Tafuta

Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 29 ya Mwaka C wa Kanisa: Ujumbe mkuu unahusu umuhimu wa kusali bila kuchoka, na tukifanya hivyo kwa imani Mungu atatusikiliza na kutujalia tunayohitaji. Liturujia ya Neno la Mungu Dominika ya 29 ya Mwaka C wa Kanisa: Ujumbe mkuu unahusu umuhimu wa kusali bila kuchoka, na tukifanya hivyo kwa imani Mungu atatusikiliza na kutujalia tunayohitaji.   (@Vatican Media)

Tafakari Neno la Mungu Dominika 29 Mwaka C: Udumifu Katika Sala

Ujumbe ynahusu umuhimu wa kusali bila kuchoka, na tukifanya hivyo kwa imani Mungu atatusikiliza na kutujalia tunayohitaji. Maadhimisho ya Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni katia Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, ujumbe mkuu ni matumaini hayati Papa Francisko alichagua kauli mbiu: "Wamisionari wa Matumaini kwa Watu Wote." Waamini wote wanakumbushwa juu ya wito wetu wa msingi wa kuwa, katika nyayo za Kristo na wajumbe wa matumaini.

Na Padre Paschal Ighondo, - Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya 29 ya mwaka C wa kiliturujia katika Kanisa, kipindi cha kawaida. Ujumbe mkuu unahusu umuhimu wa kusali bila kuchoka, na tukifanya hivyo kwa imani Mungu atatusikiliza na kutujalia tunayohitaji. Maadhimisho ya Dominika ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni katika Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, ujumbe mkuu ni matumaini (taz. Bull Spes Non Confundit, 1), hayati Baba Mtakatifu Francisko alichagua kauli mbiu: "Wamisionari wa Matumaini kwa Watu Wote". Lengo la Kauli Mbiu hii ni kutukumbusha sote juu ya wito wetu wa msingi wa kuwa, katika nyayo za Kristo, wajumbe na wajenzi wa matumaini. Tukiongozwa na Roho wa Mungu na kwa bidii takatifu, tunaalikwa kuwa washiriki katika msimu mpya wa uinjilishaji katika Kanisa ili kuvishinda vivuli vya giza ulimwenguni (taz. Fratelli Tutti, 9-55). Liturujia ya Neno la Mungu, inatoa mwelekeo wa pekee kwa waamini kutafakari maana ya sala na udumifu katika maisha ya sala, kama sehemu ya ujenzi wa mahusiano na majadiliano kati ya mwamini na Muumba wake. Mababa wa Kanisa wanasema, Sala ni majadiliano kati ya mwamini na Mungu, kielelezo cha juu kabisa cha mafao katika maisha ya mwanadamu. Ni nuru katika moyo wa mwanadamu, inayomwonjesha mwamini ile furaha ya uzima wa milele. Kusali ni silele mama ni jambo linalohitaji majiundo makini, ubunifu na utamaduni wa kusali daima na kamwe kusali kusiwe ni sehemu ya mazoea kwani mwelekeo kama huu unaweza kupotosha maana na umuhimu wa sala katika hija ya maisha ya mwamini hapa ulimwenguni. Kristo Yesu kwa kutambua ugumu wa sala, alijitaabisha kuwafundisha wanafunzi wake namna ya kusali vyema na akawakabidhi kwa namna ya pekee, ile Sala kuu, muhtasari wa Injili na mafundisho makuu ya Kristo, yaani sala ya Baba Yetu.

Udumifu wa sala katika maisha
Udumifu wa sala katika maisha   (@Vatican Media)

Ni katika muktahda huu zaburi ya wimbo wa mwanzo inasema: “Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika, utege sikio lako ulisikie neno langu. Ee Bwana, unilinde kama mboni ya jicho, unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako” (Zab. 17:6, 8).  Lakini ili sala zetu zipate kibali mbele za Mungu, tunapaswa kuyafanya mapenzi yake kwanza. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali: “Ee Mungu Mwenyezi wa milele, utuwezeshe kufuata daima mapenzi yako matakatifu, na kuitumikia fahari yako kwa moyo mnyofu.” Kwa kufanya hivi njia ya kwenda mbinguni, itakuwa wazi kwetu na tutastahilishwa kuurithi uzima wa milele. Somo la kwanza ni la Kitabu cha Kutoka (Kut 17:8-13). Mhusika mkuu ni Musa akisali sala ya maombezi, kuomba msaada wa Mungu, kwa ajili ya taifa lake liweze kushinda vita dhidi ya Waameleki, uzao wa Esau kaka ya Yakobo, Israeli (Kumb 25:17-19). Sala ya Musa ni sala ya mwenye imani, isiyo na mawaa, sala ya mtu mwenye mikono safi, ndiyo maana kila alipoiinua, Isareli ilishinda, alipoishusha kwa uchovu, Isaraeli ilishindwa. Hivyo ikabidi Haruni na Huri waitegemeze mikono yake kwa mawe, ndipo Musa alipodumu katika kuomba, akiwa ameinua mikono yake, hata jua lilipokuchwa Israeli akashinda vita dhili ya Waameleki. Katika maisha ya kiroho, sala ni silaha ya maangamizi dhidi ya adui shetani. Na kwa maisha ya kawaida, mafanikio yanategemea kufanya kazi kwa juhudi na maarifa, na kufuata maongozi ya Mungu kwa njia sala. Ni katika tumaini hili zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Nitayainua macho yangu niitazame milima; msaada wangu utatoka wapi? Msaada wangu u katika Bwana, aliyezifanya mbingu na nchi. Asiuache mguu wako usogezwe, Yeye akulindaye asisinzie. Naam, hatasinzia wala hatalala usingizi, Yeye aliye mlinzi wa Israeli. Bwana ndiye mlinzi wako; Bwana ni uvuli, husimama mkono wako wa kuume, Jua halitakupiga mchana, wala mwezi wakati wa usiku. Bwana atakulinda na mabaya yote, atailinda nafsi yako. Bwana atakulinda utokapo na uingiapo, tangu sasa na hata milele” (Zab. 121:2, 7-8).

Dominika 29 Mwaka C: Umuhimu wa Sala katika maisha
Dominika 29 Mwaka C: Umuhimu wa Sala katika maisha   (@Vatican Media)

Somo la Pili ni kutoka katika Waraka wa Pili wa Mtume Paulo kwa Timoteo (2Tim 3:14-4:2). Ni wosia na mawaidha ya namna anavyopaswa kuishi mkristo, kujiandaa kikamilifu na kuwa tayari kutenda kila tendo jema wakati wote, na kuzishika kweli za imani zinazofundishwa na Neno la Mungu, ili kwazo apate kuhekimishwa na kupata wokovu kwa njia ya Yesu Kristo. Na ili kufanikiwa katika maisha, ni muhimu na la lazima kulitilia maanani Neno la Mungu. Ni katika muktadha huu Kuhani lazima alitangaze, alihubiri na kulifundisha Neno la Mungu kwa watu, alitumie kwa kukaripia, kukemea, na kuonya. Na Mkristo, ili aweze kukomaa na kukua katika imani, anapaswa kujishikamanisha kwa kulisoma na kuliishi Neno la Mungu. Neno hili lazima litumike katika liturujia kwani ni chanzo cha sala za maombi, shukrani na sifa kwa Mungu, kwa sababu lina “nguvu ya Roho Mtakatifu”, “Pumzi ya Mungu”, ndiyo maana linafaa kwa kuwafundisha, kuwaonya, kuwaongoza, na kuwaadibisha watu kwa haki. Nasi tujibidishe kulisoma, kulitafakari na kuliishi Neno la Mungu, ili lituongoze katika maisha ya hapa duniani, tukiwa katika safari ya kuelekea kwenye uzima wa milele mbinguni.

Jifunzeni kusali na kudumu katika sala
Jifunzeni kusali na kudumu katika sala   (ANSA)

Injili ni kama ilivyoandikwa na Luka (Lk 18:1-8). Ni fundisho la Yesu kuhusu umuhimu wa kusali bila kuchoka wala kukata tamaa. Katika kufikisha fundisho hili, Yesu anasimulia kisa chenye wahusika wawili; mama mjane na kadhi dhalimu. Ili kulielewa vyema fundisho hili ni vizuri kuwafahamu wahusika hawa, wasifu wao na hadhi zao katika kijamii. Kwanza kabisa, ni Kadhi, mtu mwenye madaraka ya kuamua kesi kisheria, mwamuzi katika migogoro. Mhusika huyu katika simulizi hili ana sifa mbaya mbili: Hamchi Mungu na hajali watu. Na kwa kuwa hamchi Mungu, hafuati sheria, hivyo anafanya maamuzi kwa vipimo vyake. Katika mazingira haya hawezi kutenda haki inavyompasa. Hali hii inajidhihirisha kwa namna alivyolichukulia ombi la mama mjane, kwa muda mrefu hakutaka kumpa haki yake. Mhusika wa pili ni mama mjane, mwanamke aliyefiwa na mume wake. Katika Agano la Kale ili kuwatambua, wajane walivaa nguo maalumu ili kuwatofautisha na makahaba na wanamke wasio wajane. Kisa cha Yuda na Tamari kinaweka wazi suala hili; “Tamari alipoambiwa, Baba mkwe wako yuko njiani kwenda Timna kukata kondoo wake manyoya, alivua mavazi yake ya ujane, akajifunika kwa shela ili asifahamike, akaketi kwenye mlango wa Enaimu, ambao upo njiani kuelekea Timna…Yuda alipomwona, alifikiri ni kahaba...Pasipo kutambua kuwa ni mkwe wake akamwendea…na kumwambia; “Njoo sasa, nikutane na wewe kimwili” (Mwa 38:13-16). Kutokana na mazingira magumu waliyokuwa nayo, ziliwekwa sheria za kuwalinda wao, watoto wao na mali zao. Na laana ilitangazwa kwa wale ambao hawakuwafanyia haki. Tunasoma hivi; “Na alaaniwe apotoshaye hukumu ya mgeni na yatima na mjane aliyefiwa na mume wake, na watu wote waseme, Amina” (Kumb 27:19).

Jifunzeni kusali vyema
Jifunzeni kusali vyema   (@Vatican Media)

Mjane anayesimuliwa katika Injili alikuwa na shida, alinyimwa haki yake, naye anataka apewe. Naye kwa mda mrefu hakuipewa, pengine kutoka na mazingira ya rushwa. Lakini yeye ana silaha moja tu, kumwendea Kadhi tena na tena, kiasi bila kuchoka wala kukata tamaa, kumuomba haki yake. Kitendo hili kilimuudhi, Kadhi hata akaamua kumpa haki yake akisema: “kwa kuwa mjane huyu ananiudhi, nitampatia haki yake, asije akanichosha kwa kunijia daima” (Lk 18:4b-5). Kwa kutumia mfano huu Yesu anatuuliza kama Kadhi dhalimu anaweza kumpa mjane haki yake, Je, Mungu Baba yetu aliye mwema, hatafanya zaidi? Ni katika muktadha huu anatusihi na kutuasa kusali daima bila kuchoka wala kukata tamaa. Basi tuwe watu wa sala, tusali katika kila jambo tunalotaka kufanya kuomba maongozi ya Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu, tukiiga mfano wake Yeye ambaye daima alisali katika matukio muhimu katika maisha yake hapa duninia; Kabla ya kubatizwa (Lk 3:21), kabla ya kuwateua Mitume wake 12 (Lk 6:12), kabla ya kugeuka sura (Lk 9:27-28), kabla ya kukamatwa na kuteswa (Lk 22:42; Mt 26:39-42), na kabla ya kukata roho na kufa msalabani (Mt 27:46).

Jengeni utamaduni wa kusali katika jumuiya, Familia na kama mtu binafsi
Jengeni utamaduni wa kusali katika jumuiya, Familia na kama mtu binafsi   (@Vatican Media)

Tukumbuke daima kuwa sala ni kama mafuta yanayoifanya taa ya imani yetu ibaki imewaka daima. Tukipuuzia sala, imani yetu itafifia na kuweza kuzimika, na kupotea kabisa. Tutenge muda wa kusali katika familia zetu, tushiriki Sadaka ya Misa Takatifu Dominika, na sala katika jumuiya zetu ndogo ndogo za kikristo. Na tunaposali, tuwe wavumilivu, wenye subira, maana Mungu hafungwi na muda, hivyo atatupatia anachoona kinatufaa kwa muda mwafaka. Lakini tutambue kuwa sala ya mtu mchafu, mtu mwenye dhambi, ni kelele mbele za Mungu, haisikilizwi wala kujibiwa. Hivyo kabla ya kupeleka maombi yetu mbele za Mungu, tujiandae kwanza kwa kujipatanisha sisi kwa sisi na kujipatanisha na Mungu. Hatua za kufuata na namna tunavyopaswa kusali: Kwanza, jipatanishe kwa njia ya Sakramenti ya Kitubio, ili sala zako zipate kibali mbele za Mungu. Huu ni mwongozo na agizo la Yesu mwenyewe; “Basi ukileta sadaka madhabahuni, na ukakumbuka kwamba ndugu yako ana neno juu yako, iache sadaka yako mbele ya madhabahu, nenda ukapatane naye kwanza, kisha urudi ukatoe sadaka yako” (Mt 5:23-24). Tusisali kama wanafiki: “Nanyi msalipo, msiwe kama wanafiki, maana wao hupenda kusali wakiwa wamesimama katika masinagogi na kando ya barabara ili waonekane na watu”. Tena, “mnaposali msiseme maneno kama wafanyavyo watu wasiomjua Mungu. Kwa maana wao hudhani kwamba watasikiwa kwa sababu ya wingi wa maneno yao. Msiwe kama wao…” Basi, “wewe unaposali, ingia katika chumba chako cha ndani, funga mlango na umwombe Baba yako aliye sirini. Naye Baba yako aonaye sirini atakupa thawabu yako”. (Mt 6:5-8.)

Udumifu katika sala ni jambo muhimu sana
Udumifu katika sala ni jambo muhimu sana   (@Vatican Media)

Tusali kwa imani, kwa saburi na bila kuchoka: “Ni nani mwenye rafiki akimwendea usiku wa manane na kumwambia, ‘rafiki yangu nikopeshe mikate mitatu, kwa sababu rafiki yangu amefika kwangu kutoka safarini nami sina cha kuweka mbele zake…kwa vile asivyoacha kuomba, ataondoka na kumpa kadiri ya mahitaji yake” (Lk 11: 5-8). Tusali kwa unyofu na unyenyekevu kama mtoza ushuru aliyesali akisema: “Ee, Mungu uniwie radhi mimi mwenye dhambi” (Lk 18:9-14). Daima tumshirikishe Roho Mtakatifu, “Roho wa kweli”, kwa kupitia kwa Kristo na kuwa ndani ya Kristo (KKK 2615). Ni katika tumaini hili mama kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba utuwezeshe kukutumikia kwa uhuru kwa vipaji vyako. Ututakase kwa neema yako na kwa sadaka hii tunayokutolea”. Na katika sala baada ya komunyo anapohitimisha maadhimisho haya anasali; “Ee Bwana, utuwezeshe kupata maendeleo ya roho tunaposhiriki mara nyingi mambo haya matakatifu. Tujaliwe riziki za hapa duniani na hekima katika mambo ya mbinguni”. Na hili ndilo tumaini letu katika maisha yetu ya sala. Tumsifu Yesu Kristo.

Dominika 29 Mwaka C wa Kanisa
18 Oktoba 2025, 10:32