Tafuta

Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Imani ya kweli inasimikwa katika unyenyekevu na moyo wa shukrani, chemchemi ya toba na uponyaji wa ndani. Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Imani ya kweli inasimikwa katika unyenyekevu na moyo wa shukrani, chemchemi ya toba na uponyaji wa ndani.  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 28 ya Mwaka C wa Kanisa: Unyenyekevu na Moyo wa Shukrani

Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya 28 ya Mwaka C wa Kanisa inawaalika waamini kutafuta na kuambata ufunguo sahihi wa kuvuta neema, baraka, faraja, miujiza na uponyaji kutoka kwa Mwenyezi Mungu kuwa ni: Imani thabiti, Utii unaofumbatwa katika fadhila ya unyenyekevu na kwamba, matokeo yake ni baraka na uzima wa milele. Huu ni mwaliko wa kuwaiga Jemedari Naaman pamoja na Msamaria aliyetambua: nguvu, ukuu, utakatifu na utukufu wa Mungu.

Na Padre Joseph Herman Luwela, - Vatican.

UTANGULIZI: Karibu mpenzi msikilizaji na msomaji wa tafakari ya neno la Mungu kutoka hapa Radio Vatican leo Dominika ya 28 MWAKA C. Dominika leo tunaalikwa kutafakari juu ya neema ya uponyaji, shukrani ya kweli, na wito wa kudumu wa matumaini. Katika mwaka wa Jubilei ya Matumaini (Pilgrims of Hope), Kanisa linatualika kutembea pamoja kama wafuasi wa Kristo katika safari ya imani yenye tumaini, shukrani na huruma. Masomo ya leo yanatufundisha kwamba imani na shukrani ni milango ya neema na ukombozi, hasa tunapopita katika magumu ya maisha. Ni Oktoba yenye heri tukitafari mafumbo ya ukombozi wetu kwa kusali Rozari Takatifu, ikiwa haujasali Rozari tangu mwezi huu umeanza anza sasa… Leo Neno la Mungu linatupatia uhalisia wa changamoto za mwanadamu, hitaji la imani na matumaini katika nguvu ya Mungu na halafu kuwa watu wa “shukrani.” Somo I (2Fal 5:14-17) hili linatufundisha juu ya Naamani, jemedari wa Siria aliyekuwa na ukoma. Ingawa mwanzoni aliona maagizo ya Elisha kama ya ajabu, aliponywa alirudi na shukrani kuu, akakiri kwamba hakuna Mungu mwingine ila Mungu wa Israeli. linazungumzia Naaman Jemadari wa jeshi la Shamu alivyoponywa ukoma wake na Mungu kupitia Nabii Elisha, naye Kristo katika Injili anawaponya wakoma 10… Nyakati za Kristo watu wa aina 4 walihesabika wamekufa: masikini, vipofu, wasiozaa na wenye ukoma. Ukoma ni ugonjwa uliowatesa sana, kumtibu mkoma ilikuwa sawa na kujaribu kumfufua mtu (2Fal 5:7). Elimu ya afya haikuwa kubwa hivi hata magonjwa ya kawaida ya ngozi yalichukuliwa kama ukoma mfano fungus, upele, mapunye, madoamadoa au ukungu fulani ulioambukiza nguo na kuta za nyumba. Magonjwa kama malaria, typhoid nk hayaelezewi sababu yalikuwa bado kugundulika. Marabi/walimu waliuita ukoma “mzaliwa wa kwanza wa kifo.”

Muhimu: Imani, utii na unyenyekevu
Muhimu: Imani, utii na unyenyekevu   (@Vatican Media)

Wakoma walitengwa na jamii (Law 13:45-46), hawakunyoa wala kuchana nywele, walivalishwa kengele ili wajulikane wapitapo na walipomwona mtu asiyeumwa walitakiwa kumpigia kelele kwa mbali “sisi wakoma, usitusogelee” ndio maana leo wanamwita Yesu kwa mbali “Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu”, wengi wao walikuwa ombaomba... Katika hali hii utaona ni furaha kuu kiasi gani aliipata mtu aliyepona na kurudi tena kwenye jumuiya... Kuhani ndiye aliyesema “huyu ni mgonjwa” na mtu huyo alitoka kwenye jamii na kunyanyapaliwa kwa kuishi vinyunguni, jangwani au msituni. Akipona alijionesha tena kwa makuhani na kutoa sadaka. Sherehe ya utakaso ilichukua siku 8. Mtu aliyepona ambaye hadi wakati huo alihesabiwa kuwa mfu alitoa “kifo” hicho kwa kuchinja ndege na kumimina damu ya ndege huyo kwenye chungu cha maji safi na kujipatia uhuru kwa kumwachia ndege wa pili apae baada ya kumnyunyizia damu ya ndege wa kwanza, kisha kuhani alimnyunyizia mtu huyo damu ya ndege mara saba, kisha mgonjwa alioga, akanyoa na kusubiri siku 7 ndipo aliporuhusiwa kuingia tena kwenye jumuiya na kushiriki mambo yote ya kidini, kijamii na kifamilia, baada ya siku nane ataleta kondoo wawili na kumalizia ibada ya utakaso (Law 14:1-32). Mtume Paulo akiwa kifungoni, anamwandikia Timotheo akimkumbusha asimwache Kristo, ambaye alifufuka na ni uzao wa Daudi. Paulo anatufundisha kuhusu uvumilivu kwa ajili ya Injili, akisema: “Tukiwa waaminifu, yeye hudumu kuwa mwaminifu; kwa maana hawezi kujikana mwenyewe.”  Yesu anamsifia: “Imani yako imekuponya.” Hii ni zaidi ya uponyaji wa mwili – ni wokovu wa roho. Kwa uponyaji wa wakoma 10 tunajifunza mambo kadhaa… Mosi, wapo 10 na sio mtu mmoja.

Waamini wajenge moyo wa shukrani
Waamini wajenge moyo wa shukrani   (Vatican Media)

UFAFANUZI: Yesu anaponyesha watu kumi wenye ukoma, lakini ni mmoja tu, Msamaria, anayerudi na kumshukuru Mungu.ibiblia namba 10 inawakilisha jumuiya, hivi wakoma 10 wanasimama badala ya jumuiya nzima inayougua madhila mengi… kwa muktadha huu ukoma una maana ya hali ya dhambi, hali mbaya ya watu, kujitenga na Mungu kwa dhambi.. hakuna mwenye nafuu, sote tunamuhitaji Kristo ili atutakase. Pili, kwenye kundi hili kuna msamaria mmoja na wayahudi tisa, hawa walikuwa maadui na hawakukaa pamoja, kumbe shida zinampata yoyote na watu wanaweza kupatana wakati wa shida kuliko wakati wa raha, umoja na mapatano yetu viwe nyakati zote… Tatu, wakoma wanasali sala ya pamoja “Ee Yesu Bwana mkubwa, uturehemu!” sisi tunasali namna gani? kama hawa jamaa au kila mmoja anashughulika tu na wokovu wa roho yake?.. Nne, wanapona wakiwa “njiani”... Ukristo ni safari ndefu na ngumu, uponyaji wa kiroho ni hatua kwa hatua, tunapona polepole kwa sala, mazoezi, nidhamu na kujikania. Tano… shukrani ... aliyerudi kushukuru ni 1 tu kati ya 10, kilitokea nini? kwa nini Yesu anahoji kitendo cha wale 9? Je, hakuwatuma mwenyewe wakajioneshe kwa makuhani? huenda walipanga kujitakasa kwa makuhani na kupokelewa tena na jamii, halafu wakasalimie familia ambazo walikuwa wamezimisi kitambo, ndipo wakisindikizwa kwa nderemo na vifijo na ndugu, jamaa na rafiki zao wangekuja kwa Yesu na kumshukuru, ikibidi kumpa chochote… Tumesema namba 10 inawakilisha jumuiya.

Moyo wa imani, toba na wongofu wa ndani huvuta neema na baraka
Moyo wa imani, toba na wongofu wa ndani huvuta neema na baraka

Katika Waraka wa Kitume wa Hayati Papa Francisko, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 yanayoongozwa na kauli mbiu: "Spes non confundit" yaani "Tumaini halitahayarishi" anahimiza Kanisa kuwa, “Wahudumu wa huruma, wajumbe wa matumaini, na mashahidi wa shukrani ya kweli katika dunia iliyochoka na kukata tamaa.” Kama Naamani, tunaitwa kutambua miujiza ya Mungu katika maisha yetu na kuishi kwa shukrani. Kama Timotheo, tunapaswa kuhimili kwa matumaini ili kuwashirikisha wengine Injili. Kama Msamaria aliyerudi, tunaalikwa kuonyesha imani hai kwa maisha ya ibada, huruma na kushukuru. Hivi ni Msamaria pekee ndiye aliyempa mapema Mungu utukufu na sifa, ndiye aliyegundua haraka kwamba Ufalme wa Mungu umefika kwa njia ya Yesu Kristo wa Nazareti aliye Mshenga wa Mungu na watu, amepakwa mafuta ili kuwaponya watu na udhaifu wao wa kila aina... Wale 9 walibaki na mapokeo na mila wasione kitu zaidi ya kupona miili yao basi. Hivi ndivyo jamii ilivyo, kuna watu wanauona haraka mkono wa Mungu.. lakini wapo, labda ni wengi zaidi, wanaokawia au kutomuona Mungu kabisa katika mambo yanayowatokea kila siku.. wao wanamuona tu mtu anayewapa hela, dawa, kazi na vitu basi. Msamaria alipuuza mapokeo na kuona katika Kristo Kuhani mkuu na wa milele. Ukoma kama ugonjwa sio tishio tena leo, lakini ukoma wa kiroho bado upo na unatutafuna sana viungo. Msamaria maskini alishukuru kupona kwake. Je ndugu, ni lini ulipomshukuru Mungu kwa namna ya pekee kwa mema unayojaliwa? Hata tu kwa paji la uhai, ulinzi na usalama? tushukuru kwa kila jambo... shukuru kwa ajili ya afya yako na ya ndugu zako, shukuru kwa ajili ya wana na binti zako, mume mtulivu, mke mzuri, jirani wema, kazi na kipato chako, mahusiano mazuri, shukuru tuu… Shukrani ni utu, ni uungwana, ni ukomavu, shukrani ni ubinadamu.

Moyo wa shukrani ni mlango wa neema na ukombozi
Moyo wa shukrani ni mlango wa neema na ukombozi   (Vatican Media)

Mwito wa maisha ya kila siku, kwa familia,  jengeni utamaduni wa kushukuru, hata kwa mambo madogo. Katika jamii: Kuwa “mjumbe wa matumaini” kwa waliovunjika na kupondeka moyo moyo au waliokataliwa ni muhimu kuwasemea wanyonge na wasio weza dhidi ya mifumo kandamizi, na katika Kanisa, jitolee kuwa sehemu ya huduma za huruma: kuwatembelea wagonjwa, kusaidia maskini, na kuwafariji wanaoteseka. Ndio kusema tunahitaji utakaso tupate kuponywa ukoma wetu na kuchuchumia uhuru wa Kikristo, tuwe waungwana, wacha Mungu, tusimnyanyapae yeyote bali tutumikiane kwa mapendo. Jamii iliyo huru na ukoma ni ile isiyojali matunda ya mwili, inakumbatia matunda ya roho (Gal 5:19-23)... tustahimili yote, amesema Mt Paulo katika somo II (2Tim 2:8-13), kwa ajili ya wenzetu ili wao nao waupate wokovu ulio katika Kristo Yesu.. Ni mwezi wa Mama Maria, tusali Rozari ili Mama atuombee tuweze kupona kila mmoja kadiri ya ukoma wake ili jioni ya maisha yetu tuonekane na afya njema kwa sifa na utukufu wa Mungu. Mabadiliko ya kweli ya maisha huanzia kwa unyenyekevu na utii. Shukrani ni jibu la kiroho kwa tendo la neema; Naamani hakurudi tu na zawadi, bali alibeba imani mpya. Kama Naamani, pia sisi tunaitwa kutambua wema wa Mungu katika maisha yetu ya kila siku, hasa kwa njia ya mateso na uponyaji. umaini si hisia tupu, bali ni msimamo wa moyo unaojengwa juu ya ahadi ya Kristo. Kuwa Mkristo wa kweli ni kubeba mateso kwa matumaini kwamba tutashiriki utukufu wa Kristo. Wengi hupokea neema, lakini wachache hurudi kushukuru, Shukrani ya kweli huenda sambamba na imani. samaria alitambua kwamba muujiza wake haukuwa tu kuondoka kwa ugonjwa, bali kukutana na Mponyaji - Yesu mwenyewe. Shukrani ni jibu la imani. Tumaini ni matokeo ya imani hai. Katika Dominika hii ya 28 ya Mwaka C, tunaitwa kuwa kama yule Msamaria aliyerudi tukimshukuru Mungu si kwa maneno tu bali kwa maisha yenye ushuhuda, ukarimu, na matumaini. Katika mwaka huu wa Jubilei, tuwe mahujaji wa matumaini, tukijua kwamba: “Tukiwa waaminifu, Yeye hubaki kuwa mwaminifu.” (2Tim 2:13) Ee Bwana, tupe macho ya kuona matendo yako mema, moyo wa kushukuru kwa neema zako, na imani ya kuvumilia hadi mwisho.  Amina.

Liturujia D 28 Mwaka C
10 Oktoba 2025, 16:33