Tafuta

Ujumbe makuu unahusu umuhimu wa fadhila ya unyenyekevu ambayo kimsingi ni kanuni ya dhahabu inayomwezesha mwamini kukua na kukomaa katika fadhila ya imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani Ujumbe makuu unahusu umuhimu wa fadhila ya unyenyekevu ambayo kimsingi ni kanuni ya dhahabu inayomwezesha mwamini kukua na kukomaa katika fadhila ya imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani  (@Vatican Media)

Tafakari Dominika 30 Mwaka C wa Kanisa: Unyenyekevu na Haki ya Mungu

Ujumbeunahusu umuhimu wa fadhila ya unyenyekevu ambayo ni kanuni ya dhahabu inayomwezesha mwamini kukua na kukomaa katika fadhila ya imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani; kinyume chake ni madhara ya kiburi, kujikweza, kujikinai, kuwadharau wengine na kujiona wenye haki zaidi. Tunaaswa tutambue kuwa; “Bwana ndiye mhukumu mwenye haki wala hakijali cheo cha mtu” bali wenye moyo wa unyenyekevu huwapa kibali cha kuishi kwa furaha.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, Dominika ya 30 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe makuu unahusu umuhimu wa fadhila ya unyenyekevu ambayo kimsingi ni kanuni ya dhahabu inayomwezesha mwamini kukua na kukomaa katika fadhila ya imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani; kinyume chake ni madhara ya kiburi, kujikweza, kujikinai, kuwadharau wengine na kujiona wenye haki zaidi. Tunaaswa tutambue kuwa; “Bwana ndiye mhukumu mwenye haki wala hakijali cheo cha mtu” (YbS 35:12), bali wenye moyo wa unyenyekevu huwapa kibali cha kuishi kwa furaha. Ni katika muktadha huu Zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema hivi; “Ufurahi moyo wao wamtafutao Bwana. Mtakeni Bwana na nguvu zake, utafuteni uso wake siku zote” (Zab. 105:3-4). Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anatuombea akisali hivi; “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuzidishie imani, matumaini na mapendo. Utuwezeshe kupenda unayoamuru, tustahili kupata na hayo unayoahidi.” Somo la kwanza ni la kutoka katika Kitabu cha Yoshua bin Sira (YbS 35:12-14, 16-19). Ni katekesi kuhusu ubora na nguvu ya sala ya mtu wa haki na mnyenyekevu, kuwa hupenya mawingu na kufika katika makao ya Mungu, na kusikilizwa. Lakini sala ya mwenye kiburi, na sadaka za wadhalimu, wanyonyaji, walafi, wezi, na wanyang’anyi wa maskini na wanyonge, hazifiki kwa Mungu wala haziwezi kusikika mbele zake. Kwa maana Yeye ni mwenye haki, mtetezi wa yatima, wajane, wanyonge na maskini. Hivyo daima anasikiliza sala zao waliodhulumiwa, hayadharau kamwe malalamiko yao, bali huzipokea, sala na dua zao, na zikifika mbele zake haziondoki hata atakapoziangalia, akaamua kwa adili, na kutekeleza hukumu yake. Mungu mwenyewe anatutahadharisha akisema hivi; “Usimdhulumu mjane wala yatima. Kama ukifanya hivyo nao wakinililia, hakika nitasikia kilio chao. Hasira yangu itawaka, nami nitakuua kwa upanga…” (Kut. 22:22-24).

Unyenyekevu katika maisha ya sala ni muhimu sana
Unyenyekevu katika maisha ya sala ni muhimu sana   (@Vatican Media)

Kwa kuwa Mungu hapokei sala za kinafiki na sadaka za uovu. Basi tujitahidi kumtolea sadaka safi tunayoipata kihalali kwa neema zake, ili sala zetu zipate kibali machoni pake, Yeye atatukuzwa nazo, nasi tutakatifuzwa. Ni katika muktadha huu zaburi ya wimbo wa katikati inasema; Maskini huyu aliita Bwana akasikia. Nitamhimidi Bwana kila wakati, sifa zake zi kinywani mwangu daima. Katika Bwana nafsi yangu itajisifu, wanyenyekevu wasikie wakafurahi. Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, ili aliondoe kumbukumbu lao duniani. Walilia, naye Bwana akasikia, akawaponya na taabu zao zote. Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, na waliopondeka roho huwaokoa. Bwana huzikomboa nafsi za watumishi wake, wala hawatahukumiwa wote wamkimbiliao” (Zab. 34:6, 1-2, 16-18, 22).Somo la pili ni kutoka katika Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Timotheo (2Tim 4:6-8, 16-18). Ni mawaidha yake ya mwisho mwisho ya namna mkristo anavyopaswa kuishi. Mtume Paulo, mzee, mfungwa gerezani, anatoa ushuhuda wake alivyoishi wakati uliopita, anavyoishi wakati uliopo na atakavyokuwa wakati ujao. Kuhusu wakati uliopita anaelezea namna alivyofanya utume katika mazingira mbali mbali, akitumia lugha ya kivita anasema; “nimevipiga vita vilivyo vizuri”, akitumia lugha ya mashindano ya riadha anasema; “mwendo nimeumaliza”, na katika uaminifu anasema; “Imani nimeilinda.” Kuhusu maisha yake ya wakati uliopo, anasema yuko karibu “kumiminwa”, kutolewa sadaka, kuuwawa, kufa kwa ajili ya Injili, na hana wasi wasi wala woga, kwa maana ameweka tumaini lake lote kwa Mungu hakimu mwenye haki, naye atamwokoa na kila baya, na kumhifadhi. Na kuhusu wakati ujao yuko tayari kupokea “taji ya haki”, uzima wa milele mbinguni. Naye akitambua madhaifu ya wengine, na ukuu wa huruma na upendo wa Mungu, aliwaombea msamaha walioiongopea imani, kwa hofu, woga, na mashaka, kuwa wasihesabiwe hatia. Naye aliweza kufanya aliyoyafanya kwa kuwa alimtumaini Kristo Yesu, naye akawa pamoja naye akimtia nguvu. Nasi tusikate tamaa na kuikana imani yetu, tuweke tumaini letu lote kwa Kristo, ili awe pamoja nasi, Yeye ambaye utukufu una Yeye milele na milele. Amina.

Waamini washinde hofu na kujikabidhi mikononi mwa Mungu
Waamini washinde hofu na kujikabidhi mikononi mwa Mungu   (@Vatican Media)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk 18: 9-14). Fundisho lake kuu ni umuhimu wa unyenyekevu na madhara ya kiburi, kujikinai, na kuwadharau wengine; kwa maana mbele za Mungu hakuna aliye bora kuliko mwingine, na uzima wa milele ni zawadi ya Mungu kwetu, hakuna anayeweza kujistahilisha mwenyewe kwa nguvu zake. Fundisho hili Yesu analitoa kwa mfano wa watu wawili walioenda Hekaluni kusali; Farisayo na mtoza ushuru, na kila mmoja alisali kwa namna yake, kulingana na mtazamo wake aliokuwa nao kuhusu Mungu na namna anavyojiona yeye mwenyewe ndani mwake na mbele za Mungu. Hivyo sala ya mtu, inamfunua jinsi alivyo yeye na namna anavyojiona na kuwaona wengine. Sala ya Farisayo, mshika sheria, ni sala ya majivuno, kiburi na kujisifu. Akiwa amesimama, alijisemea mwenyewe; “Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, walevi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma na natoa zaka katika mapato yangu yote” (Lk 18:11-12). Farisayo alijiona ni mkamilifu, yote yanategemea nguvu na uweza wake, tena hakufurahia uwepo wa mtoza ushuru, mtu mwenye dhambi hekaluni. Huku ni kujikinai na kujiona mwenye haki mbele za Mungu. Ni katika muktadha huu, Yesu alikemea tabia hii ya ufarisayo: ole wenu mafarisayo, kwa kuwa mnatoa zaka za mnanaa na mchicha wa kila mboga, lakini mmeacha mambo makuu ya sheria; adili, rehema, imani, na upendo wa Mungu, mliyopaswa kuyafanya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili (rej. Lk 11:42; Mt 23:23).

Amani na utulivu wa ndani ni muhimu sana katika sala
Amani na utulivu wa ndani ni muhimu sana katika sala   (@Vatican Media)

Lakini sala ya Mtoza ushuru, mtu aliyejulikana kuwa ni mdhambi, aliyedharauliwa na kutengwa na jamii kwa kazi aliyofanya, kukusanya kodi kwa utawala wa Kirumi, ni sala ya kuomba msamaha. Hivyo alijiachia mbele ya Mungu kama alivyo na makosa yake, akiomba huruma na msamaha, amejawa na hofu ya Mungu kiasi kwamba hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipigapiga kifuani mwake akisema: “Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi” (Lk 18:13). Hii ni sala ya toba, ni kuzionea aibu dhambi, na kuziungama. Naye “alishuka kwenda nyumbani kwake amehesabiwa haki kuliko farisayo kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliywe atakwezwa” (Lk.18:14). Tunajifunza nini katika sala ya Farisayo na Mtoza ushuru? Kwanza, tusiwe wanafiki; “Tena mfungapo msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao ili waonekane na watu kuwa wamefunga. Amini nawaambia wamekwisha kupata thawabu zao” (Mt 6:16). Pili, tusiwahukumu, wala kuwadharau wengine kama farisayo kwa mtoza ushuru. Hii ni dhambi mbaya sana. Daima tukumbuke kuwa Yesu alikufa Msalabani kwa ajili ya ukombozi wa wote. Matunda ya dhambi zetu ni kuteswa kwake hata kufa Msalabani. Kila binadamu ni mdhambi kwa kiwango chake, hivyo hakuna mwenye haki ya kumuwekea Mungu mipaka katika kutoa neema na baraka zake. Tatu, huruma ya Mungu ni zawadi, hatuwezi kuinunua wala kuidai, tunaistahilishwa na kuipewa kwa kujinyenyekesha na kukiri ukosefu wetu waziwazi mbele za Mungu. Kwenye Sakramenti ya Kitubio, tunapoomba msamaha, hatupaswi kusimulia mema tuliyofanya, wala kusema dhambi na makosa ya watu wengine, huo ni ufarisayo. Bali tunapaswa kutaja dhambi zetu tu, tena zote tunazozikumbuka.

Tumaini la wenye haki liko mikononi mwa Bwana
Tumaini la wenye haki liko mikononi mwa Bwana   (@Vatican Media)

Kutokutaja dhambi unazozikumbuka kwa sababu ya aibu, na kuziweka kwenye kundi la zilizosahaulika, ni kufuru ya Sakramenti, na hivyo mtu hapokei msamaha wa dhambi zake. Tukumbuke kuwa Mungu ajua yote, hadanganywi wala hadanganyiki. Hivyo, tuziungame dhambi zote bila aibu, tukitambua kuwa hakuna dhambi kubwa mbele ya Mungu ambayo atashindwa kuisamehe, na hakuna dhambi ndogo mbele ya Mungu ambayo hataichukulia maanani. Basi tunaposali tuepuke vizingiti vinavyoweza kubatilisha sala zetu. Tuishinde hofu, tujiachie mikononi mwa Kristo, ili yeye atutendee kadiri apendavyo, yote ikiwa ni kwa sifa na utukufu wa Mungu ili kwao sisi tutakatifunze. Ni katika tumaini hili mama kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba upokee dhabihu tunazokutolea wewe mtukufu, ili ibada tunayofanya iwe hasa kwa ajili ya utukufu wako”. Ni katika kufanya hivyo tunabaki na muunganiko na Mungu, na mda ukifika wa “kumiminwa”, tutaweza kusema kama Mtume Paulo: “Nimevipiga vita vilivyo vizuri, imani nimeilinda, sasa nasubiri taji ya uzima wa milele mbinguni”. Kwa nguvu zetu hatuwezi. Ndiyo maana mama Kanisa katika sala baada ya Komunyo anatuombea akisali hivi: “Ee Bwana, tunaomba neema ya sakramenti zako zitukamilishe, ili hayo tupokeayo katika maumbo, tufahamu ukweli wake”. Basi tumaini la Mtume Paulo alilosema: “Bwana ataniokoa na kila neno baya, na kunihifadhi hata nifike ufalme wake wa mbinguni. Utukufu una Yeye hata milele na milele. Amina” (2Tim 4:18), liwe ni tumaini letu pia. Tumsifu Yesu Kristo!

Dominika 30 Mwaka C wa Kanisa
21 Oktoba 2025, 15:49