia mbele ya haki basi, tutafakari siku hii. Katika siku hii maalumu ambayo imewekwa na Mama Kanisa, kwa ajili ya kuwakumbuka marehemu wote tunaongozwa na imani yetu moja kwa moja katika kutumaini ufufuko. Tungeishi kwa kulia na kuhuzunika bila kukoma kama kusingekuwa na tumaini la ufufuko, lakini kwa vile Kristo alizaliwa duniani akateseka, akafa, akazikwa na akakamilisha ukombozi wetu kwa kufufuka, basi ni faraja ya pekee kuona kwamba ndugu zetu ambao kwa ubatizo wao wameshiriki mateso na kifo chake Kristo na ufufuko u pamoja nao kwa kuwa wana kigezo tayari cha kukombolewa na Kristo tunaye muamini ambaye katika Enjili zibathibitisha kama vile Injili ya Marko:“Yeyote atakaye amini na kubatizwa ataokoka,”(rej.Mk 16:16,) Tuna wajibu mkubwa na muhimu wa kuwaombea marehemu wetu kwa sababu katika imani yetu tunaelezwa kwamba baada ya kifo na kabla ya ufufuko kuna yanayoendelea.
Mungu anatupenda na anataka wote tufike kwake kwa njia hiyo, wale waliokufa katika hali ya dhambi ambao bado mlango wa Mbingu uko wazi kwa ajili yao wanahitaji sala na maombi yetu katika hatua yao ya kusafishwa huko toharani ili kuwa safi na kuingia mbinguni. Hili ni eneo tunalokutana na sala mbalimbali kwa ajili ya wenzetu walio tutangulia zinazo lenga kuwaombea msamaha wa dhambi zao ili kuwa safi na kuingia mbinguni ambako ndiyo lengo, dhumuni na hitimisho la safari yetu ya maisha tuliyo ya anza hapa duniani. Majonzi, simanzi na huzuni kupitiliza vitatuponza kuonesha kwamba hatuna matumaini, yoyote, bali mioyo yetu itajaa furaha na miili yetu itaimarika na kupata nguvu pale tunaposadiki katika tumaini la ufufuko kama vile Yesu Kristo alivyo fanya. Hatuna haja ya kuhangaika na kuhofu sana juu ya marehemu wetu, ikiwa tunafahamu kwamba wamekufa katika sakramenti zao ambazo waliunganika na Kristo ambaye ndiye chimbo la wote waliolala.
Kanisa linatufundisha kwamba sisi tulio hai tupo katika Kanisa la kwanza, Kanisa linalo safiri, na hawa marehemu wetu wapo katika Kanisa la pili yaani kanisa la wafu. Furaha ni kwamba Kanisa la wafu sio la mwisho kwamba, tuzike matumaini yetu kuishia hapo, hapana. Kuna Kanisa la tatu ambalo awali tulianza na tafakari ya Watakatifu na hivyo ni kanisa la Watakatifu huko mbinguni lililojaa furaha ya milele, Kanisa ambalo wafu wetu wapo katika kulielekea, na ambao wanahitaji sana msaada wetu wa sala Tuhamasishane kuwaombea ili walifikie. Raha ya Milele Uwape Eee Bwana….(3)
Tumsifu Yesu Kristo.