Uumbaji na Mazingira:Uhusiano mzuri kati ya mwanadamu na uumbaji
Na Pd.Bona Maro,C.pp.S na Sr. Grace Theresa Hashim Paul - Tanzania.
Tushirikishane Tone la Upendo. Karibu mpenzi katika Makala hii maalum ambao tumekuandalia mada ihusuyo “Uumbaji na Mazingira.” Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake. Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu(Mwanzo 1:26) na akakabidhiwa vitu vyote vilivyoumbwa na Mungu ili avitawale na kuvitunza. Hii ni kwa sababu ya nafasi ya pekee kabisa aliyo nayo mwanadamu katika uumbaji wa Mwenyezi Mungu kama tunavyosoma katika Zaburi ya 8:15 kwamba, “Mtu ni ni kitu gani hata umkumbuke, na binadamu hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko Malaika, umemvika taji ya utukufu na heshima.
Uhusiano kati ya Mwanadamu na Mazingira, msingi wake katika maandiko matakatifu
Mwanadamu ameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu(imago dei). Tunasoma katika kitabu cha Mwanzo 1:26-28. Mwenyezi Mungu alimpa mamlaka ya kuvitawala viumbe vyote katika uumbaji wake. Lakini mamlaka haya ya kuvitawala viumbe vyote yaani Radah kwa lugha ya kiebrania au dominion kwa lugha ya kiingereza yapaswa kueleweka vyema katika maandiko matakatifu. Kutawala haina maana ya kutumia vibaya na kuharibu. Kutawala si kumiliki bali ni kwa maana ya kutunza, kama wakili tu kwa uaminifu na uwajibikaji kwa niaba ya Mungu ambaye kimsingi ndiye aliye chanzo cha vitu vyote alivyo navyo mwanadamu. Neno hili la kiebrania radah lina maana pia ya kuchunga au kutunza, kazi ambayo kimsingi ni ya mchungaji. Kumbe tumepewa mazingira tuyatunze, tuyachunge. Mwenyezi Mungu mara baada ya kumwumba mwanadamu, alimweka katika bustani ya Edeni ili ailime(abad) na kuitunza(shamar), tunasoma katika kitabu cha Mwanzo 2:15. Hakuwekwa tu katika bustani ili atumie vilivyokuwepo na kuviharibu bali avitunze na kuviendeleza. Hapa tunakutana na maneno haya mawili muhimu sana kutoka katika lugha ya kiebrania, abad na shamar.
Neno abad hapa limetumika kumaanisha kulima, lakini pia neno hili lamaanisha kuhudumu. Neno la pili ni shamar likiwa na maana ya kulinda na kutunza. Kumbe Adamu hapa alipewa wajibu wa kulima, kuhudumia, kutunza na kulinda uumbaji wa Mwenyezi Mungu. Kumbe kila mwanadamu kimsingi tangu Mwanzo ana wajibu huu mkubwa kama mtunzaji na mlindaji wa uumbaji wa Mungu katika nyanja zote. Kumbe mwanadamu ni sehemu na muhimu sana katika uumbaji. Mwenyezi Mungu alimfanya mtu kutoka katika mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai, mtu akawa nafsi hai(Mwanzo 2:7). Kumbe sisi ni viumbe wa kidunia na kiroho. Hadhi yetu na asili yetu chanzo chake ni Mungu, na wito wake umefungamanishwa na wajibu wa kulinda, kutunza, kuthamini, kuhudumia na kuendeleza mazingira yake. Kumbe mwanadamu hana mamlaka na haki ya kuyaharibu mazingira kwa kuyatumia vibaya vile atakavyo. Anapaswa kutumia njia bora na rafiki kwa uwajibikaji na uwakili, katika kuhusiana kwake yeye vyema na mazingira yake.
Kosa la wazazi wetu wa kwanza na kuvunjika kwa mahusiano mema katika uumbaji
Mahusiano ya mwanadamu na viumbe vingine vyote kabla ya anguko la wazazi wetu wa kwanza yalikua ni mema. Hakukuwa na uadui kati ya mwanadamu na uumbaji wa Mungu. Kulikua na amani na mahusiano mema. Anguko la wazazi wetu wa kwanza, (Mw 3:1-24) liliharibu mahusiano haya mema ambayo yalikuwapo tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Matokeo ya kosa la wazazi wetu wa kwanza yakapelekea uadui, kati ya mwanadamu na uumbaji. Ardhi ambayo mwanadamu alikabidhiwa ili ailinde na kuihudumia ikalaaniwa. Mwenyezi Mungu alimwambia Adamu: “Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti iambao nalikuagiza nikisema usiyale, ardhi imelaaniwa kwa ajili yako, kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako”(Mw 3:17). Ardhi iliyobarikiwa na Mungu ili izae na kuwapatia Chakula, sasa imelaaniwa na kwamba itazaa michongoma na miiba.
Dhambi ya wazazi wetu wa kwanza
Uhusiano mzuri kati ya mwanadamu na uumbaji, unahama kutoka mwanadamu kama mtawala na mtunzaji, mlindaji, mlimaji na mchungaji na kuwa vita ya kogombania rasilimali hizi za Mungu. Kumbe dhambi ya wazazi wetu wa kwanza ilivuruga kabisa muafaka wa asili ambao aliuweka Mwenyezi Mungu tangu Mwanzo. Iliharibu mahusiano kwanza kabisa na Mungu, kwa kuondolewa katika bustani aliyowapa Mungu ili waitunze, pili mahusiano kati yao wao kwa wao, hakuna tena undugu, tutaona baadaye Kaini anamwua ndugu yake Abeli akidai kuwa yeye sio mlinzi wa ndugu yake, na kisha uhusiano kati ya mwanadamu na mazingira ukaharibika, hakuna undugu tena, ukaingia uadui kati ya mwanadamu na viumbe vingine alivyoumba Mungu, tabu na mateso na kisha kifo vikaingia katika historia ya mwanadamu na uumbaji ambao Mungu aliuumba katika wema na uzuri wake wote.
Mpango wa Mungu wa ukombozi na uumbaji mpya kwa njia ya Kristo
Baada ya kosa la wazazi wetu wa kwanza, Mwenyezi Mungu hakumwacha mwanadamu katika dhambi na mauti. Anaanzisha tena mpango wa ukombozi ambao ulikamilishwa kwa sadaka ya Kristo, yaani mateso, kifo na ufufuko wake wakati utimilifu wa nyakati ulipowadia. Mpango wa ukombozi ulikua ni kupatanisha tena vitu vyote na Mungu. Neno wa Mungu ambaye alikuwapo tangu kuumbwa kwa ulimwengu, anatwaa mwili, anaingia tena katika ulimwengu, anatwaa udhaifu wetu na anaupatanisha tena ulimwengu wote na Baba wa milele, kama anavyotufundisha Mtume Paulo katika waraka wake kwa Wakolosai 1:16-20 kwamba; “Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo duniani na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana….na kwa yeye alivipatanisha vitu vyote na nafsi yake akiisha kufanya amani kwa damu yake msalabani, kwa yeye ni vitu vilivyo juu ya nchi au vilivyo mbinguni…” Wito wetu sisi sote kama wana wa Mungu kwa njia ya Kristo ni kuendeleza upatanisho kati yetu na uumbaji wote wa Mungu. Kulinda mazingira ni wajibu na utume wetu siku zote. Kwa kufanya hivyo tunafanya ulimwengu kuendelea kuwa sehemu salama ya kuishi kama vile alivyopanga Mungu tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Tunashiriki na kuendeleza kazi ya Mungu ya uumbaji na ukombozi.
Wajibu wetu sisi katika uumbaji wa Mungu, katika Mazingira yetu
Mwenyezi Mungu kama alivyompa Adamu wajibu na mamlaka juu ya uumbaji na viumbe vyote, sisi nasi kila mmoja wetu ana wajibu huo huo wa kuendeleza, kutunza, kuulinda na kuuthamini uumbaji wa Mungu kama mawakili tu kwa niaba ya Mungu ambaye dunia na vyote vilivyomo ni mali yake (Zaburi ya 24:1). Je, kama wakili wa Mungu, niliyeumbwa kwa sura na mfano wake, wajibu wangu ninautekeleza namna gani katika kuhakikisha dunia inakua mahali salama pa kuishi? Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? Ndugu yetu wa kwanza ni mazingira yetu ambayo bila hayo kimsingi hakuna uhai. Je, ninayalinda mazingira kwa kutokua chanzo cha uharibifu wa ulimwengu mzuri namna hii aliouumba Mungu? Ninalinda na kuthamini zawadi ya uhai na maisha? Tunaishi katika ulimwengu uliogubikwa na wimbi kubwa la uharibifu katika nyanja mbalimbali. Ulinzi unaanza na mimi na wewe.
Mwenyezi Mungu anatualika pia kutumia baraka za uumbaji wake katika kuwasaidia walio wadogo. Kujitahidi kuona na kuguswa na matatizo mbalimbali yatokanayo na madhara ya uharibifu wa uumbaji wa Mungu na kuyatafutia majibu sahihi kulingana na alama za nyakati. Wapo watu wengi wanaoteseka kwa sababu ya athari za mabadiliko ya tabia ya nchi, njaa, majanga ya asili kama vile mafuriko, ukame, matetemeko ya ardhi, magonjwa mbalimbali yatokanayo na uharibifu wa mazingira, nk. Tunyooshe mikono yetu, tuyaponye mazingira yetu.
Mtakatifu Francis wa Assisi na Mazingira: Wimbo wa Sifa kwa viumbe
Katika kumbukizi ya Mtakatifu Francis wa Assisi pia tunatambua na kuthamini mchango wake mkubwa kama mmoja wa Watakatifu waliothamini na kutunza kwa namna ya pekee zawadi ya uumbaji wa Mungu. Mtakatifu Francis wa Assisi mnamo mwaka 1224 hadi 1225 ambapo mwishoni kabisa mwa maisha yake aliandika Wimbo maarufu sana uliojulikana kama Laudato Sì, yaani, “Sifa kwa Bwana” Mtakatifu Francis wa Assisi alikuwa ni mtu wa sala na upendo mkubwa sana kwa Mungu. Hivyo aliona dunia na viumbe vyote kama kaka na dada kutoka kwa Baba mmoja wa Mbinguni. Aliita Ndugu Jua, Dada mwezi na nyota, ndugu upepo na hewa, dada maji, ndugu moto, dada dunia. Pia alitaja Dada ‘kifo,’akionesha kuwa hata kifo ni sehemu ya mpango wa Mungu. Wimbo huu umekuja kuwa Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Fransisko, uliochapishwa rasmi mnamo tarehe 24 June 2015. Ni hati rasmi ya Kanisa Katoliki inayoshughulikia hasa mada kubwa ya mazingira na utunzani wa nyumba yetu ya pamoja.
Sasa tumeujua mchango wake katika utunzaji wa Mazingira, hebu sasa tuone maana tano zilizoutajirisha Wimbo huu wa Mtakatifu Francis...Maana ya Wimbo wa Mtakatifu Francis wa Assisi, kwanza kabisa Uhusiano wa pekee kama familia moja wa viumbe yote na mazingira. Lengo la Wimbo huu maarufu wa Mtakatifu Fransisko wa Asizi ni kuonesha uhusiano wa karibu na wa pekee kabisa uliopo kati viumbe vyote vya Mungu. Kwa mtakatifu Fransisko wa Asizi, viumbe vyote havikua mali ya mwanadamu pekee, bali ni familia moja ya Mungu. Aliamini kuwa binadamu hawako juu ya viumbe ili wavitumie vibaya, bali wako katika mshikamano wa pamoja na viumbe vyote. Hii kimsingi ndio maana ya wajibu ule aliopewa mwanadamu na Mungu alipokabidhiwa bustani ya Edeni ili ailime na kuitunza.
Pili: Sifa kwa Mungu muumba wa vitu vyote. Kila kiumbe kilimkumbusha Mtakatifu Fransisko juu ya ukuu wa Mungu. Aliamini kuwa viumbe vyote vinamsifu na kumwimbia Mungu kwa namna yao, nasi wanadamu wote tunapaswa kuungana nao katika sifa. Hivyo mazingira ni kioo kinachoakisi utukufu wa Mungu. Hapa anatutafakarisha juu tena juu ya Zaburi ya 8, ambapo mzaburi anaona ukuu wa Mungu azitazamapo mbingu, kazi ya mikono ya Mungu, Mwezi na nyota za mbinguni na Mwanadamu aliyemwumba mdogo kidogo tu kuliko yeye mwenyewe, akamvika taji ya utukufu na heshima.
Tatu maisha ya unyenyekevu na kumtegemea Mungu. Mtakatifu Francis kwa kumwita dada dunia au ndugu moto, alikiri kwamba, binadamu anategemea uumbaji kila siku, kwa Chakula, kwa hewa, kwa joto, kwa maji na mahitaji mengine mengi ambavyo kimsingi ndivyo ilivyo. Hii inatufundisha kuwa wanyenyekevu, kutambua thamani ya mazingira yetu na kukiri kuwa, hatuwezi kuishi pasipo mazingira hayo. Mwenyezi Mungu alitupatia mazingira haya ili tuweze kuishi, tuyajali, tuyatunze, tuyaendeleze ili iwe ni nyumbani kwetu sisi sote kama Watoto wa Mungu.
Anne anatufundisha Ekolojia ya Kiroho. Wimbo huu wa Mtakatifu Fransisko wa Asizi, ni mfano wa kwanza kabisa wa teolojia Kikristo kuhusu mazingira. Wimbo huu unaunganisha imani yaani kumtukuza Mungu na maisha yetu ya kila siku yaani kuilea na kutunza dunia, uumbaji ambao kwao tunamtukuza Mungu. Mtakatifu Francis kwa wimbo huu maarufu, wa Sifa kwa Bwana anakuwa ndiye Mtakatifu wa Ekolojia. Yaani Mtakatifu anayeeleza uhusiano wa uliopo kati ya viumbe na mazingira, ambao kimsingi ndio unaowezesha maisha kuendelea kuwapo katika uliwengu huu.
Tano Maisha, mateso na matumaini. Mtakatifu Francis ikumbukwe kwamba aliandika Wimbo huu akiwa mgonjwa sana na karibu kuwa kipofu, mwaka 1224 au 1225 hivi. Hata hivyo hakusita kuendelea kuimba kuhusu uzuri wa dunia na upendo wa Mungu. Hii inamaanisha kuwa hata katika nyakati za maateso na giza, bado kuna uzuri na tumaini katika Mungu na katika uumbaji wake.
Wimbo huu una ujumbe gani kwetu katika ulimwengu wa sasa?
Kwanza uharibifu wa mazingira duniani. Dunia yetu ya leo inakabiliwa na changamoto kubwa. Mabadilio ya tabia ya nchi ambayo kimsingi yametokana na uharibifu mkubwa wa mazingira, yamepelekea ukame, ongezeko la joto kali duniani kutokana na kuharibika kwa Ozone layer, mafuriko, njaa, magonjwa mbalimbali, nk.
Uchafuzi wa hewa na maji umehatarisha kwa kiasi kikubwa sana afya ya binadamu na Wanyama hali kadhalika. Ukataji wa miti hovyo umepelekea uharibifu mkubwa sana wa uoto wa asili, kupotea kwa Wanyama pori na ongezeko la hewa ya ukaa yaani. Kupotea kwa bayonuai yaani aina mbalimbali za viumbe zimepotea kabisa kutokana na kuharibiwa kwa mazingira yao yaliyowawezesha kuishi na kuendelewa kuwepo. Kwa kuzingatia changamoto hizi tajwa ambazo, kimsingi zimeukumba na kuuathiri kwa kiasi kikubwa ulimwengu, Baba Mtakatifu Fransisko, akiwa na Mawazo yale yale kama Mtakatifu Fransic wa Assisi, aliona hili sio tu tatizo la kisayansi bali pia ni tatizo la kiroho, kimaadili na kijamii. Ndiyo maana akajibu changamoto zinazokumba mazingira kwa wakati wetu kwa kukurejea Wimbo huu maarufu wa Mtakatifu Francis wa Assisi wa Laudato sii, kwa Waraka uliotolewa rasmi tarehe 24 June mwaka 2015.
Tunapotafakari dhima hii muhimu ya uumbaji na mazingira, waraka huu, kuna athari za uharibifu wa mazingira kwa maskini na wanyonge. Papa Fransisko mara nyingi alikuwa akisema, “kilio cha dunia na kilio cha maskini ni kitu kimoja.” Wahanga na waathirika wakubwa wa uharibifu wa mazingira kimsingi ni maskini. Wakati mazingira yanaharibika, maskini ndiyo wa kwanza kuathirika kwa ukame, kwa njaa, kwa uchafuzi mkubwa hewa, mafuriko, magonjwa na athari nyingine nyingi. Baba Mtakatifu alisema, “wenye mali wanaweza kujilinda, lakini wanyonge hawana msaada wowote.” Hivyo Waraka wa Laudato si, ukiwa umeingia mwaka wake wa 10 mwaka huu 2025, unataka kutukumbushia juu ya mwito wa haki ya kijamii.
Wito na mshikamano wa pamoja katika kuilinda nyumba yetu ya pamoja. Laudato Sì, siyo Waraka kwa Wakatoliki tu, bali kwa watu wote wenye mapenzi mema. Papa Fransisko alitaka dini, sayansi, siasa na jamii nzima zishirikiane kutunza nyumba yetu ya pamoja. Ni sisi sote kama wana wa Mungu, ambao Baba yetu ni mmoja na nyumba yetu ni moja, kushiriki kwa kina na kwa mshikamano katika juhudi za kulinda athari zozote dhidi ya mazingira yetu. Baba Mtakatifu Fransisko katika Waraka wake huu anazungumzia juu ya Ekolojia Fungamani. Hii maana yake ni nini hasa? Anatufundisha kuwa, maisha ya binadamu, jamii, Uchumi, siasa na mazingira yameunganishwa kabisa. Hatuwezi kuzungumzia Imani na maendeleo ya binadamu bila kuzungumzia hali ya mazingira. Kwa mfano, ukataji miti hovyo katika upande mmoja wa dunia, unaathiri kwa kiasi kikubwa dunia nzima.
Wito wa uwajibikaji wa pamoja: Laudato sii yatukumbusha kuwa, kila mmoja wetu ana jukumu, kwanza, la kupunguza Matumizi yasiyo ya lazima, kupunguza kwa kiasi kikubwa taka za plastiki, kupanda miti kwa wingi ili kulinda vyanzo vya maji na kupunguza hewa ukaa, kupunguza Matumizi ya kemikali hatarishi katika shughuli za kibinadamu katika mazingira. Ni wito kwa serikali na mashirika kutunga sheria na sera madhubuti za kulinda maizira yetu. Ni wito wa ushirikiano wa kimataifa katika kupunguza kwa kiasi kikubwa uchavuzi wa mazingira ambao madhara yake ni kwa nchi zilizo maskini. Baba Mtakatifu Fransiko alitualika pia kuwekeza katika Matumizi ya gesi safi ili kupunguza utegemezi wa miti kama chanzo cha nishati.
Wito wa kutunza vizazi vijavyo. Dunia tuliyo nayo kimsingi siyo yetu peke yetu, bali ni urithi kwa Watoto na wajukuu wetu kwa siku za baadaye. Hiyvo kuiharibu dunia ya leo ni sawa na kuiba mustakabali wa vizazi vijavyo. Kumbe amri ya Mungu kwa mwanadamu kuilima na kuitunza Bustani ya Edeni ni amri ya vizazi na vizazi. Ni wajibu wa lazima kwa vizazi vyote. Kilio cha dunia ni kilio cha Mungu mwenyewe anayesema, tazama nitafanya yote kuwa mapya (Ufu 21:5). Hivyo tunavyoishi kwa hekima kwa maisha ya sasa tukiwa na jicho yakinifu kwa maisha ya vizazi vijavyo, tunashiriki katika mpango wa Mungu wa wokovu. Tunashiriki pamoja na Kristo katika kazi ya kuupatanisha ulimwengu mzima (Kol 1:20). Baba Mtakatifu anatukumbusha kuwa kuyatunza mazingira ni kitendo cha kiroho kwa kuwa, dunia ni zawadi ya Mungu. Kuitunza ni kumshukuru Mungu kwa zawadi hiyo na kuipuuza hali kadhalika ni dhambi dhidi ya Mungu na Jirani.
Hitimisho
Utunzaji wa Mazingira ni jambo letu sote, si jambo linalowahusu watu wa umri, dini, kabila, cheo au wadhifa fulani, hivyo ni wito wetu sote kuitunza nyumba yetu ya pamoja kwa kuifanya iwe sehemu bora zaidi na salama ya kuishi. Wito wa kutunza mazingira ni wito wangu mimi na wewe, ni wetu wa kila mmoja aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Ni mwaliko kuheshimu uumbaji kimsingi kama zawadi kutoka kwa Mungu. Ni wito wa kusikiliza kilio cha maskini wanaoteseka kwa matokeo ya dhambi ya kutojali uharibifu wa nyumba yetu ya pamoja, yaani mazingira yetu. Ni mwaliko wa kushiriana kwa pamoja, kufanya kwa vitendo na mshikamano ili dunia iwe mahali salama pa kuishi kama vile Mungu alivyopanga iwe tangu kuumbwa kwa ulimwengu, kwa vizazi vya sasa na kwa vizazi vijavyo.
Asante sana kusoma makala hii. Kama unataka kubaki na sasisho, tunakualika kujiandikisha hapa ili kupata habari za kila siku: cliccando qui