Tafuta

Majilio ni maandalizi kuelekea  Sherehe ya Kuzaliwa kwa Bwana. Majilio ni maandalizi kuelekea Sherehe ya Kuzaliwa kwa Bwana. 

Domenika I majilio mwaka A:Kesheni maana hamjui siku atakayokuja Bwana

Katika Kalenda ya liturujia,Mama Kanisa ametenga vipindi vikuu sita ili kuyakumbuka kwa kuyaadhimisha maisha ya Yesu hapa duniani ambayo kwayo sisi tumekombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti kwa ajili ya uzima wa milele.Vipindi hivi ni Majilio, Noeli,Kwaresma,Pasaka,Pentekoste na kipindi cha kawaida cha mwaka.Majilio ni kipindi cha kujiandaa kwa ujio wa pili na kuzaliwa kwake Kristo.Kumbe kwa Dominika ya Kwanza ya kipindi cha majilio tunaanza sehemu ya kwanza ya mwaka wa Kiliturujia.

Na Padre Paschal Ighondo – Vatican.

Tafakari ya Neno la Mungu, dominika ya kwanza ya majilio mwaka A wa kiliturujia katika Kanisa. Kabla ya kuyatafakari masomo ni vyema kujikumbusha yafuatayo: Katika Kalenda ya liturujia, Mama Kanisa ametenga vipindi vikuu sita ili kuyakumbuka kwa kuyaadhimisha maisha ya Yesu hapa duniani ambayo kwayo sisi tumekombolewa kutoka utumwa wa dhambi na mauti kwa ajili ya uzima wa milele. Vipindi hivi ni Majilio, Noeli, Kwaresma, Pasaka, Pentekoste na kipindi cha kawaida cha mwaka. Majilio ni kipindi cha kujiandaa kwa ujio wa pili na kuzaliwa kwake Kristo. Noeli ni kipindi cha kuadhimisha kuzaliwa kwake Kristo. Kwaresma ni kipindi cha kukumbuka mateso na kifo chake nasi kukubali kuteseka na kufa kuhusu dhambi; Pasaka kipindi cha kufufuka pamoja na Kristo katika upya wa maisha; Pentekoste kipindi cha kumpokea Roho Mtakatifu, mfariji na kiongozi wetu katika kweli na uzima, na Kipindi cha kawaida cha mwaka ni cha kuishi ndani ya Roho Mtakatifu tukiwajibika kuusimika Ufalme wa Mungu mpaka Kristo atakapokuja tena.

Kumbe kwa Dominika ya kwanza ya kipindi cha majilio tunaanza sehemu ya kwanza ya mwaka wa Kiliturujia. Neno majilio, tangu zamani wapagani walilitumia kuashiria ujio wa miungu yao, katika siku maalum ambayo walizionesha wazi sanamu zake ili kuzisujudia na kuziabudu, ziwapatie baraka, neema na fanaka. Lakini pia lilimaanisha mda wa maandalizi kwa ziara rasmi ya mfalme. Wakristo wa mwanzo walichukua maana hizi mbili: kumaanisha kipindi cha maandalizi ya kumpokea Mungu wa kweli na ujio wake duniani, kujifunua na kujidhihirisha katika nafsi ya Mwanae, Bwana wetu Yesu Kristo. Kwetu sisi hiki ni kipindi cha kujiandaa vyema kiroho kumpokea Yesu Kristo, Emanueli; Mungu pamoja nasi, katika maisha yetu na kukumbuka kwa kuadhimisha kuzaliwa kwake hapa duniani na Bikira Maria.

Kipindi hiki kinadumu majuma manne na kimegawanywa katika sehemu kuu mbili. Sehemu ya kwanza ni kuanzia dominika ya kwanza ya majilio mpaka tarehe 16 Disemba. Mama Kanisa katika liturujia ya sehemu hii, kupitia masomo, nyimbo, sala na maombi, anatuongoza kutafakari juu ya ujio wa pili wa Yesu Kristo katika utukufu wake, kuwahukumu wazima na wafu. Ujumbe wake umejikita katika kutualika tujiandae vyema kwa ujio huku akituambia: “Itengenezeni njia ya Bwana, yanyosheni mapito yake. Bwana yu karibu. Atakuja kuliokoa na kulihukumu taifa lake”. Ni katika tumaini hili wimbo wa mwanzo unasema hivi; “Ee Bwana, nakuinulia nafsi yangu, ee Mungu wangu, nimekutumainia wewe nisiaibike milele, adui zangu wasifurahi kwa kunishinda. Naam, wakungojao hawataaibika hata mmoja”. Na mama Kanisa katika sala ya mwanzo anasali; “Ee Mungu Mwenyenzi, tunakuomba utujalie sisi watumishi wako neema hii, ya kwamba Kristo atakapokuja tumlaki na matendo mema, atuweke kuume kwake, tustahili kupata ufalme wa mbinguni”. Na katika utanguzi wa wakati huu anasali hivi: “Sasa tunangojea kwa hamu siku ile atakapokuja mara ya pili Kristo katika utukufu wake”.

Sehemu ya pili inaanza tarehe 17 hadi 24 Desemba. Masomo, nyimbo na sala za sehemu hii yanatuongoza kutafakari juu ya ujio wa kwanza wa Yesu Kristo, kwa kutazama jinsi Wasraeli walivyomsubiri kwa hamu kubwa mkombozi. Katika liturujia ya sehemu hii Mama Kanisa anajifananisha na taifa la Mungu la Agano la Kale linalotarajia kwa hamu kubwa ujio wa Mkombozi akiyaangalia na kuyaona mateso na maumivu ya kila mtu ambaye hajakombolewa bado, lakini amejaa matumaini yenye furaha ya kumngojaea Mkombozi aliyeahidiwa na Mungu, ambaye ujio wake ulitangazwa na manabii. Wakati huu ni wa matayarisho ya kusherehekea sikukuu ya kuzaliwa kwake Kristo katika historia.

Ni katika mukadha huu ni vyema kuchukua tahadhani hii: Tusifikiri na kudhani kuwa hakuna jipya katika kipindi hiki tunachokianza na kipindi kilichopita cha mwaka wa kiliturujia. Tukumbuke kuwa kila adhimisho la kiliturujia la tukio lolote katika historia ya wokovu wetu linapoadhimishwa na mama Kanisa lina hali mbili; kwanza kutukumbusha yaliyotokea katika historia na pili kuhuisha na kupyaisha maisha yetu ya kiroho katika kumfusa Kristo kwa maadhimisho ya tukio hilo. Hivyo kila mwaka wa kiliturujia ni mpya na wa pekee na hakuna unaofanana na mwingine, kwani kila adhimisho lake linapyaisha na kuhuisha maisha yetu ya kiroho na kutuleta karibu zaidi kwa Mungu. Hivyo matukio yote ya kiliturujia yanapotukumbusha yaliyotokea zamani, yanafanya sehemu ya maisha yetu na yanatufanya tuonje upendo wa Mungu katika mafumbo tunayoadhimisha katika kila hatua ya maisha yetu hapa duniani, tunapoelekea katika maisha ya umilele mbinguni. Kumbe tusikianze kipindi hiki kwa mazoea kana kwamba hakuna jipya lolote, bali tufungue mioyo yetu tuweze kujichotea neema na baraka zitokanazo na kipindi hiki kwa njia ya Yesu Kristo Bwana na Mwokozi wa maisha yetu.

Somo la kwanza ni la kitabu cha Nabii Isaya (Isa. 2:1-5). Ni utabiri wa ujio wa Masiha atakayeyafanya mataifa yote kumwelekea Mungu; naye atawapa amani, heri na baraka. Kristo ndiye Masiha aliyetabiriwa, naye amekwisha kuja, ameuweka imara mlima wa nyumba ya Bwana yaani Kanisa, na akatupandisha katika mlima huu kama Mwandishi wa barua kwa Waebrania anavyosema; “Lakini ninyi mmefika katika mlima Sayuni, kwenye mji wa Mungu” (Waebr.12:22). Utimilifu wa utabiri huu, utadhihirika katika ujio wa pili wa Masiha, Yesu Kristo. Katika kuusubiri huo ujio wake wa pili, hatupaswi kuwa katika hali ya huzuni, majonzi, wala malumbano, wala vita, bali katika amani na utulivu, hali inayopatikana kwa kuziishi amri na maagizo ya Mungu na kuzibadili zana za kivita kuwa zana za uzalishaji mali – panga kuwa majembe, na mikuki kuwa miundu, kukomesha vita kati ya mtu na mtu, au kati ya taifa na taifa.

Hili ni dokezo la ulimwengu mpya, uzima wa milele mbinguni. Ni katika tumaini hili zaburi ya wimbo wa katikati inasema; “Nalifurahi waliponiambia, na twende nyumbani kwa Bwana. Miguu yetu imesimama ndani ya malango yako, Ee Yerusalemu. Ee Yerusalemu uliyejengwa kama mji ulioshikamana, huko ndiko walikopanda kabila, kabila za Bwana. Kwa ajili ya ndugu zangu na rafiki zangu, niseme sasa, Amani ikae nawe. Kwa ajili ya nyumba ya Bwana Mungu wetu, nikutafutie mema” (Zab. 122: 1-4, 8-9).

Somo la pili ni la waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi (Rum. 13:11–14). Ujumbe ni kuwa Mwanga uliotabiriwa na nabii Isaya ni Yesu Kristo. Nasi kwa ubatizo tumeupokea Mwanga huo kwa mara ya kwanza kwa imani yetu. Tutakutana nao tena katika maisha ya uzima wa milele baaada ya kifo, ambapo kutakuwa na amani ya milele. Ili tuweze kuifikia hii amani, tunapaswa tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru, tuenende kwa adabu, si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu. Ni mwaliko wa tumvaa Kristo Yesu, ili tusiwashwe na tamaa za kimwili.

Injili ni ilivyoandikwa na Mathayo (Mt. 24: 37–44). Ujumbe mahususi ni huu, kwa kuwa hakuna anayejua siku wala saa ya kufa kwake na kupokea hukumu yake, basi tuwe tayari mda wote. Yesu anatuambia tuweni macho, tukeshe, kwa kutoa mifano mitatu: mfano wa kwanza ni wa nyakati za Nuhu. Nyakati hizo kulikuwa na makundi mawili ya watu; kundi la kwanza ni la wale waliokuwa wamezama katika shughuli na mambo ya kidunia: kula, kunywa, kuoa na kuolewa, wakamsahau Mungu na amri zake, wakaangamizwa na gharika kuu katika uovu wao. Kundi la pili ni la waliokesha na kumsikiliza Mungu, hao ndio waliookoka na gharika. Mfano wa pili unawahusu wote wanaofanya shughuli mbali mbali za kila siku: kulima, kuvuna na kusaga nafaka. Nao pia hawana budi kukesha. Mfano wa tatu ni wa mwizi ambaye hatangazi muda aendapo kufanya uhalifu.

Mifano hii inatutahadharisha kuwa tayari kwa kifo siku na wakati wowote. Na kwa kuwa kila mtu akifa anahukumiwa peke yake pale pale kadiri ya hali aliyokutwa nayo wakati huo. Basi ni vyema kuwa tayari wakati wote. Tusilale usingizi katika dhambi, usiku umekwisha na mchana umekaribia, tuamke katika wema. Kama una ugomvi na yeyote yule, umalize mapema, jipatanishe naye, jipatanishe na Mungu. Kama hupokei Sakramenti kwa sababu ya vizuizi, vitoe mapema, usiseme baadaye kidogo, maana hiyo baadae inaweza kutanguliwa na kifo. Wala usiseme mimi bado kijana nikifikia uzeeni nitajipatanisha na Mungu, huna kibali cha kufika uzeeni. Usisubiri ukiwa kufani uombe mpako wa wangojwa kwani hauna mkataba wa kuwa utaugua na hautakufa kifo cha ghafla.

Nawatakieni mwanzo mwema wa mwaka mpya wa kiliturujia na majilio mema, tujiandae vyema kiroho ili siku ya Noeli, Kristo Yesu, Masiha wetu, Emanueli, Mungu pamoja nasi, azaliwe upya ndani mwetu, atuhuishe kiroho na kutuweka karibu zaidi na Mungu Baba yetu. Tukumbe kuwa maisha yetu yote ni kipindi cha majilio, mwendelezo wa kumsubiri Kristo hadi atakapokuja tena kutuita kwa njia ya kifo tukaishi milele yote mbinguni. Ni katika tumaini hili mama Kanisa katika sala ya kuombea dhabihu anasali hivi; “Ee Bwana, tunakuomba dhabihu tunazokutolea kutokana na mapaji uliyotujalia tuyatumie kwa ajili ya ibada hapa duniani, yatupatie tuzo la ukombozi wa milele”. Na Katika sala baada ya komunyo anasali hivi: “Ee Bwana, tunakuomba mafumbo haya tuliyoadhimisha yatufae sisi tunaotembea katika malimwengu, nawe utufundishe kupenda mambo ya mbinguni na kuzingatia ya milele”. Na hili ndilo tumaini letu.

Tumsifu Yesu Kristo.

TAFAKARI YA MAJILIO
28 Novemba 2025, 17:26